Saturday, May 29, 2010

TAFAKARI YA LEO: JE, MUNGU AKIKWAMBIA OMBA UTAKALO NIKUPE, UTAOMBA NINI?

'Mfalme Suleman akaagiza mtoto yule akatwe kichwa'

Tafakari ya leo ningependa tusome katika 1 WAFALME 3:5-13. kisha tutafakari kwa pamoja.

“Na huko Gibeoni BWANA akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku Mungu akamwambia omba utakalo nikupe Sulemani akasema umemfanya mtumwa wako Daudi baba yangu fadhila kuu kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli na haki na katika unyofu wa moyo pamoja nawe, nawe umemwekea fadhila hii kubwa maana umempa mwana wa kuketi kitini mwake kama ilivyo leo na sasa.

Ee BWANA Mungu wangu umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu nami ni mtoto mdogo tu, sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia na mtumwa wako yu kati ya watu wako uliowachagua watu wengi wasioweza kuhesabiwa bila kufahamiwa idadi yao kwa kuwa ni wengi kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako na kupambanua na mabaya maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi.

Neno hili likawa jema machoni pa Bwana ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia kwa kuwa umeomba neno hili wala hukujitakia maisha ya siku nyingi wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako wala hukutaka roho za adui zako bali umejitakia akili za kujua kuhukumu basi tazama kama ulivyosema.

Tazama nimekupa moyo wa hekima na wa akili hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale yote usioyaomba yote nimekupa mali na fahari hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe siku zao zote.

Nawe ukienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu, kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi nitazifanya siku zako kuwa nyingi. Naye Sulemani akaamka, na kumbe! Ni ndoto. Akaenda Yerusalem, akasimama mbele ya sanduku la agano la BWANA, akatoa sadaka za kuteketezwa, akatoa sadaka za amani; akawafanyia karamu watumishi wake wote.”

Na katika hiyo hiyo Wafalme hebu tusome katika
1 WAFALME 3:16-28.

“Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake. Na mwanamke mmoja akasema, Ee, Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani.
Kisha siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu.
Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia. Akaondoka kati ya usiku akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu. Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe! amekufa.
Hata asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa. Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.

Ndipo Mfalme Suleman akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo, bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu. Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu.
Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme, kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee Bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai , wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, asiwe wangu wala wako; na akatwe. Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake.

Na Israel wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme; wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.”
Labda wewe unayesoma hapa, nikuachie swali hili utafakari, ‘Je, mungu akikwambia omba utakalo nikupe, utaomba nini?


Tafakari hii itaendelea Jumamosi ijayo……….

Thursday, May 27, 2010

NAELEKEA UZEENI SASA!

Naelekea uzeeni sasa!

Msione kimya jamani ni majukumu yamenizidi tu.

Kwani nashindwa nijigawe vipi.

Kuna wakati mtu unashindwa kujua, ni kitu gani nikipe umuhimu, kati ya mambo mawili ninayoyapenda sana.

Napenda sana kublog na naomba nikiri kuwa kublog ni kitu ambacho kimenibadili sana kifikra tofauti na nilivyokuwa awali.

Lakini pia ninayo majukumu ya kiofisi na ya kifamilia kama mwanamke.

Ni hivi karibuni nimesherehekea miaka 25 tangu kuwepo kwangu hapa duniani.

Safari ya kuelekea ukubwani ndio imekwishaanza na ni lazima niwe mtulivu kimwili na kiakili.
Lakini nitapata wapi muda huo ilhali majukumu yamenizidi mie mtoto wa mzee Mkundi.

Mawazo yamenisonga nashindwa hata la kusema.
Kama kuna kitu ambacho hamkijui, ni kwamba, tasnia ya blog imejaa msongamano wa watu wenye akili tofauti, ukitaka kublog kwa amani ni lazima uwe na akili kama za mwendawazimu.

Ni mengi yamesemwa, lakini, mweh! Nimeyaacha yapite, kwani baada ya kitambo kidogo yatapita na kuyasahau.

Mambo mengi nimeyaona na mengi nimejifunza tangu kuanza kublog, naelekea uzeeni sasa ni lazima nitumie busara.

Nimejifunza kwa wasomaji na wanablog wenzangu na naamini wao pia wamejifunza kupitia fikra zangu hizi za kiwendawazimu.

Dunia imenielemea na ninahisi nina deni ambalo ni lazima nililipe, kwani kuna watu nyuma yangu ambao wananihitaji niwasemee.

Ohh! Koero mie, Nitapata wapi muda huo?

Nadhani nahitaji nijipange sawa sawa,.

Na ninajua nitashinda.

Majaribu ni mengi sana na mitihani nayo pia ni mingi.

Naomba mnivumilie kwa kipindi hili, ambacho nimeadimika, na ninaamini mpaka wiki ijayo nitarejea kama zamani.

Msione kimya bado ningalipo………..

Saturday, May 22, 2010

TAFAKARI YA LEO: SIJUI NIKUPE NINI PASCOLINA!

Nikauacha mkoba wangu hapa!

Kuna jambo ambalo lilinitokea miezi mitatu iliyopita ambalo ningependa katika tafakari ya leo tutafakari kwa pamoja.

Kusema kweli ni uzoefu ambao ulinifanya nijifunze jambo fulani ambalo sikupata kulifahamu hapo kabla.

Nakumbuka ilikuwa ni siku ya Ijumaa, majira ya asubuhi na mapema. Nilitoka nyumbani kuelekea ofisini. Lakini wakati nakaribia kufika mjini maeneo ya Maktaba nikakumbuka kuwa nilikuwa niwalipe watu fulani fulani ambao wana tenda yaku-supply bidhaa mbalimbali pale ofisini. Kwa kuwa ninakaimu nafasi ya Cashier kwa muda baada ya nafasi hiyo kuwa wazi, nilikuwa na jukumu la kufanya malipo kila ifikapo Ijumaa.

Nilikumbuka kwamba sikuwa na hela ndogo ndogo za kutosha kwani kwa utaratibu wa mambo ya uhasibu kila hela ina thamani hata iwe ndogo kiasi gani.

Nililazimika kusimama pale Akiba na kupaki gari pembeni kisha nilivuka barabara kuwafuata wale vijana waliokuwa wakiuza chenchi pale akiba ili ninunue ili ziweze kunisaidia wakati wa malipo hayo.

Nilitoa kiasi cha shilingi elfu thelathini na kumuomba kijana mmoja muuza chenchi anisaidie chenchi ya shilingi mia mia, aliniambia kuwa atanikata shilingi elfu moja kwa kila elfu kumi hivyo nilitakiwa kukatwa shilingi elfu tatu katika elfu thelathini ambapo ningebaki na kiasi cha shilingi elfu ishirini na saba. niliafiki, lakini kwa kuwa kijana yule hakuwa na chenchi za kutosha alimuita mwenzie ili wachange.

Walinihesabia zile pesa na kunipa ambapo nilizikusanya na kuziweka kwenye mkoba wangu, kisha nikavuka barabara na kuondoka zangu kuwahi ofisini.
Nilifanya kazi hadi jioni na kurejea nyumbani ili kuandaa Sabato. Siku iliyofuata yaani Jumamosi niliamka asubuhi na mapema na kujiandaa kwenda kanisani. Baada ya kujiandaa niliondoka peke yangu na kuwaacha baba na mama wakijiandaa kwa ajili ya misa ya pili, nilitaka niwahi misa ya kwanza kwa kuwa nilikuwa na mizunguko yangu siku hiyo.

Nilifika kanisania na nilikuta ibada imekwishaanza. Ni pale wakati wa kutoa sadaka ndipo niliposhangaa kukuta fedha pungufu ndani ya mkoba wangu, je fedha nyingine zimeenda wapi? Nilijiuiza. Nakumbuka nilikuwa na kiasi cha shilingi laki moja na elfu ishirini ndani ya mkoba wangu ambazo ndizo nilizoondoka nazo nyumbani, lakini wakati napekua ili nitoe sadaka ndipo nikakuta kuna shilingi elfu thelathini.

Nikajua nimeibiwa, kwani nina uhakika kwamba nilikuwa na kiasi cha shilingi laki moja na elfu ishirini, na sasa nakuta shilingi elfu thelathini, je elfu tisini zimeenda wapi? nikaanza kubabaika, maana sikuwa na uhakika wa gari langu kuwa na mafuta ya kutosha, ikabidi nipekue zaidi, na katika hali ya mshangao nikazikuta zile shilingi laki moja na elfu ishirini, zikiwa kwenye pochi ndogo ndani ya mkoba wangu. Je hizi elfu thelathini zimetoka wapi? Lilikuwa ni swali gumu sana kwangu.

Nilikwenda kutoa sadaka na baada ya ibada kwisha nilitoka na kuondoka kurudi nyumbani ili kujianda na mizunguko yangu mingine kwa siku ile.

Lakini nilipokuwa njiani kurudi nyumbani, nilikuwa nimesongwa sana na mawazo juu ya zile fedha ambazo nilikuwa na uhakika kuwa hazikuwa ni zangu, bado nilikuwa najiuliza zimetoka wapi?Huwa nina tabia moja ya kutopenda kutumia kitu ambacho sio mali yangu, hivyo kukuta fedha ambazo sio zangu ndani ya mkoba wangu ambapo nilikuwa na uhakika kabisa wa kiasi cha fedha nilichokuwa nacho ndani ya mkoba kulininyima raha kabisa.

Unaweza kushangaa kuwa kwa nini nikose raha. Ni hivi, mimi nina tabia moja ya ajabu sana, ninapokutana na kitu ambacho sio cha kawaida basi huenda nikashinda kutwa nzima nikijiuliza juu ya jambo hilo, ndivyo nilivyo.

Sina fedha nyingi kiasi cha kusahau pesa ninazotembea nazo ndani ya mkoba wangu, sasa iweje nikute pesa ambazo nina uhakika kuwa sio zangu? Je kuna malaika gani kaniwekea fedha ndani ya mkoba wangu yarabila-ala-mina! Nilizidi kujiuliza.

Nilifika nyumbani na kumuuliza mama kama aliweka fedha ndani ya mkoba wangu, lakini alikanusha kuwa hakuweka.

Nililiacha hilo swala kama lilivyo, na kuendelea na ratiba yangu kama kawaida. Nilirudi nyumbani usiku majira ya saa mbili hivi na baada ya chakula cha usiku, ni pale ambapo tupokuwa tukisoma lesson ndipo nilipokumbuka juu ya zile elfu thelathini nilizozikuta ndani ya mkoba wangu, na kilichofanya nikumbuke ni kutokana na somo la siku hiyo ambalo lilikuwa linahusu uaminifu. Muongozaji wa somo hilo alikuwa ni baba na alianza kwa kutuuliza maswali, akianza na mimi, aliniuliza, ‘Koero, kwa mfano ukienda dukani kununua kitu halafu mwenye duka akakuzidishia chenchi, utafanya nini’

‘nitamrudishia kiasi cha fedha alichonizidishia na kuondoaka zangu’ nilimjibu baba.
Kisha akamgeukia mdogo wangu Jerome na kumuuliza, ‘Joram, hebu nawe nieleze kama ukipanda daladala na kondakta akakuzidishia chenchi utafanya nini’
Kama mimi, Jerome naye alijibu kuwa angemrudishia kondakta yule kiasi cha fedha kilichozidi.

Baba alisherehesha somo lile kwa kutufundisha juu ya umuhimu wa kuwa waaminifu mahali popote na wakati wote na hiyo itautufanya tumpendeze Mungu.

Baada ya kumaliza somo lile ndipo nilipowaleza juu ya wasiwasi wangu kuhusiana na kile kiasi cha shjilingi elfu thelethini nilichokikuta ndani ya mkoba wangu. Mama alishauri tuombe ili mungu anifunulie kuhusiana na zile fedha.

Tuliomba kisha tukaenda kulala. Ilipofika usiku wa manane singizi wote ulipotea ghafla kisha ikanijia ile kumbukumbu ya lile tukio la kukuta fedha ndani ya mkoba wangu ambazo nilikuwa na uhakika kuwa hazikuwa zangu.

Nilianza kuvuta kumbukumbu za tangu ijumaa asubuhi nilipoondoka nyumbani. Nilikumbuka kuwa niliondoka na shilingi elfu sabini kisha nikanunua mafuta ya gari ya shilingi elfu ishirini, ikabaki elfu hamsini, nikaja nikanunua chenchi ya shilingi elfu thelathini ikabaki elfu ishirini ambapo nilikuja kuongeza laki moja asubuhi ya siku hio ya Jumamosi na kuwa na shilingi laki moja na elfu ishirini, je hii elfu thelathini imetoka wapi? Lilikuwa bado ni swali lililoniumiza kichwa.

Hivi kweli niliwalipa wale vijana walionipa chenchi pale Akiba? Nilijiuliza…….nadhani sikuwalipa, niliwaza….Mhmmm…….Sasa nimeanza kukumbuka sikuwalipa wale vijana pesa zao…..Oh…masikini, nimekumbuka sasa, sikuwalipa vijana wale. Niliendelea kuwaza nikiwa pale kitandani. Niliamka na kuchukua note book yangu na kuandika juu ya wale vijana wa akiba na ile elfu thelathini, kisha nikarejea kulala.

Nilishikwa na usingizi na nilishtuka baada ya mama kuniamsha, duh! Kumbe ni saa mbili za asubuni sasa! Nilimsimulia mama juu ya ile kumbukumbu yangu, mama alinisisitiza kuwa Jumatatu nikienda kazini niwapitishie hela zao.

Siku ya Jumatatu niliamka asubuhi na mapema na kujianda kwenda kazini, nilipitia pale Akiba na kupaki gari kisha nikavuka barabara na kuwafuata wale vijana wanaouza chenchi. Lakini kulikuwa na tatizo moja. Sikuwa na kumbukumbu ya sura zao, nilimfuata kijana mmoja anayeuza chenchi na wale vijana wengine waliokuwa karibu walisogea pale kila mtu akijinadi kutaka kuniuzia chenchi.

Niliwatazama usoni lakini sikuweza kukumbuka sura ya wale vijana wawili walioniuzia chenchi siku ile ya ijumaa. Niliwaambia wale vijana waliokuwa wamnizunguka kuwa kuna kijana mmoja aliniuzia chenchi lakini alinipa fedha pungufu, ndiye ninayemtafuta, wale vijana waliposikia hivyo wakaanza kutawanyika kila mtu akienda upande wake kwani walijua kuwa ile itakuwa ni kesi.

Niliendelea kuangaza macho huku na huko nikiwatafuta wale vijana lakini sikuweza kumkumbuka hata mmoja, nilikata tamaa nikaamua kuondoka zangu.

Nilipokuwa najianda kuvuka barabara, nikamuona kijana mmoja akikimbilia daladala moja ili kuuza chenchi na nilipomuangalia kwa makini nikakumbuka ile sura. Ndiye mmoja wa wale vijana wawili walioniuzia chenchi juzi, nilimsbiri auze chenchi kisha nikamfuata na kumsalimia. ‘Vipi mambo kaka’

‘Salama tu sister, je unataka chenchi?’ alinijibu na kuniuliza swali….
Ndi….ndio nataka chenchi, nilimjbu kwa kubabaika kidogo kwani sikuwa na uhakika kama ndiye, kwa asilimia mia moja….

‘Samahani, kaka hivi unanikumbuka’ nilimuuliza
Aaa…hapana….sikukumbuki kwani vipi sister, una shida gani? Alinijibu na kunitupia swali

Juzi ijumaa nilinunua chenchi kwako asubuhi na mapema, hunikumbuki kabisa…nilijitahidi kumkumbusha…..
Ahaaaaa……nimekukumbuka si ni wewe ulikuja na kuchukua chenchi ya shilingi elfu thelathini na kuondoka bila kulipa sio wewe kweli?……alisema

Nilibaki nikitabasamu……………………………

Rashidiiii, Rashidiii,……..yule sister wa juzi kaja na hela yetu……alimuita mwenzie.
Nilimuona mwenzie akija kwa kasi na alipofika pale akaanza kushangilia na kuwaambia wenzie yaani wale wauza chenchi, ‘si niliwambia kuwa yule sister atarudi, mie nilimuona sura yake haikuonesha kuwa ni mtu mkorofi na nilijua tu kuwa ameghafilika’

Nilitoa kile kiasi cha pesa ndani ya mkoba wangu na kuwapa pesa zao na kutokana na furaha waliyokuwa nayo walitaka kunirudishia zile shilingi elfu tatu walizonichaji kama ada ya kunipa chenchi siku ile lakini nilikataa.

Hata hivyo walinipa offer ya kupata chenchi bure kwao kila nikihitaji, niliwakubalia na kuondoka.

Nilijisikia nafuu sana siku ile kwani nilihisi kama vile nimeutua mzigo mzito kichwani mwangu.

Kwa nini nimelikumbuka tukio hilo?

Ni hivi, wiki mbili zilizopita, nilipokuwa nikienda kazini nilipitia kituo cha mafuta pale Victoria kujaza mafuta. Nilitoa mkoba wangu na kuuweka juu ya roof ya gari na kutoa kiasi cha pesa na kumlipa muuza mafuta kisha nikaondoka zangu kuelekea ofisini.

Nilifika ofisini kisha nikapaki gari, lakini nilipoangalia mkoba wangu sikuuona, nilibabaika sana, kwani vioo vyote nilikuwa nimevifunga, Je mkoba wangu umeenda wapi? Nilijiuliza….

Baada ya kufkiri kidogo nikakumbuka kuwa nilitoa mkoba wangu ili kumlipa muuza mafuta pale kituo cha mafuta Victoria. Nitakuwa nimeacha mkoba wangu pale kwenye kituo cha mafuta. Niliwasha gari na kurudi hadi pale kwenye kituo cha mafuta Victoria. Nilimuuliza yule binti muuza mafuta kamaliuona mkoba wangu, akanijuibu kuwa sikuacha mkoba wangu pale.

Nilichanganyikiwa, kwani kulikuwa na makabrasha fulani muhimu ya baba ambayo yalikuwa yafanyiwe kazi kwa siku ile, pamoja na simu yangu ya kiganjani na pesa kidogo kama kiasi cha shilingi elfu ishirini hivi.

Nilirudi ofisini nikiwa nimeishiwa na nguvu kabisa kwani sikujua ningemuleza nini mzee Japheti Mkundi siku hiyo.

Nilifika ofisini na kuingia ofisini kwangu bila kumsemesha baba kwani nilihitaji muda kutafakari. Mara alikuja mmoja wa wafanyakazi wa pale ofisini na kunijuza kuwa baba ananiita ofisini kwake.

Nilinyanyuka nikiwa mnyonge kabisa na kwenda kumuona,. Nilipofika nilimkuta binti mmoja akiwa amekaa na baba ofisini. Nilimsalimia yule binti huku nikiwa nimesimama pale mlangoni nikiwaza,……mawazoni mwangu nilifikiri kuwa labda yule binti amefika pale kwa ajili ya usaili, na baba alitaka kunishirikisha, lakini kutokana na kuwa kwangu katika hali ambayo siyo ya kawaida sikutaka kushiriki katika usaili ule. Pita ukae Koero, nilistuliwa na sauti ya baba akinitaka nikae,…. lakini nilisita….’Samahani baba sijisikii vizuri nahitaji kupumzika kidogo’ nilimwambia baba.

Lakini baba alinitaka nikae kwani kuna jambo anataka kuniuliza, nilikaa lakini nikiwa sina raha kabisa. ‘Koero Mkoba wako uko wapi?’ Baba aliniuliza huku akiwa amenitumbulia macho…….

Nilibabaika sana na sikujua nimjibu nini….nimeupoteza wakati nakuja kazini asubuhi hii… nilimjibu baba huku nikiwa nimetahayari kabisa. Sasa kwa nini hukunieleza? Aliniuliza baba kwa upole kwani aliniona dhahiri nikiwa nimebabaika.

Ni….ni …..nilikuwa bado natafakari, nilimjibu huku nikiwa nimejiinamia.

Alitoa mkoba kutoka kwenye droo yake na kuuweka mezani, je huu sio mkoba wako…..nilishikwa na mshangao…..Heeee….baba umeupata wapi!!!!? Nilimuuliza baba kwa hamaki!!!

Mkoba wako umeokotwa na huyu binti, maeneo ya Victora ukiwa pembezoni mwa barabara karibu na kituo cha mafuta, alipekua na kukuta simu ambapo alimpigia mama yako na ndipo mama alipomuelekeza hapa ofisini na ndo akauleta. Alisema baba…..

Mhh…..Pascolina, huyu ndiye Koero na ndiye mwenye Mkoba nilimrukia yule binti na kumkumbati kwa furaha na kumshukuru sana…..nilitoka naye hadi ofisini kwangu ambapo tulikunywa chai pamoja na kupiga soga kidogo, kisha nikamsindikiza Pascolina hadi nje ya ofisi akaondoka kwa ahadi ya kuwasiliana zaidi ili tupange siku nimkaribishe nyumbani kwa ajili ya chakula cha jioni.

Hakuna siku ambayo nilikuwa na furaha ya ajabu kama siku hiyo, na furaha hii itaendelea kubaki katika kumbukumbu zangu milele. Pascolina ameendelea kuwa rafiki yangu mwema kama walivyo wale vijana wauza chenchi pale akiba na tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara na Mungu akipenda kesho tutajumuika naye nyumbani kwetu kwa ajili ya Dinner na kufahamiana vizuri zaidi.

Nilikuja kugundua kuwa, kumbe baada ya kumlipa muuza mafuta niliacha mkoba wangu juu ya roof ya gari na kuondoka kwa pale kituo cha mafuta ambapo mkoba huo ulianguka mita chache kutoka pale kituoni pembezoni mwa barabara. Lakini kama bahati wakati Pascolina akielekea kazini kwake alipita pale na kuuona mkoba wangu ambapo aliuokota na kuanza kuupekua, na kitu cha kwanza kuona kilikuwa ni simu yangu amabyo ndiyo aliyoitumia kumpigia mama.

Najua kuna wanaume wakware watataka kumjua Pascolina zaidi, jamaniieeee ana mchumba na anatarajia kufunga ndoa hapo mnamo Novemba 2010.

Hii ndio tafakari ya leo.

Tuesday, May 18, 2010

WACHAGA NA ‘KITOCHI,’WAPARE NA ‘KIBARA CHA MAWA!’

Bila Kitochi kwa Wazee wa Kichaga, mazungumzo hayatanoga!

Jana nilikuwa natafakari kauli ya Rais wetu Mheshimiwa Jakaya Kikwete juu ya hekaya za Wachaga na Kitochi, Wakati alipokuwa akiongea na viongozi wa dini juu ya mustakabali wa nchi yetu kuelekea uchaguzi mkuu.

Raisi alisema kuwa ni vigumu kudhibiti takrima katika uchaguzi mkuu, akatolea mfano kuwa kule Klimanjaro ni vigumu kuwakusanya Wazee wa Kichaga bila kuwapa Kitochi. Kitochi kwa kule Kilimanjaro ni kipimo cha pombe ambacho naambiwa kina ujazo wa nusu lita.

Sina haja ya kurejea kile alichokieleza Rais kwa undani kwa sababu hata hivyo msajli wa vyama amedai kuwa ule ulikuwa ni utani tu wa Rais kwa iongozi wale.

Katika kutafakari kwangu niliwaza, hivi na Wapare nao wakidai 'Kibara cha Mawa' itakuwaje? Maana kila kabila lina mila zake za kuwaita wazee na kuwakutanisha pamoja. Kama ilivyo kwa Wachaga kuita Kitochi, wapare nao wana utaratibu wao wa Kibara cha Mawa. Yaani kibuyu cha pombe.

Mara nyingi Kibara cha Mawa hutumika pale mtu anapowakusanya wazee ili kuzungumza nao jambo au kama mtu ameleta posa na anataka ijadiliwe na wazee au hata mashauri mbalimbali yanayowakutanisha wazee, basi Kibara cha Mawa ni lazima kiwepo.

Je kwa makabila mengine kama Wasukuma, Wangoni, Wahaya, Wakurya, Wajita, Warundi, Wanyakyusa, Wahehe na makabila mengine wanaitaje utaratibu huu?

Sunday, May 16, 2010

HATIMAYE YAMETIMIA: DDT KUANZA KUTUMIKA KUDHIBITI MALARIA

Kuna wakati niliwahi kushauri serikali iridhia matumizi ya dawa ya kuuliwa wadudu ya DDT ili kuteketeza mazalia ya mbu, ukitaka kujikumbusha unaweza kubofya hapa. Pia baada ya uzinduzi wa Zinduka malaria Haikubaliki niliandika hapa kibarazani kwangu kumshauri Rais kwamba ni vyema angetumia fursa ile ya uzinduzi kuhalalisha matumizi ya dawa hii ya DDT bila kujali kelele za wanamazingira na wafanyabiashara. Ukitaka kujikumbusha unaweza kubofya hapa

Leo hii nimefarijika baada ya kusoma katika Gazeti la Mwananchi kuwa hatimaye serikali imeridhia matumizi ya dawa hiyo. Hao wanaopiga kelele wajaribu kuangalia nchi zilizofanikiwa kuwatokomeza hao mbu kwa kutumia dawa hiyo bila kuleta madhara kama wanavyodai. Mbona hapo Zanzbar dawa hiyo imekuwa ikitumika na hakuna athari zilizoripotiwa kama inavyochagizwa na hao wahafidhina?

Tuacheni unafiki, Tufikie mahali tukubali kuwa inatosha na tuitokomeze malaria kwa nguvu zetu zote.

******************************************


DDT kuanza kutumika kudhibiti malaria

Na Sadick Mtulya wa Gazeti la Mwananchi.


SERIKALI imesema pamoja na kwamba inagawa bure vyandarua ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa malaria, ipo mbioni kupuliza dawa ya DDT ili kuua mazalia ya mbu.Kufuatia mpango huo, serikali imewataka watanzania wasiwe na hofu kuhusu DDT na kwamba madhara yake si makubwa kama inavyoelezwa.
Akizungumza na Mwananchi juzi jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa alisema nchi nyingi Dunia zimefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa malaria kwa kutumia DDT na kwamba dawa hiyo itakuwa ikipuliziwa katika kuta na dari za nyumba.“Wananchi waondokane na hofu kuhusu DDT kwani hadi sasa hakuna ushahidi wa kimaabara unaoonyesha kuwa kuna mtu ameathiriwa na dawa hiyo.
Dawa hii itakuwa ikinyunyuziwa katika kuta na dari za nyumba na mbu akitoa eneo hilo hufariki,” alisema Profesa Mwakyusa Profesa Mwakyusa alisema dhana iliyojengeka kuwa DDT inasababisha saratani si ya kweli na kwamba hadi sasa hakuna mtu aliyeripotiwa kupata ugonjwa huo kutokana na dawa hiyo.
Alisema DDT itakuwa ikipuliziwa kutegemeana na eneo ambalo watu wanaugua kwa wingi ugonjwa wa malaria na kwamba mpango huo, umeanza katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.Waziri Mwakyusa pia alisema tayari vyandarua milioni tisa vya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa malaria vimegawiwa bure nchini kote.

Alisema idadi hiyo ni kati ya vyandarua milioni 14 vilivyotolewa na serikali pamoja na taasisi na mashirika binafsi.“Vyandarua milioni tisa vimekwisha gawiwa bure nchini kote,” alisema Profesa MwakyusaKatika hatua lingine, matokeo ya utafiti wa hali ya magonjwa ilivyo nchini, inatarajiwa kutolewa mwezi juni mwaka huu.Hatua hiyo inafuatia timu ya waataalamu wa afya kukamilisha utafiti wa magonjwa yote, ulionza mwaka jana.

“Mwezi Juni mwaka huu, wizara yangu itatangaza matokeo ya utafiti wa jinsi hali ya magonjwa ilivyo nchini. Hii ni baada ya timu ya wataalam wa afya kukamilisha utafiti ulionza mwaka jana,” alisema Profesa Mwakyusa.Profesa Mwakyusa alisema Tanzania ilianza utaratibu wa kufanya utafiti wa magonjwa mwaka 1996 na kwamba kila baada ya miaka minne utafiti huo hufanyika.

Saturday, May 15, 2010

HATIMAYE NIMEPONA!

Kuugua sio kufa jamani......

Baada ya kusumbuliwa na homa ya matumbo ambayo inavutia zaidi ukiita Typhoid, namshukuru muumba kwa kuniponya na sasa ninatarajia kurejea hapa na kuliendeleza libeneke hili la Vukani.

Naomba nitoe shukurani kwa Daktari Aliyenipatia tiba na Wanablog wenzangu wakiwemo wasomaji wa kibaraza hiki kwa kuniombea ili nipone haraka.

Nimefarijika sana na pole zenu na nimejisikia fahari kuona kuwa kumbe kupitia blog hii nimejijengea marafiki wengi kupindukia.

Najua kutoweka kwangu katika mtandao kutokana na kuumwa kuliwakosesha kusoma ujinga wangu ambao kupitia kwayo mmekuwa mkijifunza pia.

Kwa bahati mbaya kutokana na kuumwa nimeshindwa kuandika Tafakari ya Leo. Najua kuna watu ambao watasononeka kutokana na kukikosa kipengele hiki wiki hii, lakini naomba mniwie radhi kwani nitajitahidi wiki ijayo kipengele hicho kiwepo.

Jamani kuugua sio kufa, nimerejea tena…………

Tuesday, May 11, 2010

NIMEAMBIWA ETI NINA TYPHOID

Ukimya wangu sio bure, kulikuwa na mkono wa shetani, nimesumbuliwa na homa za usiku kwa atakribani wiki moja na juzi nilipokwenda hospitalini, na baada ya vipimo kadhaa nikaambiwa eti nina ugonjwa unaoitwa typhoid.

Unajua kuna maradhi mengine ukiyatamka kwa kiingerza yanavutia tofauti na kuyatamka kwa kiswahili. kwa mfano ni vyema kusema nina typhoid badala ya kusema nina homa ya matumbo. au ni vizuri ukisema una diarrhea badala ya tumbo la kuhara.

Vile vile ni vyema kusema unaumwa tonsils badaya ya kusema unaumwa mafindofindo, au kusema unaumwa AIDS badala ya kusema una UKIMWI.

Si mmeona majina ya maradhi yakitamkwa kwa kiingereza yanavyovutia......
ndio sababu na mie nikasema naumwa Typhoid badala ya homa ya matumbo.

Inasemekana nimekunywa maji yasiyochemshwa na ndio sababu ya kupata ugonjwa huo, ingawa nakunywa maji ya chupa sijui nayo nahitaji kuyachemsha?


Mwenzenu naumwa.......................

Sunday, May 9, 2010

RABIA: MALARIA IMENIFANYA NIWE MWALIMU MLEMAVU WA KUSIKIA...

Mwalimu Rabia Abdallah

“Mwaka 1996 hadi 1998, nikiwa nasoma chuo cha ualimu Korogwe mkoani Tanga, nilidharaulika sana na kuonekana kama kituko kwa baadhi ya walimu na wanafunzi, huku wengine wakishangazwa nami kwa jinsi nilivyoweza kumudu masomo yangu wakati sina uwezo wa kusikia,’’ ndivyo anavyoanza Rabia Abdallah (34) ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya viziwi Buguruni akielezea jinsi matatizo ya kusikia yalivyomfanya aonekane kituko wakati alipokuwa akisoma.

Anasema jinsi alivyokuwa akisoma ni Mungu tu ndiye aliyekuwa akimsaidia kwani hakuwa akisikia chochote zaidi ya kusoma vitabu baada ya walimu kumaliza kufundisha na njia hiyo ya kusoma vitabu ndiyo iliyomwezesha kushinda mitihani yake na kufanikiwa kutunukiwa Diploma yake ya Ualimu.

“Wengi hawakuamini na walifikiri naigiza lakini wengine waliamini lakini hawakuweza kunisaidia kwa kuwa hakuna aliyekuwa akiweza kuzungumza kwa ishara kwani hata mimi mwenyewe sikuweza kuwasiliana kwa ishara kwa wakati huo, hivyo maisha ya masomo pale Korogwe yalikuwa magumu mno kwa upande wangu…,’’

anasema Mwalimu huyo ambaye hivi karibuni amepokea barua ya uhamisho ikimtaka kuhamia katika darasa maalumu la wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) katika shule ya msingi Temeke. Rabia kwa sasa ana watoto wawili, anasema alifikiri kuwa kupata Diploma kungekuwa mwisho wa matatizo yake kumbe ndiyo kwanza matatizo yalizidi kuongezeka, kwani baada ya hapo alikumbana na tatizo la kupata kazi kwani kila alikoomba kazi ya kufundisha alikataliwa kwa kutokana na matatizo yake ya kusikia.

“Tatizo liliibuka upya nikaanza kudharaulika tena kila nilipokuwa nikiomba kazi kwani waliniita kiziwi nisiye na uwezo wa kufanya lolote na walishangaa ilikuwaje nimepewa Diploma wakati ninamatatizo hayo, waliamini kuwa mwenye matatizo ya kusikia hawezi kusoma tena maishani mwake,’’ anasema Rabia.

“Hapo nikalazimika kuomba kazi za kawaida ambapo nilipata kazi ya muda katika taasisi ya CCBRT ambapo nilifanya hapo kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, nikaona tangazo la kazi kwenye gazeti, likieleza kuwa manispaa ya Ilala inataka mwalimu wa kufundisha walemavu wa kusikia katika shule ya Buguruni Viziwi, nikaomba na nilipokubaliwa nikaacha kazi CCBRT,’’ anasema Rabia.
Anasema hata hivyo haikuwa rahisi kama alivyodhani hapo alitakiwa kusoma kwanza katika chuo cha walimu wanaofundisha elimu ya watu wenye ulemavu wa kusikia katika chuo cha Patandi kwa ngazi ya Diploma ndipo apate kazi ya kudumu alikubali na kwenda kusoma.

“Nilikwenda huko lakini nilipoomba wanipatie fedha za kunisomesha walisema nitumie zangu kisha baada ya kumaliza manispaa ingelipa lakini tangu 2005 hadi leo sijalipwa chochote na ndiyo kwanza nimepokea barua ya uhamisho wa kutakiwa kwenda Temeke lakini nao hauna fedha za uhamisho, hata sijui kwa nini,’’ anasema Rabia.

Hata hivyo licha ya kusoma katika chuo hicho maalumu kwa walimu wa kufundisha watu wenye ulemavu wa kusikia, Rabia anasema alipomaliza masomo yake hakuwa akijua kutumia ishara jambo lililomlazimu kujiunga na chama cha walemavu wa kusikia ambapo alijifunza na kufahamu vizuri lugha ya ishara.

Akizungumzia jinsi alivyopata ulemavu wa kusikia, Rabia anasema alizaliwa akiwa anasikia kama kawaida lakini alipofika darasa la nne akapatwa na malaria kali ambayo ilimlazimu kutumia dawa kwa muda wa mwezi mzima na baada ya kupona taratibu uwezo wa kusikia ukawa ukipotea na hatimaye hakuweza kusikia tena hadi leo.

Rabia ambaye ni mkazi wa Ilala Sharifu Shamba anasema kipindi hicho alikuwa na miaka nane.

“Taratibu nilijikuta nikipoteza uwezo wa kusikia lakini kipindi hicho nilipata shida sana kwani wazazi na ndugu zangu walidhani nimeanza jeuri hivyo walikuwa wakinipiga makwenzi na kunidhihaki sana bila kujua kuwa nilikuwa sisikii,’’ anasema Rabia kwa kusikitika.

“Unajua hawakuwa wakijua kama nimepoteza uwezo wa kusikia, kwa kuwa mara kwa mara mama alikuwa akiniita lakini sikuwa nikiitika kwa kuwa nilikuwa sisikii hivyo alikuwa akikasirika sana na kunipiga mara kwa mara na ndugu zangu nao pia walikuwa wakinipiga makonzi, iliniuma sana lakini sikuwa na jinsi ya kuwaeleza wasifanye hivyo,’’ anaendelea kueleza Rabia.

Anasema hali hiyo iliendelea kwa muda mrefu lakini baadaye baadhi ya majirani waliingiwa na wasiwasi na hali hiyo na kumweleza mama yake na ndugu zake kuacha kumpiga makonzi kwani huenda mtoto huyo akawa na matatizo ya kusikia hivyo walimtaka mama yake kwenda kumchunguza masikio hospitalini na alipofanya hivyo iligundulika kweli hakuwa na uwezo wa kusikia.

“Matokeo hayo yalimuhuzunisha sana mama, nilimuona akijisikia vibaya kwa kuwa alikuwa akinipiga makwenzi kwa kudhani kuwa nilikuwa jeuri, lakini hakukuwa na la kufanya, kipindi hicho hakukuwa na shule za wenye ulemavu huo hivyo nikalazimika kusoma kwa kuchanganyika na wanafunzi wasio na matatizo kama yangu,’’ anaeleza Rabia.

Kwa masikitiko Rabia anasema kuwa yeye alikuwa katika hali ngumu kwani ilipofika kipindi cha mitihani hasa somo la Imla hakuwa akiambua kitu na wala hakuwa akipata msaada wowote kwa kuwa walimu wenyewe waliokuwa wakisimamia mitihani hawakuwa wakijua kuzungumza kwa ishara.

‘‘Hivyo katika mitihani yangu yote kuanzia darasa la nne nilikuwa nikikosa maswali yote ya Imla na yale ambayo yalikuwa yamekosewa na kubadilishwa kwa kusomwa kwa kuwa sikuwa nikisikia kitu zaidi ya kuhisi baadhi ya mambo, lakini nashukuru Mungu licha ya kushindwa Imla katika kila mtihani wangu, Mungu alinisaidia nikafaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Kisutu,’’ anasema Rabia.

Anasema sekondari nako kulikuwa kugumu zaidi kwani alikuwa hasikii na lugha iliyokuwa ikitumika ni Kiingereza ikawa ngumu kutambua kwa kuangalia mdomo wa mwalimu kwa kuwa maneno hayo hakuwa akiyafahamu, ikawa ngumu kwake kung’amua lolote hata alipojaribu kumuangalia mwalimu wa somo anavyotamka maneno.

Rabia alimaliza sekondari na kupata daraja la nne la pointi 26 hivyo akachaguliwa kujiunga na Ualimu katika chuo cha ualimu Korogwe Tanga.

“Nina ombi kwa serikali, naomba wabadilishe mfumo wa mitihani ya shule za msingi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia, maswali yasifanane na wasio na matatizo hayo ili kila mtu awe na uwezo wa kujibu na pia wasimamizi wa mitihani hiyo wawe walimu wenye uelewa na watu wa namna hiyo,’’ anasema Rabia.

Makala haya yameandikwa na Festo Polea wa Gazeti la Mwananchi

Saturday, May 8, 2010

TAFAKARI YA LEO: TUENDELEE NA SOMO LA IMANI

Akaukemea upepo, akaiambia bahari, nyamaza utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.

Katika mfululizo wa tafakari ya leo nimeona tuendelee na somo letu la imani.
Ningependa leo tusome Marko Mtakatifu 4:35-41

Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia. Na tuvuke mpaka ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba moja kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwepo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, sikitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, nyamaza utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga ? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Mara nyingi Bwana Yesu alikuwa akifundisha kwa mifano, na haiyumkini kuna matukio ambayo yalikuwa yanamtokea ili wanafunzi wake wapate kujifunza kupitia kwake.

Hebu tuangalie mfano huo hapo juu, wanafunzi hawa wamekuwa wakitembea na Yesu kutwa nzima na walikuwa wakimuona akitenda miujiza mbalimbali kwa kuponya watu, kufufua wafu na miujiza mingine mingi tu.

Na hata kufikia kuwaeleza kuwa hata wao wanaweza kutenda miujiza iwapo watakuwa na imani. Lakini wanafunzi hawa pamoja na kuwa walikuwa na Yesu mle chomboni lakini bado walikosa imani kuwa wanaweza kuukemea upepo ule na ukatulia. Walikuwa wamekata tamaa kabisa ikabidi wamwamshe Yesu ili awaokoe.

Naye Yesu kwa kutambua kuwa wanafunzi wake hawajaiva katika somo la imani akaamka na kuukemea upepo ule hadi ukatulia, lakini hakuwaacha hivi hivi, akawaambia ‘Mbona mmekuwa waoga ? Hamna imani bado?’

Yesu aliwashangaa wanafunzi wale, kuwa pamoja na kufundisha kote lakini bado tu somo hili la imani halijawaingia? Ajabu kweli!

Leo Yesu hayupo, lakini ametuachia somo hili kubwa kabisa la kuwa na imani.

Tukio hilo la Baharini, naweza kulifananaisha na misukosuko iliyopo hapa duniani.
Dunia yetu hii imejaa misukosuko mingi sana ya kimaisha, kama ilivyo misukosuko ya baharini, kuna matukio mengi ya kukera na kukatisha tamaa.

Kama ilivyo bahari kukumbwa na upepo mkali na mawimbi, na wakati mwingine kuwa shwari na ndivyo maisha yetu yalivyo.

Kuna wakati tunakuwa na furaha na amani lakini kuna wakati hali hugeuka na kuwa ya kukatisha tamaa kutokana na misukosuko ya kimaisha.

Hali hiyo hatuwezi kuiepuka, hadi tutakapoiacha hii miili yetu (tutakapokufa). Hatuwezi hata siku moja kuishi bila kukabiliana na changamoto za hapa duniani. Kama Yesu aliweza kukabiliana na cnagamoto mbalimbali za kimaisha iweje sisi tusikabiliane na changamoto hizo.

Kwa kulitambua hilo, ndipo bwana Yesu anapotueleza kuwa sisi pia tunaweza kufanya miujiza pale tunapokabiliana na changamoto za kimaisha.

Kama wewe ni ni mwanafunzi na una wasiwasi wa kufaulu mtihani, basi amini tu kuwa unaweza kufaulu, kwa kusoma kwa bidii na kuzingatia masomo, jitihada hizo na imani inaweza kukuvusha. Kama umetafuta kazi kwa muda mrefu bila mafanikio, umelima kwa muda mrefu bila kupata mazao ya kutosha au kukosa kabisa, umefilisika katika biashara zako au umepata hasara katika bishara zako, maisha yako yamekuwia magumu, umempoteza mwenzi wako, umeachwa na mchumba wako, usikate tamaa, weka imani yako kwa mungu, hakika kila utakaloomba na kuamini litawezekana.

Tunaweza kuvuka vikwazo na viunzi mbalimbali vya kimaisha kwa kuamini tu kuwa hayo ni mapito. Hatuna haja ya kusononeka wala kukata tamaa.

Tukutane Jumamosi ijayo……………..

Thursday, May 6, 2010

DALILI HIZI SIO ZA KWELI.............


Shhhhhhhhhhhhh!!!!!!!!!!!!!!!!


Kuna makala ameweka mwanablog mwenzangu Kamala katika kibaraza chake yenye kichwa cha habari kisemacho, 'Kublog ni elimu' na kama ukitaka kujikumbusha unaweza kubofya hapa kusoma habari nzima.

Nimevutiwa na makala hiyo, lakini naomba nikiri kuwa nami nimeelimika vya kutosha katika tasnia hii ya blog, katika namna tofauti. Maana naamini suala la blog siyo la kulifanyia mzaha au la kupita, ni elimu tosha ukiwa makini kwa blog makini.

Labda kuna jambo moja ambalo nilikuwa sijalijua kutoka kwa wanaume na kwa hakika ndiyo maana nasema blog zimenipa uelewa huo, sasa nafahamu kwa kiasi chake. Kwahiyo baada ya kuanza kublog nimejikuta nikiwafahamu wanaume kwa upande mwingine, yaani kufahamu hulka zao na mambo mengine yanayowahusu.

Nakumbuka mwanzoni kabisa wakati naanza kublog nilianza kupata baruapepe nyingi sana kutoka kwa wanaume mbalimbali ambao walikuwa wakinipa moyo na kunipa maelekezo ya hapa na pale juu ya kublog na mambo mengine yatokanayo.

Kupata baruapepe hizo ilikuwa changamoto kubwa na faraja kwangu, kwani sikutegemea sana ingawa nilifahamu nitawasiliana na watu mbalimbali iwe wanablog au wasomaji wasio wanablog. Wapo waliokuwa wakinitumia baruapepe za kutaka kunifahamu zaidi na sikuwaficha kitu nilikuwa nawaeleza historia yangu kwa ufupi.

Kwakuwa natambua kwa ufupi huo unaweza kuwasaidia kunifahamu kwa kiasi fulani.
Kuna baadhi yao ambao nilikuwa nikiwasiliana nao mara kwa mara. Na katika kuwasiliana kwetu huko kwa njia ya baruapepe tulitaniana na kufanyiana mzaha wa hapa na pale ambayo kwangu lilikuwa jambo la kawaida kabisa.


Hata hivyo kuna wakati niliduwazwa na mambo kadhaa ambayo yalinifanya nijisaili maradufu,na kashangaa zaidi. Nasema katika hali ya kushangaza, kwasababu kuna baadhi naona walikwenda mbali zaidi ya mzaha wenyewe. Maana haikuwa utani tena bali kukawa na jambo jingine limeingizwa humo. Sikutarajia hilo kwakuwa kwangu nilikuwa nawasiliana kwa heshima na taadhima.

La haula! nikaanza kutongozwa, tena bila kificho. Aaaah! mweeh! nikaona makubwa haya nitayaweka wapi, madogo yana nafuu. Yaani kumbe yale mawasiliano yetu wenzangu wameyageuza mapenzi? Kumbe ule mzaha umegeuka kitongozeo’?

Nikaduwaa zaidi, kisha nikajiuliza kidogo, lakini nikaishia kunyamaza. Yaani ile midadi ya mzaha ikageuzwa na kudhani nimevutiwa nao kimapenzi.

Haki ya nani hivi! Kaaaazi kweli kweli!

Lakini naomba niweke wazi kuwa hao sio miongoni mwa wanablog wenzangu, na wale tunaowasiliana kwa heshima zote na taadhima, maana hao nimeendelea kuwasiliana nao na tumekuwa tukiheshimiana sana.

Na heshima hii imenipa hamasa zaidi ya kublog na kushirikiana nao daima. Sasa, kuna baadhi ya wanaume huziona dalili za mwanamke kumtaka kimapenzi kwa namna ambayo siyo kabisa.

Na ndio maana mara nyingi mwanamke anapomchangamkia mwanaume na kuwa naye karibu kimazungumzo katika hali ya kawaida, anaweza akajiaminisha kwamba hiyo ni dalili ya kupendwa na mwanamke husika.

Sijui niseme namna gani, lakini hayo ni mawazo ya ajabu kabisa. Jamani hata kuchangamkiana itafsiriwe ni ‘kunogea penzi’? Aaah!

Wallahi hii siyo kabisa, haikubaliki. Na hiyo dalili huwapa wakati mgumu sana wanaume pale wanapogundua kuwa mwanamke husika hakuwa na fikra za kuwa na uhusiano nao kimapenzi kama walivyodhani.

Hayaishii hapo, inatafutwa njia mbadala, ndipo fedha na nguvu itatumika ili kuhakikisha anampata mwanamke huyo na wakati mwingine hata vitisho pale njia hizo mbili zinaposhindwa kutoa matokeo anayotarajia.

Tabia hii ya baadhi ya wanaume inaleta hitilafu. Yaani anaweza kuamini kabisa kuwa mwanamke fulani amempenda kimapenzi, wakati sio kweli. Na anapomtongoza mwanamke huyo na kukataliwa, hapo ndipo mbinu chafu zinapoanza kutumika kwa kuwa wanaume hawakubali kushindwa katika jambo hilo.

Kwa kawaida wanawake na wanaume, wanayo mikabala tofauti katika kuonesha dalili za kupenda. Wakati kwa wanaume kuchekewa, kuchangamkiwa na kutaniwa na mwanamke, kuna maana ya mwanamke huyo kumpenda mwanaume husika. Lakini kwa mwanamke, kufanya chochote kati ya hayo au kufanya yote hakuna maana ya ‘kumpenda’ mwanaume huyo.

Na hapo ndipo suala la kuwa waangalifu linapokuja, hususan tunapofanya masihara na baadhi ya wanaume maana wenzetu wanaweza kutafsiri ‘tunahitaji penzi au kujitongozesha’.

Kwani ule utani na ukaribu wetu kwao unatafsiriwa vibaya. Kila mwanamke anayo dalili ya kuonesha kuvutiwa na mwanaume lakini sio kwa dalili za wazi kiasi hicho.

Waama, Waswahili walikwisha kusema, 'ada ya mja hunena, muungwana ni vitendo'. Kwa kawaida wanawake huonesha vitendo kuliko maneno....LOL

Wednesday, May 5, 2010

JE, UTABIRI WA BALDWIN ZACHARIA JUU YA RAIS KIKWETE UMETIMIA?

Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete

Mnamo Novemba 9, 2005, katika Gazeti la Jitambue, ambalo halichapishwi kwa sasa kutokana na mhariri wake ndugu Munga Tehenan kuupoteza mwili, kulikuwa na makala moja iliyokuwa ikitabiri utawala wa Rais Kikwete utakavyokuwa iwapo angeshinda.

Utabiri huo ulifanywa na Mtabiri na mwandishi wa makala za kiutambuzi wa gazeti hilo ndugu Baldwin Zacharia. Pamoja na kutabiri juu ya ushindi wa Rais Kikwete jambo ambalo wadadavuaji mbalimbali wa nyota na wachambuzi mbalimbali wa kisiasa hapa nchini walitabiri, lakini mtabiri huyu alikwenda mbali zaidi na kueleza utawala wa Raisi utakavyokuwa kutokana na nyota yake.

Leo hii akiwa ndio anaelekea kutimiza miaka mitano akiwa Ikulu, nimeona nirejee utabiri huo ili kuangalia kama utabiri wake umetimia au la.

Naomba uungane nami katika kuusoma utabiri huu kama ulivyoandikwa na Mtabiri huyu Baldwin Zacharia.

**************************
KIKWETE ATAKUWA RAIS WA MAAJABU NCHINI

Na Baldwin Zacharia.
Gazeti la Jitambue la Jumatano 9, Novemba 2005

Mimi ninaamini katika nyota na huwa ninachambua nyota. Nimeamua, kwa kutumia utaalamu wangu kuchambua nyota ya mgombea wa wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete.

Ni kwa nini yeye?

Ni kwa sababu, anatajwa katika tafiti zilizofanywa hapa nchini na jumla ya maoni ya wengi kwamba, ana nafasi kubwa ya kuwa Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikwete amekuwa katika utumishi wa wa chama chake kwa miaka 30 na katika utumishi wa serikali katika nafasi mbalimbali za uwaziri kwa miaka 17.

Baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, mwaka 1975 na kupata shahada ya uchumi, akiwa na umri wa miaka 25, Kikwete alijiunga katika utumishi wa chama cha TANU (Tanganyika African National Union). TANU ndiyo iliyoongoza mapambano ya kudai uhuru nchini na Februari 5, mwaka 1977, ilijiungana na chama kilichoasisi mapinduzi ya Zanzibar, ASP (Afro-Shirazi Party) na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi yaani CCM.

Jakaya Mrisho Kikwete alizaliwa Oktoba 7, mwaka 1950 katika kijiji cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. Ni motto wa sita wa mzee Khalfani Mrisho Kikwete.

Huenda Kikwete haamini katika nyota, lakini akisoma uchambuzi huu atalazimika kuanza kujiuliza kuhusu nguvu za nyota, kwani atajiona akiwa anazungumziwa yeye, hata kwa mambo ambayo hajawahi kumwambia mtu anayo au anayafikiri.

Kwa kuzaliwa Oktoba 7, kama wengine wote waliozaliwa kati ya Septemba 23na Oktoba 22, Kikwete anaangukia kwenye alama za jua (Sun Sign) ya Mizani (Libra). Hii ni alama ya saba katika mpangilio wa mwenendo wa sayari.

Kwa wale wanaojua kuhusu nyota watakubaliana nami kwamba, alama hii inahusika na uhusiano, ushirikiano, mawazo, maoni, siasa, diplomasia, muziki, amani, uwezo wa kujidhibiti na tabia nzuri.

Nyingine ni pamoja na kuwa na mvuto kwa kutazamwa, uwezo wa kuboresha hali, utanashati, mawazo yenye mantiki ya kupima na mawazo kuhusu unafuu kwa jamii inayomzunguka mwenye nyota hii.

Hata kama wewe sio mtaalamu wa uchambuzi wa nyota, unaweza kusoma kwenye vitabu mbalimbali, ili uweze kuona sifa za mtu wa nyota ya Mizani. Kwenye nyota, Mizani ndiyo inayoonekana kwamba, ni bora zaidi, kwani imetulia na iko mahali ambapo inatengeneza urari au usawazisho wa mambo mengi, ndio maana imeitwa Mizani.

Kwa tabia za watu wa nyota hii, kama Kikwete atachaguliwa kuwa Raiswa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watu watarajie kitu gani?

Watarajie kuona mtu mtendaji zaidi kuliko mtu wa nadharia. Ingawa atachukua muda mrefu kutafakari jambo (ndivyo watu wa nyota yake walivyo), lakini kutenda ni lazima, pale anapoona jambo linaweza kufanyika bila kuumiza watu.

Kwa nini nataja kuumiza watu katika suala hili? Utaona mbele kwenye uchambuzi wangu, namna watu wa nyota ya Kikwete wanavyohusiana na wengine kwenye maisha.

Kama atakuwa Rais wananchi wategemee kuona mtu mbaye kabla hajatoa uamuzi, atakaa kwa muda kutafakari. Watu wa nyota ya Mizani huwa hawaamui kwa jazba au haraka.

Kama Kikwete hana furaha na yuko katika ugiligili (Frustration) ataonesha tabia zifuatazo.ambazo sio nzuri sana. Ndivyo watu wa nyota yake walivyo: Atakuwa ni mwenye hasira za haraka na anayependa makuu yasiyo na kitu. Atakuwa ni mwoga na asiye na uwezo wa kufanya uamuzi hata pale ambapo kila kitu kiko wazi.

Lakini pia atakuwa ni mtu anayetumia wengine kwa faida yake. Hivyo hutokea kuwa mtu anayependa kuwadhibiti au kuwaendesha wengine kwa njia yenye kukera sana.

Hata hivyo kila anayemfahamu Kikwete, anajua kwamba hayuko kwenye ugiligili na ana furaha karibu muda wote. Kwa hiyo ni Mizani ambaye anatarajiwa kuonesha upande mzuri wa nyota hiyo, siyo huo mbaya.

Kwa upande mzuri, Mizani ni watu wanaojua sana kushirikiana na wengine, wanakubalika kwa wengi, kwani wanaingilika kirahisi, ni watu ambao wanaweza sana kuzungumza na kufanikisha muafaka kati ya watu wanaogombana, wanapenda sana haki au uhalali katika kutenda, hupenda kuongoza kwa faida ya wale wanaowaongoza zaidi, kuliko kwa faida yao. Kama nilivyosema, hufikiri vizuri sana kabla ya kutenda na ni watu wa vitendo badala ya maneno.

Kwa kumtazama Kikwete na kutazama kila alikopita tangu akiwa shule ya msingi ya Lugoba, sekondari Kibaha, sekondari Tanga, na Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na baadae makazini, nimegundua kwamba, ameathiriwa n asana na nyota yake, tena athari za upande mzuri.

Kwa hali hiyo, Kikwete anatarajiwa kuwa Rais aliyetulia sana na anayemudu kuficha hofu zake na kubabaika kirahisi. Ana uwezo wa kudhibiti hali ambayo kwa mwingine angebabaika sana. Lakini watu wa Mizani wana hofu ya kuwa peke yaona ndio maana mara nyingi wanakuwa na kundi la marafiki au ‘kampani’ kama tunavyoita. Je, Kikwete hayuko hivyo?

Ukweli ni kwamba, Kikwete anaweza kuwa Rais wa ajabu ambaye nchi hii haijawahi kumshuhudia kwa sababu ana athari za wazi ambazo ni chanya za nyota yake. Kwani kwa nyota yake anatarajiwa pia kuwa rais mwenye upendo sana na mwenye kusikiliza kwa makini mawazo ya wengine.

Lakini anaweza kukasirika kupindukia na kupinga sana pale atakapotakiwa kufuata amri. Mizani ni wajanja kupindukia, tofauti na wanavyoonekana au namna wanavyozungumza. Ni watu wanaopenda sana kuzungumza na wengine, labda wakitafuta mawazo au kujivua na upweke. Lakini kwa bahati mbaya, wanaweza kuamini watu wasio wakweli bila wenyewe kujua na watu hawa wakawathiri.

Kwa athari za sayari ya Zuhura (Venus) ambayo ndiyo yenye kuongoza nguvu ya kinyota ya Mizani, mtu aliyeathiriwa na nyota yake kama Kikwete anakuwa ni mpenda amani sana na hana mazungumzo ya kumwaga damu au kukomesha. Lakini anapokerwa hadi kufikia ukomo, hufanya mambo ambayo wengi wanaweza wasiyasahau kirahisi.

Kinajimu Zuhura ni sayari ya thamani, nafsi, umiliki, uzuri, na upendo. Kwa maana hiyo, Kikwete akiwa Rais wa nchi, atasababisha thamani ya nchi kupanda kupitia kwake, umiliki kuwa mkubwa zaidi, utanashati yaani kutakata kwa watu na uhusiano mzuri na amani kuongezeka.

Kuhusu mwonekano, kwa kawaida hakuna mwonekano wa mtu kufuata nyota yake. Lakini watu wa nyota ya Mizani, hutokea kuwa na kishimo cha shavu au kidevuni. Wana ung’avu wa sura na kuonekana kuwa wazuri au wa katikati, yaani wasio wazuri au wabaya. Ni watu wanaopenda sana kujikagua asubuhi kabla hawajatoka kwenye shughuli zao. Kubadili nguo kutwa mara mbili siyo ajabu kwao, mradi hali inawataka wafanye hivyo.

Lakini kwa kawaida watu nyota hii, hata wanapokuwa wamekasirika, nyuso zao hazioneshi kutisha. Mara nyingi sana wanakuwa na tabasamu pana au lenye kuvutia, ambalo si la kinafika. Sijapata nafasi ya kumkagua Kikwete kwenye mambo haya, lakini waliowahi kuwa naye karibu wanaweza kusema.

Akiwa nyumbani ambako hupapenda sana baada ya kazi, mtu wa nyota ya mizani hupenda kusikiliza muziki na kusoma. Ni mtu anayependa sana kubishana na familia yake kuhusu chochote kwa makusudi tu, ili kuchangamsha familia. Sijui kuhusu kikwete anapokuwa nyumbani, lakini hivi ndivyo anavyotakiwa kuwa.

Ni mtu mabaye pia anapokuwa nyumbani hupenda wageni na kuwakarimu ambapo pia huwa na mazungumzo mazuri, yenye kuvutia. Anapenda vile vile kuona watoto wake wakipata uhuru wa kufanya mambo yao. Hata hivyo kwa kutaka kwake kutoikera familia huweza kujikuta akiimiliki kama mali yake.

Kazini ni mtu ambaye, huchukua muda kuyaweka mambo sawa, kwani hataki kubahatisha, ni mwaminifu na ambaye anachangia zaidi mawazo kwenye mambo anayohusishwa kuliko wengine. Ni mwenye uwezo wa kujenga mtandao mzuri wa uhusiano na wengine kiofisi au na ofisi nyingine.

Mtu wa nyota ya Mizani hushauri majibu au suluhu ambazo wengine wanaweza kuziona za kushangaza awali, lakini ndizo sahihi mara nyingi. Anakauwa hatua moja mbele katika kuona suluhu. Katika kuamua huwa anaangalia hali halisi, sio visasi au sifa, ingawa anajisikia vizuri watu wakimhusudu.

Kwa kawaida mtu wa nyota ya mizani hatagemei kuishi kwa majungu au umbeya. Anapenda sana kila kitu kiende wazi na kufanyika bila lengo la kuumiza mwingine. Huyu ndiye atakayekuwa Raisi wa awamu ya nne hapa nchini, endapo Kikwete ndiye atakayepita.

Ni mtu anayeweza au kupenda kuwa kati kama msuluhishi. Kama nilivyosema, hupenda amani na anajua kusuluhisha. Hana kawaida ya kuwa mkatili au mjeuri, ingawa ana misimamo inayoweza kumfanya akaonekana kuwa hivyo.

Mizani ni watu ambao hupenda sana kujihusisha na masuala ya kisheria, siasa na mambo ya kimataifa. Bila shaka msomaji unaweza kudhani naandika haya kwa sababu Kikwete ni waziri wa mambo ya nje na ni mwanasiasa, hapana. Jaribu kutafuta vyanzo vingine ujifunze kuhusu upendeleo kitaaluma wa watu wa nyota ya Mizani.

Pengine sifa moja ya watu wa nyota ya Mizani, ambayo ni vema sana kuitaja ni ile ya kupenda kuwatumikia watu. Watu wa nyota hii hupenda kuona kila wanachofanya kinagusa watu na kuwafaidisha, ndipo wanaporidhika ndani mwao.

Mizani hawajali sana kuhusu fedha, yaani hawatoi jasho kiasi hicho. Wakiwa nayo wanaona ni sawa, lakini wakiona hawana haiwafanyi wakose amani. Lakini wanajua ubahili pia kwa namna fulani, kwani hupenda sana kuweka kwa ajili ya baadae.

Lakini huchukia sana kubishana kunakohusisha kelele badala ya mantiki. Huchukia pia ugoigoi hasa unaofanyika hadharani au unaowahusu watu wengi (jamii). Hii ikiwa na maana kwamba wanapenda kuona watu wakiwajibika.

Sifa zilizotajwa hapa kuwahusu watu wa nyota Mizani nyingi ni zile chanya. Nimeamua kuzitaja hizo kwa sababu baada ya kumsoma Kikwete kwenye maeneo mengi kimaisha nimebaini kwamba ameathiriwa vizuri (Positive) na nyota yake. Hii ina maana athari nzuri za nyota hii anazo.

Watu maarufu duniani waliokuwa au wenye nyota hii ya Mizani ni pamoja na Mahatma Gandhi (Kiongozi wa kidini na kijamii wa India) Bob Geldof (Mwanamuziki na mchangaishaji kusaidia wengine) Oscar Wilde (Mtunzi wa vitabu) na wengine wengi.

Shukrani za pekee zimwendee kaka Shabani Kaluse wa kibaraza cha Utambuzi na Kujitambua kwa kufanikisha kupatikana kwa kumbukumbu hii.

Sunday, May 2, 2010

UCHAWI DHANA INAYOSUMBUA MAISHA YA KAWAIDA YA BINADAMU

Mganga akipiga Ramli
Kuna maelezo mengi sana ya uchawi. Lakini uchawi ambao umekuja kujulikana duniani kwa jinsi dunia yenyewe ilivyo,umekuwa ukibadilika kimwelekeo lakini kimsingi sayansi hii ambayo kwa miaka mingi hufundishwa kwa siri na wanaojua kwa wanaotaka kuijua na wakati mwingine kurithisha, ni ada ya wanadamu wengi hasa katika Bara la Afrika.

Wale wasomi hukataa na kukana uwapo wake, wanaikataa dhana yenyewe na wanasema kwamba si kitu kujadili na mgeuko wake ni fikra za dini tulizonazo za Kiislamu na Kikristo ambazo zinatambua uwapo wake na kusema ni kazi ya shetani na matumizi mabaya ya maarifa ambayo ni nadra kila mtu kuyajua.

Unaweza kujua vitu au kitu kinachoitwa uchawi kutokana na mambo kadhaa hasa yaliyoandikwa au kufanyiwa masimulizi katika vitabu mbalimbali vikiwamo vya Kurani na Biblia. Kila mwaka wenzetu wa Haiti,vitukuu na vilembwe vya waliofikishwa utumwani hufanya tamasha kubwa la wachawi, wao wana dini yao ambayo ni ya kuabudu kitu wanachoita voodoo.

Watu hawa wanachofanya kwa wengine ni uchawi lakini kwao ni imani kali ya kujisalimisha kwa roho mbalimbali zisizoonekana ambazo ndizo wanazodai kuwatawala. Nadharia na suala zima la uchawi limezungumziwa na kujadiliwa tena na tena na watu mbalimbali na kwa namna mbalimbali. Lakini taabu kubwa ni tafsiri ya uchawi.

Hivi unawezaje kuuzungumzia uchawi ukasahau wanga na uganga, upo wakati uchawi , uganga na wanga huwa ni kitu kimoja kwa wengi wetu. Uchawi umewekwa katika dhana kwamba watumiaji na waathirika ni washenzi lakini kama utakuwa umesikiliza gumzo la Ng'wanamalundi ipo tafsiri ndani ya waungwana kuhusiana na shauri hili na kusema kwamba uchawi unawahusu watu washenzi, kidogo inapoteza ukweli wa mambo.

Katika filamu ya Ng'wanamalundi, mchawi aliyewakilisha kundi la wachawi alisema yale ni maarifa na ufundi wa kufanya mambo, sasa kama washenzi wanayapata maarifa haya sijui inakuwaje hasa. Lakini tafsiri ya karibu kabisa ya watu kuhusu uchawi na hata katika makamusi yetu ni matumizi mabaya ya maarifa aliyonayo mtu kudhuru mtu mwingine au mali zake. Kamusi ya Kiswahili sanifu inasema kwamba uchawi ni ufundi wa kutumia dawa, aghalabu mitishamba na vitabu maalumu vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe.

Katika hili ni wazi siri ndio jawabu la maana la maana ya uchawi , ufundi wa kuleta madhara. Mwanga kwa upande wake ni mcheza mahepe afanyaye mazingaombwe ya kichawi usiku. Ni tatizo sana kuzungumzia uchawi kama sihiri lakini shauri la kusema watu washenzi yaani wasiostaarabika ni kasheshe kubwa kwani wapo wachawi wanaoendelea na matajiri wakubwa wakiabudu uchawi kama chanzo kikuu cha utajiri wao, sasa nini hasa kipimo cha uchawi? Uchawi huu ambao huathiri viumbe kuna wakati hutumika kwa manufaa makubwa, ikiwa ni pamoja na kuzuia uharibifu mkubwa wa madhara ya uchawi katika jamii kwa kuwapo na mtu anayedhibiti wachawi wadogo na kuwaumbua.

Zipo nadharia zinazozungumza shauri zima la uchawi na Profesa Haward Safari katika mada yake ya uchawi katika Riwaya za Kiswahili mwaka 1993, alizungumzia shauri zima la uchawi na ushahidi wake. Alikuwa anazungumza katika mkeka mkubwa na waandishi wa vitabu, UWAVITA, na mfano wake wa bomu na nyutroni unaweza kukuweka hoi.

Ni kweli kuwa utaalamu wa kutengeneza bomu hili ni siri kubwa na wataalamu wake wanalindwa sana, kwa hiyo kama shauri hili la ufundi na usiri ni uchawi basi nyutroni ni uchawi na umetengenezwa kwa minajili ya kudhuru binadamu. Imani za kiuchawi ambazo zimekumba nchi yetu kwa kasi, ipo pia katika Bara la Afrika na Ulaya ambako ndiko inakoaminika imeanzia katika karne za kati.

Hapa nchini vipo vitabu vingi vinazungumzia dhana hiyo katika mifumo mbalimbali ingawa vinavyoeleza kwa lugha ya kukua sana ni kama Mirathi ya Hatari kwa upande wa hadithi za kubuni, hadithi za dini hasa hadithi ya taaluma ya uchawi , Maalim Kisisina na ile ya Mussa na Wachawi wa Farao katika Biblia.

Katika simulizi la Maalim Kisisina, inaelezwa kulizuka matatizo makubwa wakati wa kunyang'anyana kitabu cha uchawi kati ya Jibril na maalim huyo na mwishoni Jibril alimwachia maalim huyo kitabu na ndio uchawi uliopo sasa duniani. Hadithi ya maalim huyu ipo katika Kurani na Biblia, kwa namna yake imezungumzia shauri la Musa na wachawi wa Farao ambao nao waliweza kugeuza fimbo zao kuwa kama nyoka kwa jinsi Musa alivyoweza. Kama kwa Jibril, Musa naye alionyesha ukuu wa uchawi dhidi ya shauri la Mungu na Mungu kuonekana kuwa mkubwa wa yote, fimbo ya Musa iliwalamba nyoka wale wa Farao.

Mashauri ya uchawi yapo hata Ulaya. Nchi kama Uingereza na Ujerumani ndizo zinazoongozwa kwa masimulizi ya uchawi kwa kuungama kwa wahusika. Kimsingi uchawi ni sanaa ambayo ipo katika kila mahali na ina vitisho vikubwa.

Siku za karibuni kumezuka mganga anayejulikana kwa jina la Manyaunyau ambaye anatoa vitu vinavyoitwa vya kichawi na watu wanashukuru kwa kufanyiwa hivyo. Watu katika hekaheka hizo wanaokumbwa na mikasa ya kunaswa katika anga za mganga Manyaunyau, wanazungumzia ndege zao wanazosafiria nyingine zikiwa na uwezo wa kubeba hadi abiria 16 (sawa na Cessna), kitu kinachoitwa mwanga chenye jicho moja kama kilichodaiwa kudakwa huko Kimara King'ongo ambacho kilifanyiwa hila ya kunaswa.

Si Kimara tu maeneo mengi ya Dar es Salaam yana matatizo hayo kukiwa na historia ya kitaifa ya uganga na ulozi. Mathalani watu wengi hawatasahau Mandondo wa Korogwe, Tekelo wa Dar es salaam, Kabwere wa Tanga, hao walikuwa waganga maarufu wa kufichua wachawi bila kumsahau mganga Kalembwana wa Malinyi.

Katika mtafaruku huo kuna mafuvu, vyungu vya kupikia nyama za watu, mikono ya biashara ya watu waliokufa ilipatikana. Kuna sababu nyingi za uchawi lakini nyingi ni za kiuchumi zaidi hasa kupata msukule, mifugo, mavuno na kimantiki majina haya ya msukule, ndondocha na kizuu yanaashiria mambo yaliyopo katika jamii na yote haya ni mashauri ya kiuchumi. Kuna mauaji yanafanyika katika Nyanda za Juu na Kanda ya Ziwa, siri kubwa ni uchumi watu wanataka kupatiwa utajiri kwa kuchanganya dawa na sehemu za mtu aliyeuawa.

Maiti zinazokatwa sehemu za siri zinadaiwa kufanywa hivyo kuvutia biashara, kwa hiyo shauri la kiuchumi husababisha kukomaa kwa imani hizi za kishirikina. Sifa na ujasiri ni sababu nyingine ya kichawi huku starehe ikiwa ni ya mwisho.

Yapo maelezo kwamba wachawi wanatumia uchawi kuwafanyia fidhuli watu, kula nyama zao, kucheza uchi usiku na watu huwapora wake wenzao kwa kuthubutu kuua waume zao. Uchawi ni sehemu ya utamaduni na inaonekana wazi uchawi hustawi zaidi katika umasikini.

Kinjeketile alitumia uchawi kuhamasisha watu kupambana na Wakoloni je kwanini leo wachawi wasitumie kuleta maendeleo kwa jamii? Hii taaluma yao ya kuingia maeneo bila kujulikana, kuruka na taaluma nyingine nyingi walizonazo, ni kwa nini wasiwafundishe watu bila kificho?

Chanzo hiki hapa:
http://www.habarileo.co.tz/biasharaFedha/index.php?id=10036

Saturday, May 1, 2010

TAFAKARI YA LEO: JE, SISI TUNAOMBA?

Hata Yesu pia aliomba!

Tafakari ya leo, ningependa kuzungumzia kuhusu maombi na nguvu ya maombi.
Hebu tusome katika Mathayo 7: 7-10

"Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye hufunguliwa.
Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? Au akiomba samaki atampa nyoka?"

Kuna watu ambao hawajui kuomba na hawajawahi kuomba kabisa katika maisha yao. Unaweza kushangaa kuwa miongoni mwa watu hao wapo pia wakristo.

Kuomba maana yake ni nini?

Kuomba ni kumsogelea mungu na kumweleza shida zako, pale tunapopambana na majaribu au dhiki na shida ni wajibu wetu kumsogelea mungu na kumweleza shida zetu.

Yesu anaposema 'Ombeni nanyi mtapewa;' alimaanisha kwamba huwezi kupata kile unachokitaka bila kuomba. Kwa mfano unaweza kuwa na shida ya pesa je unadhani yupo mtu mahali fulani ataota tu kuwa una shida ya pesa na kukuletea bila kuomba? Haiwezekani ni lazima uombe na ndipo utakapo pewa. Inawezekana ukamuomba mtu moja kwa moja na akakupa pesa au kupitia maombi yako kwa mungu akatokea mtu akajua shida yako na kukuletea pesa kwa namna ya kushangaza kidogo. Hii ina maana kwamba haiwezakani ukapata kile unachohitaji bila kuomba.

Na aliposema ‘tafuteni nanyi mtaona;’ Je alikuwa na maana gani?
Labda nikuulize wewe unayesoma hapa, hivi inawezekana ukaona kitu unachokitafuta bila kukitafuta kitu hicho? Hiyo haiwezekani , kwanza ni lazima ujue unatafuta nini , halafu pia ujue kitu hicho kinapatikana wapi na ndipo uelekeze macho yako huko katika kukitafuta kitu hicho.

Yesu anaendelea kusema ‘bisheni nanyi mtafunguliwa;’ akimaanisha kwamba kuomba ni mpaka uende kwa muhusika nakubisha hodi na ndipo utakapofunguliwa. Kwani kubisha maana yake ni kuusogelea mlango na kubisha hodi na ndipo ufunguliwe mlango.
Huwezi kubisha hodi ukiwa mbali inabidi uukaribie mlango na ndipo ubishe. Je ni mlango gani huo? Ni kumsogelea mungu kwa sala na maombi, huku tukirutubisha sala zetu kwa matendo mema, na ndipo sala zetu na maombi zaitakapokuwa na nguvu

Na ndio maana akazidi kusherehesha kwa kuwaambia wanafunzi wake,

‘kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye hufunguliwa.
Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? Au akiomba samaki atampa nyoka?’

Ni kwamba, sisi huwa tunapokea kile tunachoomba. Hata siku moja Mungu hawezi kukupa kile ambacho hukuomba. Na ndio maana kuna msemo mmoja usemao ‘utavuna kile ulichopanda’

Katika Mathayo 6: 26, Yesu alisema:
Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?

Hapa Yesu anakumbusha kwamba, ikiwa Ndege wa angani hawavuni na wala hawakusanyi lakini Mungu ameweza kuwalisha seuze sisi wanadamu ambao ni bora kuliko hao ndege.

Sisi tumejaaliwa vipawa vyote. Tumepewa akili ya kutuwezesha kufikiri na kupambanua, tumepewa uwezo wa kubuni na kuumba vitu mbalimbali, mfano ndege, magari, majengo marefu. Karibu kila kitu kilichopo katika uso huu wa dunia ni matokeo ya kufikiri kwa wanaadamu.

Lakini hata hao ndege warukao nao sio kwamba wanapewa kila kitu watakacho, bali inategemeana na mazingira waliyopo, haiwezekani ndege walioko katika maeneo ya panapolimwa mpunga akatamani kula mtama wataupata wapi, hiyo itawalazimu waruke maili nyingi kutafuta mahali palipooteshwa mtama ili kukidhi kiu yao.

Na hata sisi kila tunapoomba tunaangalia mazingira tuliyo nayo. Kwa mfano unaomba kupata pesa, sawa lakini je unakipawa cha thamani gani cha kubadlishana na pesa.
Mungu hatoi pesa bali anatoa njia mbadala ya kupata pesa.

Tunapojiwekea malengo makubwa, ni lazima tujue pia tutafikaje huko, kwa kuwa safari ya kuelekea huko pia yaweza kuwa ndefu. Kuna mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema, “Ukitaka kuung’oa mlima mrefu, basi anza kwa kuondoa mawe madogo madogo”

Lakini pia ikumbukwe kwamba haihitaji kuomba kwa sauti au kutamka kwa vinywa vyetu ili jambo liwe, hata kufikiri kwetu pia ni namna mojawapo ya kuomba,

Katika Mathayo: 6: 7-8, Yesu anawaambia wanafunzi wake:
“Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba.”

Hii ina maana gani?
Ina maana kwamba Mungu anafahamu lile lililo katika mioyo yetu, kama tunafikiri katika maanguko basi tutaishia kuanguka na hatutofanikiwa kamwe, lakini kama tunafikiri katika kumudu hakika tutamudu, kwa kuwa sisi wenyewe ndio mainjinia wa kile tulicho nacho leo.

Kamala anazungumzia sana juu ya tahajudi, (Meditation) hii ni njia mojawapo ya namna ya kuratibui kile kinachoingia ndani yetu, kwa kufanya tahajudi tunakuwa na uwezo wa kuwa karibu na mungu nakumweleza shida zetu.

Niliwahi kuzungumzia juu ya imani huko nyuma, lakini pia ni lazima ifahamike kuwa imani bila kuomba ni kazi bure.
Yatupasa kuomba kwanza na ndipo imani inafuata.

Tukutane Jumamosi ijayo………………