Wednesday, March 3, 2010

CHOZI LA MWANAMKE! NAOMBA KUTOA HOJA

Bado hamuamini tu?

Hivi karibuni nimeweka makala hapa kibarazani ambayo niliiambatanisha na taswira inayoonyesha wanawake wa vijijini jinsi wananyotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Nimepata changamoto kutoka kwa wadau mbalimbali wakionekana kupingana na kile nilichojaribu kukionesha katika makala hiyo.
Imeonekana kama vile hawakubaliani na kile kinachoonekana machoni kwao.
Naomba leo niweke ufafanuzi hapa wa kile nilichomaanisha katika makala yangu.
Wakati mnamo tarehe 08/03/2010 ni siku ya wanawake Duniani ni vyema tukayazungumzia madhila ya wanawake bila ya unafiki wala kuongeza chumvi.

Kuzaa kwa shida:

Hivi ni nani asiyejua madhila wayapatayo wanawake sio tu wa vijijini hata wa mijini. Ni mara ngapi tunaoneshwa picha za wanawake waliojifungua katika Hospiali za mijini wakiwa wamelala wawili wawili kwenye kitanda na wengine wakiwa wamelazwa chini ya sakafu na vichanga vyao, huku vikipigwa na baridi. Huko vijijini napo kuna mengi yanasimuliwa, kuna idadi ya wanawake tena ya kutosha wanaojifungulia majumbani huku wakikosa huduma muhimu za kiafya, achilia mbali wale wanaojifungulia maporini kutokana na umbali mrefu kutoka nyumbani hadi vilipo vituo vya afya.
Sisimulii hadithi za alinacha hapa au hadithi za kufikirika, bali ninachokizungumza nina uhakika nacho na ninakifahamu kwa kuwa muda wangu mwingi nimekuwa nikiutumia vijijini hususana Arusha na Moshi.

Kulea kwa shida:

Hili la kulea kwa shida nalo halihitaji maelezao marefu, kwa kuwa kila kitu kiko wazi, kuna idadi ya kutosha ya wanawake wengi vijijini na hata mijini ambao aidha wametelekezwa na waume zao au wameolewa na wanaume amboa ni nusu wafu, yaani sio wazalishaji na badala yake huwaachia wanawake ndio wawe wazalishaji huku wakibeba majukumu mengine ya kifamilia, hebu tembelea kule feri au kwenye masoko ya mboga mboga kwa hapa jijini Dar, kuna idadi kubwa ya wanawake amboa huacha vitanda vyao aliajiri kuwahi feri kununua samaki au masokoni kununua mbogamboga na kuzichuuza. Huko vijijini napo naamini wengi mtakubaliana na mimi kuwa kuna mfumo dume ambao umetamalaki na wanawake wengi wa vijijini hawajui haki zao za msingi. Wanawake wengi wa vijijini hubeba majukumu ya kulea familia wenyewe huku wanaume wakijipa majukumu haba ambayo hayalingani na yale wanayoyabeba wake zao. Je hili nalo linahitaji ushahidi?

Kutafuta maji umbali wa kilomita kadhaa tena ya kisima:
kama kuna watu wanaotaabika na shida ya maji, basi ni wanawake na sio wa vijijini tu bali pia wa mijini, ukizungumzia shida ya maji, ni sawa na kuzungumzia madhila wayapatayo wanawake, kwa kule vijinini unaweza kukuta mke na mume wanatoka shamba na wakirudi nyumbani wakati mume anajipumzisha kivulini akipunga upepo, mke hakai chini anachukua ndoo ya maji na kwenda kutafuta maji umbali mrefu tu kwa ajili ya kuogea na kupikia. Kwa huku mijini napo, hata kama wote ni wahangaikaji kwa maan ya kutafuta mkate wa kila siku wa familia, lakini wakirudi nyumbani bado jukumu la kuteka maji linaachiwa mwanamke, niliwahi kukaa kwa mama yangu mdogo kwa muda kule kigogo., kama inavyojulikana kuwa kuna shida kubwa ya maji hasa katika maeneo mengi ya uswahilini katika jiji la Dar, nakumbuka siku hiyo tulikuwa umepanga foleni ili kuteka maji, ilikuwa ni folni ndefu ajabu, lakini cha kushangaza kila akija mwanaume na ndoo anapishwa ateke maji na kuondoka, nilipouliza niliambiwa kuwa wanaume hawapaswi kuweka foleni kwa kuwa wao eti ni watafutaji, kwa hyo wanaruhusiwa kuteka maji ili wakatafutie familia zao mkate wa kila siku. Ia walidai kuwa inawezekana mwanaume akawa anauguliwa na mkewe sasa ni vyema apewe nafasi ya kuteka maji ili awahi kumhudumia mgonjwa. Hizo ni busara za wakaazi wa Kigogo, lakini kwangu hilo halikuwa na mantiki, kwamba wanaume ni watafutaji na ndio sababu ya kupewa fursa ya kuteka maji bila ya kupanga foleni! Na wale wanawake ambo nao ndio watafutaji katika familia zao wanatambuliwa na kupewa nafasi hiyo? Je mnaona jinsi mfume dume ulivyotuingia vichwani?

Kutafuta kuni umbali wa kilomita kadhaa:

Kutafuta kuni umbali mrefu, kama ilivyo katika kutafuta maji hili nalo ni shiranga jingine linalowaadhiri wanawake wa vijijini. Wengi tunafahamu ni kiasi gani wanawake wanataabika katika kutafuta kuni umbali mrefu. Hata watoto wa kike kule vijijini wengi hukwama kuendelea na masomo kutokana na kubebeshwa majukumu mengi ya nyumbani ukilinganisha na watoto wa kiume na hili la kutafuta kuni ni moja ya majukumu ambayo watoto wa kike hubebeshwa tofauti na wale wa kiume.

Kilio cha mwanamke wa Kiafrika ni nani akisikie!?:

Niliposema kilio cha mwanamke, nilikuwa naangalia majukumu aliyobebeshwa mwanamke ukilinganisha na wanaume. Lakini pamoja na kubebeshwa majukumu yote hayo bado mwanamke huyu ameendelea kustahimili na kubeba majukumu hayo kwa unyenekevu mkubwa.
Kuna simulizi nyinge zinazohusu madhila wayapaayo wanawake katika vyombo vyetu vya habari kila uchao mpaka zimezoeleka masikioni mwa wanaume na ndio maana inaonekana kama vile wanawake ni walalamishi.
Naamini kuwa ufafanuzi huu utakidhi kile nilichoandika awali ili kuondoa shaka kwa wale ambao hawakuelewa kwamba nilitaka kufikisha ujumbe gani.

14 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ndio maana mnaitwa MAMA, ni haki yenu na nikazi zenu

Yasinta Ngonyani said...

Kamala Unamaanisha nini usemapo kazi zetu? kwa nini zisiwe kazi za wote Ule umoja umekwenda wapi?

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Da Yasinta! Usemacho chaweza kuwa sawa lakini mpaka mambo fulani yaachwe ambayo ni socially and culturally constructed!

Kwa mfano ati wanawake hawatakiwi kula mayai n.k.

Kuna Mama mmoja Prof ambaye nimekutana naye ambaye amewahi kukaa ughaibuni na mumewe na akanambia kuwa YEYE KAMA ACTIVIST na FEMINIST mambo ya haki za akina mama alikuwa akiyaacha sebuleni ama ofisini kwa kuwa alikuwa (baada ya kupiga kelele juu ya usawa/umoja) akirejea nyumbani alikuwa ni PERFECT african woman!

Sijui kama unaloliongelea lina mashiko kwa kuwa tumeshuhudia wamama wanaopinga ukeketaji wakiwapeleka mabinti zao kwa ngariba usiku :-(

Anonymous said...

Nimekusoma 10/10 Koero.
Nikianza kushiriki malalamiko ya akina mama tangu kijijini Mgongo (Ira) rudi Ubungo-Kibo (Dar) katiza hadi Kwa Semangube (Tanga) usogee kidogo ufike Mrieny (Kilimanjaro) halafu nimalizie na Unga Limited (Arusha) sijui kama nitamaliza ku-transcribe maelezo yao. Naifahamu kazi niliyoifanya, watu niliokutana nao na machungu yao waliyonihadithia hata unipatie kalamu zenye wino wa maji yote ya bahari na karatasi za miti yote ya dunia, sitaweza kuyaelezea machungu ya wanawake katika maeneo hayo niliyoyataja (hapo sikufanya kazi mikoa yote ya Tanzania) na sijajumuisha hadithi za wafanyakazi wenzangu. Wengine huwa tunayabeba moyoni na kuyatafutia ufumbuzi kama yetu wenyewe. Wakati mwingine unafika nyumbani unalia bila kutaka. Unapatwa na hasira bila sababu. Unawaza kwa uchungu masumbufu yao. Kesho yake unapiga kiguu na njia kutafuta suluhisho. Mengine yanasuluhika, mengine tayari ni kama kizalia.
Sitaacha kuwashukuru wale wote wanaofanya kazi binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na yale ya kiserikali ambayo yapo bega kwa bega katika kutatua matatizo na si kufanya mashirika hayo mradi au sehemu ya kujipatia faida.
He who sees the heart sees more than the eye can see.
Mungu awabariki Wanawake wote wanaoteseka. Thx Koero for posting these posts, they touch my feelings to the core. I literally twitch as I write. Working in the health-care industry and seeing these people is something else. Keep posting Koero.

chib said...

Mengine yanarekebishika, suala la kuzaa ni la mama pekee, lakini pale wanapolazwa zaidi ya mmoja kitandani, ni uelekeo mbovu wa uongozi. Lakini hata ukienda wodi za watoto hospitali za watu wote, utakuta hadithi ni ile ile, sasa sijui hapo tena kuna akina mama basi ndio inakuwa hivyo.....
Kuna mtu alisema... suala la ukombozi kwa wanawake, litaanzia kwa wanawake wenyewe.....
Mambo ya kusutana kwa tarumbeta yaishe nk
Je wanawake mko tayari? Au kimebaki ni kilio cha walio wanyonge tu!! Na wale wenye uwezo wamekaa kimya tuuuu

Albert Kissima said...

Kuna kina mama waendao umbali mrefu kuteka maji lakini kwa kutumia magani, wapo pia wanawake waendao umbali mrefu kuchukua kuni na mkaa kwa magari,kwa kuwa tu anaendesha gari au huduma hizi zipo karibu(lkn swala ni lile lile la utekaji wa maji au uletaji wa mkaa) hapa haionekani kama ni unyanyasaji,na hakuna aulizaye waume zao wako wapi.

Wapo wanawake wafuao lundo la nguo za waume zao. Kwa sababu tu umechukuliwa kama utaratibu,basi hata wanawake wenyewe hawaoni kwamba ni unyanyasaji bali ni wajibu wao. Kijana amekuwa akifua nguo zake hadi alipooa lakini baada ya kuoa,swala la kufua linakuwa si wajibu wake tena,kwani tayari yupo mtu mahsusi.Kuna makabila fulani ambayo mwanamke ili amsalimie mwanaume ni lazima apige magoti,au akimkaribisha mwanaume chakula lazima apige magoti,makabila mengine chakula kikitengwa,wanaume wanakula kwanza,wakishiba,kinachobaki ndio wanawake huanza kula. Ajabu kabisa,wanawake wa jamii hizi wanaridhika kabisa na yote haya. Nataka tu kusisitiza pointi ya Ndugu Chacha Wambura kuwa kuna some social and cultural factors lazima zibadilishwe. Kingine ni kuwa tunajaribu kulinganisha mazingira tuliyokulia sisi na mazingira waliokulia watu wengine na kisha tuna conclude kuwa upande ambao unaishi chini ya standard yangu basi unanyanyasika na bila kujua kuwa pamoja na mgawanyo wa majukumu,wanawake wanalazika kukabiliana na hali halisi ya mazingira yao. Kama nilivyotangulia kusema,wakati mwamke wa kijijini anatembea umbali mrefu kuteka maji na kuchanja kuni,mwanamke wa mjini anaendesha gari umbali mrefu kuchukua maji au mkaa au kuni au kwa sababu huduma ya maji ipo karibu basi haoni tabu wala kuhisi ananyanyaswa bali anaona ni wajibu wake.


Ninachoshauri hapa ni kuwa,mbali na kuelezea madhila yawakutayo wanawake ktk mazingira waliyopo,pia fursa nyingi zitumike kutoa elimu juu ya namna rahisi ya kukabiliana na hali halisi za mazingira yao,kutoa elimu kwa jamii juu ya usawa wa kijinsia,uhamasishaji kwa jamii mbalimbali juu ya kuachana na tamaduni na kanuni ambazo zinamlazimisha mwanamke kukubali na kuona mambo fulani (ambayo kimsingi hayakuwa haki yake) kuwa sehemu ya maisha yake na mwisho kuihamasisha jamii na serikali juu ya uboreshaji wa mazingira waishio ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii na zilizo ktk ubora unaotakiwa.

John Mwaipopo said...

Koero asante kwa hii makala. nadhani mimi ni mmoja wa walengwa wa makala hii.

tofauti na chapisho lililopita, hili linaongelea zaidi sera na sio kuonewa ama mfumo dume kama ambavyo matatizo ya wanawake yamekuwa yakitafutiwa mchawi.

tunaposema matatizo ya wanawake tusisahau kuna matatizo ya wanaume hata kama hawayasemi. post iliyopita ilikuwa inamfanya mwanaume aonekane chanzo cha matatizo ya wanawake, kitu ambacho nilitoa angalizo kuwa umetuonyesha wanawake wakitaabika lakini hukuonyesha wanaume zao wako wapi na wanafanya nini. kujifungua ni wajibu wao na nilisema tutamuuliza mungu kwa nini wajifungue wanawake tu. nikauliza hao waume zao wako wapi ili tubaini unyanyasaji huu. sijapata jibu bado.

matatizo ya wanawake mara nyingi yanahusishwa na wanaume. ni kama vile matatizo ya afrika yanapohusishwa na ukoloni kila uchao pasi na kujiangalia kwanza sisi wenyewe. matatizo aliyokuwa nayo mama yangu katu hayakusababishwa na baba yangu.

kwa mfano unaongelea wakinamama kurundikana mawaodini wakati na baada ya kujifungua. sidhani kama hili linasababishwa na wanaume wao. wanaume wao wanakuwa wamehusika na kuwapa mimba tu. hili ni la kisera na kiuongozi kama alivyosema chib. katika hili wote wanawake na wanaume wanahusika. sio wanaume peke yao. tanzania tuna uchaguzi wa kuiweka serikari madarakani kila baada ya miaka mitano. wanaojitokeza kupiga kura wengi ni wanawake. sasa kwa nini wasichague serikari ambayo itajenga mahospitali ambayo hawatalala wawili-waili. watawachagua walewale ambao hawanunui vitanda na hawajengi hospotali.

suala la maji nalo ni kama hilo hapo juu. ni la uongozi ambao sote, wanawake na wanaume, tunauweka madarakani.

Umeongelea kulea kwa shida kuwa wanawake wanahangaika mfano feri kuchuuza samaki kwa ajili ya malezi ya watoto wao. kwanza sidhani kuwa suala la kuzaa ni bahati mbaya. ni makubaliano ya mwanamke na mwanaume kuzaa isipokuwa kama mama alibakwa. Pili kibaolojia tu mtoto akiwa mdogo atakuwa karibu na mama yake ili ahudumiwe ipasavyo. hii haimaanishi baba zao hawajishughulishi na malezi ya watoto. unapotoa mfano wa wakinamama pekee kurundikana feri kuchuuza samaki, pia usisahau ni akina baba wangapi wanasukuma mikokoteni (ukilinganisha na wanawake),wanapiga debe na kadhalika ili kupata kipato cha kusaidia kulea watoto wao. kati ya wafungwa wa wakina mama na akinababa wapi ni wengi ambao walidiriki kujihusisha na uhalifu ili kusaidia familia zao. jibu unalo.

bado hujabainisha unaongelea jamii ipi. kwenye post iliyopita nilikuuliza vipi jamii za kipemba na baadhi kule tanga na hata dar es salaam ambako mwanamke ni marufuku hata kwenda sokoni kununua dagaa kwa pesa alizotafuta mumewe. kaziye ni kupaka hina mwili mzima. haruhusiwi kujishughulisha kwa lolote.

ili tuimbe wimbo mmoja naomba mnisaidie haya mambo.sidhani kuwa matatizo ya wanawake yanaletwa na wanaume. huwa najiuliza hivi kwa nini wanawake wengi ma-activists huwa ama wameachika kwa wame zao ama ndoa zao ziko alijojo. hili sijapata jibu kokote kule.

Anonymous said...

Naona unataka watu wote wakubaliane na wewe kwa kila unachosema. This is not your first time to complain. Ukipingwa au kuhojiwa kiduch tu "Oh, you people hamnielewi"....

You are missing the big picture. One goal ya kuanzisha blogu ni pamoja na kuwa ready to be criticized, querried etc. Not everytime watu wakikuquestion unaanza kulalamika. Anakuwa questioned professor Mbele sembuse wewe!

Your argument here is flawed because you are trying to look at women problems in ISOLATION. May be you need to look at comparative data across Africa; then you will be able to make informed claims. Women problems are deep rooted and will not be dealt with properly by superficial attraction of sympathy.
Next time you see women going to fetch water, ask yourself and then ask them why?

Bear this in mind!

Msomaji Wako said...

Nimependa sana waliochangia wote hasa waliokusahihisha, hasa Albert na John. Hakika hao ni wachambuzi makini, na nimefurahia ya kwamba hata hawachoki kukukosoa kila mara.
Una nia nzuri ya kuwatetea wanawake wenzako lakini kwa njia mbovu, maana wewe unaenendeshwa na hisia na hasira kali badala ya kutumia busara na hekima. Hujiulizi chanzo na hulka za watu, unaiga malezi ambayo si ya kiafrika na wakati huo unawatetea waafrika. Ni sawa na wale wanaotetea ushoga uwepo Afrika bila kuzingatia maadili ya kiafrika.
Hoja zako ni za chuki kwa wanaume, unawaona kama mashetani, kama ukiondoa dhana hiyo utagundua wewe una hisia tu, na kulazimisha wasomaji wako waamini kwamba wanawake wanafanyiwa ukatili na wanaume na ndio maana umezungumzia kuzaa kwa shida, sasa ulitaka wanaume na wao wazae!!! Huu usawa ukitumiwa vibaya ndio utaona watu wanalazimisha kuoana wakiwa wa jinsia moja. Hoja yako ni kupandikiza chuki na wala sio kutetea wanawake.
Kuna baadhi ya wanawake ni makatili kuliko hata wanaume, zingatia yule mama wa Mbagala aliyekuwa anamtesa mtoto wa kike wa kambo mpaka kumsokomeza vitu kwenye njia ya kizazi, je huyo mama ni mwanaume!Mbona hujamzungumzia!!
Wanaharakati wa kike ambao wanakuja kwa hasira sana kama zako huishia kuachana na wanaume wao. Utawakuta wote wenye midomo fyongo hawana wanaume, maana wako kwenye kilele cha chuki na hawaambiliki.
Nakuhakikishia wanawake wengi wakimwona mwenzao anamwachia mume wake kufagia nyumba, kumtawaza mtoto, kupika, kupepeta mahindi, kudeki, kubeba kuni,nk watashamshangaa mwanamke mwenzao huyo hata kama huyo mwanamke atakuwa anapasua mawe, kupiga debe, kubeba watu kuvuka mto wakati wa mafuriko, kuzibua au kuchimba choo na makaburi nk
Unapaswa kuelewa kuna tofauti ya mwanamke na mwanaume, usilazimishe usawa wakati hata kimaumbile kuna tofauti.
Rudi kwenye biblia usome, maana hata Mungu alisema mwanadamu atazaa kwa uchungu, kama unapingana na Mungu, nakutakia kila la heri, na nitashauri uende pale Muhimbili kitengo cha magonjwa ya akili. Kama una sikio la kufa, basi hapa tunampigia mbuzi zumari.
Mwisho ukiona kila mtu hakuelewi, basi ujiulize kwa nini, maana wewe ndio unaweza kuwa tatizo, nyani haoni..........

Anonymous said...

Naona watu wanazungumza kwa hisia kali sana, karibu wamevuka mipaka karibu ya kumkashifu hata na Koero!
Ni kweli Koero unaandika makala na kuhitimisha bila hisia ya kisayansi. Unatakiwa ufanye utafiti uwaulize hao wakina mama kama kweli wanaona wanafanya kazi wasizostahili. Usikurupuke na kumwaga hasira kwenye blogu yako.
Mie nina mke mfanyakazi na kipato chake ni zaidi ya cha kwangu, na kila mtu nyumbani anafurahia majukumu yake hata kama mimi nimechelewa kurudi nyumbani, natekeleza yale yanayonihusu.
Huo usawa unaoupigania ni wanaume kuchukua majukumu ya kina mama, lakini mbona haupiganii wakina mama kwenda kugonga kokoto, kuchimba madini kama akina wana apolo, kwenda kuvua samaki usiku wa manane na wanaume wawahi feri asubuhi kuja kununua samaki. Mbona pale kunapotokea vita ni wanaume wengi ndio wanaenda huko kuuwawa na wanawake wanabaki kutunza familia. Huoni ni mgawanyo wa kazi, au hujui?!.
Kwa ujumla kazi za wanaume ni hatarishi kuliko za wanawake, lakini wanaume wameumbwa na mioyo migumu na kijasiri, badala ya kulalamika tu.
Mija alisema wanawake mnapenda sana upendeleo, ni kweli kabisa, na hiyo inawadhalilisha, inabidi mjitutumue lakini sio kwa kuchukulia mambo kijuujuu na hasira ya mfumo dume.
Mara ngapi kwenye misururu akiwepo mwanamke pekee wanaume wanampa fursa ahudumiwe kwanza, ni sawa na bomba la maji hapo Kigogo.
Mnasahau ya kwamba wanawake ndio wana maamuzi yote nyumbani ya kitu gani kitapikwa nyumbani, nini anunue nk. Ukiwapa wanaume utalia
Wanaume tupo tayari kwa usawa lakini iwe pote, piganieni na nyie kuwa matopazi, ingieni vitani, bebeni mizigo hapo kariakoo, geuzeni wanaume wazae na kunyonyesha. Ukipata mtoto wa kiume anayetaka kuolewa na kidume mwingine mpe haki yake nk.
Pole Koero, acha jazba, andika kama mwanaharakati na wala sio kama mbeijing!
Wanaume watakuwa tayari kubadilika wakiletewa hoja zenye maana na sio za kufikirika

Upepo Mwanana said...

Hii mada imenichanganya kidogo hasa baada ya kusoma hisia za watu!
Mimi namshukuru Mungu kwa kunipa baba aliyenipa muongozo wa kuishi na watu wote, nawashukuru na kaka zangu kwa kunipa heshima kubwa kama mtoto wa kike. Imenipa fursa ya kufanya kazi na wanaume huku nikiwa naheshimika kama ninavyowaheshimu na wao, na nimekuwa planner wakati wao wamekuwa watekelezaji bila kupunguza heshima.
Kwa mtazamo wangu siulaumu kwa hisia kali mfumo dume, nahisi tatizo lipo kwetu wanawake pale tunaposhindwa kujitambua ya kuwa tunatakiwa kuwa ngangari kwenye kila kitu tukija na nguvu ya hoja na sio hoja ya nguvu.
Matatizo mengi ya akina mama yanahusiana na mfumo mbaya wa kiungozi au kisiasa, kukosekana kwa hospitali za kujifungua sio sababu ya mfumo dume, kwani wanaokufa ni wengi wakiwemo watoto na wanaume pia.
Sababu za akina mama kuzaa majumbani ni tatizo la akina mama wenyewe, kwani kuna ushahidi kuna sehemu wakunga wa jadi huwalazimisha mabinti wawapo hospitali kuondoka wakati wa kujifungua ukikaribia, pia wauguzi wakunga wengine (tena wanawake), wana matusi mabaya sana wakati wa uchungu, pia kukosekana wa zana za kujifungua watu hunyang'anywa walizokuja nazo kuwasaidia wasio nazo, hivyo akina mama wajawazito huchelewa makusudi ili zana zao zisichukuliwe, na pia kuepuka kulala wengi kitanda kimoja. Mfumo dume hauna chochote hapa.
Hulka ya waafrika pia ni chanzo cha baadhi ya MATATIZO YA AKINA MAMA.
Kwa mtazamo wangu nafikiri hatuwezi kuubadili kwa ghafla mfumo huu, tunahitaji kuwaelimisha akina mama wenzetu kwanza na ndipo hapo shughuli ya kuweka huo usawa wa kweli utakuja, lakini siamini ya kuwa total reversal is fair, yaani leo baba aanze kulea mtoto nyumbani, afue nk, je akina mama usawa utakuwa wapi, kwenda kufanya kazi ngumu? La hasha, tunapaswa kuheshimiana na kupendana, we need badly each other. Hakuna mambo ya visasi au kukomoana. Mimi naona wanawake tuache kufikiria kupendelewa au kuonewa huruma kwanza, tuingie kwenye ushindani wa kikweli na wanaume kama tunataka usawa. Angalau huo ndio mtazamo wangu binafsi

Mija Shija Sayi said...

Kusema ukweli mada hii imenifanya nizidi kujielewa zaidi mimi kama mwanamke. Upepo Mwanana nimekukubali.

*Wanaume nao kumbe wakali wakichokozwa.

Koero asante kwa mada.

MARKUS MPANGALA said...

Mmmmhhhhhhh

MARKUS MPANGALA said...

CHAGUA MOJA! kusuka au kunyoa,
KUNYAMAZA AU KUSEMA.... ni bora tukinyamaza tunaonyesha hekima, na kwa maoni nimechagua KUNYAMAZA hoja nzito zimechanganywa na hisia k.............

SWALI TATIZO HAPA NI WANAUME,MFUMO DUME AU NINI? Maana mimi ni kati wanaopingana na hili dude linalopachikwa jina la MFUMO DUME... lakini naomba kunyamaza kwani kwangu MFUMO DUME SIUONI ILA SAIKOLOJIA ZETU ZINAKASORO ZIMEVILIA.

Jamani maoni yenu... mmhh NGOJA NINYAMAZE