Wednesday, March 31, 2010

UKIONA KINYESI KWENYE KOFIA YA MTU USIHANGAIKE KUULIZA.

Hapa ni kazi tu, katu sirudi nyuma

Kwa kauli zetu tu, au matendo yetu yanaweza kubainisha kuwa sisi ni watu wa namna gani. Lakini pia tunaweza kujiuliza, SISI NI NANI? Endapo sisi ni elimu,mavazi,sura,uzuri,uwezo wa kifedha au maisha bora n.k, bado swali linabaki sisi ni nani?

Hata kama tunaelewa sisi ni nani, lakini tunatakiwa kujiuliza, ukiwa msomi wewe ni nani na usipokuwa msomi wewe ni nani? Vivyo hivyo tujiulize tunapokuwa na maisha mazuri au pesa nyingi sisi ni nani na tusipokuwa navyo sisi ni nani?

Lakini kwa mtazamo wangu, swali la SISI NI NANI, jawabu lake ni kwamba SISI NI MAWAZO YETU. Mawazo haya yana mantiki yake katika kujiridhisha kuelewa masuala mbalimbali. Mawazo yetu ndiyo msingi wa kuchanganua hoja mbalimbali.

Lakini tunapaswa kuelewa kwamba kila binadamu anao ubongo wake na unamwezesha kufikiri. Kufikiri tu hakutoshi endapo tunakosa kuelewa uhuru wa kufikiri, hivyo basi hata mwendawazimu anaweza kufikiri na anao uhuru wa kufikiri. Nitoe mfano huu!

Nakumbuka wakati fulani, nilipokuwa kidato cha sita mwalimu wetu mmoja aliwahi kutuambia kuwa ukiona kinyesi kwenye kofia ya mtu, basi usihangaike kuuliza kujua hali ya nguo yake ya ndani ilivyo.

Yalikuwa ni maneno ambayo yalinishangaza kidogo kwa kuwa, nilikuwa na uelewa mdogo, sikuweza kung’amua alikuwa anamaanisha nini.

Lakini hata hivyo alitufafanulia maana ya maneno yake yale kwa sababu karibu darasa zima hatukumuelewa.

Kuna binti mmoja mwanafunzi mwenzetu, alianza kuwa na vituko sana darasani, na wengi wetu tulikuwa tukimshangaa, kutokana na mabadiliko yake ya kitabia ambapo alifikia kuwa kero kwa kila mtu.

Siku hiyo mwalimu wetu huyo alikuwa akitufundisha somo la biashara, lakini mwenzetu katika hali ya kushangaza alianza vituko pale darasani na kuwa kero mpaka mwalimu akamtoa nje ya darasa.

Alikuwa ni binti ambaye alikuwa akiyamudu vyema masomo, lakini hata hakuna aliyejua masaibu yaliyomkuta mwenzetu hata akaanza kuwa na vituko.

Alipotoka darasani ndipo mwalimu yule alipotoa kauli ile. Hata hivyo, mwalimu yule alituambia kuwa haihitaji mtu kutumia akili za mwanasayansi aliyegundua ‘missile’ ili kujua kuwa mwenzetu yule anatumia Bangi, alituomba tumshauri mwenzetu aache kuvuta Bangi.

Ni kweli baadaye tuligundua kuwa yule mwenzetu alikuwa amejiingiza kwenye makundi ya wavuta bangi huko mtaani na pale shuleni. Kwa kuwa alikuwa hakai bwenini ilikuwa ni rahisi kwake kupitia vijiweni ambapo ndipo alipokuwa akivuta bangi na wenzie walioshindikana makwao.

Hata hivyo uwezo wake darasani haukushuka na aliendelea kuyamudu vyema masomo yake. Kuna wakati niliwahi kuzungumza naye juu ya mabadiliko yake kitabia, alikiri kutumia Bangi na sababu ya yeye kujiingiza katika tabia ile ni kutokana na baba yake kuoa mke mwingine na kumtelekeza mama yake na kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa baba yao, mama yake aliamua kujitoa roho na kumuacha yeye na mdogo wake wa kiume mikononi mwa mama wa kambo.

Mama huyo alikuwa akiwatesa sana kiasi cha kusababisha mdogo wake kutoroka hapo nyumbani akiwa kidato cha pili na kuishia mitaani, yeye aliamua kubaki pale pale nyumbani na kuvumilia mateso ya mama yule wa kambo ili amalize masomo yake na kama akifaulu aendelee elimu ya juu.

Na ili amudu kuvumilia mateso hayo ndipo alipoamua kuvuta Bangi ili kuondoa msongo wa mawazo. Hiyo ni baada ya kushauriwa na rafiki yake wa karibu.

Niliongea naye mambo mengi sana na nilijitahidi kumshauri aachane na tabia ile ya kuvuta bangi lakini nasikitika kuwa hakubadilika, kwani alidai kuwa bila bangi hawezi kuishi na mama yake wa kambo.

Bila shaka, unaweza kushangaa kuwa binti yule alifaulu na kuendelea na masomo yake ya elimu ya juu….! Sasa fikiri!

Tunazaliwa na kukulia katika mazingira tofauti, na walezi wetu na jamii iliyotuzunguka ndio wanaokuwa mainjinia wazuri wa tabia tulizo nazo leo hii, haiyumkini kuwa tabia tulizo nazo zinatokana na kile tulichojifunza utotoni kutoka kwa watu tuliokuwa nao karibu sana.

Wakati mwingine unaweza kushangazwa na tabia za mtu au matendo yake, hasa pale inapotokea mtu huyo kufanya jambo ambalo hukulitarajia. Ni vigumu sana kuamini kile kilichotendwa na mtu huyo kutokana na jinsi ulivyokuwa ukimuona.

Na baadhi ya wanazuoni wanasema watu wanaofanya matendo ya kushangaza kama hayo wakati mwingine huongozwa na ‘ubongo wa mjusi’. Huu ni ubongo unaoratibu matendo yanayostajabisha hususan tabia za kushangaza zaidi.

Hivyo ubongo wa mjusi huu unawasukuma baadhi ya watu kutenda matendo ambayo kwa kawaida hayawezi kutendwa. Ubongo huu upo kati yetu haijalishi ni msomi au siyo msomi. Matendo mengi yenye kila dalili za ubongo wa mjusi yametamalaki katika jamii yetu.

Zamani kidogo mtu msomi ndio alitumika kama kipimo cha mtu mwenye busara, mtu msomi licha ya kuheshimika katika jamii lakini pia alitumika kama mshauri katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kitaaalamu au hata ya kijamii, pale itakapohitajika ushauri katika kupata suluhu iwapo kutatokea kusigishana katika jamii.

Lakini siku hizi usomi pekee, hauwezi kupambanua kiwango cha busara na hekima alizo nazo mtu, na hii inatokana na jinsi wasomi wetu walivyofinyangwa kuanzia katika malezi mpaka huko mashuleni.

Hebu tuangalie mfano wa binti huyo niliyemzungumzia hapo juu. Je iwapo atamaliza elimu yake ya juu, tutarajie kuwa atakuwa ni mtu wa namna gani katika jamii? Siyo kwasababu ya bangi tu, bali jamii yetu ndiyo inayotutengeneza, kwahiyo hata kuwa na ubongo wa mjusi kunatengenezwa pia.

Tumekuwa tukishuhudia migogoro isiyokwisha katika vyuo vyetu vya elimu ya juu na licha ya hiyo migogoro, pia tumekuwa tukisoma kutoka katika vyombo vya habari juu ya tabia na mienendo ya wasomi wetu hawa ambao tunatarajia kesho ndio wawe viongozi wetu au wataalamu wetu katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

Natambua migogoro mingi inatokana na suala la sera, lakini katikati ya sera hizo kuna wasomi ambao hutumia bongo zao kuzitunga. Lakini sera hizohizo zinatesa wengine, sitakosea kuwaita watunzi wake wana ubongo wa mjusi, ni inapotokea kwamba hatutaki kutofautiana kimtazamo, basi tunakosa kuheshimu uhuru wa kufikiri.

Nimekuwa nikisoma mijadala mbalimbali katika mitandao yetu hii, kuanzia Blogu mbalimbali, Jamii Forum na ule wa wanabidii, inashangaza kidogo pale inapotokea mada ambayo inahitaji watu watafakari na kuleta changamoto zao, lakini utashangazwa na baadhi ya wasomaji watakaochangia mada husika.

Maana kama sio kupotosha mada kwa makusudi kabisa, basi watamshambulia mtoa mada kwa matusi na kejeli ili kumshushia hadhi. Huu ni uhaini wa uhuru wa kufikiri. Haigombi kushambualia, lakini endapo kujadili mada husika kunatazamwa kwanza nani aliyetoa, inapoteza maana husika.

Wakati fulani ilitokea Mbunge wa Kigoma Mheshimiwa Zito Kabwe alitangaza kujitoa katika mtandao wa Wanabidii kutokana na tatizo hilo, kwa kuwa watu wanaacha kujadili mada husika na kukimbilia kumjadili mtoa mada kwa kumshambulia kwa kila aina ya kashfa.

Sawa, ni uhuru wa kufikiri, lakini endapo tungeweza kumshambulia mtoa mada kwa hoja ingeeleweka zaidi. Lakini kushambulia kwa kashfa na matusi ni ubongo wa mjusi, hii inatoa taswira kwamba hatujui sisi ni nani.

Lakini katika mitandao yetu tunajadili kitu gani na kwanini?.
Tatizo la kumjadili mtoa mada lilimkimbiza Mheshimiwa Zito katika mtandao wa Jamii Forum, na sasa yuko katika hati hati za kujitoa katika mtandao wa Wanabidii.

Inashangaza kuona kwamba, wasomi wetu tunaotarajia walete chachu ya mabadiliko ya kisiasa,kiuchumi na kijamii hapa nchini ndio hao ambao wameshindwa kujiheshimu. Kwao wao matusi, kashfa na kejeli ndio aina ya maoni waliyo nayo katika kuchangia mada.

Sikatai watu kutofautiana kimtizamo katika masuala mbalimbali, lakini hivi hakuna lugha nzuri inayoweza kutumia katika kufikisha ujumbe kwa njia ya busara zaidi isipokuwa kutumia matusi na kejeli? Kuna watu ambao kwa makusudi kabisa wanaficha utambulisho wao na kuwakashifu watoa mada kiasi cha kuwashushia heshima. Hawa naweza kusema wanatumia ubongo wa mjusi.

Mwalimu wetu aliposema kuwa,ukiona kinyesi kwenye kofia ya mtu, basi usihangaike kuuliza kutaka kujua hali ya nguo yake ya ndani ilivyo, hakuwa na maana nyingine isipokuwa kutanabaisha kuwa unaweza kujua kiwango cha ufahamu wa mtu kutokana na matamshi au matendo yake.

Kwamba elimu pekee haitoshi kupambanua kiwango cha hekima na busara alizo nazo mtu. Na kama elimu ndiyo kipimo cha busara, ni dhahiri leo kusingekuwepo ufisadi,ubadhirifu ambayo hufanywa na wasomi wanaotegemewa.

Nami kupitia blog hii, nimeshawatambua watu wa aina hiyo, na ninawakaribisha sana kutoa changamoto zao hapa kwa lugha yoyote waitakayo iwe ni ya matusi, kejeli au hata kukashifu, kwani hiyo haitanifanya nirudi nyuma katika kuelimisha jamii.

Nawakaribisha mstari kwa mstari, neno kwa neno bila kujali matumizi ya tamathali za semi. Kwasababu hiyo ninaomba niyanukuu maneno haya ‘Know your enemy, know yourself and you can fight a hundred battles without disaster’ (SUN TZU).

6 comments:

Yasinta Ngonyani said...

nimenukuu "Kwamba elimu pekee haitoshi kupambanua kiwango cha hekima na busara alizo nazo mtu. Na kama elimu ndiyo kipimo cha busara, ni dhahiri leo kusingekuwepo ufisadi,ubadhirifu ambayo hufanywa na wasomi wanaotegemewa." mwisho wa kunukuu.

Nakushukuru sana Koero kwa mada hii. Ni kweli watu tumetofautiana na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa hili. Fikiria kama wote tungekuwa aina moja, yaani tungekuwa na huo ubongo wa mjusi.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kama unapinga elimu mbona sasa makala yako inatuelimisha, tusiisome nini???

(MMN) said...
This comment has been removed by the author.
Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Dhana ya "usomi" inatatanisha sana. Ndiyo maana hata mimi niliwahi kuuliza hapa:

http://matondo.blogspot.com/2010/02/fikra-ya-ijumaa-ati-msomi-ni-nani.html

Kuhusu lugha ya kutukanana na matusi nadhani hili umelieleza vizuri. Hii ndiyo sababu mojawapo Ze Utamu iliinukia kuwa tovuti maarufu sana. Huko watu waliweza kutua mizigo yao ya hasira, wivu, utoto, ulimbukeni, ugumu wa maisha na mengineyo: http://matondo.blogspot.com/2009/06/ati-ze-utamu-imetufundisha-nini.html

Kama ambavyo nimeshawahi kusema mara nyingi kuhusu maluweluwe ya u-Homo Sapiens wa binadamu, binadamu ni mnyama na japo anavaa nguo na kuuficha unyama wake kwa nje, tabia zake nyingi na mambo anayotenda mara nyingi yanathibitisha unyama wake. Kwa hivyo hili la kutukanwa si neno na kusema kweli linategemewa. Tena mara nyingi hao watukanaji ni watu wa karibu na mnaofahamiana vizuri. Wao pia ni wanyama na ni lazima watimize matakwa yao ya kinyama.

Kwa hivyo jambo hili lisikuumize kichwa. Ni jambo la kawaida, na kama umeamua kublogu basi haliepukiki! Ni mwanablogu gani ambaye hajatukanwa au angalau kurushiwa madongo na hawa ma-anony?

Ma-anony hawa wana mchango wao wa maana na mtu unapotukanwa au kupigwa madongo basi tuchukulie kama kichocheo na kusonga mbele tena kwa "ARI Mpya, NGUVU mpya na KASI mpya!"

Napenda jinsi ulivyothubutu kuwakaribisha "mstari kwa mstari, neno kwa neno bila kujali matumizi ya tamathali za semi" Ngoja tuone watasemaje! Happy Fools Day!

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Sina neno saidi kwa kuwa waungwana washasema.

Si kila wenye vidato wameelimika la sivo nji hii ingekuwa na maendeleo kama singapore.

Wakilisha dada, tuko pamoja!

MARKUS MPANGALA said...

NANUKUU....."Tena mara nyingi hao watukanaji ni watu wa karibu na mnaofahamiana vizuri. Wao pia ni wanyama na ni lazima watimize matakwa yao ya kinyama"(MWISHO WA KUNUKUU).

Kaka Nzuzullima umeeleza kitu kinachonihuzunisha hadi leo hii.....Naweka wazi kuwa kitu hiki ninanifanya nikose raha kwasbabu tu nilidhaniwa kufanya kitu ambacho sijawahi kufanya na sikuja kukifanya kwalo.

NIMEAMUA KUSEMA HILI INGAWA SIKULISEMA MWANZO.

katika Mda ya dada Yasinta ya kuongelea WAAFRIKA/WATANZANIA KUOLEWA NA WAZUNGU kuna maoni ya Anony aliandika kwamba "WENGINE MNAOLEWA NA WAZUNGU ILI KUONDOA UMASIKINI NA KUWASAIDIA WAZAZI WENU"(MWISHO WA KUNUKUU).

Kwakuwa kaka Nzuzullima amezungumzia ni watu wanaofahamiana, NAMWAGA MCHELE rafiki yangu kipenzi dada Yasinta(sijui ilikuwa utani au la) baada ya kumweleza kuwa maoni yale kwangu yalinikera lakini sikuweza kuzuia anonny kama unavyosema kaka kwamba wanamchango wao, BASI MAONI YALE YANILETEA SHIDA NA JAKAMOYO HADI LEO kwani rafaiki yangu alisema waziwazi kuwa maoni yale niliandika mimi.

Wakati mwingine najiuliza neno "NILIDHANI' linapunguza tu ukali wa suala husika, kwamba mtu anaamua tu kupunguza kusema moja kwa moja, kwahiyo hilo limenigusa na linanisononesha sana. Kweli namfahamu Yasinta lakini hawa watu mnaofahamiana inakuwaje kutoa lugha mbovu kiasi hicho?

Ni kama hapa Koero anavyosema kuwa yupo tayari kukabiliana nao. Namini alichelewa kuwatambua watu hawa. Lakini ndiyo kuna umuhimu wao kwahiyo wanabomoa mlango hawavunji nyumba.
Kwa dada yangu na rafiki yangu KWELI ILINILETEA SHIDA ingawaje ni suala dogo lakini .............. basi nisiseme sana ONLY GOD CAN JUDGE IT