Hayati Mwalimu wakati wa kudai uhuru
Nimesoma kwa masikitiko makubwa maoni ya kaka yangu, Paroko mstaafu Markus Mpangala, kuhusiana uamuzi wa vijana wengi kujiingiza katika siasa kwa wingi na kwa namna ya pekee tofauti na miaka ya nyuma.
Naomba niweke wazi kuwa uamuzi wangu wa kutangaza nia ilikuwa ni kutaka kuamsha ari kwa vijana ili wahamasike kugombea nafasi mbalimbali za uwakilishi hapa nchini. Binafsi naamini kuwa sisi vijana tuko timamu kabisa kuingia katika kinyang’nyiro hicho. Lakini kutokana na watu wenye maono yasiyo na tija kama ndugu yangu Markus, wanaanza kuwakatisha tamaa kwa maelezo kwamba hawajaandaliwa.
Lakini hata hivyo kuna jambo moja najiuliza, hivi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Rais wa kwanza wa nchi hii baada ya kujipatia uhuru kutoka kwa Waingereza aliandaliwa na nani?
Jambo moja muhimu linalopaswa watu kama Markus kulifahamu ni kwamba historia huwa haifutiki. Na ndio maana hata leo tunaweza kujua matukio muhimu yaliyoikumba nchi yetu kabla na baada ya uhuru.
Wakati ule tulipopata uhuru, tulikuwa na wasomi wachache sana ambao wengi wao walikuwa ni makarani wa wakoloni, lakini kutokana na vuguvugu la kutaka uhuru likiongozwa na wazee wa Dar es salaam ambao wengi wao hawakuwa na elimu ya kutosha wakati huo, lakini kwa kumtumia Mwalimu Nyerere walifanikiwa kwa kaisi kikubwa.
Baada ya uhuru wale waliokuwa wakiwatumikia wakoloni wengi wao wakiwa ni makarani ndio wakajikuta wakibebeshwa majukumu katika nafasi muhimu za uongozi ambapo walikuwa hawana hata uzoefu, wa kutosha katika uongozi wa juu serikalini hususana katika nafasi za uwaziri.
Leo hii kuna mabadiliko makubwa, vijana wengi ni wasomi waliobobea katika taaluma mbalimbali, na wana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo kwa namna ya pekee, lakini kutokana na ufinyu wa kufikiri watu wanakaa na kudai kuwa vijana hawajaandaliwa. Je, kina Rashid Kawawa, Tewa Said Tewa, Mzee Opiyo, Mzee Kisumo, Bibi Titi Mohamed, Bi, Lucy Lameck, Bi, Thabidha Siwale na wengineo wengi waliandaliwa na nani?
Ikumbukwe kwamba wakati ule kulikuwa na changamoto nyingi, tofauti na sasa, lakini wenzetu hao walifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Leo hii vijana wanajitokeza kutaka kukushika nafasi za uongozi ili kuleta mapinduzi ya kifikra na kuleta tija hapa nchini, wengine wanaibuka na kusema kuwa hatujaandaliwa…….!
Bado nauliza, Je Hayati Mwalimu Nyerere aliandaliwa na nani?