Wednesday, November 30, 2011

WANAPOJIREMBA KUPITA KIASI INA MAANA GANI




Siku hizi, kuna ugumu wakati mwingine, kujua kama mtu ni mwanamke au ni mwanaume. Vijana na hata watu wazima wengi wanaume hujipamba sana kwa kutumia vipodozi, ambavyo kwa kawaida, vimekuwa vikitumiwa na wanawake. Kuna wanaume wanaopaka nyuso zao dawa za kung’arisha na kupambana kabisa na ndevu.


Hawa ukiwatazama nyuso zao ni kama za wanawake, kwani mwanaume mwenye uso mororo sana huonekana kama mwanamke kwa kiasi cha kutosha. Kuna wanaume wanaovaa hereni, bila hata kujua wazivae kwa namna gani. Uvaaji wa hereni kwa wanaume, ambapo inasemekana ulianzia kule Marekani, ulikuwa ukifanywa kwa sababu maalum na kwa namna maalum.


Kwa mfano kuna waliokuwa, au wanaovaa ili kuonesha upendeleo wao kimapenzi (kwa mfano ushoga) na wengine kwa sababu mbalimbali.Kwa kawaida mwanaume anapotoga sikio moja tu, hasa la upande wa kulia na kulivisha hereni, inamaanisha kwamba, mwanaume huyo ni shoga! Kwabahati mbaya hapa kwetu kuna vijana ambao hutoga sikio moja la kulia na bado wanaamini kwamba, wako salama. Ukweli ni kwamba siku akikutana na raia wa Marekani wanaotafuta mashoga, hawatasita kumwita na kumtongoza.


Ndio maana yake, kwani nyie mlidhani vipi?Kwa kawaida wanaume wamekuwa wakikataa kuvaa mapambo na kujipodoa kama wanawake katika kuonesha kwamba, mwili wao hauhitaji vitu hivyo kwani ni mwili wa kazi hususan za nguvu na hivyo mapambo hayawezi kuwa na maana kwao. Ndio maana najiuliza kujipodoa na kujipamba huku kwa wanaume na kuvaa hereni na makorokoro mengine yanaashiria jambo gani?




Friday, September 30, 2011

MABALAA HUMUANDAMA MTOTO WA KIKE TANGU AKIWA TUMBONI………!






Tatizo hili hufahamika kama Female Infanticide, yaani mauaji ya kukusudia yanayofanywa kwa mtoto wa kike. Achilia mbali kile kitendo cha mtoto kuuawa muda mfupi tu baada ya kuzaliwa, utelekezwaji wa mtoto wa kike mara tu anapozaliwa na kutoa mimba baada ya ugunduzi kwamba, ni mtoto wa kike, zote ni njia za kumuondoa mtoto wa kike duniani. Tatizo hili liko katika jamii zote zinazomchukulia mtoto wa kike kama balaa na yule wa kiume kama Baraka kwa familia.


Kwa hapa nchini mtoto wa kike huuawa kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Watoto wa kike hudharauliwa na kuachwa linapokuja swala la elimu katika familia. Ukichunguza hata wewe utabaini kwamba, katika familia nyingi, ambapo watoto wa kiume wamepata elimu bora, watoto wa kike katika familia hizo wamepuuzwa na hata kutopewa kabisa elimu.


Watoto wa kike, haswa wale wanaozaliwa nje ya ndoa wametelekezwa kirahisi, wamekataliwa na baba zao kirahisi, ukilinganisha na watoto wa kiume. Idadi ya watoto wa kike wanaokufa kutokana na kutelekezwa na kukataliwa na baba zao ni kubwa kuliko ya watoto wa kiume. Hata zile kesi nyingi za watoto kukataliwa na baba zao zinahusisha watoto wa kike zaidi.


Ni jambo la kushangaza kwamba ndoa ambayo ina watoto wa kike watupu hutazamwa kwa bezo na dharau ukilinganisha na ile yenye watoto wa kiume watupu. Hata wale wanawake wanaozaa watoto wa kike watupu hujihisi vibaya na kuamini kwamba walistahili kuzaa watoto wa kiume pia.


Kwa maeneo ua vijijini na katika familia masikini, watoto wa kike hutazamwa kama, ‘biashara ya kesho’ ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu. Na ndio maana mtoto wa kike anaposhindwa kuolewa huanza kuonekana kama mzigo usio na thamani, na hata kuzongwa hutokea.


Ili kujinasua na tatizo hili, msichana huenda kwa mwanaume yeyote kama kwa kujilazimisha. Kila mtu anajua kuhusu wazazi hapa nchini, ambao wamekuwa wakiwalazimisha binti zao kurudi kwenye ndoa za mateso kwa hofu ya kurejesha mahari. Kinachotokea ni binti hao kuuawa na waume zao. Ni wazi hii ni njia ya makusudi ya kuwapunguza wanawake, bila kujali mtu ataieleza vipi……………….


Chanzo........Jamii Forum


Monday, September 5, 2011

MCHUMBA ANGU YUKO FINLAND!

Naelekea Uzeeni sasa!




Ni miaka 16 sasa tangu nifahamiane naye, alikuwa ndio kwanza amemaliza kozi yake ya uhasibu na kuajiria katika ubalozi wa mmojawapo ya nchi za Ulaya hapa nchini.


Alipoanza kujitegemea, alipata nyumba iliyoko jirani na nyumbani kwetu, na huo ukawa ndio mwanzo wa kufahamiana naye. Alikuwa akijiheshimu sana na hakupenda kujichanganya na watu. Alitumia muda wake mwingi nyumbani kwake na kama akiamua kutoka mara nyingi alipenda kuwatembelea ndugu zake a marafiki zake waishio maeneo ya mbali.


Nilibahatika kufahamiana naye wakati fulani ilipotokea shida ya maji, na kwa kuwa, nyumbani kwetu kulikuwa na kisima, alikuja kuomba msaada wa maji na huo ukawa ndio mwanzo wa kufahamiana.


Naam, urafiki wetu ulimea na kukua, kiasi kwamba tulikuwa tukitembeleana mara kwa mara, alitokea kufahamiana na wazazi wangu pia na walimkubali sana, kutokana na jinsi alivyokuwa akijiheshimu.


Jambo moja lililonishangaza, ni kwamba sikuwahi kumsikia akizungumzia juu ya mahusiano yake, nilishikwa na udadisi na siku moja nikamuuliza kma anaye mchumba. Alinijulisha kuwa mchumba ake yuko Finland kwa masomo, nilimdadisi zaidi kama yuko huko kwa muda gani, akanijibu kuwa ni miaka miwili sasa. Alinijulisha kuwa mchumba ake huyo anasoma kule na itamchukua miaka 3 hadi kumaliza masomo yake na ndipo atarejea nchini na kuungana naye.


Ukweli ni kwamba rafiki yangu huyu alikuwa akifuatwa na wanaume wengi tu tena wa kutosha wakitaka kuwa na uhusiano naye, nadhani ni kwa sababu alikuwa ni mrembo sana, lakini alikuwa akiwakataa kwa maelezo kwamba, anaye mchumba tayari ambaye yuko nje ya nchi kwa masomo.


Nilimuheshimu sana kwa msimamo wake. Mwaka uliofuata binti yule alihama katika numba ile na kuhamia maeneo ya Sinza. Nilipoteana naye kwa takriban miaka 16. Ni hivi karibuni nimebahatika kukutana naye, alionekana dhahiri kuwa umri umekwenda.


Alinikaribisha nyumbani kwake maeneo ya Kimara, alinijulisha kuwa amebahatika kujenga nyumba yake mwenyewe. Wiki iliyofuata nilimtembelea nyumbani kwake. Alikuwa amejenga nyumba nzuri na alikuwa ameizungushia ukuta na kuweka geti. Alinikaribisha sebuleni kwake. Alinitambulisha kwa mdogo wake wa kike aliyekuwa akiishi naye ambaye alikuwa akisoma Chuo Kikuu Dodoma, na pia kwa msichana wake wa kazi.


Nilishikwa na udadisi wa kutaka kujua alipo mume wake, na labda kama ana mtoto. Alicheka sana na kisha akanishika mkono na kunipeleka chumbani kwake. Alikuwa na chumba kikubwa chenye nafasi ya kutosha na pia kulikuwa na meza kubwa ambayo ilikuwa imepambwa vizuri na vifaa vya ofisini pamoja na lap top, kwa ajili ya kazi zake.


Aliniacha kwa muda ili niridhishe macho yangu, kisha akaanzisha mazungumzo.


Mwenzangu, alianza simulizi yake, …….. unadhani kipindi kile wakati nakwambia kuwa ninaye mchumba na yuko masomoni Finland ilikuwa ni kweli, la hasha, haikuwa kweli, bali nilikuwa nadanganya tu kwa sababu sikutaka kusumbuliwa na wanaume. Si unajua wanaume wa siku hizi wanapenda kuwachezea wanawake!, sasa mimi kwa kuliepuka hilo nikaona nitumie mbinu hiyo ili kuepuka usumbufu. Nilibaki mdomo wazi….


Basi bi dada………… aliendelea…….. nilipohama pale Mikocheni, na kuhamia Sinza, niliendelea na msimamo mwangu, sikuwapa wanaume nafasi, nilikuwa na malengo yangu na nilitaka nihakikishe yanatimia.


Ni malengo gani hayo…… nilimdadisi……


Kwanza, nilitaka nijenge nyumba yangu mwenyewe, na pia ninunue gari na kuanzisha biashara zangu na sasa nimetimiza malengo yangu, sasa tatizo linakuja.


Tatizo gani tena………..nilimuuliza.


Sitongozwi na wanaume……… na wananiogopa!..............haki ya Mungu Koero, yaani nina wakati mgumu kweli.


Mh! Niliguna…… wewe unadhani tatizo ni nini? Nilimuuliza,


Sijui sababu, lakini, naona kama vile hakuna anayevutiwa na mimi, najitahidi kuongea na wanaume lakini tunaishia kupiga stori tu, na wengine wananitongoza lakini ni waume za watu. Mwenzio naogopa kweli, mpaka nimejenga wasiwasi kuwa labda nimelogwa.


Mh……….Nilishusha pumzi……….Vumilia dada Jane, utampata atakayekufaa, muombe sana Mungu, atakupa mume aliye mwema, nilimpa moyo.


Mh, Koero, umri huu? Unajua mwakani natimiza miaka 39, mwenzio nazeheka hivyo, atanioa nani…. Nimekuwa nikibadilisha makanisa kama nini, katika kuombewa na kote huko naona maombi yangu hayajibiwi.


Marafiki zangu karibu wote wameolewa na wanaishi na waume zao, mimi tu, sijui nina mkosi gani…. Nilimuona Dhahiri machozi yakimlengalenga….


Nilimpa moyo na kumshauri asikate tamaa. Nilimwambia arudi kwenye kanisa lake la awali na ajiunge na kwaya ikiwezekana ashiriki kwenye kamati mbalimbali za kanisa na zitakazomfanya akutane na watu mbalimbali. Nilimwonya awe makini sana na wanaume walaghai kwani wapo wengine wanawezakutumia mwanya huo kummimbisha na kumtelekeza.


Alikubaliana na mimi na tukamaliza mazungumzo yetu kisha nikaondoka kurejea nyumbani…….. mweh dunia hii……. Habari ya dada Jane si kwamba tu ilinishangaza, bali pia ilinisikitisha. Yaani zaidi ya miaka 16 aliishi kwa kusema uongo ili kuwakwepa wanaume! Alichokuwa akikiogopa kwa wanaume ni kitu gani hasa?


Nilibaki nikijiuliza maswali chungu mzima na sikupata majibu. Ndio maana mie nasema wazi, jamaniee sijaolewa na wala sina mchumba Mbeya, Lundu Nyasa, Marekani wala Ulaya, niko Single, ready to mingle….leteni maombi na sifa zenu mtajibiwa…………LOL


Friday, September 2, 2011

WANAUME BWANA, HIVI MKIONA UCHI WA MWANAMKE MNAPATA NINI?

Wanaume wengine hata wakiona hivi huchanganyikiwa!



Kuna wakati huko Berlin, nchini Ujerumani, kulikuwa na unesho ambapo wanawake walikuwa wakionesha maungo yao kwa malipo. Wanawake hao walikuwa wakionesha maungo hayo kwa wanaume ambao wanaamini kwamba, kuona sehemu uchi wa mwanamke ndicho kilichowaleta hapa duniani.


Hebu sikia ujinga huo zaidi. Waandaaji wa onesho hilo ambalo lilihusisha wanawake wapatao 100 wa umri wa miaka 19 hadi 65 walilazimika kuwaita Polisi ili kudhibiti midume iliyokuwa ikifanya fujo wakati wa kukata tiketi kila mmoja akitaka awe wa kwanza kuingia kwenye onesho hilo.


Kila mmoja alikuwa akitaka awahi yeye kuona sehemu za siri ambazo bila shaka mkewe na watu wengine wa jinsia ya kike wanaomzunguka wanazo!


Mwandaaji wa onesho hilo, Vanessa Beecroft, ambaye ndiye mgunduzi wa njia hii ya kujipatia fedha kirahisi kutoka kwa wanaume hao wasio na haya, hufanya maonesho haya kwa jina la VB55 kwa nyakati na miji tofauti Ulaya.


Msije mkashangaa siku akija na huku Afrika kujichotea mamilioni ya dola, au akajitokeza mjanja mwingine huku Afrika na kuanzisha hayo maonesho, naamini wanaume watauana wallahi.

Monday, August 29, 2011

HATIMAYE MTUHUMIWA AJISALIMISHA!!!!



Haya jamani kilio cheni nimekisikia, jana ndio nimefika Dar nikitokea Tanga, Nilikuwa Tanga, kwa dada yangu ambaye alifanikiwa kuongeza idadi ya watu hapa duniani mwezi uliopita. kwa kuwa hakuwa na mtu wa kumsaidia, nililazimika kwenda kule kumpikia uji na mtori.

Nimerudi na tupo pamoja.


Monday, June 20, 2011

NIMEULIZWA TENA HILI SWALI: KWA NINI NILIAMUA KUITA BLOG YANGU VUKANI?

Vukani


Blog hii itakuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo. Pamoja na yote naamini pia italeta changamoto na migongano ya mawazo, ndio maana nikasema VUKANI.




KWA NINI NILIAMUA KUIITA BLOG YANGU, VUKANI?


Neno VUKANI nimelitohowa kutoka katika lugha ya mama yangu ya kipare.
Neno hili lina maana ya AMKENI, nadhani kaka Mkodo Kitururu atakuwa anafahamu vizuri kwa kuwa ni lugha yake.

Nakumbuka wakati fulani nilikwenda likizo kijijini huko upareni kuwasalimia bibi na babu yangu wanaomzaa mama yangu, basi kila siku asubuhi bibi alikuwa na kawaida ya kutuamsha ili tusali pamoja na alikuwa akitumia neno Vukani. Nilipouliza maana yake nikaambiwa ni Amkeni au kwa msisitizo wa kiingereza WAKE UP. Basi kuanzia siku hiyo nikatokea kulipenda sana hili neno, sijui ni kwa nini lakini lilikuwa linanihamasisha sana kuamka kifikra badala ya kuamka asubuhi tu.

Wakati nilipokuwa nafungua Blog yangu nilikuwa tayari nimeshachagua jina hili, na cha kushangaza nilipoliingiza kwenye mtandao nikagundua kwamba neno hili linatumiwa na makabila mawili ya Ki Zulu na Ki-Xhosa ya nchini Afrika ya Kusini, likiwa na maana moja, yaani Amkeni.

Si hivyo tu bali pia lipo gazeti moja maarufu nchini humo, linaloitwa Vukani.

Kwa maelezo zaidi bofya hapa.

Amkeni nionavyo mimi sio kuamka kutoka usingizini tu bali ni kuamka kifikra na kuhoji kila tulichofundishwa au kuambiwa kama kina ukweli kiasi gani? Si hivyo tu bali pia ni kuamka na kuachana na ile tabia ya kufikiri kwa mazoea na kutenda kwa mazoea. Kila jambo unalolifanya ujue sababu ya kufanya hivyo, sio eti kwa sababu, mama, baba, bibi, babu, mjomba, shangazi, na jamii iliwahi kufanya hivyo.

Nakumbuka wakati fulani nilihudhuria semina ya mambo ya uongozi, basi yule mwezeshaji kutoka nchini Marekani alitutolea mfano mmoja wakati alipokuwa akitufundisha namna ya kuepuka kufanya mambo kwa mazoea.

Kisa chenyewe ni hiki:

Kulikuwa na mama mmoja alikuwa na tabia, kila akitaka kuoka samaki ni lazima amkate mkia kabla ya kumuweka kwenye kikaango, ndipo amuoke. Hata kama samaki mwenyewe ni mdogo.


Siku moja binti yake aliyekuwa na umri wa miaka 10 akamuuliza mama yake sababu ya kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka, mama yake akamjibu kuwa mama yake alikuwa na kawaida ya kufanya hivyo. Alipomuuliza kama aliwahi kumuuliza mama yake sababu ya kufanya hivyo, mama yake akajibu kwamba hakuwahi kuuliza.

Basi wakati fulani bibi yake alipokwenda kuwatembelea, kama bahati mama yake alikuwa akiandaa samaki ili amuoke kama ilivyo kawaida akamkata mkia, binti akaona huo ndio wakati muafaka wa kuujua ukweli maana bibi yupo. Ndipo akamuuliza sababu ya mama yake kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka.

Si mnaona watoto wa wenzetu walivyo wadadisi?

Bibi akamwambia akamuulize mama yake sababu ya kufanya hivyo, yule binti akamjibu bibi yake kwamba, mama yake alimwambia kuwa yeye yaani bibi, ndiye aliyemfundisha kukata mkia wa samakai kabla ya kumuoka. Yule bibi akafikiria kidogo, kisha akamjibu, kwamba alikuwa akikata mkia wa samaki kwa sababu kikaango chake kilikuwa ni kidogo, hivyo ili samaki aweze kuenea kwenye kikaango alikuwa analazimika kukata mkia.

Yule binti akamwambia bibi yake, “Mbona sisi kikaango chetu ni kikubwa na isitoshe tunavyo vikaango vingi tu vya saizi tofauti tofauti, je kuna ulazima gani mama aendelee kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka?

Bibi akamjibu kwamba hakuna ulazima wowote.
Basi kuanzia siku hiyo yule mama akawa hakati tena mkia wa samaki.

Si mnaona jinsi mtoto huyu alivyokataa kulishwa kitu bila ya kijua sababu?
Naamini kwamba wote mtakubaliana na mimi kwamba sisi tumelelewa hivi, tunaambiwa tukate mikia ya samaki kabla ya kuwaoka na tunafuata, na wala hatuulizi sababu.

Kwa hiyo ninaposema VUKANI ninamaanisha AMKENI, ili muweze kuhoji baadhi ya mambo tunayofundishwa au kuambiwa ambayo hayana mantiki.


Monday, June 6, 2011

AKATUPA KILE KIATU!

Akakitupa hapa!




Alikuwa yuko Bar moja maarufu iliyoko maeneo ya Kinondoni hapa jijini Dar na hawara yake ambaye ndio nyumba yake ndogo pamoja na marafiki zake kadhaa wakikata maji (Pombe), Bwana Tesha (sio jina lake halisi) alikuwa na furaha siku hiyo kwani alikuwa amefanikiwa kupata tenda moja ya bajeti kubwa ambayo ilimhakikishia kupata faida ya kutosha.




Bwana Tesha anamiliki kampuni yake ya Ujenzi hapa jijini na alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini kwa muda mfupi tangu amalize masomo yake ya Chuo Kikuu pale Mlimani alimudu kujiajiri katika sekta ya ujenzi na kupata mafanikio makubwa katika sekta hiyo.



Akiwa bado anakata maji na marafiki zake pamoja na hawara yake alipigiwa simu na mkewe. Kwa kuwa kulikuwa na kelele za walevi katika Bar hiyo aliamua kwenda kupokelea simu ile ndani ya gari lake. Simu ile haikuwa na taarifa nzuri, alijulishwa na mkewe kuwa mama mkwe wake yaani mama wa mkewe amefariki ghafla kwa presha huko Moshi mkoani Kilimanjaro.


Alirudi kwenye meza aliyokuwa amekaa ma wenzie na kuwajulisha juu ya taarifa ile, wenzie walimpa pole na kumshauri arudi nyumbani ili kumfariji mkewe. Hata hivyo alilazimika kwanza kumpeleka hawara yake nyumbani kwake maeneo ya Mwenge ndipo aende nyumban kwake maeneo ya Mbezi ya Kimara.



Wakati huo hawara yake alikuwa amelewa chakari na alikuwa hajitambui, hivyo ilimlazimu kumbeba na kumuingiza ndani ya gari yake aina ya Toyota RAV 4. Aliondoka hadi kwa hawara, aliteremka na kufungua mlango wa nyumba kisha akambeba hawara yake ambaye alikuwa hajitambui hadi ndani na kumlaza kitandani. Kwa kuwa alikuwa na funguo za akiba, alifunga mlango na kuondoka zake kuwahi nyumbani kwake.



Alifika nyumbani kwake majira ya saa nne usiku, na kukuta baadhi ya ndugu zake na ndugu wa mkewe. Baada ya mashauriano, walikubaliana yeye na mkewe waondoke kesho alfajiri, kwa kuwa yeye hahitaji kuomba ruhusa kazini.


Baadhi ya ndugu zake na ndugu wa mkewe alipanga kuondoka baadae na mabasi baada ya kuomba ruhusa kazini kwao. Walifungasha haraka haraka usiku huo huo kisha wakalala. Ilipofika alifajiri ya saa kumi za usiku waliondoka kuelekea Moshi. Ndani ya gari walikuwa wanne, mwanae wa kwanza wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 12 alikaa kiti cha mbele, mkewe pamoja na mwanae mwingine wa pili wa kike aliyekuwa na miaka 7 walikaa kiti cha nyuma. Kwa kuwa bado walikuwa na usingizi, wote walilala, na kutokana na ufinyu wa nafasi mama aliweka miguu yake katikati ya viti vya mbele na kujiegemeza kwa nyuma akimuacha mwanae wa kike amlalie mapajani mwake.



Mzee Tesha aliendesha gari kwa tahadhari sana ili kuepuka ajali. Wakati kunapambazuka alikuwa amekaribia maeneo ya mto Wami, na alijisikia kubanwa haja ndogo. Alilazimika kusimama na kuteremka ili kuchimba dawa. Alimaliza kuchimba dawa na kurejea ndani ya gari, lakini kabla ya kuondoa gari akashangaa kuona kiatu kinachofanana na kile alichovaa hawara yake usiku wa jana kikiwa chini ya kiti cha mbele cha abiria. Bwana Tesha akashtuka, akajua kile ni kiatu cha hawara yake ambaye atakuwa amekiacha mle katika gari kwa kuwa alikuwa amelewa chakari. Akageuka na kumwangalia mkewe aliyekuwa amelala kiti cha nyuma.



Aliwakagua wote ili kutaka kujua kama wamelala, na alipohakikisha kuwa wote wamelala, alikichukua kile kiatu na kukitupilia mbali, kisha akaondoa gari, akiwa amefarijika kuwa kiatu kile hakijaonwa na mkewe ambaye wanaaminiana sana tangu waoane miaka kumi iliyopita.


Aliendesha gari kwa mwendo wa wastani na ilipofika saa nne asubuhi walikuwa wako Segera, walisimama pale ili kupata staftahi. Baada ya kupaki gari aliteremka na wanae wawili na kutangulia mghahawani na kumwacha mkewe nyuma akijiweka sawa kabla ya kuteremka ndani ya gari.



Akiwa ndani ya mghahawa mkewe alimpigia simu na kumtaka aende kwenye gari kuna dharura, alitoka mghahawani na kumfuata mkewe kule kwenye gari, ili kujua kulikoni. Alipofika, alishtuka kumkuta mkewe kashikilia kiatu kimoja kinachofanana na kile alichokuwa amevaa hawara yake usiku wa jana walipokuwa kule Bar, akajua siri imefichuka, lakini akawahi kuficha mshtuko wake, na kumuuliza mkewe, “Vipi kuna nini mke wangu?”


Mkewe akamwambia kuwa ameshangaa haoni kiatu chake kimoja. Bwana Tesha akajua kiatu kisichoonekana ni kile alichokitupa kule mto Wami. Lakini alikuwa mwerevu….




“Mke wangu ana uhakika ulivaa viatu vyote viwili?” Alimuuliza mkewe akiwa na mshangao.



“Mume wangu pamoja na kuwa nimefiwa na nina uchungu sana lakini sijapoteza fahamu zangu kiasi cha kujisahau na kuvaa kiatu kimoja.” Mkewe alimjibu kwa upole.


Bwana Tesha alijifaragua akijifanya anakitafuta kiatu cha mkewe kwa bidii hasa, baada ya kupekua sana alikuja na ushauri mwingine, ambapo alimshauri mkewe wanunue kandambili avae kwa muda kwa madai kuwa wakifika Moshi watakitafuta kwa umakini.



Mkewe alikubali, lakini bado alikuwa na mashaka kidogo juu ya tukio lile. Walinunua kandambili na baada ya kupata kiamsha kinywa waliondoka. Walipofika Korogwe, Bwana Tesha alisimama na kwenda dukani ambapo alimnunulia mkewe Viatu vingine kisha wakaondoka kuwahi Mazishi.




Baada ya kufika Moshi habari ya upotevu wa kiatu kimoja ilisimuliwa na cha kushangaza tukio lile likahusishwa na mambo ya kishirikiana sambamba na msiba ule. Na hiyo ndio ikawa ndio salama ya Bwana Tesha kuepukana na fedheha ile ya kutupa kiatu cha mkewe baada ya kukifananisha na kiatu cha hawara yake.



Wednesday, June 1, 2011

AKANIAMBIA NIKIZEEKA NA KUWA BIBI KIZEE NISIJE NIKAMUOMBA UGORO!

Ni jana majira ya jioni nikikatiza mitaa ya Msasani, nikakutana na mateja wako wachafu wamekaa kijiweni wakipiga soga. Mara akaijitokeza teja mmoja na kuanza kuniita kwa sauti ya mlegezo (sauti ya mlegezo ni voice tone inayotumiwa na mateja), “Oyaa sister eee..hebu nisubiri basi nikuulize” mie sikumjibu wala kugeuka, niliendelea kuchapa mwendo.



Oyaa sister unajifanya uso wa mbuzi sio (hata sikumwelewa ana maana gani), niliendelea kuchapa mwendo bila kugeuka, na mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kwa woga maana niliona dhahiri anaweza kunikaba, kwani nilipita vichochoroni.


Baada ya kuona simjibu wala kugeuka, akaanza kumwaga maneno ya kifedhuli…….


Unajifanya mzuuuri kumbe huna lolote, uzuri wenyewe uko wapi? Sana sana unatumia mgorogo tu, we nini bwana ….. unadhani tuna shobokea mademu sisi,…… shika time yako, huna lolote mshamba tu wewe……


Tena sikiliza…. Ukizeeka na kuwa bibi kizee usije ukaniomba ugoro, maana hamkawii nyie, ukizeeka na kimkongojo chako……(akainama kuonesha mfano wa bibi kizee na mkongojo) lazima utakuja tu …. Kisha akaanza kuigiza sauti ya bibi kizee na kusema, “Mzee naomba kaugoro hapo nitulize kiu yangu”


Sitakupa ng’oooo…….. Ishia huko………


Mie na watu waliokuwa karibu tulivunjika mbavu kwa kicheko, maana ilikuwa kama mchezo wa kuigiza vile.




Wednesday, May 25, 2011

NI MIAKA 26 SASA TANGU AZALIWE, LAKINI MIKASA, VISA NA VIJIMAMBO, VIMEENDELEA KUMTIA NGUVU.




Ilikuwa ni siku ya Jumamosi ya Sabato ya May 25, 1985, majira ya saa nne usiku ndipo binti huyu alipozaliwa. Alizaliwa akiwa na afya njema na uzito wa kuridhisha, ambapo siku iliyofuata mama wa binti huyu aliruhusiwa kutoka na kurejea nyumbani na kichanga chake.


Kalikuwa ni katoto kazuri ka kike ambako kalileta faraja katika familia ile ambayo tayari ilikuwa na watoto watatu wa kike na wawili wa kiume na hivyo kakawa kameongeza idadi ya watoto wa kike na kuwa wanne na kufanya idadi ya watoto katika familia hiyo kuwa na watoto sita.


Naambiwa kuwa binti huyu alikuwa na kipaji cha ajabu, hadi kiliwatisha wazazi wake, zile hatua za makuzi ya mtoto alizipitia lakini akiwa amewahi zaidi, kwa maana ya kuwahi kukaa, kusimama, kutembea na hata kuongea.


Akiwa na umri wa miaka miwili, tayari alikuwa amemudu kuwasha luninga na kubadilisha channel atakavyo, na si hivyo tu, alikuwa ni mdadisi na alikuwa ni mtoto anayependa kujifunza kila jambo.


Binti yule aliendelea kukua kwa umri na kimo huku akiwa na afya njema. Ni pale alipofikisha umri wa miaka mitano ndipo jambo lisilo la kawaida lilipomtokea binti huyu na kubadilisha kabisa historia ya maisha yake.


Inasimuliwa kuwa ilikuwa ni majira ya usiku ndipo binti huyu alipopatwa na homa kali sana, ambayo iliambatana na kile kinachoitwa degedege.


Kuumwa ghafla kwa binti yule kuliistua familia ile, na katika jitihada za kutaka kuokoa maisha yake alikimbizwa hospitali ya binafsi iliyopo jirani na pale kwao.


Alipofikishwa Hospitalini mama wa binti huyu alishauriwa na Daktari amkande na maji ya baridi ili kushusha joto la mwili ambalo lilikuwa limepanda kiwango cha kutisha. Daktari yule alitoa ushauri kuwa itakuwa ni jambo la hatari kuanza matibabu huku mgonjwa akiwa na joto kali kiasi kile.


Kwa kuwa Daktari alikuwa amemaliza zamu yake aliondoka nakuacha maagizo kwa Daktari na Muuguzi waliokuwa zamu akiwaelekeza hatua za kuchukua kulingana na maelekezo aliyoyaandika kwenye cheti.


Baada ya joto la mwili kupungua mama alimwita yule Muuguzi wa zamu na kumjulisha kuwa joto la mwil limepungua. Yule Muuguzi akiwa bado ana hali ya kuonesha kuwa katoka usingizini alisoma cheti na kisha akaenda kuchukua dawa.


Alirejea akiwa na vichupa vya dawa na sindano, na kumchoma sindano binti yule. Ile sindano ilisababisha binti kupoteza fahamu. Kuona hivyo alikimbia kumwita Daktari wa zamu.


Daktari wa zamu alipofika alimpima binti yule na kutoa maelekezo achomwe sindano nyingine haraka na kisha atundikiwe Drip. Maelekezo ya daktari yalifanyiwa kazi lakini binti yule hakuzinduka, ilibidi zifanyike Juhudi za kumhamishia Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ambapo alipelekwa moja kwa moja chumba maalum kwa wagonjwa mahututi (ICU). Alikaa kule kwa siku tano, na alipopata nafuu, akarudishwa kwenye wodi ya watoto na kuendelea na matibabu.



Binti aliendelea kupata nafuu, lakini kulikuja kugundulika kuwa amepatwa na tatizo lingine, nalo ni la kupoteza uwezo wa kusikia. Juhudi za Madaktari wa masikio kumtibu binti huyo zilishindikana, lakini mwishowe wakasema kuwa lile ni tatizo la muda tu, na limetokana na sindano ya kwinini aliyochomwa katika zahanati aliyotibiwa awali, hivyo ikiisha nguvu atarudisha uwezo wake wa kusikia.


Habari ile haikuwafurahisha wazazi wa binti, lakini wafanye nini, na limeshatokea. Walisubiri kwa taktiban mwaka mzima, lakini hapakuonekana dalili yoyote ya kupona wala kupata nafuu. Ni dhahiri sasa walizidi kupata wasiwasi, kwani binti yao kipenzi alikuwa hana uwezo wa kusikia na ule uchangamfu, udadisi, na utundu aliokuwa nao, ulitoweka. Hali hiyo iliwanyima usingizi.


Hawakukata tamaa, wakageukia kwenye maombi, lakini maombi yao hayakujibiwa haraka kama ambavyo watu wengi wangependa. Wakakata shauri kwenda nchini Afrika ya Kusini, kwa matibabu zaidi. Walipofika kule, Daktari aliyewapokea, alimfanyia binti vipimo na kwa kushirikiana na Madaktari wenzie walitoa pendekezo wamfanyie binti upasuaji, ili kurekebisha ile hali.


Lakini siku iliyofuata, ambapo ilikuwa afanyiwe vipimo zaidi kabla ya upasuaji, yule Daktari alibadilisha uamuzi na badala yake akatoa pendekezo binti anunuliwe vifaa vya kumuwezesha kusikia, (Hiring aid) halafu baada ya mwaka mmoja warudi kwa ajili ya vipimo zaidi.


Kwa kifupi walisema kuwa ni mapema mno kukimbilia upasuaji kwa kuwa waliamini kwamba kuna uwezekano mkubwa binti akapata uwezo wa kusikia baada ya dawa aliyochomwa kuisha nguvu.


Walirudi nchini, na kuendelea na maisha, na baada ya mwaka mmoja hali haikuonekana kutengemaa, waliporudi Afrika Kusini maelezo yalikuwa ni yaleyale. Waliambiwa warudi Tanzania na kama kutakuwa na tatizo basi waende Muhimbili, kwani tatizo la binti linaweza kutatuliwa hapo. Juhudi mbalimbali za kitabibu zimefanyika lakini bado hazijazaa matunda.


Hali hiyo imemfanya Binti huyo kuwa mbali na mawasiliano ya simu hususan za mkononi akitumia zaidi Ujumbe wa badala ya kuongea, kutokana na tatizo hilo. Mawasiliano mengine anayopendelea anapotaka kuwasiliana na ndugu jamaa, wanablog, wasomaji wa blog na marafiki ni kwa kutumia barua pepe, kwani hiyo imemjengea marafiki wengi na amekuwa akiwasiliana nao kiurahisi zaidi.


Leo hii ni miaka 26 kamili tangu alipozaliwa binti huyu, na ni miaka 21, tangu alipopatwa na tatizo hilo ambalo ki-ukweli bado linaaminika kuwa lilisababishwa na muuguzi ambaye alimchoma sindano ya kwinini, badala ya kumtundikia Drip, kama alivyoandikiwa na Daktari aliyempokea binti huyo.


Bado anawaza ni wangapi baada ya mkasa wake wamepata matatizo kama haya? Ni wangapi wamesababishiwa maumivu, ulemavu na hata kifo kwa maamuzi finyu ya kutofuata maelezo ya Madaktari?


Anawaza ni wauguzi ama Madaktari wangapi ambao wametenda makosa kama haya na kuonywa ama kuwajibishwa kwa namna yoyote ile ili matatizo wanayosababisha kwa jamii yasiwe kitu kinachotokea kila mara?


Anawaza ni wangapi ambao tofauti na yeye hawawezi kuendelea na masomo kwa kuwa hawawezi kupata HEARING AID kulingana na gharama zake? Na hivyo kushindwa kuonyesha vipaji vyao halisi kwa matumizi ya nchi na dunia?


ANAWAZA namna ambavyo mimi nawe tunaweza kuwa suluhisho la matatizo haya ambayo YANAUMIZA SANA. ..........


Hata hivyo hali hiyo haikumkatisha tamaa kwani alimudu kusoma katika shule mbalimbali za kawaida huku akitumia vifaa maalum vya kusikia, ambapo alimudu kufika hadi kidato cha sita. Binti huyu hakutaka kuendela na elimu ya juu, na badala yake aliamua kujiingiza katika biashara akiwa ni mjasiriamali mchanga lakini mwenye matarajio makubwa.


Si hivyo tu, bali pia amekuwa ni mwelimishaji katika tasnia ya Blog akiwa anamiliki Blog yake ambayo imekuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo, lakini pia pamoja na yote anaamini kuwa blog hiyo imeleta changamoto na migongano ya mawazo, jambo lililowa “amsha” wengi na ndio maana akaiita VUKANI.


Hata hivyo hawezi kujivunia hapo aliopofikia katika tasnia ya Blog bila kuwataja wanablog wote wenye kumiliki blog za kiswahili, wasomaji wa blog, wazazi wake, marafiki na wale ambao kwa njia moja ama nyingine walifanikisha uwepo wa blog hiyo ya VUKANI. Hata hivyo HASITI kuwataja Kaka Markus Mpangala, kaka Mubelwa Bandio, na Dada Yasinta Ngonyani, hawa amekuwa akiwasumbua sana pale anapohitaji ushauri kabla ya kuweka bandiko katika kibaraza chake.


Asingependa kuwasahau Mzee wa Mataranyirato Chacha o'Wambura, Ngw'anambiti, Kamala Lutatinisibwa, Fadhy Mtanga, Christian Bwaya, Simon Mkodo Kitururu, Godwin Meghji, Evarist Chahali, Dada Subi, Faith Sabrina Hilary, Shaban Kaluse, Mwanamke wa Shoka Mija Sayi, Mariam Yazawa, Emuthree, Ramadhan Msangi, Salehe Msanda, Ma-Annonymacy............. na wengineo wengi, ambao kwa kweli wamekuwa mstari wa mbele katika kuifanya blog hiyo ya VUKANI kufikia hapo ilipo


WAKATABAHU


NI MIMI KOERO JAPHETI MKUNDI

Monday, May 16, 2011

HARUSI YA WAPEMBA.

Mbwembwe za nini? Kimya kimya tu Mwali akaondoka!



Siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, wakati niko nyumbani majira ya mchana akaja jirani yetu mmoja Mpemba akitaka kumuona baba. Kwa bahati mbaya baba alikuwa hajarudi kutoka katika shughuli zake za kuganga njaa, hivyo akamuachia mama ujumbe kuwa alikuja kutujuza kwamba mdogo wake anaolewa siku hiyo ya Ijumaa majira ya usiku baada ya swala ya Waislamu ya Insha. Alituomba tujumuike nao itakapofika hiyo saa mbili usiku ili kufanikisha shughuli hiyo ya ndoa.


Mie nilishangaa kidogo kwa kuwa tangu asubuhi pale kwa majirani zetu ambao nyumba yao iko mkabala na ya kwetu, kulikuwa kuko swari kabisa na hapakuonesha dalili yoyote kuwa kuna pilika pilika za kufungwa ndoa au Harusi. Kwa kawaida nafahamu kuwa nyumba yenye maandalizi ya Kufungwa ndoa huwa inakuwa bize na pilikapilika za hapa na pale hasa kwa zile shughuli zinazofanyikia nyumbani, kwa kawaida huwa ni lazima kunakuwa na shughuli mbalimbali zitakazowafanya hata majirani wajue kuwa kuna jambo hapo kwa wenzetu, lakini mweh! Kulikuwa kuko shwari tu kutwa nzima.


Ni kweli majira ya saa mbili hivi tukaona majamvi yanatandikwa kibarazani, na sie kama majirani, yaani mie, mama na baba tukaenda kuungana nao. Mie na mama tuliingia moja kwa moja sebuleni ambapo tulikuta pametandikwa majamvi na akina mama kadhaa wakiwemo baadhi ya majirani zetu walikuwa wamekaa na baba alifikia pale kibarazani ambapo aliungana na wazee wengine ambao walikuwa wamekaa pale nje. Kwa kawaida waislamu wanawake hawachangamani na na wanaume kwenye shuguli zao, na ni lazima mjitande ushungi. Waswahili wanasema ukienda kwa waroma basi vaa kama waroma, nasi yaani mie na mama tulijitanda ushungi.


Baada ya muda kidogo, tukasikia watu wakisalimiana huko nje, na mie ili nisipitwe, maana napenda sana kupekua mambo, nikajisogeza karibu na mlango, ili nione yatakayojiri hapo nje. Nilipata sehemu nzuri ambapo niliweza kuwaona watu waliokaa pale nje vizuri tu. Karibu watu wote pale nje walivaa kanzu, akiwemo baba yangu. Mzee mkundi naye anayo kanzu yake ambayo huivaa akipata mialiko ya aina hii.


Basi mara kikaletwa chetezo na ubani ukawekwa, wakanyanyuka wazee kadhaa na wakiongozana na kaka wa binti na kuingia ndani ambapo walielekea katika chumba ambacho alikuwa amewekwa huyo Bi harusi ambaye kiukweli sikumfahamu. Baadae niliambiwa kuwa alikuwa akiishi na dada yake huko Kinondoni na baada ya kupata mchumba ikabidi shughuli za posa na ndoa zihamishiwe kwa kaka yao mkbwa ambaye ni huyo jirani yetu, na ndio maana, wahudhuriaji wengi sikupata kuwafahamu.


Baada ya kitambo kidogo, wakatoka, na kurejea sebuleni. Nilisikia bwana harusi akiulizwa kama mara tatu hivi kuwa amekubali kumuoa huyo Binti ambaye alitajwa kwa jina la Salha kwa mahari ya elfu sabini na tano? Ambapo alishatoa elfu hamsini na kuna deni la elfu ishirini na tano. Bwana harusi mara zote alikubali.


Lakini jambo lililonifrahisha zaidi ni kile kiwango cha mahari, sikujua kama kuna watu bado wanatoza kiwango kidogo cha mahari kiasi kile. Sikusita kuonesha mshangao wangu, na mama mmoja aliyekuwa amekaa jirani namie akaniambia kuwa hata hivyo yule (Yaani bwana harusi) kagongwa, yaani katozwa kiasi kikubwa cha mahari, eti kwa kawaida waislamu hususan Wapembahutoza kiwango kidogo sana cha mahari hata kufikia elfu ishirini na tano!, ndio elfu ishirini na tano!


Nilimuangalia mama, nikamkonyeza kwa mbali, naye akatabasamu akijua ninamaanisha kitu gani, kwani wao kwa dada zangu watatu walioolewa, walilamba zaidi ya laki tano kwa kila mmoja! Na hapa nazungumzia tukio la miaka zaidi ya mitano iliyopita!


Sijui kati ya Fadhy, Markus au Kitururu, atakayebahatika kunichumbia atagongwa ngapi, maana kwa jinsi ugumu wa maisha ulivyopanda, sijui kama watamudu dau la Mzee Mkundi…………LOL


Haya baada ya kusomwa dua kadhaa na shughuli ikawa imeisha, na tukatangaziwa kuwa tusubiri Sadaka kabla hatujaondoka.


Mnajua ilikuwa ni nini? Mh! Tuliletewa chai iliyoungwa vizuri na viungo toka Pemba, na vijiandazi vidogo, baada ya hapo, shughuli ikawa imeisha, na jamaa mmoja akaenda barabarani na kudaka Hiace moja ya Kipawa akaikodi na kuja nayo pale, Bwana na Bi harusi walikaa mbele na wapambe walikaa nyuma kisha wakondoka kimya kimya hapakuwa na vigelegele wala nini. Nilipouliza kwa nini hapakuwa na shamrashamra, nilijibiwa kuwa ni kharamu. Mweh! Mwenzenu nilishangaa kweli, maana kusema kweli ile ilikuwa ni mara yangu a kwanza kuhudhuria shughuli ya ndoa ya kimya kimya.



Nimejifunzazjambo kwa kweli.

Saturday, May 7, 2011

JAMAA AKASAHAU KIFANYIO NDANI YA GARI!


Waliamua kumalizia hapa


Jana niliamua kutoka na kuwatembela rafiki zangu ambao nilipoteana nao kwa muda mrefu sasa. Ilikuwa ni furaha iliyoje kukutana na rafiki zangu hawa ambao baadhi nilisoma nao na wengine nilijuana nao kwenye mishe mishe za kutafuta Ngawira. Baada ya kupigiana simu na kutumiana ujumbe wa simu zetu za kiganjani, tukakubaliana tukutane kwenye mghahawa mmoja ulioko maeneo ya Masaki maarufu kwa kutengeneza Pastries unaojulikana kwa jina la Epidor.




Nilifika pale majira ya saa kumi za jioni na kuwakuta wenzangu wanne wameshafika, na walikuwa wakiendelea kupashana habari za hapa na pale. Nilijumuika nao, na tukaanza kukumbashana stori zetu za zamani hususana vituko tulivyokuwa tukifanya wakati tulipokuwa shule na vituko vya Waalimu wetu. Si mnajua wanafunzi wa zamani wanapokutana hukumbushana ujinga wao wa zamani?


Wakati tukiendelea na stori zetu akaja Shoga yangu Zulfa na kijana mmoja aliyemtambulisha kuwa ni Binamu yake anayejulikana kwa jina la Kishindo, Alikuwa ni kijana mtanashati lakini mwenye maneno mengi. Kwa muda mfupi alikuwa ameshachukua nafasi ya kuwa mzungumzaji mkuu akanifunika hata mie, ambaye najulikana kama kiranja wa kupiga soga. Alikuwa ni mtu wa masihara na mwepesi kudakia jambo na kuligeuza Comedy, naamini mnawajua watu wenye tabia za Comedy au Chale Chaplin ambao ukikaa nao ni lazima ucheke. Basi ngoja nifupishe maelezo, kwa kifupi ni kwamba wakati tunapiga tiralila zetu, akatupa stori mbili tatu hivi ambazo zilituvunja mbavu wote tuliokuwa pale, lakini kubwa zaidi zilituacha na maswali. Moja ya stori ambayo ningependa kuwashirikisha ni hii ya KIFANYIO. Tega sikio…………



Kuna jamaa mmoja alikuwa na rafiki yake anayeishi maeneo ya Ukonga naomba nimtambulishe kwa jina Ulimbo , sasa siku moja wakapanga na rafikiye anayeishi maeneo ya Tabata, (naomba huyu tumuite Kizito) wakutane kwenye Baa moja maneo ya Mwenge wajumuike pamoja na kupata moja moto moja baridi. Kizito alifika pale na usafiri wake na akamkuta Bwana Ulimbo ameshafika zamani . Wakati wanendelea kupata kilaji a.k.a ugimbi, Bwana Kizito akapata mgeni, hakuwa mwingine bali mfanyakazi mwenzie ambaye alifika mahali pale kama nasibu tu (Coincidence), Bwana Kizito akamtambulisha yule Binti kwa Bwana Ulimbo ambaye hakuwa ameoa, na kisha wakajumuika pamoja na kuendelea kupata vinywaji.



Muda wote wakati wanakunywa, Ulimbo alionekana kuvutiwa na yule Binti, hivyo muda wote alikuwa bize akimdadisi kutaka kumjua zaidi. Walizoeana ghafla na hatimaye walibadilishana namba za simu. Ilipofila usiku, yule Binti aliomba kuondoka, lakini Ulimbo akaomba kumsindikiza, walipofika nje ya Baa, yule Binti akamuaga Ulimbo kuwa anawahi kupanda Daladala kwani ilikuwa ni usiku majira ya saa nne hivi.


Ulimbo alimuuliza kama anaishi wapi, yule Binti alimjulisha kuwa anaishi Mwananyamala, Kizito alimuomba amsubiri pale nje, akamuage Bwana Kizito ili aje amsindikize. Ulimbo alikwenda kumuomba Kizito Gari lake kwa kuwa yeye hakuwa na usafiri ili amsindikize kimwana maeneo ya Mwananyala. Kizito alimpa gari lakinialimtahadharisha kuwa aendeshe kwa makini ili kuepuka ajali. Ulimbo alimhakikishia Kizito kuwa atarudi salama. Alichukua gari na kuondoka na yule binti kuelekea Mwananymala, walipofika njiani Ulimbo alisimamisha gari kwenye duka la dawa na kumuomba binti amsubiri ili akanunue dawa, kwani mdogo wake anasumbuliwa na Malaria na kuna dawa aliandikiwa angependa kumnunulia.



Baada ya muda alirejea ndani ya gari, na kuondoka, walipofika maeneo ya Mwananyamala, Ulimbo alisimamisha gari tena na kudai kuwa anajisikia kwenda haja ndogo, yule binti alimshauri waendelee na safari kwani nyumbani kwake anapoishi sio mbali hivyo wakifika atajisaidia hapo kwake kuliko kujisaidia njiani. Ulimbo alikaidi ushauri wa yule binti akidai kuwa amebanwa. Alishuka na kuzunguka nyuma ya gari aliporudi akazima gari na hadithi ikageuka, ilikuwa ni kama Swala ndani ya himaya ya Chui, Ulimbo hakukubali kumrejesha binti yule bila kumuonja, na kweli baada ya kutumia maneno matamu kama asali hatimaye binti akajikuta akikubali kumpa ulimbo utamu lakini kwa masharti ya kutumia Kifanyio a.k.a Condoms.



Kumbe Ulimbo aliposimama kwenye duka la Dawa hakuwa akitaka kununua dawa bali alitaka kununua Condoms kwa kuwa alishayapima maji na kuyaona kuwa hayakuwa na kina kirefu hivyo isingemuwia vigumu kuvuka hata bila mtumbwi (Yaani isingemgharimu kutafuta Guest House ya chapchap).


Sharti la kutumia Kifanyio lililotumiwa na Binti halikuwa kikwazo, Ulimbo alishakuwa nazo zamaani, (Wanaume waasherati huwa wana akili za ziada) Zoezi likafanyika mle mle ndani ya gari kisha akampeleka Binti nyumbani na kumshusha na kuagana kwa Mabusu kemkem. Alirudi pale Baa na kumkuta Kizito akiwa na ameungana na jamaa wengine wawili, hivyo wakaendelea kupata vinywaji hadi usiku wa saa sita hivi. Kwa kuwa Kizito ni mtu na familia yake akawaaga wenzie na kuondoka zake kurudi nyumbani.




Asubuhi mkewe Kizito alimuamsha mumewe na kumuomba funguo za gari ili waende Kanisani, kwani Kizito alidai kuchoka hivyo alimuomba mkewe aende na watoto, yeye wamwache apumzike.Mkewealipofika kwenye Gari aliamua kulifanyia usafi kwa kutoa Kapeti za gari na kuzikung’uta na kisha kuzirejesha ndani ya gari, alianza na kapeti za mbele na alipotoa kapeti za nyuma……….. Lahaullah……….. akakutana na Kifanyio kilichotumika kikiwa bado kina ubichi………….


Mwanamke yule alikurupuka na kwenda ndani kumuita Mumewe na kumtoa nje….walipofika kwenye Gari alifungua mlango wa gari wa nyuma na kumuonesha mumewe kile Kifanyio kilichotumika…… Mumewe alishikwa na Butwaa na kujikuta akitamka…………….. "Aaaaaaakh Ulimbo umeiponza masikini"…………… Msimuliaji hakufanya hitimisho, alituachia tafakuri kuwa, Je mume atawezaje kumuelewesha mkewe mpaka amuelewe?

Wednesday, May 4, 2011

JIONI HII PALE POSTA JIJINI DAR




Shiranga la foleni Jijini Dar linatisha, maana leo imenilazimu nijitulize ndani ya mjengo huo jirani na kupata kinywaji barrrrdi ili kuvuta muda foleni iishe, lakini hiyo bei ya vinywaji ni balaa tupu kwa siye tuliyozoea soda za mia tano, roho inauma kweli..............wanapaita Holiday Inn.


Tuesday, April 19, 2011

BALAA GANI HILI!?

Msinielewe vibaya waungwana, hata mie nashangaa tu!!!!!!

Saturday, April 16, 2011

MPIGA DEBE WA DALADALA AMWAGA NGELI NA KUWASHANGAZA WENGI………





Leo asubuhi nimekutana na kituko cha mwaka, naomba nikiri kwamba hata mimi nilikuwa ni mjinga kwani sikutarajia kwamba jambo hilo nililolishuhudia linawezekana. Naomba nikiri kuwa hata mie nilikuwa nawapa watu hawa mtazamo tofauti kabisa nikidhani labda mie ni mjanja kuliko wao, lakini hili nililolishuhudia asubuhi ya leo, nimenifunza jambo moja muhimu sana maishani, kwamba kamwe usimhukumu mtu kutokana na muonekano wake.


Ilikuwa ni majira ya saa kumi na mbili alfajiri, niko maeneo ya Msasani, nikisubiri daladala la kuelekea Kariakoo, mara likaja basi moja hivi aina ya Toyota Coster. Kama kawaida abiria wakiwemo wanafunzi tulilikimbilia na kuanza kugombea kupanda kila mtu akijaribu kuwahi kiti. Japokuwa hatukuwa wengi, lakini nilishangazwa na jinsi abiria walivyokuwa wakigombea kupanda utadhani watakosa nafasi ya kukaa. Lakini cha kushangaza ni kwamba vurugu zote zile ilikuwa ni ili kuwahi viti vya Dirishani!


Pale mlangoni alisimama mpiga debe mmoja ambapo kwa hapa Dar hujulikana kama Mateja, yaani watumia madawa ya kulevya, ambaye alikuwa amevaa nguo kuu kuu na zilikuwa chafu ajabu. Alikuwa pale mlangoni kuzuia wanafunzi wasipande. Kwa hapa Dar ni jambo la kawaida wanafunzi kuzuiwa wasipande kwenye basi na abiria wakabaki wakiangalia tu, kama vile haiwahusu. Kule Arusha mambo ni tofauti kidogo, wanafunzi huwa hawaachwi, tena kama hajavuka barabara, hasa watoto wadogo, kondakta anamfuata na kumvusha ili apande kwenye basi, kwa kweli nilishangazwa na ustaarabu wa makondakta wa daladala za Arusha.


Baada ya abiria wote kupanda, yule mpiga debe aliwaambia wale wanafunzi kuwa atachukua wanafunzi sita tu, wengine waende kwenye mabasi mengine. Pale chini kulikuwa na wanafunzi zaidi ya kumi na tano hivi na wote walionekana wakitaka kupanda kwenye hilo basi ili kuwahi shule. Yule kijana mpiga debe aliongea kwa usataarabu akiwaelewesha wale wanafunzi, akiwaambia kuwa hata yeye anajua adha ya usafiri kwa wanafunzi lakini ile gari ina Hesabu, yaani wanatakiwa wafikishe kiwango fulani cha hela kwa mwenye gari na wao wabaki na chochote, na kwa kuzingatia kuwa leo ni Jumamosi, ni ngumu sana kupata hesabu ya tajiri.


Lakini kulitokea kutoelewana kati ya wale wanafunzi na yule mpiga debe, wanafunzi walimjia juu wakimwambia aache siasa, wao wanataka kuwahi shule na hawahitaji Lecture pale. Kulitokea kutoelewana, lakini yule mpiga debe alisisitiza msimamo wake wakutaka wapande wanafunzi sita tu. Ni kweli walipopanda wanafunzi sita, aliwazuia wengine wasipande na kuruhusu dereva aondoe gari. Baadhi ya wanafunzi walioachwa pale chini walilazimisha kuning’inia mlangoni, lakini yule mpiga debe aliendelea kuwazuia huku gari likianza kuondoka mdogo mdogo..


Wakati zogo kati ya wanafunzi na yule mpiga debe likiendelea, ghafla akaibuka abiria mmoja, akaanza kumfokea yule mpiga debe, akimuonya kwamba kama hatawaruhusu wale wanafunzi wapande basi atalipeleka basi lile Polisi, yule Mpiga debe hakumjibu alikuwa akiendelea kuzozana na wanafunzi.


Yule abiria alianza kumtolea yule mpiga debe maneno ya kashfa huku akimtisha kuwa atampiga. Basi liliondoka na baadhi ya wanafunzi waliachwa pale kituoni, ndipo yule mpiga debe akamgeukia yule abiria na kumuuliza kisa cha kumkashifu wakati yuko kazini.


Yule abiria akawa kama amechokozwa, alimshambulia yule mpiga debe kwa maneno makali na kumkashifu kuwa hajasoma na ni mvuta unga tu na kibaka wa mtaani.


Yule mpiga debe akamwambia, ni kweli hajasoma, kwa sababu ingekuwa ni jambo la kustaajabisha kukuta mpiga debe msomi, hata hivyo hakuishia hapo, akamtupia swali yule abiria………


"inaonekana mwenzangu umesoma sana eh!….. hivi una degree ngapi mpaka sasa, au una masters?” Yule abiria aliendelea kumtolea maneno ya kashfa yule mpiga debe huku akisisitiza kuwa hajasoma na ni mjinga tu.


Yule Mpiga debe akaonekana kukerwa na yale maneno kutoka kwa abiria mkorofi, akamgeukia na kumwambia, kwa kiingereza, ngoja nimnukuu hapa……..


“Listen my friend, don’t judge me because of what I am doing, I have good education background than you. To be a Daladala tout does not justify that I am ignorant. For your information, I am educated enough to work for a white-collar job. I am here because of frustration, after being fired from my job; I had a nice job with a lot of benefits and privileges, I am not a fool ok!”


Wakati anamwaga kiingereza, kwanza abiria walishikwa na butwaa, na baadae wakaanza kumshangilia wakiwemo wale wanafunzi waliokuwa wakitetewa na yule abiria mkorofi. Hata hivyo yule abiria aliposikia jamaa anamwaga kiingeza, alikaa kimya asiamini masikio yake,hakujibu kitu.


Abiria waliendelea kumchagiza mpiga debe aendelee kutoa dozi kwa mshkaji, na yeye ili kupata ujiko zaidi akaendelea kumwaga ma-vitu, palikuwa ni patamu hapo…….


“You know sometimes people think all daldala touts are drug users and they are not educated ……..… No, you are totally wrong my friend, for this job I am earning more than enough, I can make your salary which you get from you Boss Indians for 10 days. Although I have been fired but I decided to work as a daladala touts rather than stealing someone’s money.”


Kisha akaendelea…..


“Why you are quiet, talk now Mr. Educated” ………… “You see,” akatugeukia sisi abiria na kutuambia ……….. “Mr. Educated have failed to speak even two English words”


Jamaa akajikakamua na kumjibu,


“Hebu ondoka na kiingereza chako cha kuombea maji, mwenyewe unajiona umeongea kiingereza hapo, hamna kitu,unachapia tu”


Mpiga debe hakumkawiza akamjibu…….


“Ok, my English is just for begging water, where is yours, if you can speak only two English words, I will give you ten thousand, right now, in front of passengers, I am not joking”


Yule mpiga debe akatoa elfu kumi na kumpa abiria mwingine aishike, ili kuthibitisha kuwa hatanii. Kumbe jamaa alikuwa ni mweupe, hajui Ngeli, yaani ilikuwa ni aibu, karibu abiria wote wakawa wana mzodoa kwa maneno ya kejeli.


Tulipofika kituo cha Namanga jamaa akashuka kwa aibu na ninadhani alikuwa hajafika safari yake, naona alishuka ili kujisitiri na aibu iliyomkumba mle ndani ya basi.


Nakwambia ilikuwa ni gumzo ndani ya basi lile kila mtu akisema lake wapo waliosema kuwa yule mpiga debe ni mpelelezi wa Polisi, wapo waliosema ni shushushu yaani anafanya kazi usalama wa Taifa. Na hilo ndilo tatizo tulilonalo Watanzania, yaani mtu akijibainisha tofauti na muonekano wake basi ataitwa shushushu…….. Basi na yule mpiga debe akapewa cheo cha ushushushu pale pale, kisa kaongea Kiingereza, kuna wengine walisema sio Mtanzania bali ni Mkenya, kwa kuwa hakuna Mtanzania anayejua Kiingereza kama vile halafu afanye kazi ya kupiga debe, ili mradi kila mtu alisema lake.


Tulifika Kariakoo kilamtu akashika hamsini zake, nimerejea nyumbani jioni hii nikaona niwashirikishe wasomaji wangu katika kisa hiki ambacho hata mie kiliniacha mdomo wazi.

Thursday, April 14, 2011

MHUBIRI WA INJILI KITAANI ADUNDWA

Mhubiri akiwa kazini




Hii niliishuhudia katika viunga vya pale Mwenge jiji Dar jana wakati naenda Hospitali. Nilikuwa nimesimama kwenye duka moja la kuuza Dawa kuulizia dawa fulani ambayo niliandikiwa hospitalini. Upande wa pili wa barabara kutoka katika duka hilo kulikuwa na jamaa mmoja aliyejitambulisha kama Mtumishi wa Mungu, alikuwa akimwaga neno la Mungu, kuwaasa watu waache matendo ya Dhambi, na kumrejea Mungu.


Jasho lilikuwa likimtoka kwelikweli na alikuwa akiongea kwa jazba kama vile anagombana, lakini katika mahubiri yake alikuwa akiwananga wapita njia hususan wanawake ambao walivaa vimini au suruali za kike.


Ilikuwa kila akipita mwanamke mwenye kimini au suruali ya kike alikuwa akimwambia…….. ngoja nimnukuu hapa. ‘wewe mwanamke mwenye suruali acha dhambi, hayo mavazi uliyovaa hayampendezi mungu kamwe na ninakuhakikishia utakwenda motoni, na wewe mwanamke mwenye kimini na hakika hutauona uzima wa milele, utaishia motoni’ mwisho wa kunukuu.


Kibaya zaidi alikuwa akitumia kipaza sauti na alikuwa akiwafuata nyuma (hao wanawake) huku akiwamwagia maneno makali na ya kudhalilisha


Wakati akiendelea na mahubiri yake akapita dada mmoja ambaye alikuwa amefuatana na mvulana, sikuweza kujua kama walikuwa na uhusiano wa kimapenzi au walikuwa ni ndugu, yule mhubiri kama kawaida yake akaendelea kumwaga maneno ya kuwakashifu wanawake wenye kuvaa suruali.


Kutahamaki nikamuona mhubiri kakunjwa shati na yule kijana, aliyekuwa na yule binti, mara ghafla yule kijana akaanza kumchapa makonde yule mhubiri mara kichwa, hajakaa sawa akalambwa mtama, mhubiri chali……………..


Kisha yule kijana akamshika mkono yule dada, wakaondoka wakimuacha mhubiri akijizoa zoa pale chini. Niliondoka katika eneo lile maana umati wa watu ulianza kusogea katika eneo hilo ili kujua kulikoni.


Kilichojiri nyuma yangu sijui.


Tuesday, April 12, 2011

BODA BODA ILIPONITEGUA MGUU.

Juzi katika harakati zangu za kutafuta mikwanja, nikajikuta nikipigwa defrao na Bodaboda maeneo ya Msasani.

Niliwahishwa Hospitali na ikaonekana nimeteguka kifundo cha mguu wa kushoto. nimefungwa POP na sasa naendelea vyema.

Friday, April 1, 2011

BIBI KOERO NA KIKOMBE CHA BABU AMBILIKILE

Misitu kama hii ni hazina kubwa kwa dawa za miti shamba



Hivi karibuni nilimtembelea bibi Koero kule kijijini, nilipitia huko wakati nikitokea Arusha kurudi Dar. Nilimkuta yu buheri wa Afya, na kama kawaida yake alinipokea kwa bashasha kubwa pamoja na tabasamu pana usoni pake.


Mara zote anajua mjukuu wake nina hamu ya simulizi zake zinazonipa tanuri la fikra, kwa kweli Bibi yangu huyu ananipenda sana.Daima napenda sana udadisi,napenda kuchokonoa, kudadavuliwa na kudadavua niwapo na bibi Koero, kama vile alivyo Yasinta na mie siko nyuma katika Ukapulya.


Yaani ni zaidi ya falsafa na wazo ndani ya neno ya kaka Kitururu pamoja na chakula kitamu kiliwacho.


Basi katika hali ya utani nikamuuliza kuwa kwa nini na yeye asiende Loliondo kwa Babu Ambilikile Mwasapile kupata Kikombe? Nilimuuliza hivyo baada ya kuniambia kuwa juma lililopita alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya mgongo na kichwa.


Bibi Koero aliniangalia, kisha akacheka kwa dharau. Nikajua kuna jambo lenye wazo na chakula kitamu kusimulia. Alicheka kisha akasema kwa dharau, ‘umri huu niende kwa Babu Loliondo kufanya nini?, umri huu nilio nao (Bibi Koero anatimiza miaka 92 mwaka huu) siwezi kujisumbua kiasi hicho, nimeshakula chumvi nyingi na hivyo nasubiri kupumzika’.


Alinishika mkono na kuniambia nimfuate, kwani wakati huo alikuwa kwenye kijishamba chake akipalilia Tangawizi zake. Tukajongea kwenye kivuli cha mti ulioko jirani tukakaa chini. Akaanza riwaya zake zenye maono; sikiliza mjukuu wangu, alisema bibi Koero, kisha akaendelea………..Kuibuka kwa huyo Babu Ambilikile sio jambo la kustaajabisha, ni mambo ya kawaida kabisa, na inawezekana wakaibuka wengine na wengine (wakati tunazungumza ilikuwa bado hazijasikika habari za kuibuka kwa kijana mwingine huko Mbeya, Morogoro na Mama wa Tabora ambao wote wamedai kuoteshwa dawa na Mungu).


Aliendelea, Kabla ya ujio wa tiba za Hospitali, Watu walikuwa wakiugua na kutibiwa kwa miti shamba, na sio kwamba kulikuwa hakuna maradhi kama wakati huu, yalikuwepo, tena maradhi mengine yalikuwa ni ya kutisha, Je watu hao walikuwa wakitibiwa na nani kama sio Mungu? Labda kitu ambacho watu wa kizazi chenu msichokifahamu, ni kutokujua utendaji kazi wa Mungu.


Zamani kulikuwa na imani ya kuamini Mizimu Matambiko au Mizungu na kadhalika na kupitia imani hizo mambo mengi yalifanyika. Ujio wa hizi dini za Mapokeo, ambazo hata hivyo mimi ni mmojawapo ya watu tuliojikuta tukibadilika kutoka katika imani zetu tulizorithi kutoka kwa mababu zetu na kuingia katika imani hizo za dini za mapokeo, tulijikuta tukiziacha na kuzibatiza jina la imani za Kishenzi kwa kuwa tu tulilazimishwa kuzikana. Sasa basi kwa upande wa utendaji kazi wa Mungu, kwa kweli hilo ni jambo ambalo bado linazusha maswali kila uchao. Mungu yupo na anayo namna yake ya kuwasiliana na wanaadamu, kama alivyofanya tangu huko zamani.


Wanaadamu walipitia nyakati tofauti na kila nyakati zilikuwa na kitabu chake, yaani historia yake. Msomaji keti kitako…,..ngoja nikusimulie mkasa huu uliompata baba yetu.Wakati nilipokuwa binti mdogo kigori. Baba yetu aliumwa sana, kiasi cha kulala kitandani kwa mwaka mzima, kama ingekuwa ameugua kipindi hiki labda mngesema kuwa ni huo ugonjwa wenu wa Ukimwi. Tulifika mahali tukakata tamaa, tulimpeleka kwa waganga mbalimbali wa asili wenye sifa za kutibu maradhi yaliyoshindikana lakini hawakuweza kumtibu, tulibaki kumuomba Mungu.


Ilifikia mahali ikabidi sasa tubadilishe sala zetu, kwamba badala ya kumuombea apone, tukamuomba Mungu ampumzishe kwa sababu alikuwa ameteseka sana kwa maradhi hayo.



Ilitokea siku moja Mjomba wake na baba aliyekuwa akiishi Kijiji kingine alikuja nyumbani alfajiri na mapema, na sisi tulijua kuwa amekuja kumuona mgonjwa, lakini alipofika tu, aliomba jembe na panga, kisha akamchukua kaka yetu mkubwa na kwenda naye kwenye Msitu wa Shengena.


Sikiliza hili, msomaji, msitu wa Shengena ni miongoni mwa Misitu yenye maajabu makubwa hapa nchini, msitu huo uko jirani na kijiji alichozaliwa mama yetu yaani hapo Mamba Miamba wilayani Same mkoani Kilimanjaro. Simulizi juu ya maajabu ya Msitu huo yanahitaji makala inayojitegemea. Nitawasimulia nikipata muda.


Bibi Koero aliendelea kusimulia, walirudi baada ya saa kama tatu hivi wakiwa na mizizi na majani ya mti tusioujua. Mjomba alitueleza kuwa siku mbili zilizopita alioteshwa na kuoneshwa dawa itakayomtibu baba, awali alipuuza, lakini kwa mara nyingine siku iliyofuata alioteshwa tena na kuoneshwa dawa hiyo.


Kwa mujibu wa maelezo ya mjomba alidai kuwa akiwa usingizini, aliona kivuli cha mtu pembeni ya kitanda, alikuwa ni mtu mwanaume na alikuwa akimuamsha kwa kumwita kwa jina lake lakini kwa kunong’ona, aliamka na yule mtu akamuonesha ishara kuwa amfuate, alinyanyuka na kumfuata, mjomba alidai kuwa hawakupitia mlangoni, bali kulitokea uwazi kwenye ukuta wakapita na ule uwazi ukajifunga na walipokuwa nje mavazi ya yule mtu yalikuwa yanang’aa kama theluji na hivyo kutoa mwanga.


Kwa kuwa kulikuwa na giza totoro, ule mwanga ulimwezesha kuona njia na waliendelea kutembea kuelekea mahali asipopajua.


Walitembea mwendo mrefu hadi wakafika msituni, na ndipo akaambiwa achimbe mizizi ya mti fulani baada ya kuchimba ile mizizi walienda kwenye mti mwingine na kukata majani ya ule mti kisha wakarudi nyumbani.


Walipofika walipitia pale pale ukutani na walipoingia ndani yule mtu aligeuka kuwa kivuli na kisha akamwambia kwa kunong’ona kuwa ile ni dawa ya kumtibu mjomba wake ambaye ni baba yetu.


Alimwelekeza namna ya kuitayarisha ile dawa kabla ya kumpa mgonjwa kisha akatoweka.Mjomba alistuka usingizini na kumsimulia mkewe, juu ya ndoto ile, shangazi alimshauri aende kwa mtaalamu ili kupatiwa tafsiri ya ile ndoto, lakini alipuuza, siku iliyofuata alioteshwa tena, na ndipo akakata shauri kuitafuta hiyo dawa ambayo kwa kweli ndiyo iliyomtibu Baba.


Baada ya baba kupona hakupata kuumwa tena zaidi ya maradhi madogo madogo hadi alipofarikia akiwa na miaka tisini na ushee.


Muda wote wakati Bibi Koero akinipa simulizi hiyo ya kuvutia nilikuwa nimemtumbulia macho nikiwa nimeshika tama.


Hivyo basi mjukuu wangu, aliendelea Bibi Koero, Mungu amekuwa akiwasiliana na wanaadamu hadi hivi leo, lakini wengi waliokuwa wakioteshwa hapo zamani walikuwa wakifanya siri, na hata hivyo hapakuwepo na wingi wa vyombo vya habari na mawasiliano kati ya eneo moja hadi jingine yalikuwa ni magumu na ndio sababu habari hizo hazikupata kuvuma kama hivi sasa.


Labda jambo lingine na lile la wananchi kukata tamaa na gharama za matibabu katika Hospitali zetu kuwa juu, hiyo nayo ni changamoto nyingine ambayo inaikabili sekta hiyo ya afya sio kwa hapa nchini tu bali dunia nzima kwa ujumla.


Kwa kifupi alinieleza kuwa Mungu yupo na ataendelea kuwasiliana na wanaadamu kwa namna tofauti kulingana na jinsi anavyoona. Lakini hata hivyo, alisema kuwa sio kwamba wote watakaotumia dawa hiyo watapona, haiwezekani, wapo watakaopona na wapo ambao hawatapona kwani kuponya kwa dawa za namna hiyo kunatokana na imani watakayokuwa nayo watumiaji.


Kwa ujumla tuliongea mengi na bibi Koero ikiwemo kutahadharisha juu ya kuibuka kwa Matapeli watakaosingizia nao kuotesha dawa na Mungu kwa ajili ya kujipatia fedha kwa hila na kujijengea umaarufu, kwani katika msafara wa Mamba hata Kenge nao pia wapo.


Hata hivyo msichoke kupitia kibaza hiki maana nikipata muda nitamalizia mazungumzo yetu na Bibi Koero sehemu ya pili ikiwa ni mwendelezo wa kile tulichojadili. Mmmh! Kumbe kikombe cha babu hakikuanza leo!