Saturday, May 22, 2010

TAFAKARI YA LEO: SIJUI NIKUPE NINI PASCOLINA!

Nikauacha mkoba wangu hapa!

Kuna jambo ambalo lilinitokea miezi mitatu iliyopita ambalo ningependa katika tafakari ya leo tutafakari kwa pamoja.

Kusema kweli ni uzoefu ambao ulinifanya nijifunze jambo fulani ambalo sikupata kulifahamu hapo kabla.

Nakumbuka ilikuwa ni siku ya Ijumaa, majira ya asubuhi na mapema. Nilitoka nyumbani kuelekea ofisini. Lakini wakati nakaribia kufika mjini maeneo ya Maktaba nikakumbuka kuwa nilikuwa niwalipe watu fulani fulani ambao wana tenda yaku-supply bidhaa mbalimbali pale ofisini. Kwa kuwa ninakaimu nafasi ya Cashier kwa muda baada ya nafasi hiyo kuwa wazi, nilikuwa na jukumu la kufanya malipo kila ifikapo Ijumaa.

Nilikumbuka kwamba sikuwa na hela ndogo ndogo za kutosha kwani kwa utaratibu wa mambo ya uhasibu kila hela ina thamani hata iwe ndogo kiasi gani.

Nililazimika kusimama pale Akiba na kupaki gari pembeni kisha nilivuka barabara kuwafuata wale vijana waliokuwa wakiuza chenchi pale akiba ili ninunue ili ziweze kunisaidia wakati wa malipo hayo.

Nilitoa kiasi cha shilingi elfu thelathini na kumuomba kijana mmoja muuza chenchi anisaidie chenchi ya shilingi mia mia, aliniambia kuwa atanikata shilingi elfu moja kwa kila elfu kumi hivyo nilitakiwa kukatwa shilingi elfu tatu katika elfu thelathini ambapo ningebaki na kiasi cha shilingi elfu ishirini na saba. niliafiki, lakini kwa kuwa kijana yule hakuwa na chenchi za kutosha alimuita mwenzie ili wachange.

Walinihesabia zile pesa na kunipa ambapo nilizikusanya na kuziweka kwenye mkoba wangu, kisha nikavuka barabara na kuondoka zangu kuwahi ofisini.
Nilifanya kazi hadi jioni na kurejea nyumbani ili kuandaa Sabato. Siku iliyofuata yaani Jumamosi niliamka asubuhi na mapema na kujiandaa kwenda kanisani. Baada ya kujiandaa niliondoka peke yangu na kuwaacha baba na mama wakijiandaa kwa ajili ya misa ya pili, nilitaka niwahi misa ya kwanza kwa kuwa nilikuwa na mizunguko yangu siku hiyo.

Nilifika kanisania na nilikuta ibada imekwishaanza. Ni pale wakati wa kutoa sadaka ndipo niliposhangaa kukuta fedha pungufu ndani ya mkoba wangu, je fedha nyingine zimeenda wapi? Nilijiuiza. Nakumbuka nilikuwa na kiasi cha shilingi laki moja na elfu ishirini ndani ya mkoba wangu ambazo ndizo nilizoondoka nazo nyumbani, lakini wakati napekua ili nitoe sadaka ndipo nikakuta kuna shilingi elfu thelathini.

Nikajua nimeibiwa, kwani nina uhakika kwamba nilikuwa na kiasi cha shilingi laki moja na elfu ishirini, na sasa nakuta shilingi elfu thelathini, je elfu tisini zimeenda wapi? nikaanza kubabaika, maana sikuwa na uhakika wa gari langu kuwa na mafuta ya kutosha, ikabidi nipekue zaidi, na katika hali ya mshangao nikazikuta zile shilingi laki moja na elfu ishirini, zikiwa kwenye pochi ndogo ndani ya mkoba wangu. Je hizi elfu thelathini zimetoka wapi? Lilikuwa ni swali gumu sana kwangu.

Nilikwenda kutoa sadaka na baada ya ibada kwisha nilitoka na kuondoka kurudi nyumbani ili kujianda na mizunguko yangu mingine kwa siku ile.

Lakini nilipokuwa njiani kurudi nyumbani, nilikuwa nimesongwa sana na mawazo juu ya zile fedha ambazo nilikuwa na uhakika kuwa hazikuwa ni zangu, bado nilikuwa najiuliza zimetoka wapi?Huwa nina tabia moja ya kutopenda kutumia kitu ambacho sio mali yangu, hivyo kukuta fedha ambazo sio zangu ndani ya mkoba wangu ambapo nilikuwa na uhakika kabisa wa kiasi cha fedha nilichokuwa nacho ndani ya mkoba kulininyima raha kabisa.

Unaweza kushangaa kuwa kwa nini nikose raha. Ni hivi, mimi nina tabia moja ya ajabu sana, ninapokutana na kitu ambacho sio cha kawaida basi huenda nikashinda kutwa nzima nikijiuliza juu ya jambo hilo, ndivyo nilivyo.

Sina fedha nyingi kiasi cha kusahau pesa ninazotembea nazo ndani ya mkoba wangu, sasa iweje nikute pesa ambazo nina uhakika kuwa sio zangu? Je kuna malaika gani kaniwekea fedha ndani ya mkoba wangu yarabila-ala-mina! Nilizidi kujiuliza.

Nilifika nyumbani na kumuuliza mama kama aliweka fedha ndani ya mkoba wangu, lakini alikanusha kuwa hakuweka.

Nililiacha hilo swala kama lilivyo, na kuendelea na ratiba yangu kama kawaida. Nilirudi nyumbani usiku majira ya saa mbili hivi na baada ya chakula cha usiku, ni pale ambapo tupokuwa tukisoma lesson ndipo nilipokumbuka juu ya zile elfu thelathini nilizozikuta ndani ya mkoba wangu, na kilichofanya nikumbuke ni kutokana na somo la siku hiyo ambalo lilikuwa linahusu uaminifu. Muongozaji wa somo hilo alikuwa ni baba na alianza kwa kutuuliza maswali, akianza na mimi, aliniuliza, ‘Koero, kwa mfano ukienda dukani kununua kitu halafu mwenye duka akakuzidishia chenchi, utafanya nini’

‘nitamrudishia kiasi cha fedha alichonizidishia na kuondoaka zangu’ nilimjibu baba.
Kisha akamgeukia mdogo wangu Jerome na kumuuliza, ‘Joram, hebu nawe nieleze kama ukipanda daladala na kondakta akakuzidishia chenchi utafanya nini’
Kama mimi, Jerome naye alijibu kuwa angemrudishia kondakta yule kiasi cha fedha kilichozidi.

Baba alisherehesha somo lile kwa kutufundisha juu ya umuhimu wa kuwa waaminifu mahali popote na wakati wote na hiyo itautufanya tumpendeze Mungu.

Baada ya kumaliza somo lile ndipo nilipowaleza juu ya wasiwasi wangu kuhusiana na kile kiasi cha shjilingi elfu thelethini nilichokikuta ndani ya mkoba wangu. Mama alishauri tuombe ili mungu anifunulie kuhusiana na zile fedha.

Tuliomba kisha tukaenda kulala. Ilipofika usiku wa manane singizi wote ulipotea ghafla kisha ikanijia ile kumbukumbu ya lile tukio la kukuta fedha ndani ya mkoba wangu ambazo nilikuwa na uhakika kuwa hazikuwa zangu.

Nilianza kuvuta kumbukumbu za tangu ijumaa asubuhi nilipoondoka nyumbani. Nilikumbuka kuwa niliondoka na shilingi elfu sabini kisha nikanunua mafuta ya gari ya shilingi elfu ishirini, ikabaki elfu hamsini, nikaja nikanunua chenchi ya shilingi elfu thelathini ikabaki elfu ishirini ambapo nilikuja kuongeza laki moja asubuhi ya siku hio ya Jumamosi na kuwa na shilingi laki moja na elfu ishirini, je hii elfu thelathini imetoka wapi? Lilikuwa bado ni swali lililoniumiza kichwa.

Hivi kweli niliwalipa wale vijana walionipa chenchi pale Akiba? Nilijiuliza…….nadhani sikuwalipa, niliwaza….Mhmmm…….Sasa nimeanza kukumbuka sikuwalipa wale vijana pesa zao…..Oh…masikini, nimekumbuka sasa, sikuwalipa vijana wale. Niliendelea kuwaza nikiwa pale kitandani. Niliamka na kuchukua note book yangu na kuandika juu ya wale vijana wa akiba na ile elfu thelathini, kisha nikarejea kulala.

Nilishikwa na usingizi na nilishtuka baada ya mama kuniamsha, duh! Kumbe ni saa mbili za asubuni sasa! Nilimsimulia mama juu ya ile kumbukumbu yangu, mama alinisisitiza kuwa Jumatatu nikienda kazini niwapitishie hela zao.

Siku ya Jumatatu niliamka asubuhi na mapema na kujianda kwenda kazini, nilipitia pale Akiba na kupaki gari kisha nikavuka barabara na kuwafuata wale vijana wanaouza chenchi. Lakini kulikuwa na tatizo moja. Sikuwa na kumbukumbu ya sura zao, nilimfuata kijana mmoja anayeuza chenchi na wale vijana wengine waliokuwa karibu walisogea pale kila mtu akijinadi kutaka kuniuzia chenchi.

Niliwatazama usoni lakini sikuweza kukumbuka sura ya wale vijana wawili walioniuzia chenchi siku ile ya ijumaa. Niliwaambia wale vijana waliokuwa wamnizunguka kuwa kuna kijana mmoja aliniuzia chenchi lakini alinipa fedha pungufu, ndiye ninayemtafuta, wale vijana waliposikia hivyo wakaanza kutawanyika kila mtu akienda upande wake kwani walijua kuwa ile itakuwa ni kesi.

Niliendelea kuangaza macho huku na huko nikiwatafuta wale vijana lakini sikuweza kumkumbuka hata mmoja, nilikata tamaa nikaamua kuondoka zangu.

Nilipokuwa najianda kuvuka barabara, nikamuona kijana mmoja akikimbilia daladala moja ili kuuza chenchi na nilipomuangalia kwa makini nikakumbuka ile sura. Ndiye mmoja wa wale vijana wawili walioniuzia chenchi juzi, nilimsbiri auze chenchi kisha nikamfuata na kumsalimia. ‘Vipi mambo kaka’

‘Salama tu sister, je unataka chenchi?’ alinijibu na kuniuliza swali….
Ndi….ndio nataka chenchi, nilimjbu kwa kubabaika kidogo kwani sikuwa na uhakika kama ndiye, kwa asilimia mia moja….

‘Samahani, kaka hivi unanikumbuka’ nilimuuliza
Aaa…hapana….sikukumbuki kwani vipi sister, una shida gani? Alinijibu na kunitupia swali

Juzi ijumaa nilinunua chenchi kwako asubuhi na mapema, hunikumbuki kabisa…nilijitahidi kumkumbusha…..
Ahaaaaa……nimekukumbuka si ni wewe ulikuja na kuchukua chenchi ya shilingi elfu thelathini na kuondoka bila kulipa sio wewe kweli?……alisema

Nilibaki nikitabasamu……………………………

Rashidiiii, Rashidiii,……..yule sister wa juzi kaja na hela yetu……alimuita mwenzie.
Nilimuona mwenzie akija kwa kasi na alipofika pale akaanza kushangilia na kuwaambia wenzie yaani wale wauza chenchi, ‘si niliwambia kuwa yule sister atarudi, mie nilimuona sura yake haikuonesha kuwa ni mtu mkorofi na nilijua tu kuwa ameghafilika’

Nilitoa kile kiasi cha pesa ndani ya mkoba wangu na kuwapa pesa zao na kutokana na furaha waliyokuwa nayo walitaka kunirudishia zile shilingi elfu tatu walizonichaji kama ada ya kunipa chenchi siku ile lakini nilikataa.

Hata hivyo walinipa offer ya kupata chenchi bure kwao kila nikihitaji, niliwakubalia na kuondoka.

Nilijisikia nafuu sana siku ile kwani nilihisi kama vile nimeutua mzigo mzito kichwani mwangu.

Kwa nini nimelikumbuka tukio hilo?

Ni hivi, wiki mbili zilizopita, nilipokuwa nikienda kazini nilipitia kituo cha mafuta pale Victoria kujaza mafuta. Nilitoa mkoba wangu na kuuweka juu ya roof ya gari na kutoa kiasi cha pesa na kumlipa muuza mafuta kisha nikaondoka zangu kuelekea ofisini.

Nilifika ofisini kisha nikapaki gari, lakini nilipoangalia mkoba wangu sikuuona, nilibabaika sana, kwani vioo vyote nilikuwa nimevifunga, Je mkoba wangu umeenda wapi? Nilijiuliza….

Baada ya kufkiri kidogo nikakumbuka kuwa nilitoa mkoba wangu ili kumlipa muuza mafuta pale kituo cha mafuta Victoria. Nitakuwa nimeacha mkoba wangu pale kwenye kituo cha mafuta. Niliwasha gari na kurudi hadi pale kwenye kituo cha mafuta Victoria. Nilimuuliza yule binti muuza mafuta kamaliuona mkoba wangu, akanijuibu kuwa sikuacha mkoba wangu pale.

Nilichanganyikiwa, kwani kulikuwa na makabrasha fulani muhimu ya baba ambayo yalikuwa yafanyiwe kazi kwa siku ile, pamoja na simu yangu ya kiganjani na pesa kidogo kama kiasi cha shilingi elfu ishirini hivi.

Nilirudi ofisini nikiwa nimeishiwa na nguvu kabisa kwani sikujua ningemuleza nini mzee Japheti Mkundi siku hiyo.

Nilifika ofisini na kuingia ofisini kwangu bila kumsemesha baba kwani nilihitaji muda kutafakari. Mara alikuja mmoja wa wafanyakazi wa pale ofisini na kunijuza kuwa baba ananiita ofisini kwake.

Nilinyanyuka nikiwa mnyonge kabisa na kwenda kumuona,. Nilipofika nilimkuta binti mmoja akiwa amekaa na baba ofisini. Nilimsalimia yule binti huku nikiwa nimesimama pale mlangoni nikiwaza,……mawazoni mwangu nilifikiri kuwa labda yule binti amefika pale kwa ajili ya usaili, na baba alitaka kunishirikisha, lakini kutokana na kuwa kwangu katika hali ambayo siyo ya kawaida sikutaka kushiriki katika usaili ule. Pita ukae Koero, nilistuliwa na sauti ya baba akinitaka nikae,…. lakini nilisita….’Samahani baba sijisikii vizuri nahitaji kupumzika kidogo’ nilimwambia baba.

Lakini baba alinitaka nikae kwani kuna jambo anataka kuniuliza, nilikaa lakini nikiwa sina raha kabisa. ‘Koero Mkoba wako uko wapi?’ Baba aliniuliza huku akiwa amenitumbulia macho…….

Nilibabaika sana na sikujua nimjibu nini….nimeupoteza wakati nakuja kazini asubuhi hii… nilimjibu baba huku nikiwa nimetahayari kabisa. Sasa kwa nini hukunieleza? Aliniuliza baba kwa upole kwani aliniona dhahiri nikiwa nimebabaika.

Ni….ni …..nilikuwa bado natafakari, nilimjibu huku nikiwa nimejiinamia.

Alitoa mkoba kutoka kwenye droo yake na kuuweka mezani, je huu sio mkoba wako…..nilishikwa na mshangao…..Heeee….baba umeupata wapi!!!!? Nilimuuliza baba kwa hamaki!!!

Mkoba wako umeokotwa na huyu binti, maeneo ya Victora ukiwa pembezoni mwa barabara karibu na kituo cha mafuta, alipekua na kukuta simu ambapo alimpigia mama yako na ndipo mama alipomuelekeza hapa ofisini na ndo akauleta. Alisema baba…..

Mhh…..Pascolina, huyu ndiye Koero na ndiye mwenye Mkoba nilimrukia yule binti na kumkumbati kwa furaha na kumshukuru sana…..nilitoka naye hadi ofisini kwangu ambapo tulikunywa chai pamoja na kupiga soga kidogo, kisha nikamsindikiza Pascolina hadi nje ya ofisi akaondoka kwa ahadi ya kuwasiliana zaidi ili tupange siku nimkaribishe nyumbani kwa ajili ya chakula cha jioni.

Hakuna siku ambayo nilikuwa na furaha ya ajabu kama siku hiyo, na furaha hii itaendelea kubaki katika kumbukumbu zangu milele. Pascolina ameendelea kuwa rafiki yangu mwema kama walivyo wale vijana wauza chenchi pale akiba na tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara na Mungu akipenda kesho tutajumuika naye nyumbani kwetu kwa ajili ya Dinner na kufahamiana vizuri zaidi.

Nilikuja kugundua kuwa, kumbe baada ya kumlipa muuza mafuta niliacha mkoba wangu juu ya roof ya gari na kuondoka kwa pale kituo cha mafuta ambapo mkoba huo ulianguka mita chache kutoka pale kituoni pembezoni mwa barabara. Lakini kama bahati wakati Pascolina akielekea kazini kwake alipita pale na kuuona mkoba wangu ambapo aliuokota na kuanza kuupekua, na kitu cha kwanza kuona kilikuwa ni simu yangu amabyo ndiyo aliyoitumia kumpigia mama.

Najua kuna wanaume wakware watataka kumjua Pascolina zaidi, jamaniieeee ana mchumba na anatarajia kufunga ndoa hapo mnamo Novemba 2010.

Hii ndio tafakari ya leo.

13 comments:

Anonymous said...

...nilitaka niwahi misa ya kwanza kwa kuwa nilikuwa na mizunguko yangu siku hiyo..."

Siku ya Sabato hupaswi kufanya mizunguko yo yote. Hii ni siku ya kupumzika na kumtukuza Mungu TU!

NINA WASIWASI SANA NA USABATO WAKO!!!

Mfalme Mrope said...

Wengi tunatakiwa tuishi maisha yenye uaminifu wa namna hii na zaidi. Ni changamoto kwetu sote dada Koero. Ahsante kwa somo la uaminifu. Binafsi nitajitahidi kulitumia na kuboresha maisha yangu na ya wale wanizungukao. Sabato njema.

Yasinta Ngonyani said...

Tafakari ya leo ni somo nzuri sana na la kufunza. Imenikumb usha mwaka juzi nilipokuwa Songea nilikuwa dukani nikitaka kununua jiko la mkaa nikalipata nililolitaka nikalipa nilipofika nyumbani nikakuta nimerudishiwa påesa zaidi. Asubuhi yake nilikwenda na kurudisha ile chenchi. Nilipofgika nikajieleza na kumpa muuzaji ile chenchi kwa kweli alishangaa sana na kusema
ilikuwa ni mara ya kwanza watu kurudisha hele. ALISHANGAA SANA!! Ahsante kwa tafakari hii pia kumbukumbu hii na nasema ni kweli UAMINIFU ni kitu kizuri ukiwa mwaminifu basi na wengine watakuamini. UPENDO DAIMA na Koero SABATO NJEMA KWAKO NA PIA FAMILIA NZIMA.

Ramson said...

Annony wa May 22, huna haja ya kutengeneza tafsiri yako.....
Sabato haikatazi mtu kuwa na mizunguko, kwa mfano kutembelea ndugu, marafiki na hata wagonjwa yote yote hiyo yaweza kuwa ni mizunguko.

Swala hapa sio mizunguko yake bali ni kile tulichojifunza kupitia uzoefu wake huu.

Uaminifu ni jambo jema sana. Laiti kama Viongozi wetu wangekuwa ni waaminifu tusingeshuhudia huu ufisadi unapigiwa kelele, na nadhani kuna haja ya kuwafundisha watoto wetu juu ya swala zima la uaminifu.

Tusichokijua ni kwamba pale unapokuwa sio muaminifu, unakuwa ukijitengenezea vikwazo wewe mwenyewe. kwa mfano wa huu uzoefu wa Koero, kama asingerudisha zile pesa alizosahau kuwapa wale wauza chenchi, ni wazi angekuwa amejitengenezea nguvu hasi na kwa tukio la kudondosha ule mkoba wake isingewezekana kuupata. na ingemletea maumivu makubwa sana ya kihisia. lakini kwa kuwa alipanda mbegu chanya na ndio sababu na yeye alifanikiwa kupata mkoba wake katika njia ya kustaajabisha sana.

Kwa uzoefu huu yatupasa wote tujifunze kuwa uaminifu ni jambo la msingi sana katika maisha.

Si tunawaona wale wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanavyofedheheka hivi sasa. usidhani wana raha wale. wanayo maumivu makubwa sana ya kihisia kwa sababu walipanda mbegu hasi na sasa wanavuna majuto.

Kwa uzoefu huu wa da Mdogo Koero mimi nimejifunza, wewe je?

Albert Paul said...

Uaminifu ni jambo jema sana na mara zote humuweka mtu huru sana. Uaminifu kazini, majumbani, katika mapenzi, kwenye uongozi, kwenye nyumba za ibada n.k ni mhimili muhimu sana kwa ufanisi ktk nyanja nilizozitaja na nyingine kadha wa kadha.

Kati ya vitu ambavyo huathiri mtu, basi ni watu kukosa imani na mtu. Hili limewaathiri na linazidi kuwaathiri wengi. Wapo wanaokimbiwa na marafiki, wapenzi, wake, waume, wateja kwa mambo ya biashara, kudharauliwa n.k kwa sababu tu kwa namna moja ama nyingine walishindwa (kwa kujua au kutokua) kuonyesha uaminifu.

Umetupa uzoefu wenye fundisho la maana na lenye msaada sana dada Koero. Hakika sote tungeishi maisha yafananayo na uzoefu uliotupa, Tanzania na dunia kwa ujumla ingekuwa ni sehemu bora na salama sana ya kuishi.

nyahbingi worrior. said...

amani iwe nawe.

mdoti Com-kom said...

Ni kiasi cha hadiyhi lakini kama watu wameanza kuwa hivyo imeanza kufurahisha.

Maisara Wastara said...

mie ni mgeni hapa, nabisha hodi....

Bennet said...

Ni kweli yametokea, MUNGU AKU
BARIKI

Malkiory said...

Koero,pongezi kwa kazi nzuri ya kufundisha na kuikumbusha jamii kuhusu somo la uaminifu.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kabinti kanapenda kujisifia hapa!! mara kanatongozwa, mara kanaenda kanisani siku ya sabato, mara kanarudisha hela iliyozidi, mara sura ake inaonyesha sio kajizi, mara hakapendi ngono (utadhani bila watu kupenda ngono kangezaliwa) mara mara mara!!

sifa jipe mwenyewe sio yesu pekee

Maisara Wastara said...

Nawashukuruni sana kwa kunikaribisha, ni bahati mbaya kuwa blog yenyewe imetengenezwa na mpita njia ambaye ni mteja wetu hapa ofisini kwetu.

Nawaombeni radhi kwani kuna mapungufu mengi sana na ameniahidi kuyashughulikia leo hii jioni.

Kwa kifupi, Bado blog ipo katika matengenezo madogo madogo nawaombeni sana msisite kunifahamisha pale mtakapoona kuna tatizo.

Email yangu ni hii hapa:
wastaramaisara1@gmail.com

Naomba ushirikiano wenu wa dhati kabisa.

Wakatabahu
Ni mimi mdogo wenu na dada yenu

Maisara Wastara

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___