Saturday, February 21, 2009

SIHITAJI KUKAMILISHWA NA YEYOTE.

Kamradi kangu

Hebu chukulia kama umeambiwa uandike wasifu wako kwa mtu usiyemfahamu ambaye unaamini akiusoma wasifu huo atakujua kwa asilimia mia moja kuwa wewe ni mtu wa namna gani.
Jiulize ni kitu gani hasa utaandika katika kuueleza wasifu wako ili huyu mtu msiyefahamiana kabisa akufahamu kupitia maandishi yako?

Kwa mfano labda utaanza kwa kusema, “mimi ni mwanamke au mwanaume, ni mwanafunzi; mfanyakazi au nimejiajiri nakadhalika nakadhalika.
Labda utaeleza juu ya vitu unavyovipenda na vile usivyovipenda, pamoja na tabia yako kama vile ni mwenye aibu, chakaramu, mtu wa kujirusha, mkimya, mpole, na tabia nyingine ambazo zinaweza kumfanya mtu atakayesoma wasifu wako akufahamu vizuri.

Jaribu kuchunguza tabia za marafiki zako wote pamoja na ndugu na jamaa waliokuzunguka, Je unadhani yupo japo mmoja ambaye mmetokea kufanana kwa kila kitu?
Sidhani, na kama yuko labda itakuwa ni baadhi ya vijitabia fulani mnafanana lakini haiwezi kutokea mkafanana kwa kila kitu.

Vipi kuhusu ndugu mliozaliwa tumbo moja, yawezekana kweli mkafanana kwa kila kitu? Jamani si tumezaliwa na baba mmoja na mama mmoja, Kwa nini sasa tusifanane kwa kila kitu?
Hii nadhani haiwezekani, na haitatokea iwezekane hata siku moja.

Kwa mtazamo huo basi, naamini kwamba kuna Koero mmoja tu hapa duniani, naye ni mimi, kama kuna mtu anatumia jina la Koero, basi hiyo ni coincidence, lakini hawezi kufanana na mimi hata kidogo, tembea dunia yote hii, Koero ni mimi tu. Kwa hiyo mimi ni mtu maalum kama ulivyo wewe na mwingine.
Binafsi najivunia kwa jinsi nilivyo na najikubali kwa kila kitu, kama ninayo kasoro, basi wewe ndio umeiona kwa mtazamo wako lakini mimi sijaiona.

Hivi karibuni nimetofautiana na mama yangu juu ya mustakabali wa maisha yangu.
Eti anataka nirejee chuoni ili kuendelea na Masomo, wakati nimeshadata na Biashara zangu. Baada ya lile zengwe la kurejeshwa nyumbani na chuo kufungwa nimejikuta nikipata uamuzi mwingine wa kuendesha maisha yangu, na nimeona niwe mfanyabiashara.
Elimu niliyoipata ya Kidato cha sita inatosha sana kwani nimeshajijua kuwa mimi ni nani na hata nikiendelea na masomo ya chuo kikuu sidhani kama itanisaidia sana katika kufikia malengo na matarajio yangu. Na hata kama nikisoma na kupata shahada kumi sidhani kuwa hayo ndio malengo yangu, sana sana naona ni kupoteza muda bure.

Nimeona nijikite kwenye biashara, kwa sababu naona kuwa ni kipaji changu na nina matarajio makubwa sana hapo baadae ya kuwa mmiliki wa kampuni kubwa yenye matawi karibu nchi nzima, hivyo ndivyo ninavyoiona biashara ya yangu.
Nadhani utaniuliza kama utaalamu wa kuendesha hiyo biashara nitauapa wapi? Jibu ni rahisi sana, nitaawajiri hao wasomi wenye shahada zao na kwa hakika bishara yangu itakuwa ikiendeshwa kwa ufanisi, kwani naamini naweza kuajiri hata Profesa, si ilimradi nimlipe mshahara mzuri na marupurupu?
Kwani hamjui kuwa nchi hii watu wanasoma ili wajiriwe badala ya kujiajiri?

Kwa nini mama yangu anakazania nisome? Anatafuta kuridhisha nafsi yake. Mama yangu anao ndugu zake ambao wamesomesha watoto wao mpaka vyuo vikuu na wanazo nafasi kubwa wengine wakiwa serikalini na wengine wakiwa wameajiriwa na mashirka ya kimataifa wakiwa wanashikilia nafasi za juu, sasa wakikutana kwenye vikao vyao vya ndugu, kila mmoja huanza kujisifu kuwa wanae wamesoma au wanaendela na masomo ya elimu ya juu, ilimradi kutaka kujionyesha kwa wengine kuwa watoto wao ni wasomi.
Kwa upande wa familia yetu dada zangu na kaka zangu wote ni Graduate, mimi tu ndiye nimechomoa kuendelea na elimu ya juu.

Kwa kweli baba yangu hana tatizo na uchaguzi wangu, lakini mama, Duh! Ameng’ang’ania kweli nirejee kusoma, na mimi nimekataa kabisa.

Mimi naamini kila mtu anao wasifu wake na malengo yake haihitaji mtu aje akukamilishe kwa kukupangia kuwa ufanye nini juu ya maisha yako.
Mtu kukubali kupangiwa nini cha kufanya juu ya maisha yako ni kupotea njia, ni sawa na kupanda basi la kwenda Mtwara wakati nia yako ni kuelekea Arusha!
Ukweli ni kwamba wako vijana wengi wanakabiliwa na changamoto inayonikabili sasa. Binafsi nimeweza kukabiliana nayo na ninaamini nitashinda kwani baba yuko upande wangu, lakini ningependa kuwashauri vijana wenzangu kwamba tusikubali kuburuzwa na matakwa ya wazazi, sisi ni watu kamili hatuhitaji wazazi watukamilishe.



Naomba nisitafsiriwe kama nawakatisha tamaa wale wanaotaka shahada, hapa nimeeleza malengo yangu, naamini pia ninyi mnayo malengo yenu, kama malengo yako ni kusoma, basi soma mpaka upate shahada yako ya uzamili ikiwezekana uwe hata Profesa,


Samahani nimeandika makala hii nikiwa na mchanganyiko wa hasira na msongo wa mawazo, hata hivyo naamini watambuzi watanielewa.

18 comments:

MARKUS MPANGALA said...

DUH! kama binadamu hakika tunapaswa kujiuliza ni namna gani tunaweza kutambulika kama tulivyo, Munga Tehenan asemavyo sisi ni akina nani?
Nimeongeza na mama yangu leo asubuhi kuhusu suala la kurejea Chuo, toka Songea katwanga simu kuuliza jambo hilo. Lakini jibu langu nilisema usiwe na wasiwasi ingawa sipendi elimu yetu bongo ilivyo kwani mie hainifai.

Nilijibu hivyo kifalsafa, najua mama yangu anajua majibu yangu huwa yanamaanisha nini, amekasirika, amekata simu hajaongea, amezima simu, nikasema hewalaaa jamani.

Koero hili suala hapa nilipo namumwa tena homa ya mawazo siyo kidogo, kwani inaonekana watu hawaelewi nini maana ya uamuzi na maisha. Nimejaribu kuelekeza kwa ndugu zangu, lakini hakuna kitu- nimesme yote pouwaaa hata wakinitenga na kusema mengi wals irudi chuo hata kwa hoja gani, nimeamua kula nondo za IT kwa juhudi zangu vyovyote niwezavyo kwani nachezea Kompyuta nitakavyo.

Daima suala la kuamuliwa lipo kwa namna nyingi. wengi wanapoamua maisha ya mtu hawajui ni kiasi gani yanamwathiri mhusika, kwani anafanya kitu ambacho hawezi au hakipo katika utashi wake. Watambuzi wanasema 'nyumba yako hapa nuniani'. hii ni ile kazi unayoifanya na uliyokusudiwa kuifanya kwani kila kiumbe amekuja kufanya kitu fulani.

Binafsi najua ninauwezo wa mambo ya habari, na napenda kuwa mwanahabari kama Ndesanjo Macha au Jenerali Ulimwengu.
Lakini yote nifanyayo natishwa eti nitawindwa na mambo mengine kadhaa.

ok tuache kwanza. Kwa maoni yangu Koero kama kweli dhamira unayo na maudhui yake yanakuja nafasi ya kuwaelekeza yanayokuhusu ni vema ukasema uamuzi wako ni kwa ajili yako na unataka iwe hivyo kwa nia njema.
Kama hakuelewi leo, ipo siku atakuelewa tu na hakika ataamini kuwa ulichoamua ni sahihi.

Nimewatembelea washkaji zangu kule DUCE(chang'ombe) hawa nfahamiana nao kitambo, pia nimewatembelea washkaji pale main campus, wananishangaa kwa uamuzi wangu na wananiona kama kichaa tu.

Lakini wapo wanaokiri kwamba nimecheza karata nzuri bila kutoa hoja za karata hizo. Nimewahurumia kwani siyo kwamba wanasoma bali wanawaza nini kitatokea katika elimu zao.
Nawahurumia sana washkaji zangu, lakini wssome tu, maana sitaki kujaza madeni ya akina kiwete kisa kusoma halafu huduma mbavu za mbwa.

Koero; rejea mashairi ya Nas Escobar "I CAN", Tupac shakur "UNTIL THE END OF TIME, KEEP YA HEAD UP, LETTER TO UBORN CHILD, CHANGES"
Pia msome Delai Lama. Msikilize Eminen katika "CLENING OUT MY CLOSET", WHEN I AM GONE na kibao kipya CRACK A BOTTLE"

Au sikiliza wimbo wa Mr Ebbo "MANENO MBOFUMBOFU"

ubarikiwe lakini usilie wala usiwaze ipo siku ataelewa

Jimy said...

Koero
Hiyo ni changamoto ya kutosha. But you need to take it slow,girl!!
By the way,u look good on the picture!
Jimy

PASSION4FASHION.TZ said...

Koero pole sana mpenzi,umejieleza vizuri sana naona unawakati mgumu,naomba nikushauri kidogo tu,kama ni maamuzi nakuomba saana usichukue uamuzi wowote wakati unahasira.

Sasa haya ndio matokeo ya mafisadi wanaiba mapesa ndio wanao sababisha migogoro kila kona,kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu.

Mzee wa Changamoto said...

K.
Pole sana kwa mchanganyiko wa hasira na msongo wa mawazo. Si unakumbuka Mandela aliposema "the greatest glory in living lies not in never falling, but in rising everytime we fall". Nawe sasa uko chini ama umeanguka kimawazo, kifuraha na kimipango. Lakini unapojipanga kuamka jaribu kutazama pembeni. Usije ukaamka bila kuangalia kilichokuangusha kisha ukajikuta chakuangusha tena. Nawaelewa kiasi kina Mama na licha ya kung'ang'ania kile wapendacho, wanaweza kuwa na imani fulani ambayo pengine isiwe kweli kwako ama ikawa kweli lakini hauiangalii ama kuiona aionavyo yeye. Sasa wacha nikwambie Dadangu. Jipe siku mbili tatu za kurejesha furaha yako, kisha rejea kwa Mama na umwambie sio tu hukubaliani naye, bali kwanini hukubaliani naye na muombe akwambie kwanini hakubaliani na wewe. Hapa kuna kupishana kwa uelewa tuu Dadangu. Kama ulivyosema kuwa hatuko sawa, ni kwamba pengine Mama anafikiri unaelewa anachomaanisha anaposema urejee shule nawe yawezekana unadhani anaelewa malengo yako. Uzuri ni kuba Baba anaelewa (kwa mujibu wa ulivyosema) hivyo nenda na ikiwezekana waite wote na Baba atakusaidia kuweka bayana pale utakapokwama. Lakini wewe na Mama mnaweza kukubaliana kwa urahisi kabisa ama KUKUBALIANA KUTOKUBALIANA kwa upendo na kisha kila mtu akaendelea na maisha yake ambayo mwenzake hakubaliani nayo. Hilo ndio kubwa Dadangu, kuwa HATA KAMA HAMTAKUBALIANA NA MAMA, LAKINI MHAKIKISHE KUWA MMEKUBALIANA KUTOKUKUBALIANA ILI MAMBO MENGINE YOTE YAENDELEE. Mpigiane simu kujuliana hali, kujua mnaendeleaje, kutembeleana, kwenda kanisani pamoja na mengine kasoro suala la biashara na shule.
Hii ni kwasababu una uhusiano usio wa hiari na Mama na ni vema mkaendelea kuhusiana hata mpianganapo. Lucky Dube aliimba kuwa YOU CAN CHOOSE YOUR FRIEND, BUT YOU CANNOT CHOOSE, WHO YOU'RE RELATED TO. Mama atabaki kuwa Mama, ninachoomba ni wewe kuwa na uhusiano na Mama hata kama hamkubaliani katika hili.
Nuff Respect to you & Mom too

Simon Kitururu said...

@Dada koero: Sikiliza Baba. Sikiliza Mama! Wote wanafanya kwa Mapenzi.

Lakini Koero anajua Koero.

Na Simon Kitururu anampenda Koero:-(

Mwisho wa siku ya kuchukia, ENDELEA KUFIKIRIA, fikiria, halafu Tabasamu.

Tram Almasi said...

Koero, hongera sana kwa yote.I always believe, you can be what you wanna be provided you stick to what you believe in!Go girl!
Kwa kuongeza tu, ninaguswa sana na jinsi watanzania wanavyo poteza maisha kila siku kutokana na ajali.Kwa zaidi ya miaka 10 nimekuwa nikishuhudia jinsi gani ajali zinavyoathiri maisha ya watu kila kukicha.Nimeona ni vema nikitumia experience yangu kuwaelimisha watanzania wenzangu na kutaka tuungane pamoja kupambana na jinamizi la ajali hapa nchini. Nakubaliana nawe, wakati wa kusema"ajali haina kinga sio huu". hivyo nimeanzisha blog inayoitwa Mr. Bobos Class(http://ajali-traumaclass.blogspot.com).Mr. Bobos Class, ni blog inayotoa taarifa mbalimbali juu ya madhara ya ajali mbalimbali zitokanazo na matumizi ya magari,treni, mashine au hata vifaa mbalimbali vya kazi kama mapanga na majembe.Mbali ya kutoa taarifa pia ina lengo la kuwaelimisha waliopata madhara hayo ni jinsi gani wanaweza kupata msaada baada ya kuathirika kutokana na ajali mbalimbali.Blog hii itaungana na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya ajali kwa njia moja au nyingine, kuelimisha na kutoa ushauri.Tafadhali wajulishe watanzania wote watembelee blog hii na kutoa michango yao kusaidia kupambana na janga hili. karibuni nyote.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kazi ipo.

"mheshimu baba yako na mama yako siku zako zipate kuwa nyingi"

NATAMANI WAANDISHI WA BIBLIA WANGEWAHUSISHA WATOTO PIA.

Evarist Chahali said...

Marehemu Baba wa Taifa alisema "kupanga ni kuchagua."Alikuwa na mantiki nzito japokuwa baadhi ya mipango alojaribu kwa jamii haikufanikiwa.Wakati mwingine,matokeo ndio hutoa hutoa ukumu iwapo mipango au njia zilizotumika zilikuwa mwafaka.Hata hivyo ni muhimu kuzingatia kuwa mipango mizuri hutarajiwa kuzaa matokeo mazuri,and vice versa.

Kwanza pole dada yangu,hayo ndio maisha.Pili naungana na wadau hapo juu,husasan ndugu yangu MZEE WA CHANGAMOTO kuhusu umuhimu wa kutuliza kwanza hasira kabla ya kuchukua maamuzi.Pengine ni muhimu kujiridhisha kuwa sababu pekee ya mama kupendelea wewe usome sio hiyo ya kuridhisha nafsi yake PEKEE.Well,hata kama ni hiyo tu,hudhani kwamba NAKUPENDA SANA ndio maana ataridhika kukuona chuoni.Kama suala ni kujiridhisha,mbona umeshasema kuwa kaka na dada zako wote ni graduates,implying kwamba kama kinachomsukuma mama ni kuridhika pekee basi asingejali sana kuhusu wewe bcoz wenzio katika family yenu wameshamridhisha.

Nakubaliana nawe kwamba kila mtu ana wasifu wake na malengo yake.Lakini ni muhimu pia kukumbuka kwamba njia bora zaidi ya kufikia malengo ni kuitumia kila sekunda kama muujiza ambao hautojirudia katika maisha.Je hudhani kwamba iwapo malengo yangu yalikuwa haya uliyoamua kuyafuata,then ulipoteza muda kwenda chuoni,in the first place?Sitaki kukuhukumu ila nashawishika kuhisi kwamba mtazamo wako wakati unajiunga na masomo ulikuwa positive kuliko ulivyo sasa.Na hilo sio kosa,ila la muhimu ni kujiuliza why ilikuwa positive wakati huo na sasa imekuwa a bit negative.

Mwisho naomba nitofautiane kimtazamo na wewe kuhusu kauli yako kwamba "Mtu kukubali kupangiwa nini cha kufanya juu ya maisha yako ni kupotea njia...".Hivi kwa mfano mzazi akimpangia mwanae wakiume kwamba aache kuvuta bangi,na kijana huyo akakubali kufuata ushauri huo,bado utasema huyo kijana amepotea njia?Twende kwenye mfano halisi kuhusu wewe na mama yako.Una uhakika gani kwamba ungefuata ushauri wake ungepotea njia?Je hao nduguzo graduates kuna aliyepotea njia?Tena una bahati kwamba unatoka katika familia ambayo kuna graduates hivyo ni rahisi kwako kujifunza kutoka kwao.By the way,hata ukiwa graduates bado una nafasi ya kuwa mjasiriamali.

Mwisho kabisa,kama dada yangu,nakusihi sana kaa chini na mama.Nakwambia hivi kama mtu niliyempoteza mama about 6 months ago.Huna asset kubwa maishani kama mzazi/wazazi.Mie japo sio mshika dini saaana naamini kwa nguvu zote kuwa baada ya Mungu ni wazazi,kisha ndio yanakuja masuala mengine.Pasipo baraka za wazazi,kinachoonekana mafaniko mwanzoni kinaweza kugeuka majonzi mwishoni.Na katika case yako,bora mama ndio angekuwa anaafikiana nawe na baba anapinga,kuliko vice versa...japo wote ni wazazi,mama zetu huwa karibu zaidi na watoto wa kike huku baba wakiwa karibu zaidi na watoto wa kiume.

However,uamuzi wa mwisho ubaki mikononi mwako.

Evarist Chahali said...

Paragraph ya Pili Mstari wa saba...neno lililokusudiwa ni "hudhani kwamba ANAKUPENDA SANA..."

Samahani

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ndugu evarist japo unaelekeza kwa koero lakini tuambizane mawili haya.
mzazi hawezi hata kidogo kumpangia mwanae kuacha bangi. bali anaweza tu kumshauri na wala awezi kumlazimisha, bali kumbembeleza tu.

pia imani yako baada ya mungu kwamba ni wazazi, ina maana sisi tusiona wazazi zu ambao hatujawahi kuwa na wazazi sio watu kamili?

nguvu kwa maana ya nguvu alizonazo binadamu au connection na nguvu kuu iitwayo mungu ni suala la binafsi na kila mtu ana nguu yake mwenyewe. sisi kama uwepo ni nguvu. wakristo husema, mungu alipuliza hewa na mtu akawa mtu ikiwa na maana kwamba mungu aliweka nguvu na hivyo, koero km binadamu yeyeyote yule amekamilika.

mtu kuachana na elimu sioni kama ni noma. wewe angalia nchi yetu tangu uuru imekuwa ikiongozwa na wasomi lakini haina mwelekeo karibia miaka 50 sasa! sasa elimu hiyo ni ya nini?

Fred Katawa said...

Evaristi na mamake koero mna tatizo linalolingana"kutojiamini"Mtu asiyejiamini uamini kuwa hawezi kufany jambo likafanikiwa bila baraka za wazazi au nguvu nyingine isiyoonekana.Koero ana ndoto na malengo yake ambayo hayafanani na ya mamake.Mamake Koero yapaswa amuache koero afanye atakalo ikiwa tu halimuumizi koero na analipenda

Yasinta Ngonyani said...

Hodi tena kwa mara nyingine nataka kukuambia ya kwamba nimerudi. pia kukuambia kazi nzuri tupo pamoja

Koero Mkundi said...

Ahsanteni sana kwa maoni yenu pamoja na ushauri wenu mzuri.
Unajua nimeshangaa sana kwamba pamoja na kujieleza kiasi hiki lakini kuna watu ambao hawakunielewa, sijui ni kwa nini?

Ni kweli nilikuwa na msongo wa mawazo kutokana na shinikizo la mama la kunitaka nirejee chuoni ili kuendelea na masomo, na ndio sababau nikasafiri na kuja huku Arusha kwa Mjomba angu kujipumzisha kidogo.

Nimeona siwezi kupoteza muda wangu kusomea taaluma ambayo sitaitumia ili kufikia malengo yangu.

Nimeeleza vizuri tu kuwa malengo yangu ni kuwa mfanyabiashara mkubwa na nimeshaweka msingi kuelekea huko.
Sidhani inahitaji kuwa na shahada ili kuwa mfanyabiashara mwenye mafanikio.

Nilikuwa najaribu kuwashirikisha wanablog wenzangu pamoja na wasomaji wengine kuwaeleza hisia zangu nikidhani watanielewa lakini nimeshangaa kuona kwamba kuna wengine wanajaribu kunielekeza njia ile ile ambayo kwangu naichukulia kama kupoteza muda wangu bure.

Mimi naamini kuwa kila mtu anayo haki ya kujiamulia mustakabali wa maisha yake.
Kaka Kitururu amewazungumzia Serena na Venus Williams, kwamba wao walichaguliwa future na baba yao kwa kufundishwa kucheza Tenis na sasa ni watu maarufu, nakubaliana nae lakini, kama alivyosema kwamba wale ni Serena na Venus, na mimi ni Koero, sasa mpaka hapo haoni tofauti?

Kaka Evarist naye kaeleza mengi lakini kwa bahati mbaya sijamuelewa, labda anishereheshee alikuwa na maana gani? hilo namuachia yeye.

Hata hivyo nakubaliana na Article ya kaka Mtambuzi aliyoiweka pale kibarazani kwake pale aliposema, nitamnukuu,

“Pamoja na kwamba dunia imebadilika na inaendelea kubadilika lakini bado wanataka malezi waliyolelewa nayo miaka ya 1947 bado yapewe nafasi.
Bado wanataka kufuata mlolongo ule ule wa malezi waliyopewa na wazazi wao.
Nadhani kuna haja ya wazazi kuukubali ukweli huu kwamba malezi waliyopitia hayana nafasi tena kwani dunia imebadilika sana. Kama mzazi, inawezekana akawa na ushauri kwa mtoto juu ya mustakabali wa maisha yake, lakini kama mtoto anayo malengo yake na anajua ni kitu gani anahitaji katika maisha yake basi apewe ushirikiano katika kufikia malengo yake aliyojiwekea badala ya kuburuzwa kuelekea njia asiyoitaka”.

Mwisho wa kunukuu.

Nakubaliana na ushauri wake kwa sababu ameeleza ukweli kabisa. Wazazi wetu bado wanataka kutulea kama wao walivyolelewa, bila kujali kwamba dunia imebadilika. Na sio kwamba hawajui? Wanajua kabisa ila naona mazoea yamewafunga kiasi kwamba wanashindwa kusoma alama za nyakati, wanajifanya Wa-Conservative wasiopenda mabadiliko.

Jana, baba kanipigia simu na kunijulisha kwamba wamekubaliana na uamuzi wangu, mama amekiri kuwa niko sahihi, ila ameshauri nijiendeleze kwa kusoma masomo ya Biashara Pale CBE huku nikiendelea na biashara zangu na tumeafikiana hivyo, ingawa nimewaambia kuwa swala la kujiendeleza bado litabaki kuwa ni uamuzi wangu.

Ninafikiria kuhamishia bishara zangu huku Arusha, bado nafanya utafiti kama biashara yangu italipa.

Kama kuna mwenye changamoto basi aniwekee hapa.

NB: karibu sana Dada yangu Yasinta mwana wa Ngonyani, ni siku nyingi sijakusoma mtandaoni.
Baadae nitawasiliana na wewe nyuma ya pazia kuana jambo nataka tutete kidogo.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

koeroooooooo.

majamaa yoote yanataka ujaze vyeti nymbani. yaani uharibu miaka mitatu kutafuta cheti, then basi. wengi husomea kazi wakati wao wenyewe ni kazi tayari!.

tehe, tehe, tehe...

Ivo Serenthà said...

I came to your blog through the area of Laurel Mubelwa calls, congratulations you are a beautiful girl, a greeting from Italy, good luck.

Marlow

Evarist Chahali said...

Samahani dada yangu kama sikueleweka.Anyway,naomba kkusehrehesha kwa hitimisho kwamba uamuzi kuhusu hatma ya maisha ya mwanadamu unabaki zaidi mikononi mwa mhusika mwenyewe,japo wadau (eg wazazi,marafiki,nk) wanaweza kutoa ushauri pale inapostahili.Lakini,nakumbuka Marehemu Prof Malima aliwahi kuonya kuhusu utoaji wa ushauri (namnukuu) "mtu atoe ushauri pale tu atakapoombwa ushauri,kinyume chake inaweza kutafsiriwa kama kuingilia maisha ya mtu binafsi,kujipendekeza,kumnyanyasa,nk."Hata hivyo,kwa vile miongoni mwa kanuni ngumu kuzingatiwa maishani ni kanuni za maisha yenyewe,kuna nyakati baadhi yetu tyunajisahau kuhusiana na kanuni hiyo ya ushauri.

Naomba nimnukuu Ndugu Kamala "MAJAMAA YOOOTE YANAtaka ujaze vyeti nymbani. yaani uharibu miaka mitatu kutafuta cheti, then basi. wengi husomea kazi wakati wao wenyewe ni kazi tayari!".Japo sijui MAJAMAA hayo ni yapi lakinisidhani kama ni dhambi,kosa la jinai,uhaini au upumbavu kujaza vyeti nyumbani.La muhimu ni namna vyeti hivyo vinavyotumika.Pili sidhani kwamba kutumia siku,wiki,mwezi,mwaka mmoja au mitatu kutafuta cheti ni KUHARIBU MUDA.Sio kila cheti hakina manufaa.Sidhani kama Ndg yangu Kamala unadhani kuwa hata cheti chako cha kuhitimu primary,secondary,etc pia havina maana.Cheti ni tuzo,faida au hasara zake anajua zaidi aliyekitoa au aliyetunukiwa.Cheti ni mithili ya risiti ya malipo.Hata hivyo,cheti si lazima kimaanishe mafanikio kwa vile kuhitimu na kufanikiwa ni mambo mawili tofauti just like kuwa kitandani na kulala.

Anyway,all the best dada Koero.

Koero Mkundi said...

Kaka Evarist,

Mhhh!!! Nimesoma maoni yako na nimehisi kama vile umekwazika na mtazamo wa Kamala, (kama sikosei)

Unajua wakati mwingine katika kutoa hoja au maoni katika jambo lolote kuna kutofautiana kimtazamo, lakini sidhani kama mtazamo wako hauko sahihi, nakubaliana nao kabisa ila kuna hiyari katika kufuata ushauri huo.

Ningependa kuchukuwa nafasi hii kukushukuru sana kwa ushauri wako kwani sasa nimekuelewa.

Naomba baadae tuwasiliane nyuma ya pazia kuna mengi ningependa kushea na wewe kaka yangu.

Christian Bwaya said...

Kisaikolojia baba huwa karibu zaidi na watoto wa kike kuliko wa kiume. Na mama huwa karibu zaidi na watoto wa kiume kuliko wale wa kike. Hiyo ni kanuni ya kimahusiano katika ngazi ya familia.

Aidha, baba na mtoto wa kiume huwa katika uwezekano mkubwa na kugongana kimawazo kuliko baba huyo huyo na wanae wa kike. Hali kadhalika mama na mtoto wa kike huwa katika uwezekano mkubwa wa mgongano.

Hiyo, kwa hakika, inayo nafasi muhimu sana katika uhandisi wa haiba (personality) ya mtoto husika.

Mgongano wa mtazamo husababishwa na kuibuka kwa tathmini ya haiba ndani ya mtoto anapojaribu kuilinganisha haiba yake na ile ya mzazi wa jinsia yake ili kupata haiba yake yeye mwenyewe.

Ni kwa msingi huo, ninadhani kinachotokea kati ya Koero na mama yake ni uhandisi wa haiba ya nafsi ya Koero mwenyewe.

Na bila shaka tayari ameshajitambua yeye kama yeye.

Ninachoshauri ni kwamba katika ujenzi wa falsafa yake, ni vyema akisikiliza ushauri wa wote wanaohusiana naye (kama anavyofanya hapa) hata kama hakubaliani nao, halafu kazi ya kuchambua ibakie kuwa yake mwenyewe.

Kuhusu elimu, pamoja na kwamba naamini kuwa elimu (yenye kuendana na haiba zetu) ni muhimu katika kutupanua uelewa wetu, siamini kwamba kwa kusoma masomo yasiyohusiana na kipaji/personality kunatusaidia. Kupoteza mwaka mzima kutafuta shahada isiyo na uhusiano na malengo ya mwanafunzi ni hasara kuliko kutumia miaka kumi kusomea cheti chenye mahusiano ya moja kwa moja na haiba ya mwanafunzi husika.

Pole Koero kwa yanayotokea. Mambo haya hutokea kwa tulio wengi katika mbio za kujipambanua na wazazi wetu hata kama ni wachache sana huwa wazi kama ufanyavyo wewe kwa hofu ya "...nitaelewekaje nikisema hivi...". Hongera kwa kujiamini.