Saturday, January 16, 2010

DADA YASINTA NIMEISHITUKIA JANJA YAKO

Dada yangu akiweka mikakati
Kwa dada yangu Yasinta,

Nimesikitishwa sana na kile ulichobandika katika blog yako ukidai kuwa wewe hutaki kuwa mwanaharakati wa kututetea sisi wanawake na watoto zetu, kama nilikunukuu vizuri umesema kuwa kuandika kwako makala za kutetea haki za wanawake sio kwamba unayo dhamira ya kuanzisha NGO.

Umedai kuwa hujawahi kuota na wala kuwaza kufanya kazi hiyo, bali unaamini kwamba, kuwa mwanaharakati haimaanishi kuwa na Organization. Kwamba huwezi kuwatetea wanawake na watoto isipokuwa mpaka uwe na NGO.

Pia ukabainisha kuwa umeamua kuweka mambo hadharani maana kuna vimbelembele washaanza kujifanya yule shehe wa Mwembe chai aliyetabiri kuwa mwana CCM yeyote atakayechukua fomu za kutaka kugombea urais kwa kumpinga Rais wa sasa Muheshimiwa Kikwete basi atakufa ghafla kwa kubanwa na ngiri. Vimbelembele hao wamekutabiria kuwa kwa kuandika kwako vimakala vya kujifanya una huruma sana na wanawake wanaonyanyaswa na waume zao ni kamchakato kako ka kuelekea kuanzisha Organization ya kuwatetea wanawake nchini.

Duh! Samahani dada nilisahau kukupa heshima yako. Nakupa shikamoo zako wewe na mumeo. Habari za huko ughaibuni mlipo, nasikia kuwa kuna baridi sana kiasi kwamba mabarafu yamejaa kila mahali mpaka chooni. Samahani kwa kutaja chooni, nimesahau kuwa hilo sio neno la kistaarabu, nilikuwa namaanisha toilet.

Dada kama nilivyoanza katika utangulizi wa barua hii, ni kwamba nimeishitukia janja yako. Unajua tangu uhamie ughaibuni dada umekuwa na akili sana.

Sio wewe mwaka juzi ulipokuja huku nyumbani ulianzisha NGO ya kutetea haki za wanawake na watoto kwa kushirikiana na yule binamu yako anayezaliwa na yule shangazi, ambaye analazimisha undugu baada ya kusikia kuwa umeolewa na mzungu kwa kudai kuwa eti zamani alikuwa akimbeba baba yako wakati bibi na babu yako wakienda shamba.

Huyu binamu yako ambaye inasemekana alifeli zaidi ya mara saba kuingia kidato cha pili huko Songea katika ile shule iliyoko pale Mfaranyaki, karibu na ule muembe dodo unaotumiwa na mafundi baiskeli ndiye uliamua kumshirikisha kuanzisha NGO yenu wenyewe ambayo mliipa jina la Ruhuwiko NGO for woman and children crying everyday.
Taasisi hiyo ambayo imesajiliwa na katibu kata ilikuja kwa kasi ya ajabu na inatishia kuvunja ndoa za watu, na mojawapo ya ndoa iliyovunjika ni ile ya yule mzee Ngatura mwenye wake saba.

Ndao iliyovunjika ni ya yule binti machepele wa saba kuolewa na yule mzee. Nadhani unamkumbuka yule binti aliyewahi kufumaniwa na mke wa mwalimu wa kufundisha ngoma za asili pale shuleni, na kutokana na umahiri wa kucheza lizombe yule binti alipewa Umanju wa kuongoza ngoma na mwalimu na kutokana na kupewa cheo hicho mwalimu wa ngoma akamgeuza kuwa kijumba kidogo chake na makutano yao yakawa kule kwenye shamba la kijiiji, na kama unavyojua wambea wa kijiji wakamjuza mke wa mwalimu wa ngoma na hivyo kuwekewa mtego na kufumaniwa. Si unakumbuka jinsi alivyopigwa mpaka akachaniwa nguo zote? Basi kutokana na aibu si ndio akahamishiwa katika shule ya jirani na baba yake ili kukwepa aibu.

Basi huyu binti baada ya kuachika huku akiongozwa na binamu yako wanataka mali za yule mzee zigawanywe sawa kwa sawa la sivyo kesi inapelekwa mahakaam kuu.
Hivi ninavyo kuandikia kuna mashauri zaidi ya wanawake 30 wanaotaka kuachana na wanaume zao kwa kutegemea kugawana mali walizochuma na wanaume zao. Kampeni hiyo ya kuachanisha wanandoa inaongozwa na hiyo NGO yenu na anayeingoza uasi huo wa kuvunja ndoa za watu ni huyo binamu yako.

Hivi sasa hali ni tete pale kijijini na wazee wa kijiji wameitisha kikao cha dharura kujaldili hali hiyo na wanatishia kuchangishana nauli ili waje Dar kumuona muheshimiwa rais ili anusuru ndoa zao zinazoelekea shimoni. Pia wanataka binamu yako huyo aondolewe haraka pale kijijini kwa ile staili ya kuwekewa karantini asikanyage tena pale kijijini iwe ni kwa sherehe au misiba.

Hata hivyo katika utetezi wake binamu yako huyo amejitetea kuwa eti hiyo kampeni ya kuachanisha ndoa za watu ni idea yako yaani kwa kiingereza suggestion yako maana alidai kuwa yeye siye msemaji mkuu wa hiyo NGO, bali ni mtekelezaji wa kile unachokiagiza ukiwa huko ughaibuni.

Sasa dada kwa kutaka kutuchota akili unajidai kuwa hutaki kuwa mwanaharakati wakati tayari ulishakuwa mwanaharakati tangu mwaka juzi. Kwa kuwa unatafuta umaarufu ili kutengeneza mazingira ya kupanua wigo wa hiyo NGO yako kutoka kijijini hadi kuwa NGO ya kitaifa baada ya kuona kule Ruhuwiko umeanza kupoteza umaarufu na ndio maana unataka kupata maoni ya wasomaji wako katika ile staili ya mchomeko, yaani ku bip kwa kiingereza.

Dada samahani naomba univumilie kwa haya ninayoyasema maana mie sitaki uje kuumbuka baadae, kwani Dar es salaamu sio sawa na Ruhuwiko, huku kuna ushindani wa hii biashara ya NGO, usipoangalia utatapeliwa wewe, kuna watu huku ni wasanii ile mbaya, anaweza kuja mwanamke akajidai amegombana na mumewe, na akipata msaada huyooo anaenda kuendelea na ndoa yake kama kawaida. Ukitaka kupanua wigo wa NGO yenu ihamie huku Dar inabidi utafute mganga ambaye anaweza kumwangalia mteja akajua kama huyu ana matatizo kweli au msanii tu.
Dada huku Dar NGO ni mradi wa watu wajanja ambao hutumia staili ya matatizo yenu ndio tijara yetu, na wengi wao ni wale walioshindwa kutofautisha ile dhana kujiajiri na kujitolea. Kwa wao kuitolea maana yake ni kuwekeza kwa kutumia matatizo ya wengine.

Yaani siamini kuwa na wewe umeingia katika kamtindo hako kwa kutafuta fedha kwa kutumia matatizo ya wengine. Nashawishika kuamini kuwa na wewe umefulia kimawazo, kwani hiyo mbinu yako nimeishitukia dada. Hapa Dar humpati mtu labda Kamala na Chacha kwani nao eti ni wanaharakati wa kuwatetea vijana…….LOL

Kwa leo naomba niishie hapa nikipata muda nitakujuza mengi juu ya NGO za hapa Dar.

Nakutakia siku njema.

Friday, January 15, 2010

NAJIVUNIA KUMFAHAMU

Alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuniandikia email binafsi akinikaribisha katika ulimwengu huu wa blog, hiyo ni baada ya kusoma ujio wa blog yangu na kutoa maoni yake akinitia moyo.
Kama haitoshi kaka yangu huyu alidiriki kuitangaza blog hii ya Vukani kupitia blog yake ili kuiweka katika ramani ya ulimwengu wa wanablog,
Alizaliwa Aug 10, miaka thelathini iliyopita katika hospitali ya Brackenridge iliyopo AUSTIN, TEXAS. U.S.A
Brackenridge Hospital. Austin, TX (kama ilivyoonekana Aug 1980)
Ni mtoto wa tatu kati ya watano katika Familia ya Mzee Simon na Mama Paulina. Ametanguliwa kuzaliwa na Dada wakubwa wawili na kufuatiwa na kaka zake wadogo wawili (mapacha)

Familia nzima atokayo kijana huyu.
Alianza shule ya awali maarufu kama "vidudu" Lutheran Junior Seminary mpaka alipojiunga darasa la kwanza Shule ya Mazoezi Kigurunyembe. Baadae alihama na wazazi wake kwenda Nachingwea Lindi na kujiunga na Shule ya Mazoezi Nambambo, shule ambayo ndipo alipomaliza elimu ya msingi.
Elimu yake ya Sekondari aliipata katika shule za Ndanda Masasi Mtwara na Ihungo na Iluhya zilizopo Bukoba Kagera. Kisha akaenda Dodoma kwa mafunzo ya ufundi katika fani ya ufundi mitambo, utengenezaji vipuri na ukerezaji (Fitter Mechanics) ambayo aliisomea kwa miaka minne na kupata Grade One. Pia akiwa hapo chuoni alijifunza Ufundi Magari (Motor Vehicle Mechanics)
Alirejea Dar na kuendelea na pilika nyingine na mwaka 2001 alipata kazi katika kituo cha redio maarufu cha 100.5 Times Fm ambapo alikaa mpaka mwaka 2003.

Kaka yangu huyu hakuridhika na maaarifa aliyokuwa nayo hivyo aliondoka nchini na kuelekea nchini Marekani, nchi ambayo ndipo alipozaliwa ili kutafuta maarifa zaidi.
Kwa sasa yuko shule nchini humo akichukua masomo ya awali ya fani ya UHANDISI, huku pia akifanya kazi ambayo haiko mbali na fani hiyo. Ni mtengeneza vipuri katika kiwanda kinachojishughulisha na vipuri vya ndege cha Eaton Aerospace kilichopo Beltsville Maryland.
Nilipofanya mahojiano naye alikiri kuipenda zaidi fani ya uandishi wa HABARI na UHANDISI na anajitahidi kuchukua masomo ya wali yatakayomuwezesha kuunga fani zote.
Kwa upande wa starehe alisema kuwa yeye sio aina ya vijana wanaopenda kujirusha au kuendekeza starehe, bali ni kijana mwenye kipaji halisi cha uandishi wa habari za kijamii, uchambuzi katika medani ya kisiasa na kiuchumi pamoja na habari za kisaikolojia kupitia ukurasa wake binafsi maarufu kama Blog na kama akikereka, kufurahi, kusikitika au akiwa katika mood yoyote ile anapenda zaidi kusikiliza muziki wa kihisia, maarufu kama Reggae.
Anasema muziki huu HUFUNZA, HUBURUDISHA NA KUIKOMBOA JAMII TOKA UTUMWA WA KIAKILI.
Pia alikiri kuwa kwa sasa anayo familia, akiwa na mpenzi wake wa tangu mwaka 2001 aitwae Esther na hivi karibuni wamepata baraka ya mtoto mmoja aitwae Paulina Arianna.
Katika maisha tunayoishi yapo matukio ambayo hututokea, yapo ya kufurahisha na ya kukera au ya kuhusunisha. Mengine unaweza kuyasahau na mengine ni vigumu kuyasahau. Tukio ambalo kaka yangu huyu itakuwa ni vigumu kulisahau ni lile la ajali aliyoipata Disemba 22, 1999 nchini Kenya katika eneo la Nakuru kilomita chache kutoka jijini Nairobi, wakati alipokuwa akisafiri kuelekea Bukoba kula sikukuu na wazazi wake.
Ajali hiyo ambayo ilihusisha basi la Tawfiq na lori ambalo lilipaki njiani ilisabababisha vifo vya watu zaidi ya 20 na kuacha majeruhi kadhaa akiwepo yeye ambapo amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo hadi leo, unaweza kuBOFYA HAPA ili kujua yaliyomkuta kaka yangu huyu.
Ni jambo la kujivunia kwamba pamoja na ajali hiyo ameweza kusimama na kuendelea na shughuli zake huko ughaibuni huku akiendelea kubukua kwa ajili ya kujikusanyia taaluma ili aweze kuisaidia jamii hii ya Kitanzania na dunia kwa ujumla.
Najivunia sana kumfahamu na najivunia kupendwa na yeye kwani kwangu mimi huyu ni zaidi ya kaka na nimenufaika sana na mchango wake, kwani ametumia muda wake mwingi kunikuza katika tasnia hii ya blog.
Napenda kumuombea maisha marefu yenye baraka na fanaka ili atakaporejea nchini tupate kufurahi kwa pamoja na kumshukuru mungu, maana neema zake ni za milele.
Ahsante sana kaka Mubelwa Bandio nashukuru kukufahamu

Monday, January 11, 2010

ILIKUWA NI SAFARI ILIYOJAA VITUKO

Ni mara yangu ya kwanza kusafiri kwa ndege kwenda nchi ya mbali, kwani nchi ambayo niliwahi kwenda kwa ndege ni Afrika ya Kusini tu. Ni safari ya ghafla mno ambayo sikuitarajia. Niliondoka jijini Dar mida ya saa nne usiku na ndege ya KLM, hadi Amsterdam, pale niliunganisha ndege nyingine hadi Stockholm Sweden katika uwanja wa ndege wa Arlanda. Hali ya hewa hapa ni ya baridi kweli na ingawa nilibeba makoti mazito ya baridi lakini nilihisi baridi ikipenya katika maungo yangu barabara.

Nilichukua taxi hadi kwenye Hoteli ambayo baba yangu alinifanyia booking. Safari yenyewe ilikuwa haijafika ukingoni kwani nilitakiwa kesho yake nisafiri kwa treni kwenda mji wa Uppsala ambapo ndipo chuo nilichotarajiwa kujiunga nacho kilipo.

Nililala pale na siku ya pili niliondoka na taxi hadi kituo cha treni ambapo kwa msaada wa dereva wa taxi nilikata tiketi yangu na kuingia kwenye treni. Ilituchukua takribani dakika arobaini na tano kufika katika huo mji, naambiwa kuwa kwa kawaida ni nusu saa tu, lakini kutokana na hali ya barafu iliyojaa katika njia ya reli ilibidi tutumie hizo dakika arobaini na tano.
Nilifika katika huo mji wa Uppsala na kuchukua taxi ambayo ilinipeleka hadi chuoni, na nilipoangalia saa yangu ilinionyesha kuwa ni saa sita za mchana, niliopokelewa na kupelekwa ofisini kwa mkuu wa chuo ambapo nilipata maelekezo yote ya pale chuoni kisha nikakabidhiwa kwa mama mmoja wa makamu ambaye nadhani ndiye msimamizi wa zile apartment pale chuoni, alinipeleka hadi kwenye chumba changu ambapo nilimkuta binti mwingine ambaye alijitambulisha kwangu kuwa ni raia wa Finland, tulisalimiana na akapewa maelekeza kuwa tutakuwa tukiishi pamoja katika chumba kile hadi tutakapomaliza masomo. Kusema kweli alinipokea kwa bashasha, na kutokana na kusikia sifa nyingi juu ya nchi yangu ya Tanzania pamoja na sifa za mlima Kilimanjaro, binti huyu alikuwa ana hamu ya kutaka kujua mengi juu ya mlima huo na pia mbuga zetu za wanyama.
Binti wa kizungu akaanza maswali yake akitaka kujua habari za mlima huo uko upande gani wa nchi yetu, una urefu gani, ukitaka kupanda itakuchukua muda wa siku ngapi, je mbuga za wanyama nazo, ziko ngapi, ukitaka kwenda utafikaje, na itakugharimu kiasi gani kulipia kiingilio ili mradi yalikuwa maswali lukuki.

He! wenzangu nikaona naumbuka sasa, nilichojibu ni upande ambapo mlima Kilimanjaro upo ambapo ni mashariki mwa nchi yetu yaani mkoani Kilimanjaro, mengine nilitoka kapa, na kuhusu mbuga za wanyama nilizungumzia tu mbuga ya Ngorongoro ambayo niliwahi kuitembelea mwaka jana mwanzoni, zaidi ya hapo maswali mengine nilimwahidi kumjibu wakati mwingine, kwani nilijifanya kuwa nimechoka na safari, lakini moyoni nilipanga nikipata muda niende ubalozini kwetu nikatafute zile taarifa ili kuepuka fedheha ugenini, maana hawa wazungu wanadhani kwa kuwa nimezaliwa Tanzania basi nafahamu kila kitu.

Kwa kuwa ilikuwa ni ijumaa hapakuwa na ratiba yoyote kwa sababu chuo ndio kilikuwa kikiendelea kupokeaa wanafunzi kutoka nchi mbalimbali. Niliamua kujipumzisha kidogo.Niliamka majira ya saa kumi jioni, nikaelekea katika café ya pale chuoni ili kupata kahawa kupunguza baridi, nilipofika pale café niliona call box, nikaona huo ndio wakati muafaka wa kumpigia dada yangu Yasinta simu ili kumjulisha kuwa niko Sweden kwa masomo.

Kwanza dadaYasinta hakuamini alidhani namtania, lakini baada ya kumweleza mahali nilipo yaani Uppsala aliniamini na aliniahidi kunifuata siku inayofuata yaani jumamosi ili anipeleka kwake. Dada Yasinta alifurahi sana na hata baada ya kuongea naye kwa simu nilipotoka pale nilirudi chumbani kwangu na kwa kuwa pale chumbani kwetu kuna computer room, niliingia hapo tukachat kwa takriban masaa matano, tulizungumza mengi na aliniambia kuwa familia yake imefurahia ujio wangu kwani hatimaye sasa watamuona Koero live.

Ni kweli siku iliyofuata majira ya saa nne, nilikuwa bado niko chumbani kwangu nikipitia makabrasha ya maelekezao ya namna ya kuishi pale chuoni pamoja na malezo mengine juu ya kozi yangu nitakayoichukua. Ghafla nikapigiwa simu na sekretari wa mkuu wa chuo kuwa nina wageni wako mapokezi.
Nilitoka haraka kwani nilijua tu kuwa huyo angekuwa ni dada Yasinta. Anitembeee nani hapa Sweden zaidi yake? Nilipokaribia mapokezi nilimuona dada Yasinta akiwa na mumewe na nyuso zao zilikuwa zimepambwa na tabasamu pana, walikuwa wamesimama mahsusi kunipokea na nilipowafikia dadaYasinta hakusubiri, alinirukia kwa furaha na kunibeba, na hivi nina kamwili kadogo , alinibeba utadhani mama aliyembeba mwanaye, kila mtu pale mapokezi alishangaa, lakini mumewe yaani baba Camilla alisema kitu kwa kiswidish, nadhani alikuwa akiwaeleza jambo kuhusu mimi.

Tulizungumza kwa kifupi na bila kupoteza muda niliomba fomu maalum ya kuomba ruhusa ya kutoka nje ya chuo na baada ya kuijaza fomu hiyo tuliondoka pale chuoni na gari walilokuja nalo wenyeji wangu. Njiani tulizungumza mambo mengi sana juu ya blog zetu, tuliwazungumzia wana blog wenzetu kina kaka Mubelwa, Kamala, Kitururu, Markus aka Mcharuko, Da’ Subi, Da Mija, Da Schola Mbipa, kaka Bwaya, Da’ My little world, Ka Godwin Meghji, na wengine weeeengi tu.
Ingawa safari ilikuwa ni ndefu kiasi, lakini niliiona fupi kutokana na mazungumzo. Tulipofika nyumbani nilipokelewa na Camilla na Erik kwa bashasha na walinifurahia sana. Nyumba yao ni nzuri ikiwa imezunghushiwa uzio mfupi hivi huku ikiwa imenakshiwa na maua ambayo yalikuwa yameanza kunyauka kutokana na barafu, tulipoingia ndani nilikutana na hali ya joto kutokana na hita zilizowashwa ili kupunguza baridi.
Dada Yasinta alitengeneza chai haraka haraka na tukajumuika pale mezani kupata chai huku tukiendelea na mazungumzo, pamoja na kwamba kuna dinning room lakini jiko la dada Yasinta ni kubwa kiasi kwamba kulikuna na meza kubwa na viti ambapo hutumika wakati mwingine kwa ajili ya kulia chakula pale pale jikoni.

Nililipenda sana jiko lao na mpangilio mzima wa nyumba yao. Tulizungumza sana na kutaniana na shemeji yangu huku dada Yasinta akiandaa chakula cha mchana.Dada Yasinta alinifahamisha kuwa jioni walikuwa na mpango wa kwenda kucheza mchezo wa kuteleza kwenye barafu, yaani skiing, waliniuliza kama nitaongozana nao, niliwakubaliana na walifurahi sana.

Jioni ilipofika tulifungasha mizigo yetu ambapo ilikuwa ni vifaa vya kutelezea katika barafu, kisha tukaondoka na gari hadi kwenye eneo linalotimika kwa mchezo huo, tulipofika tulikuta watu wengi sana wakicheza mchezo huo, Muafrika nilikuwa ni mimi na dada Yasinta pekee wengine walikuwa ni wazungu watupu. Tulivaa vifaa vyetu na kutokana na kuwa mgeni wa mchezo huo, Dada Yasinta alinielekeza namna ya kutumia vifaa hivyo , kisha tukaanza kuteleza.

Ingawa nilikuwa nikianguka mara kwa mara, lakini shemeji yangu Torbjorn alikuwa akinisaidia kuninyanyua na kuniekeleza namna ya kutumia vifaa hivyo, mpaka nikamudu. Nilikuwa nateleza kwa uhodari mpaka kila mtu akawa ananishangaa.

Nilikuwa nateleza kwa kasi sana, mara nikajikuta nikiwaacha wenzangu hatua kadhaa nyuma, mara ghafla nikajikuta nikielekea kwenye mteremko mkali, nilishindwa kujizuia, kumbe kulikuwa na kibao kilichokuwa kikitahadharisha kuwa mbele ya lile eneo kuna bonde na ilikuwa hairuhusiwi kuvuka pale, nilisikia watu wakipiga kelele nyuma yangu lakini nilishindwa kujizuia, nikajikuta naelekea bondeni , “ mama wee nakufaaaaaa” nilipiga kelele, lakini ghafla nilisikia mtu akiniita kwa sauti “Koero nini” Nilishtuka na kuamka, huku mapigo ya moyo yakinienda mbio na jasho likinitoka, nilimuona mama akiwa pembeni yangu.
Kumbe nilikuwa nimelala na ile ilikuwa ni ndoto tu. Mama alinijulisha kuwa nilikuwa nikipiga kelele mpaka wakaamka wakidhani labda nimevamiwa. Kwa kuwa huwa sifungi mlango wangu wa chumbani. ilikuwa ni rahisi kwake kuingia chumbani kwangu ili kuangalia kama nimepatwa na nini.

Nilipoangalia nje kulikuwa kumepambazuka, nilimuomba mama maji ya kunywa na na baada ya kunywa, nikamsimulia juu ya ile ndoto. Mama alicheka sana akanimbia kuwa ni kweli baba amenitafutia chuo nje ya nchi na si muda mrefu nitaondoka nchini kwenda kukariri ujinga wa wengine.

Saturday, January 9, 2010

DICKSON, KWA NINI ULINITENDEA HIVI?

Ni saa kumi jioni, ndio nimeamka kutoka katika usingizi wa mchana. Hapa nilipo nimesimama dirishani, nikitazama mandhari ya huko nje, kuna manyunyu kiasi na ngurumo za hapa na pale.

Hali ya hewa imebadilika katika jiji hili la Dar na kuna hali ya kijiubaridi kwa mbali na hali ya mvua za kiasi na hivyo kupunguza hali ya joto ambalo limekuwa ni la kutisha lisilo na mfano utadhani tupo katika nchi ya Sudan au Chad, naambiwa kuwa hali ya joto imefikia kiasi cha digrii 37, hiki ni kiwango cha kutisha sana tofauti na miaka ya nyuma.

Siku ya leo sikwenda kazini nilijihisi kuwa na homa ya malaria , nikaona ni vyema nikapate matibabu, na baada ya matibabu nikaona nijipumzishe.Kupitia dirishani, nawaona watoto wakicheza mpira, huku wakifurahia hii hali ya manyunyu. Wanacheza kwa furaha huku wakicheka, nadhani ni kutokana na hii hali ya hewa. Nikiwa bado nimewatumbulia macho, mtoto mmoja anaupiga mpira na kuingia ndani ya uzio wa nyumba yangu, kutokana na kuvutiwa na mchezo wao nikaamua kutoka na kuwarudishia mpira wao, nilitamani waendelee kucheza, kwani nilivutiwa sana na watoto wale kwa jinsi walivyokuwa wakicheza kwa furaha.

Baada ya kuwarudishia mpira wao, walinishukuru na kunishangilia kisha wakaendelea na mchezo wao. Ilionekana walifurahishwa na kitendo changu hicho.

Dickson, nimeamua kuchukua karatasi na kalamu ili kukusimulia haya kutokana na uchungu nilio nao, uchungu ambao kamwe sijui kama nitakuja kuusahau. Kidondo ulichoniachia bado hakijapona na kila uchao maumivu yako pale pale. Kwa kifupi sijapata tiba na sijajua ni lini kidonda hiki kitapona.

Dk, kama nilivyozoea kukuita wakati ule wa kilele cha mapenzi yetu, naomba nikuite kwa jina hili katika waraka huu, naamini haitakuwa ni tatizo kwako. Ni mwaka wa kumi sasa tangu uliponiacha na kuoa mwanamke mwingine eti kwa sababu sikubahatika kukuzalia mtoto. Pamoja na kunieleza kuwa ilitokana na shinikizo la wazazi wako, lakini naamini wewe ndiye uliyekuwa na uamuzi wa mwisho wa kuamua hatima ya mapenzi yetu. Kuwasingizia wazazi na ndugu zako naamini haikuwa ni sababu stahili ya kukwepa lawama. Dk, naomba ukumbuke kiapo chetu, uliniambia kuwa mimi na wewe mpaka kufa, lakini mbona bado tuko hai, lakini umeniacha, Dk, kwa nini lakini?

Kumbuka kwamba matatizo niliyokuwa nayo, wewe ndiye chanzo chake, na ni wewe uliyenishawishi hadi kufikia uamuzi ambao ndio uliosababisha mie kutopata mtoto.
Ilikuwa ni mwaka 1990, tulikuwa ndio tumengia kidato cha sita, na tulikuwa katika kilele cha mapenzi yetu. Ni katika kipindi hicho ndipo nilipojihisi kuwa mjamzito. Nilipokueleza ulishtuka sana, na ulinieleza kuwa hutarajii kuitwa baba kabla ya kumaliza masomo, ulinishawishi tuutoe ujauzito ule ili kuninusuru niendelee na masomo, ulidai kuwa isingekuwa vyema nisimamishwe shule kwa kuwa mjamzito halafu wewe uendelee kusoma peke yako. Tulikuwa tumejiwekea malengo, kuwa tuhakikishe tunasoma mpaka chuo kikuu, hukutaka tutibue malengo yetu.

Nilikupinga kwa maelezo kuwa hata nikisimama shule bado nitakuwa na nafasi ya kudurusu kidato cha sita baada ya kujifungua na nikakuhakikishia kuwa hata kama ukinitangulia sio vibaya, nitahakikisha namaliza chuo kikuu na kutimiza ndoto zetu. Ulinipinga sana, na baada ya kuvutana kwa muda mrefu huku miezi ikiendelea kuyoyoma hatimaye niliamua kukubaliana nawe, na tukiwa pamoja tulikwenda kuutoa ujauzito ule uliokwisha fikisha miezi minne.

Haikuwa kazi rahisi, kwani daktari aliyefanikisha operesheni ile hakuifanya kwa ufanisi kwani hata baada ya kurudi nyumbani hali yangu haikuwa nzuri, niliendelea kusumbuliwa na tumbo. Tuliporudi hospitali nilisafishwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Tulirejea shuleni na kuendelea na masomo hadi tukamaliza kidato cha sita. Kwa bahati nzuri wote tulichaguliwa kujiunga na chuo kikuu mlimani, wewe ukisomea fani ya uhasibu na mimi nikisomea fani ya sosholojia.

Tulifanikiwa kumaliza pamoja na kufaulu, tulifanya sherehe ya pamoja na kuingia katika ajira pamoja, mimi nikiajiriwa serikalini na wewe ukiajiriwa katika shirika la Umoja wa Mataifa {UN}.

Baada ya miaka miwili tangu kuingia katika ajira, tuliamua kufunga ndoa ambayo ilikuwa na mbwembwe nyingi. Maisha yetu ya ndoa yalikuwa ni ya upendo na amani. Sio kwamba tulikuwa hatugombani, la hasha, tulikuwa tunagombana lakini hiyo ilikuwa ni njia mojawapo ya kustawisha mapenzi yetu, kwani kupitia kugombana kwetu, tulipata fursa ya kila mmoja kufahamu hisia za mwenzie.

Mwaka mmoja tangu tufunge ndoa tuliamua kuzaa mtoto, na baada ya majaribio kadhaa kushindikana tuliamua kwenda kwa watalamu wa tiba ili kupata ushauri. Ni katika kipindi hicho ndipo tulipopata taarifa ambazo zilinipenya moyoni kama msumari wa moto. Tuliambiwa kuwa siwezi kupata mtoto milele kwa kuwa mirija yangu ya uzazi imeathirika baada ya kile kitendo cha kutoa mimba tulichokifanya wakati ule.

Hatukata tamaa, tuliwatembelea wataalamu kadhaa wa tiba wakiwemo wa tiba za asili lakini hatukufanikiwa kupata mtoto. Miaka minne baadae tangu tuoane ndugu zako walianza manung’uniko ya chinichini, lakini hata hivyo walifikia hatua ya kunieleza waziwazi kuwa mimi ni mgumba siwezi kukuzalia mtoto, maneno hayo yalinichoma rohoni, lakini nashukuru ulikuwa pamoja nami na uliniahidi kunilinda. Hukuishia hapo ulifikia hatua ya kula kiapo kuwa mimi na wewe mpaka kufa.

Nilifarijika na msimamo wako, na ulinipa nguvu kila wakati. Mwaka mmoja baada ya kiapo chako ulianza kubadilika, ulikuwa ukichelewa kurudi nyumbani na nikikuuliza majibu yako yalikuwa ni ya mkato. Chakula ulikuwa huli nyumbani na kama hiyo haitosh ulifikia hatua ya kunipiga kwa sababu ya kukumbusha kule tulipotoka. Mateso yalizidi sana na ndugu zako walikuja kunieleza wazi kuwa unarajia kuoa hivyo nijiandae kuwa na mke mwenza, kwa kuwa huyo mchumba wako ameshakuzalia mtoto wa kiume.
Dk, umesahau kuwa hata mie kama nisingetoa ule ujauzito ningekuwa na mtoto wa kiume kama alivyotueleza yule daktari, na uamuzi wa kutoa ule ujauzito haukuwa ni wangu bali ilitokana na shinikizo lako.

Nilipokuuliza kuhusu wanavyosema ndugu zako, ulinijibu kwa mkato kuwa ni kweli na ulidai kuwa haikuwa na ubaya wowote kwa kuwa amekuzalia mtoto, kitu ambacho mimi nimeshindwa.

Nililia kwa uchungu sana na niliamua kuondoka, sikutaka kuishi na mke mwenza kwa kuwa hiyo ni kinyume na mafundisho ya dini yetu ya kikristo. Nilifanya juhudi za kutafuta suluhu kupitia kwa mchungaji wetu lakini haikuzaa matunda na hatimaye tukatengana, na wewe kumuoa huyo binti aliyekuzalia mtoto.

Sikukata tamaa, niliamini tu kuwa iko siku nitakuja kupata mtoto siku moja. Mwaka jana niliamua kwenda nchini Afrika ya Kusini, hiyo ni baada ya kushauriwa na baadhi ya madaktari bingwa, na nilipofika kule nilipatiwa matibabu na kupandikizwa ujauzito. Hivi ninavyokuandikia waraka huu ninao ujauzito wa miezi saba, na ninatarajia kupata mtoto wa kiume mungu akinijaalia.

Hiyo yote ni kutaka kukuthibitishia kuwa kwa mungu kila jambo linawezekana. Nilipokuwa nikiwaangalia wale watoto waliokuwa wakicheza mpira, nilikuwa nimeshika tumbo langu na nilihisi mwanangu na yeye akirukaruka kwa furaha akifurahia kile ninachokiona kupitia kwangu. Naamini na yeye atakuwa ni mchezaji mpira mahiri, kwa kuwa mama yake pia ni mshabiki wa mpira wa miguu.

Naomba nihitimishe waraka huu kwa kukutakia maisha marefu ili uje kushuhudia miujiza ya Mwenye enzi mungu, kwamba kwake yeye kila jambo linawezekana.

Ni mimi mke wako wa zamani.

Kolambo Kiangi

Ndugu Msomaji, jana nilimtembelea shangazi yangu, nilimkuta amesimama dirishani akiangalia watoto wakicheza mpira. Shangazi yangu huyu amepambana na mikasa ya dunia, na baada ya kuzungumza naye ndio nikaona niandike huu waraka.

Ni mkasa wa kweli uliompata shangazi yangu, nami kwa kutaka kufikisha ujumbe kwa njia ambayo itamuwezesha msomaji kujifunza, ndio nikaandika waraka kwa mtindo huo.

NB: Jina la Dickson sio la muhusika.

Thursday, January 7, 2010

MAJIBU YA DADA SUBI KWA BARUA YANGU

Dada Subi

Kama kumbukumbu zenu haziko mbali, ni kwamba mwaka jana nilimuandikia dada yangu Subi barua ya siri nikimjuza hali halisi ya huku nyumbani na maandalizi ya uchaguszi mkuu octoba mwaka huu, kwa yule asiyekumbuka anaweza kujikumbusha kwa kubofya hapa.

Na haya ndiyo majibu ya dada Subi katiaka kujibu bara yangu. Ni jambo la kujivunia kuwa kumbe dada yangu huyu aliipata barua yangu na kupata muda wa kukaa chini na kunijibu barua yangu.

Naomba muunganr nami katia kuisoma barua hii……………………

Mpendwa mdogo wangu Koero,
Salam sana. Na baada ya salam, natumai u mzima wa afya. Ni matumaini yangu kuwa ndugu na jamaa zetu hapo Kijijini ni wazima na wanaendelea vizuri kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

Dhumuni la kuandika barua hii ni kupenda kukushukuru sana kwa barua yako uliyoniandikia tarehe 16 mwezi wa Disemba 2009 na kunieleza mengi ya hapo Kijijini. Mara ya mwisho nimepata ujumbe toka nyumbani ni pale kaka Mtoahanje aliponitumia ujumbe kuwa ametindikiwa fedha kiasi za kulipia ada ya shule, nikaahidi kumsaidia kadiri ambavyo ningeweza. Sasa umenieleza tena kuhusu hali ya henia ya babu, nilijitahidi sana kuwasiliana na Mbega kuhusu suala hilo siku mbili tu baada ya kusoma ujumbe wa Mtoahanje lakini kwa habati mbaya, Mbega amekuwa msemaji sana siku hizi kuliko mtendaji, si kama vile alivyokuwa kijana mdogo na mchapakazi. Nitajitahidi sana niwasiliane na rafiki yangu Mwelumbini, yule mototo wa mzee Shelukindo tuliyesoma naye wote Mazoezi, angalao aweze kufika na kumwona Mzee na kutafuta tiba inayofaa.

Nimefurahishwa sana na maendeleo ya usafiri kutoka baiskeli hadi pikipiki lakini nimehuzunishwa sana na mambo vijana wa mtaani wanayowatendea dada na mama zetu huko njiani. Juzi juzi hapa, rafiki yangu alipiga simu akaongea na Bibi yake ndipo aliposimuliwa masahibu yaliyompata siku moja akirejea toka shambani alikokuwa amekwenda kufunga majani ya wale ng’ombe wake (hawa wazazi wetu na ng'ombe hawaachani hata uwaagizie pikapu ya maziwa kila siku asubuhi). Basi alipokuwa katika kijia pale Komkonga, ghafla akatokea kijana mmoja wasiyefahamiana, na katika kupishana, salam akampa, ‘emcheku, urevedi?’, bibi akaitika, ‘ni jedi’, huku wakipishana kila mtu kuelekea upande wake. Sasa kwa kuwa wazazi wetu huwa na hisia za ziada, baada ya mwendo wa hatua chache, bibi alihisi kuwa kuna mtu anamfuata nyuma, lakini akapuuzia kidogo, Kabla ya kuendelea na umbali wowote wa kuhesabika, Bibi akastukia kanigwa shingoni na kupigwa ngwala, akaanguka chini pu! Majani aliyokuwa amebeba kichwani yakaanguka na kunde alizokuwa amefungia humo zikamwagika na kusambaa majanini. Kumbe kijana alikuwa amejiandaa tayari kwa kumbaka BIbi. Kwa bahati Bibi ujasiri ukamjia, akajitahidi akafungua mdomo wake kisha akamuuma kwa nguvu kweli sehemu ya mkono (kwa kuwa alizibwa mdomo na yule kijana kwa kutumia sehemu ya mkono), ndipo yule kijana alipoondoa mkono wake na kuugulia maumivu, Bibi akabeba jiwe moja la moram lililokuwa pembezoni hapo kijiani, akamkoboa nalo yule kijana kwenye kipaji cha uso upande wa kushoto. Bibi naye amekula chumvi nyingi, hivyo alijua haswa pa kuumiza, wala hakufanya ajizi. Baada ya hapo akajitahidi kupiga ukelele kwa sauti kubwa, ndipo kijana akaogopa na kwa haraka akajivuta na kukimbia, akatokomea katikati ya shamba la mahindi. Ndipo bibi akanyanyua mzigo wake wa majani, akaufunga tena vizuri pamoja na kunde chache azizoweza kusomba pale kijiani, akaendelea na safari ya kurudi nyumbani. Hivi ninavyokueleza, si kisa cha kutunga hiki, ni kweli kimemtokea huyu Bibi na alama ya jino lake dhaifu kumeguka baada ya purukushani na kumuuma yule kijana bado ipo, ndiyo sababu ya maumivu yake ya jino na kichwa hadi leo.

Hali hiyo imenishangaza sana kwani bado inaendelea japo viongozi wapo. Kwani Mzee Mkiramweni siku hizi hawamsikilizi tena anapotoa maagizo? Na vijana wanashindwa kwenda mashambani kulima au katika biashara sokoni wao wanakalia kusubiri wasafiri tu na kisha kuwabaka? Hali haikuwa nzuri wakati sisi tunakua, nakumbuka hivi vituko vya kubaka tulikuwa tukivisikia kwenye vile vikao vya wazee na akina mama mara kwa mara jioni pale kwa Mzee Mkiramweni kila kilipotokea kituko. Walikuwa wakiitwa vijana waliotenda haya makosa na kukalishwa kikao na kuadabishwa, sisi watoto tulikuwa tunasikia tu lakini hatuelewi yanayojiri kikaoni. Ila kwa wakati huu, hali inazidi kuwa mbaya na cha kusikitisha zaidi, hakuna anayewasikiliza akina Mzee Mkiramweni tena. Tunakoelekea nako yaonesha ni kubaya zaidi.

Sasa leo mdogo wangu Koero, wacha niishie hapa. Haya mengine nitayajibu nitakapopata nafasi ya kuketi tena chini kitako kwani muda huu zimebaki dakika chache kabla ya muda wa kwenda kibaruani haujawadia. Huku ng’ambo inabidi kufanya kazi kwa juhudi kweli na maarifa mengi ili kukwepa hatari ya kupoteza kazi na kukumbwa na adha ya kutafuta kazi, wakati mwingine hata yabidi kufanya kazi tatu kwa siku alimradi kujipatia fedha ya kuweza kumudu mahitaji muhimu kama vile kodi ya pango, gharama za umeme, maji na hata usafi wa mazingira ya nyumba. Kila kitu huku ni pesa na pesa yenyewe ina thamani sana, upatikanaji wake mgumu na kadiri uthamani wake unavyozidi, ndipo upatikanaji wake unavyokuwa mgumu na vitu kuuzwa kwa bei ya kuruka. Siku utakapokuja huku utaweza kujionea mwenyewe na kufahamu ni kwa nini inatuwia vigumu kuwasiliana nanyi mara kwa mara.

Nisalimie sana Babu, Bibi na akina shangazi na mjomba, hasa yule mjomba Eliewaha wa kule bonde la mpunga. Nisalimie pia rafiki zangu hapo kijijini, usisahau kuwaambia kuwa bado ninawakumbuka sana.

NB: Utakapoandika tena, ukumbuke kunitumia namba ya simu ya dukani kwa Mangi ili nikipata nafasi nipige simu niongee nanyi niweze kusikia sauti zenu.

Wasalaam,
Dada yako akupendaye,
Subi

Monday, January 4, 2010

HAIKUWA BAHATI, BALI MKOSI-SEHEMU YA MWISHO


ILIPOISHIA........

Kwa kifupi nilianza uhusiano na yule mzee na alinishauri niache kazi kisha akanitafutia nyumba kubwa nzuri maeneo ta Mikocheni.

ENDELEA KUSOMA HAPA..........

Nililazimika kuacha kazi baada mpenzi wangu kunifungulia miradi ya Duka la nguo (Boutique) maeneno ya Msasani na Salon ya kike kubwa na Mini Super market, na miradi yote hiyo ilikuwa maeneo ya Kinondoni.

Kwa mida mfupi maisha yangu yalibadilika na kuwa ya juu, nilikuwa namiliki magari matatu ya kifahari na na nilinunua Kiwanja maeneo ya Mbezi beach na kuanza ujenzi bila kumshirikisha yule mzee, ambaye ndiye mfadhili wangu.

Siku moja jioni nakumbuka ilikuwa ni Jumapili wakati nikiwa nimejipumzisha nyumbani, nilisikia mlango ukibishwa hodi, nilimtuma mfanyakazi wangu wa pale nyumbani akafungue mlango. Mara aliingia mama mmoja wa makamo hivi.

Alikuwa ni mama wa heshima, nilikmaribisha sebuleni na kumuuliza kama angependa kinyaji gani, alikataa kupewa kinyawaji chochote, lakini alionekana kuzungusha macho huku na huko kama vile alikuw aanakagua kitu, nilimuacha amalize hamu yake kwani nilidhani alivutiwa na mapambo ya pale sebuleni.

Baadae alisema, “Nadhani wewe ndiye Gifti kama sjakosea” nilimjibu kwa utulivu kuwa ndiye mimi….alishusha pumzi na kusema, “Je unamfahamu Mzee Alex?” Nilishtushwa na swali lile na nilijihisi mapigo ya moyo wangu yakienda mbio, lilikuwa ni swali la Kushtukiza sana. Nilijikakamua na kumjibu kuwa simfahamu mtu huyo.

“Sikiliza mwanangu, wewe ni sawa na binti yangu, na sijui wa ngapi, maana unaonekana kuwa bado u binti mdogo sana, kwa umri ulio nao haistahili kutembea na wanaume za watu tena baba zako ambao wanaweza hata kukuzaa, mbona vijana wenzio wako wengi tu, kwa nini usiwatafute hao, mpaka utembee na mume wangu? Nimeishi naye miaka zaidi ya 40, leo hii binti mdogo wa kukuzaa unataka kunivunjia ndoa yangu?” Aliniambia kwa upole kama vile mama aongeae na bintiye

Ukweli ni kwamba maneno yale yalinishtua sana, nilijikuta nikiwa nimemkodolea macho. Nakumbuka niliwahi kumuuliza mzee Alex kuwa familia yake iko wapi na alinijibu kuwa inaishi nchini Malawi na watoto wake wanasoma nchini Uingereza.

Nilikuwa najivinjari na huyu mzee kwa uhuru hasa na sikuwa na wasiwasi kuwa kuna siku nitakuja kukutana na mtu ambaye angekuja kunikabili na kuniambia kuwa natembea na mumewe.

“Mama samahani naona umepotea nyumba huyu mzee simjui na wala sijui unamzungumzia nani hapa,……tena nakuomba uondoke maana mume wangu atarudi hivi punde asije akakufanyia jambo ambalo utalijutia maishani mwako” Nilijikakamua na kumjibu yule mama kwa upole.

"Binti sikiliza, sipendi niingie kwenye kubishana na wewe, wakati ninao ushahidi wa kutosha kuwa unatembea na mume wangu, lakini……..sikutaka kulisema hili, ila kwa kuwa unaonekana mkaidi, nitakueleza,............ mume wangu si salama, ni muathirika, naomba ukapime afya yako, ili uanze kuishi kwa matumaini” alimaliza kusema na kunyanyuka ili aondoke.

Moyo ulinilipuka na nilijikuta nikiropoka, “He, Mzee Alex ni muathirika?” nilijikuta nikiongea kwa sauti.
"Huna haja ya kukata tamaa, bado unayo nafasi ya kuishi, nenda kapime, mimi nilijigundua miaka kumi iliyopita na mpaka sasa ninaishi kwa matumaini, hata wewe unayo nafasi hiyo” Yule mama alinijibu kwa upole na kisha aliondoka zake na kuniacha nikiwa nimeduwaa, nisijue la kufanya, nilikurupuka na kwenda chumbani, nilimeza vidonge vya usingizi na kujitupa kitandani.

Niliamka usiku wa manane kama saa nane za usiku hivi, nilikuwa na njaa, nilikwenda jikoni nikajitengenezea mkate wa nyama na juisi nikala, kisha nikakaa kitandani na kuanza kutafakari maneno ya yule mama. Niliona kama vile ile ilikuwa ni ndoto na huenda ingekwisha muda wowote, lakini hapana haikuwa ni ndoto ulikuwa ni ukweli mtupu.

Siku iliyofuata nilimpigia mzee Alex simu lakini haikupokelewa nilituma ujumbe lakini hakujibu, baadae alinijibu kuwa yuko nchini Uingereza na angerudi baada ya mwezi mmoja, kuanzia siku hiyo namba yake ilikuwa haipatikani na mawasiliano na yeye yakakatika, nikaachiwa segere nilicheze peke yangu.

Namshukuru shangazi yangu aliweza kuniliwaza na kunipeleka kupimwa na kweli niligundulika ni muathirikawa ukimwi, na ninaishi kwa matumaini sasa. Sijaanza kutumia dawa ila najitahidi sana kula vyakula vizuri na kufanya mazoezi.

Kwa kweli nina wakati mgumu sana, kwani kwa jinsi muonekano wangu ulivyo, nasumbuliwa sana na wanaume vijana na wazee, wananitaka kimapenzi na wengine wanataka wanioe, na nikiwaambia kuwa mimi si salama nimeathirika, wanabisha kabisa na wengine wanadiriki kusema hata kama nimuathirika hakuna shida hata akifa powa tu lakini atakuwa amefaidi. Yaani nashindwa kuwaamini wanaume, tena wengine wameoa na wana familia zao, lakini we kutwa kunivizia.

Namshukuru mungu nimemudu kujikubali na kuyakubali matokeo, najua ni lazima nitakufa, siku moja lakini namshukuru mungu kwa kunipa ujasiri huu nilionao mpaka sasa nimemudu kuishi kwa amani na kuepuka vishawishi.

Nawaasa vijana wenzangu hasa mabinti wa shule kuwa sio kila king’aacho ni dhahabu, ukimwi upo na unaua, tujiepushe nao.

***************MWISHO************

Saturday, January 2, 2010

HAIKUWA BAHATI, BALI MKOSI

Nikafunguliwa biashara kubwa

Tunaishi katika maisha yenye vishawishi na matamanio makubwa, kuna wakati mtu anaweza kujikuta akiwa mtegoni asijue hata kujinasua. Ama kweli dunia hii ni hadaa na ulimwengu ni shujaa, wakati unapoamini kuwa umepata bahati unaweza kushangazwa na matokeo ambayo kamwe hukuyatarajia, kuna msemo mmoja unasema kuwa kama mlango mmoja ukifungwa mwingine umefunguliwa. Kuna haja ya kuwa makini kwani kuna uwezekano huo uliofunguliwa ukawa ndio nuksi kuliko uliofungwa.
Naamini kinachohitajika zaidi ni subira kuliko kukimbilia mlango mwingine ulio wazi, kuna uwezekano kuna nyoka humo.

Hivi karibuni nilimtembelea rafiki yangu mmoja, ambaye familia yao ni family friend na familia yetu, nilipofika pale alinitambulisha kwa shangazie ambaye aliwatembelea na kutokana na uchangamfu wangu tulizoeana kwa muda mfupi, tuliongea mengi na katika maongezi yetu alinisimulia mkasa wake aliokumbana nao.
Ungana nami katika simulizi hii ya kusisimua.

Alikuja pale kazini kama mteja, lakini hilo jicho, mwenzangu mpaka niliogopa, maana jicho lake liliniganda mpaka nikaona aibu, hata hivyo alipomaliza shughuli zake aliondoka na kuahidi kurudi eti kunipa lifti nikirudi nyumbani kwangu, mwezangu nikamwambia kuwa mpenzi wangu atanifuata, hakuonekana kujali maneno yangu aliondoka na kusisitiza kurudi.

Ilipofika jioni alirudi lakini nilimkwepa na kuondoka zangu nikimwacha ndani akiongea na Bosi wangu kwani alikuwa namizigo yake na makontena Bandarini ambayo yalikuwa yanashughulikiwa na kampuni yetu kutolewa bandarini.

Siku iliyofuata alifika pale ofisini na kuniahidi kunitoa lunch katika Hoteli ya Kitalii ya Nyota Tano pale Kempinski, nilikataa ofa yake na alionekana kushangaa. Akaniambia kuwa tangu kukua kwake hajawahi kukakataliwa kitu na mwanamke, mimi nitakuwa wa kwanza kumfanyia hivyo, sikumjali sana nilimpuuza.

Baadae Bosi wangu alianza kumsifia yule mzee kuwa ni tajiri ambaye anafanya biashara katika nchi za afrika na mashariki na kati aki-supply bidhaa mbalimbali katika nchi hizo. Bosi wangu aliendelea kusema kuwa toka ameanza kufanya kazi na yeye kampuni imeingiza faida kubwa sana na kuna matarajio mazuri mwakani.

Ilipofika mchana alikuja kijana mmoja akauliza kama anataka kumuona Gift (*sio jina lake halisi) nikamwambia kuwa ni mimi, akatoa bahasha na kunikabidhi, nilipomuuliza kama imetoka wapi akanijibu kwa kifupi tu kuwa imetoka kwa mzee, kisha akaondoka zake.


Niliifungua kwa kiherehere ili kujua ina kitu gani, ndani ya bahasha ile nilkutana na cheni ya dhahabu ya Gram 10 na shilingi laki mbili, na ujumbe unaosema, “Samahani sana Gift, nilikuahidi kukutoa lunchi leo, lakini niko na kikao wizarani, nimeshindwa kutekeleza ahadi yangu, lakini hapajaharibika kitu, hiyo cheni , nilikununulia ili nikupe kama zawadi wakati wa Lunch yetu, lakini kutokana na dharura hiyo, basi pokea zawadi yangu hiyo kama ishara ya upendo nilionao kwako na hizo fedha ndio nilikuwa nimeandaa kwa ajili ya hiyo lunchi yetu, unaweza kuzitumia kwa kununua kitu chochote ukipendacho.

Nilishusha pumzi nikabaki nimeduwaa, kisha nikafyonya kwa dharau, na kuitupia ile bahasha kwenye droo ya mezani kwangu.

Jioni boy friend wangu akanifuata tukaondoka kuelekea kituoni kupanda daldala kurudi nyumbani.Kiukweli Boy friend wangu alikuwa hana kazi bali alikuwaakibangaiza kwenye ofisi ya jamaa yake fulani baada ya kumaliza masomo yake ya International Technology. Akiwa amesoma ngazi ya Diploma.

Nilikuwa na mchanganyiko wa mawazo na kutokana na mawazo hayo nilijikuta nikiwa mbali sana kiasi cha kutosikia yale aliyokuwa akiyasema Boy friend wangu, kuna wakati ilibidi anishtue kwa kuniuliza kama nimemuelewa alichokisema nilimjibu tu ndio lakini kiukweli sikumuelewa kabisa kuwa alikuwa anaongea nini.

Tulipofika Sinza ambapo ndipo ninapoishi tulishuka na kuelekea kwangu lakini karibu na nyumbani tulipisha na gari moja aina ya RAV 4, ilikuwa ikiendeshwa na kijana ninayemfahamu, alinipigia honi na kunipungia mkono, nami nilimpungia mkono. Mpenzi wangu alionekana kutofurahia kile kitendo kwani tulipofika tu nyumbani maswali yakaaza. Yule ni nani? mmejuana lini? ana uhusiano gani na wewe, mbona simfahamu? yalikuwa ni maswali mengi mfululizo ambayo sikuweza kuyajibu yote.


Tatizo la mpenzi wangu ni wivu, yaani bwana yule ana wivu utadhani dume la njiwa. Kama masihara ulizuka mzozo wa maneno kati yangu na mpenzi wangu kiasi cha kufikia kunipiga, na kisha akaondoka zake. Niliwaza sana, kwa kweli sikuwa na uhusiano na yule kijana na nilimfahamu kupitia kwa shoga yangu anayemiliki saluni ambapo ndipo ninapotengenezea nywele na yule kijana ni boy friend wake.

Nililia sana na sikuweza hata kula usiku ule nikalala na njaa. Kesho yake nikiwa ofisini yule mzee alifika tena lakini safari hii hakukaa hata kidogo, alionekana kuwa bize sana,
Ilipofika mchana Boyfriend wangu alinipigia simu lakini sikupokea, alitumia simu ya mtu mwingine kunipigia, lakini nilipopokea na kusikia sauti yake nilikata ile simu alinitumia ujumbe wa simu akiniomba radhi lakini sikumjibu, nilichukizwa sana na kitendo chake cha kunipiga siku ile.

Ilipofika jioni yule mzee akaja kunipitia pale ofisini akiwa na gari lake aina ya GX, niliamua kuondoka naye kwani alinibembeleza sana anipeleke kwangu, wakati tunaondoka nilimuona boy friend wangu akija kunifuata, nilitaka kumuomba yule mzee anishushe lakini nilisita. Yule mzee ambaye ki umri alionekana kuwa sawa na baba yangu alinifikisha nyumbani kwangu, lakini hakushuka kwenye gari, alinipa bahasha nyingine akaniambia ni zawadi yangu, nilipoingia ndani na kuifungua nilikuta dola mia mia kumi, nilishikwa butwaa.......Huyu mzee anataka nini kwangu, hivi anadhani mimi ni wa kutembea na vizee, niliwaza.

Nilishtuliwa na mtu akibisha mlangoni kwangu, nilikwenda kufungua mlango, alikuwa ni mpenzi wangu, nilishtuka sana, aliingia ndani huku akiwa amefura kwa hasira, “niliwaona sana na leo utanieleza” lilikuwa ndio neno lake la kwanza alipoingia ndani, alipitiliza hadi chumbani kwangu na zile dola zilikuwa bado ziko kitandani, nilimfuata kwa nyuma, alipoziona tu akazichukua zote.

Sasa nenda kamwambie nimezichukua na akome kutembea na wachumba za watu. aliniambia huku akizitia zile dola mfukoni, Nilijikuta nikipandwa na hasira, "Safari hii sikubali" nilijisemea moyoni, nilimrukia na kuanguka nae kitandani niliingiza mkono wangu kwenye mfuko wake alipoweka zile dola na kuzichoimoa, na yeye aliukunja mkono wangu kiasi cha kutaka kuuvunja, niliziachia zile dola zikatawanyika kitandani na pale chini, tulipigana hasa na kuvunja vitu mle ndani kosa jirani yetu mmoja kuingilia kati, tungevunja vitu vyote mle ndani.

Nilitoka na kwenda Polisi kuripoti lile tukio na nilipewa PF 3 na RB, sasa mchumba wangu alikuwa akitafutwa na Poilisi, Baada ya kusikia kuwa anatafutwa alitoweka.

Siku iliyofuata nilikwenda kazini,lakini kutokana na hali yangu iliidi niombe ruhusa ili kujiuguza majeraha ya kupigwa na mchumba wangu.

Nilipewa ruhusa ya kupumzika ya siku tatu na Bosi wangu, lakini sikwenda nyumbani kwangu bali nilikwenda kwao na mpenzi wangu Mwenge ili tuyamalize nilipofika nilimkuta shangazi yake anayeishi naye, akaniambia kuwa menzi wangu ameenda Moshi. Lakini hakumwambia shangazi yake kuwa tuligombana.

Nilimsimulia shangazie tukio zima, shangazi yake alishangazwa na habai ile na alijaribu kumpigia simu lakini simu yake ilizimwa. Niliondoka na kurejea nyumbani.
Ilipofika jioni nilisikia mlango wangu ukigongwa na nilipofungua nilikutana uso kwa uso na yule mzee, nilimkaribisha huku nikiw nimetahayari kwani sikutegeme ujio wake, nilimkaribisha ndani.
Alistushwa na hali yangu kwani macho yangu yalikuwa yamevimba na uso wangu pia, alinidadisi, nilimdanganya kama nilikutana na vibaka usiku nilotoka kwenda kununuas chipsi, alitaka kunipeleka katika Hospitali ya rafiki yake lakini nikataa kwa maelezo kuwa natibiwa na kampuni.
Hakukaa sana aliondoka, siku inayofuata alikuja asubuhi kunijulia hali na aliniahidi kunifuata mchana ili tukale lunch pamoja, nilimkubalia.

Nikweli alikuja na tulitoka pamoja hadi katika Hoteli moja iliyoko katikati ya mji, tulikula na kuongea mambop mengi sana, yule mzee a litaka kujua kama nina matarajio gani juu ya maisha yangu ya baadae nilimweleza kuwa nia yangu ni kujiendeleza zaidi kieleimu kwani elimu yangu ya kidato cha sita na diploma ya usekretari sijaridhika navyo aliniuliza kama nataka kusomea nini, nilimjibu kuwa nataka kusomea sayansi ya jamii ngazi ya shahada, aliniuliza kama ningependa kusomea nje ya nchi au hapa hapa nchini.

Nilishangazwa sana na swali lile, nilimjibu kuwa kwa kuwa sina uwezo kifedha nitasomea hapa hapa nchini, alinimabia kwa upole, “ Sikiliza Gift, kwa kuwa mimi nipo, kila kitu kinawezekana, usiwe na wasiwasi nitakusmesham tafuta shule mahali popote nitakusomesha” nilishangazwa na ukarimu wa yule mzee, na aliongea akionekana amedhamiria hasa.

Tulipotoka pale aliniambia kuwa anataka kuni-surprise, sikumuelewa kabisa, alinimbia nisubiri kidogo, tulikuwa tumesimama pale nje ya ile Hoteli na mara ikaja Toyota Rav 4 ya kijivu, na kusimama mbele yetu ilikuwa ni mpya kabisa, na yule dereva akashuka na kumkabidhi yule mzee funguo za lile gari. Yule mzee ambaye alijitambulisha kwangu kuwa anaitwa Alex, aliniuliza kama naweza kuendesha gari, nilimjibu kuwa sijui, alimuita yule dereva aliyekuja na lile gari amabye alionekana ni dereva wake na kumuamuru anipeleke kwangu na kisha anipeleke chuo chochote kizuri nikajifunze udereva.

Aliniambia kuwa lile ni gari langu ameninunulia ili kuniondolea usumbufu wa kugombea daladala.
Nilibaki nimeduwaa sikujua hata niseme nini.

Kwa kifupi nilianza uhusiano na yule mzee na alinishauri niache kazi kisha akanitafutia nyumba kubwa nzuri maeneo ta Mikocheni.
ITAENDELEA..........................

Thursday, December 31, 2009

NIMETAFAKARI MAONI YENU, VUKANI KUENDELEA KUWA MTANDAONI.

Kazi na Dawa

Ni jambo la kujivunia, kung’amua kuwa kumbe blog ya Vukani iko juu na inapendwa. Kusema kweli sikuwahi kufahamu kuwa blog ya vukani inapendwa kiasi hiki na hilo limenifanya nifikirie upya uamuzi wangu.

Ulikuwa ni uamuzi mgumu sana, lakini nimeona ni vyema niheshimu maoni ya wasomaji wa blog hii na wanablog wenzangu na hivyo nitaendelelea kublog kama kawaida. Tarajieni mabadiliko makubwa katika blog hii kwani mwaka mpya na mambo mapya…au sio?

Natoa shukrani kwa wasomaji wote, mliotumia muda wenu kutoa maoni na wengine kuniandikia email binafsi, nawahakikishieni kuwa blog ya Vukani itaendelea kuwepo kama kawaida.

Sina mengi kwa leo ngoja nijiandae kwa ujio wa mwaka mpya wa 2010.

Ahsanteni sana.

Friday, December 25, 2009

BAADA YA KUTIMIZA MWAKA MMOJA LEO TANGU KUANZISHWA KWAKE BLOG YA VUKANI KUFUNGWA RASMI LEO

Kwa herini ya kuonana

Leo tarehe 25 December 2009 Blog hii ya VUKANI Inatimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake. Ni jambo la kujivunia kwamba ndani ya mwaka mmoja nimeweza kuweka makala 100 na nimemudu kuendelea kublog hata pamoja na majukumu mbalimbli ya kifamilia niliyokuwa nayo. Nilikuwa nikisafiri mara kwa mara lakini hata hivyo niliweza kuweke post kama kawaida ili wasomaji wa blog hii waendelee kusoma ujinga wangu.

Najua tangu nianze kublog kuna watu niliwakwaza na wengine niliwafurahisha na hata kuwafikirisha, lakini halikuwa lengo langu kumuumiza mtu kihisia kwa namna yoyote ile kwani lengo la blog hii ni kuelimisha, kufikirisha, na kufurahisha. Naamini malengo ya uwepo wa blog hii yalitimia kwa kiasi fulani.

Kama nilivyosema kuwa blog hii itakuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo, naamini yote hayo yalitimia na ndio maana leo natimiza mwaka mmoja nikijivunia kile nilichokifanya hadi leo.
Najua si rahisi kufanya tathmini na kujua kama ni wasomaji au wanablog wangapi ambao kwa njia moja ama nyingine wamejifunza au wamenufaika na huu ujinga wangu, ninaouweka humu lakini naamini kwa kiasi fulani kuna wengi wamejifunza na kunufaika na uwepo wa blog hii.

Kama kumbukumbu zenu haziko mbali, kwa wale wafuatiliaji wa blog hii watakumbuka kuwa, blog hii ilianza na misukosuko mingi, kwani karibu mara mbili nilipata shinikizo la wazazi wangu kuifunga na kuachana na mambo ya kublog, baada ya kuibua hoja ya kuhoji swala zima la nadharia ya hizi dini zetu za mapokeo, kama unataka kujikumbusha bofya hapa
NIMEANZA KUZISHITUKIA HIZI DINI. Mada hiyo iliwashitua sana wazazi wangu, ambapo walinitaka niache kublog kama sina mambo ya maana ya kuandika, swala la kuhoji uhalali wa dini likaonekana halina maana.

Nililazimika kuufunga ule mjadala ili kunusuru mahusiano yangu na wazazi wangu. Mara ya pili ni pale nilipopingana na wazazi wangu juu ya swala la kuendelea na elimu, baada ya kuacha chuo na kujikita kwenye biashara zaidi, hiyo nayo ilikuwa ni changamoto nyingine, lakini kutokana na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa blog hii nilimudu kuyamaliza na hivyo kuendelea kublog kama kawaida.

Naomba nikiri kwamba uwepo wa blog hii ni kutokana na kuvutiwa na blog ya MAISHA ya dada Yasinta Ngonyani, kwani ni yeye aliyenifanya nami nianze kublog na kwa msaada wa mdogo wangu Jerome kwa utundu wake aliweza kuifungua blog hii.

Pia siwezi kuepuka kumtaja kaka Markus Honorius Mpangala aka MCHARUKO kwani na yeye kwa upande wake alichangia kuifanya blog hii ionekane kama ilivyo leo. Pia siwezi kuepuka kumtaja kaka yangu mpendwa Mubelwa Bandio kwa kuwa karibu nami akinishauri hili na lile juu ya namna nzuri ya kublog, na pia amekuwa ni mhariri wangu mahiri akinisaidia kurekebisha lugha na namna nzuri ya kujenga hoja katika makala zangu.

Salaam kwako dada yangu Yasinta ngonyani, wewe ni dada yangu mpendwa, siwezi kuwataja dada zangu Debora Damari, na Rachel bila kukutaja wewe dada yangu mpendwa. Dada kwa kweli upendo wako ni wa ajabu kwangu umekuwa karibu nami na nimekuwa nikikufanyia masihara mengi na utani mwingi licha ya kwamba umenizidi sana umri. Umekuwa ni mshauri mwema kwangu juu ya mambo mengi yahusuyo maisha. Umechangia kwa kiasi kikubwa katika kunibadili kitabia kutokana na hekima zako, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa wema wako.

Kwako dada Subi, nawe kwa upande wako ninayo mengi ya kujivunia, umenifunza mengi na umenifanya nikue kifikra, wewe umekuwa mmoja kati ya dada zangu na nimekuwa nikijivunia sana kukufahamu, pokea salaam zangu.

Kaka yangu Mbwange Simon Mkodo Kitururu, Duh! Sina la kusema, kupitia blog yako na maoni yako nimejifunza mengi. Kwani kupitia blog yako ya Mawazoni nimejifunzza kuwa hakuna lugha ya matusi, bali kuna majina yanayowakilisha viungo vya mwili, miti, wanyama na vitendo, lakini kutokana na tafsiri tulizofundishwa tumekuwa tukiamini kuwa baadhi ya majina ya viungo vya mwili, wanyama miti na baadhi ya vitendo ni matusi.

Pia siwezi kumsahau kaka yangu wa kulikoni Ughaibuni Evarist Chahali, wewe ulikuwa ni msomaji mmojawapo uliyeweka changamoto zako humu na kuibua mijadala mikubwa na hata kuleta mgongano wa mawazo, najua ni siku nyingi hatujawasiliana lakini naamini unaikumbuka VUKANI.

Kaka yangu Profesa Matondo, sijui niseme nini, lakini wewe mwenyewe unajua ni kiasi gani umenisaidia kukua kifikra, ni jambo la kujivunia kuwa pamoja na Elimu yako na shughuli zako nyingi uliweza kurudi chini na kuweza kuzungumza nami kama vile kaka azungumzaye na mdogo wake tumbo moja. Umekuwa mshauri wangu katika masuala mbalimbali ya kielimu na kijamii, heshima kwako Profesa Matondo.

Kwako kaka Shabani Kaluse, aka baba Abraham, Mzee wa Utambuzi, naomba nikiri wazi kuwa kupitia kibaraza chako nimejifunza mambo mengi juu ya utambuzi na nimebadilika sana kitabia, umekuwa ukijibu email zangu binafsi na kunishauri mambo mengi sana juu ya maisha na mafanikio. Umekuwa mhariri wangu mzuri pale ninapotaka kuweka makala za kijamii umekuwa ukinishauri namna nzuri ya kujenga hoja. Nakushukuru sana kaka kwa wema wako.

Dada Schola Mbipa, heshima kwako dada, nakushukuru kwa ushauri mbalimbali uliokuwa ukinipa ili kuiboresha blog hii.

Uuuuwiiii!!!!! Jamani nusura nimsahau Kamala Lutatinisibwa, huyu naye kwa kweli amenifundisha mambo mengi sana juu ya Utambuzi, maoni yake yamekuwa yakileta changamoto katika blog zetu hizi na kuibua mijadala ya hapa na pale, huyu ni mdau mmojawapo ambaye amenifanya nisifikirie kuacha kublog.
Ngoja niwanong’oneze siri, kusema kweli kama nikiweka makala katika kibaraza hiki halafu Kamala asiweke maoni nahisi kama mada yangu haijakamilika….LOL, kwani ni mdau mmojawapo ambaye lazima akiweka maoni utapenda kuyarudia kuyasoma mara kadhaa, sio kwa kutokuelewa bali kwa kutafakari zaidi, maoni yake mara nyingi yanafikirisha.


Najua ni wengi, wengi sana waliojitokeza katika blog hii na kuweka maoni yao au kunitumia email binafsi wakinishauri hili na lile ili kuiboresha blog hii, pia wapo waliotaka mawasiliano nami ya karibu lakini kutokana na kutingwa nimeshindwa kutekeleza hilo, lakini naomba muamini kuwa tupo pamoja.

Kwa uchache niwataje hawa wafuatao ambao kwa njia moja ama nyingine wamekuwa ni chachu ya kufanikisha uwepo wa blog hii, kaka Damas Michael, Godwin Meghji, kaka Kisima, kaka Manento Kitururu, kaka James Jim, kaka Chib, Dada My Little World, kaka John Mwaipopo, kaka Edo Ndaki, Mummy Hery, Da' Mija na wengine wengi. Niliowasahau mtanisamehe jamani nafasi ni ndogo……LOL.

Sasa naomba mniruhusu kuifunga rasmi blog hii ili niweze kufanya mambo mengine ambayo naamini yatakuwa bora zaidi ya kublog.

Ahsanteni na kwaherini wote, tutawasiliana mungu akipenda.

Ahsanteni sana kwa ushirikiano wenu katika kipindi chote nilipokuwa nikiblog.
Nawapenda wote jamani, Mungu awe nanyi milele daima…..aaaaamen

Sunday, December 20, 2009

HIVI HUYU KIJANA NI NANI?

Picha kwa hisani yake mwenyewe
Ni kijana mdogo kwa umri lakini ni mkubwa kwa umbo.
Kijana huyu ni suriama aliyechanganya kati ya makabila mawili ya Mpare kutoka milima ya upareni na Mjita kutoka kule Musoma kusikoisha vita kati ya koo za Wanchori na Wanchoka.

Alifanikiwa kupata elimu yake kupitia shule kadhaa hapa nchini kabla hajakuwa mjanja na kutowekea Ughaibuni miaka kadhaa iliyopita, akiishi katika mojawapo ya nchi za Scandinavia.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa, wakati akiwa shuleni alikuwa na kipaji maalum cha sanaa na alikuwa ni bingwa wa kucheza na misamiati na nahau. Watu waliowahi kusoma naye wanakiri kuwa alikuwa na tatizo la kutomudu kutumia Tafsida pale alipotakiwa kutoa mada fulani katika midahalo ya shule.

Tatizo hilo lilikuwa likimletea matatizo na waalimu wake kwa kuwa alionekana kama vile hana adabu japokuwa ujumbe alioutoa ulikuwa na maana sana katika jamii na wenye kufundisha na kufikirisha pia. Hata hivyo wapo waliomuelewa na wengi walijifunza mengi kupitia hoja zake hizo zilizojaa vioja. Msome kwa kubofya hapa.

Pamoja na misukosuko aliyoipata kutoka kwa waalimu wake hakukata tamaa aliendeleza kipaji chake na baada ya kutowekea ughaibuni amekuwa muelimishaji mzuri kupitia kibaraza chake alichokipachika jina la Mawazoni.

Katika kibaraza hicho amekuwa akifikisha ujumbe wake wa kuielimisha jamii kwa kutumia misamiati nahau na tilalila zake anazozijua mwenyewe na kutokana na kutotumia Tafsida wengi wamekuwa hawamwelewi kwa kuwa wakisoma kichwa cha habari tu wanachoka na wanaacha, maana tafsiri inayokwenda akilini mwao ni kitu kingine badala ya kile kilichokusudiwa.

Tatizo ninaloliona katika makala zake si lugha iliyotumika bali ni tafsiri inayokwenda vichwani mwa wasomaji kwa kukimbilia kuhukumu kichwa cha habari badala ya kile kilichomo ndani ya hicho kichwa cha habari. Kwa mfano halisi unaweza kubofya hapa au hapa.

Ni mchangiaji mzuri sana katika vibaraza vya wengine na kwa kutumia staili hiyo hiyo ya Ant tafsida, amekuwa akiwachanganya wasomaji wengi na naomba nikiri kuwa hata mimi nilikuwa ni mmoja wapo wa wale waliokuwa hawamwelewi kabisa.

Ilinichukua muda kidogo kumwelewa na kwa kutumia kamusi ya Kiswahili na vitabu mbalimbali vya Kiswahili, kikiwamo kitabu kinachoitwa Titi la Mkwe na cha Jando na Unyago, nilimudu kumuelewa kijana huyu na makala zake zilizojaa nahau na upembuzi yakinifu.

Naamini hanifahamu na mimi pia simfahamu ila kwa kupitia vibarazani mwetu tumetokea kufahamiana japo si kwa karibu sana. Pamoja na hayo bado najiuliza hivi huyu kijana ni nani?

Wednesday, December 16, 2009

BARUA YA SIRI NA USHAURI WA BURE KWA DADA SUBI

Dada Subi

Kwako dada Subi, ni matumani yangu kuwa umzima wa Afya na unaendelea na kazi zako za kila siku huko uliko. Utakapo kujua hali zetu huku nyumbani, wote hatujambo, Isipokuwa yule babu yako anayeishi kule bondeni karibu na ule muembe mkuubwa uliokuwa ukitumika kama maegesho ya baiskeli za kukodisha, anasumbuliwa sana na ile henia yake na anahitaji operesheni ya haraka. Dada unajua siku hizi sio baiskeli tena zinazoegeshwa kwenye ule muembe bali ni pikipiki maarufu kama Yeboyebo ndio zinaegeshwa na watu wanazikodisha kwa ajili ya kupelekwa wanakokwenda kwa gharama nafuu.

Lakini dada usafiri huo sio salama sana kwani kina mama na mabinti hubakwa na waendsha pikipiki wakware lakini, kesi hizi zimekuwa haziripotiwi Polisi kutokana na wanaofanyiwa vitendo hivyo kuona haya, unajua dada mtu kuwaambia Polisi wetu kuwa umebakwa ni kashfa na aibu kwani unaweza kujikuta ukizomewa mtaani baada ya polisi kuvujisha siri kuwa umeonjwa bila ridhaa yako.

Dada naona tuachane na hayo ya kubakwa, nikweleze madhumuni ya barua hii. Dada siku za hivi karibuni tumeanza kupata wageni hapa kijijini, wageni wenyewe ni wale waliokuja kijijini kwetu kwa unyenyekevu miaka mitano iliyopita wakitaka tuwape Kula ili wapate ridhaa ya kingia katika lile jumba kubwa kule Dodoma kwa ajili ya kusinzia na kujipatia posho mara mbili. Watu hao ambao wakati ule walikuja wakiwa slimu na sasa wana matumbo makubwa na mabodi gadi wa kuwalinda wamekuja na mikoba myeusi iliyosheheni vijisenti kwa ajili ya kutughilibu tena ili tuwape ridhaa nyingine ya kuendelea kula nchi ndani ya jumba kubwa kule Dodoma wakipigwa na viyoyozi.

Dada Subi kama unavyojua kuwa siku hizi mambo yemebadilika na sio kama wakati ule, wananchi wameerevuka na wanajua haki zao. Si unakumbuka jinsi viongozi wetu walivyokuwa wakipata wakati mgumu katika ziara zao kwa kupokelewa na mabango yenye ujumbe, wakati mwingine wa kejeli, na wengine kufikia kuzomewa majukwaani na wananchi tena wa kijijini ambapo awali viongozi wetu walidai kuwa watu wa vijijini ni watu wa “ndio mzee”, lakini sasa hivi wamewageuka na kuwazodoa hadharani baada ya kuchoshwa na longolongo zao.

Lakini wakazi wa Mbeya ndio walitia fora kwani wao walithubutu kupopoa mawe msafara wa mwenye nchi, ingawa hata hivyo walionja joto ya Dola, naamini unakumbuka kilichowapata masikini wale. Dada kuerevuka huko kwa wananchi kumetokana na kuangalia Luninga, si unajua Luninga ndio mwalimu mzuri wa kuelimisha jamii siku hizi. Nakumbuka matukio hayo tulizoea kuyasikia kwa majirani zetu tena kupitia redioni hasa idhaa ya Kiswahili ya BBC wakati ule wa Mwalimu, lakini siku hizi tunaona kupitia kwenye luninga zetu kila uchao, kwanini tusiige.

Kutokana na ugeni huo yule mzee Makalioni ambaye ndiye mwenyekiti wa wazee pale kijijini aliitisha kikao cha dharura ili kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuchaguliwa kwa huyo mwakilishi wetu huko mjengoni (kama yapo) ili kujua kama kuna haja ya kumpa ridhaa zetu tena.

Kwa kifupi kikao kilithibitisha kuwa kati ya yale yote yaliyoahidiwa na mwakilishi huyo kuwa atawafanyia, yaani kujenga mahosipitali kila mtaa, kujenga majosho ya ng’ombe, si unajua sisi ni wafugaji japo hatuko kama wamasai wanaohamahama, basi huyu mwakilishi aliahidi kujenga majosho ya ngombe kila kaya, kujenga barabara na vituo vya polisi kwa ajili ya usalama wetu. Pia aliahidi kutuletea wawekezaji watakaojenga viwanda na kuleta ajira kwa vijana pale kijijini ambao walikuwa wanategemea kupata kipato kwa kilimo cha jembe la mkono. Aliahidi kuleta Matrekta kwa kila mwanakijiji kama akipata ridhaa ya kuingia mjengoni.

Kikao kiligundua kuwa kati ya yote yaliyoahidiwa na mwakilishi huyo ni asilimia 0.006 tu ndiyo yaliyotekelezwa mengine yaliwekwa pending kwa ajili ya kuombea ridhaa nyingine ya kuingia mjengoni miaka mitano ijayo. Ili kutuhadaa mwakilishi huyo emekuja na Katapila na sasa linatimua mavumbi hapo kijijini kwa madai kuwa wanajenga barabara, lakini kwa bahati mbaya wanakijiji wameshitukia janja yake.

Dada katika kikao hicho wazee waliazimia kuwaita vijana wao walioko Ughaibuni ili warudi kugombea nafasi ya uwakilishi mjengoni na nafasi nyingine za uongozi hapa kijijini. Katika nafasi ya uwakilishi yalijitokeza majina matatu, jina la kwanza lilikuwa la kwako, la pili lilikuwa ni la yule mtoto wa katibu kata aliyekwenda Ughaibuni miaka kumi iliyopita na kupotelea huko na jina la tatu ni la yule kijana anayezaliwa na yule fundi maarufu wa baiskeli mwenye wake wawili…….yule anayeishi jirani na Mbuyu jirani na gulio la kijiji, inasemekana kijana wake alizamia meli mara baada ya kumaliza fom foo na kulowea huko. Baada ya wazee kuyatafakari majina yote matatu, jina lako lilionekana kung’aa, baada ya kupata kura nyingi za wazee ambao wamekubaliana kuwa uitwe ili uje kugombea nafasi hiyo ya uwakilishi wa mjengoni.

Sababu kubwa iliyowavutia ni tule tumisaada twa dawa za binadamu na madawa ya mifugo ulitotuleta wakati ule ulipokuja kuwaona. Unajua mara baada ya kumwaga madawa katika ile zahanati ya kijiji sifa zako zilivuma hadi vijiji vya jirani na hivyo ukapata umaarufu wa haraka kama ule wa Nyerere wakati ule wa kumpinga mkoloni.

Sifa nyingine iliyokufanya uwe maarufu hapa kijijini ni pale ulipotoa msaada wa dharura kwa kumzalisha yule binti wa mzee mkalimbembe ambaye alipata matatizo wakati wa kujifungua kwa mtoto wake kutanguliza mkono badala ya kichwa. Kwa Juhudi zako na kwa kushirikiana na wauguzi wa zahanati ya kijiji uliweza kumzalisha binti huyo.

Sifa hiyo imekujenga sana hapa kjijini na sasa wanataka uje ugombee uwakilishi mjengoni ili uwaletee maendeleo, wazee wanadai kwa kuwa umeishi ughaibuni, utakuwa huna tamaa za kifisadi na utakuwa umeridhika sana na maisha kutokana na kuishi na wazungu kwa miaka mingi sana.

Dada taarifa hizi ni za siri na nimekutumia kupitia njia za panya kwani yule mwakilishi akijua anaweza kukuhujumu usipate viza ya kuingia nchini. Kwa hiyo kwa taarifa hii inabidi ujiandae kwani utatumiwa ujumbe muda si mrefu.

Friday, December 11, 2009

KISA CHA BARUA YA WAZI KWA YASINTA.......

Barua yangu ya wazi kwa dada yangu wa hiyari, Yasinta Ngonyani iliwachanganya wasomaji wengi hadi wengine walinitumia email ya kutaka ufafanuzi kwamba kulikoni tena mambo ya binafsi kuwekwa kibarazani?

Nilijua hilo litatokea na kweli limetokea, nimepokea email kadhaa zikinitaka nifafanue kile nilichoandika.

Kwanza naomba nichukue nafasi hii kumshukukuru dada Yasinta kwa kuniruhusu kuweka ile barua ya wazi katika kibaraza hiki nikidai kuwa namuandikia yeye. Naomba niweke wazi kwamba ile barua ilikuwa haimuhusu yeye na wala hakuwahi kuniandikia barua yoyote. Ile barua haikuwa ni ya kweli na wala haihusiani na mimi, ila kuna rafiki yangu mmoja niliyewahi kusoma naye ambaye aliwahi kuolewa mara tu baada ya kumaliza kidato cha 4.

Nakumbuka kila tulipokutana alikuwa akiniuliza kama nitaolewa lini. Siku moja aliniambia maisha ya ndoa ni mazuri na asiyeolewa labda ana matatizo kwa kuwa anakosa tamu ya ndoa. Nilimsikiliza na kumpuuza kwa kuwa nafahamu kuwa maisha ya ndoa hayana formula, yaani yanaweza kuwa mazuri kwa huyu na yakawa mabaya kwa yule. Hivi karibuni nimepata taarifa kuwa ndoa yake imeota mbawa na aliyempora mume ni nyumba ndogo na ndio nikajikuta nakaa na kuandika ule ujinga na kuuweka hapa.

Sikuwa namsimanga yule shoga yangu bali nilitaka kufikisha ujumbe kwa watu wenye mtizamo kama wake.

Wednesday, December 9, 2009

UBUNIFU WA FULANA NA UJUMBE WA MIPASHO



Fulana zetu na ujumbe wa Mipasho

Kama ningekuwa nimelisema hili humu katika kibaraza hiki, naamini wengi mungeniita mtabiri, lakini bahati mbaya nilikuwa bado sijaanza kublog.

Nakumbuka wakati fulani niliwahi kuwaambia wanafunzi wenzangu wakati huo nikiwa shule kuwa, tunapoelekea si ajabu kukaibuka fulana zenye ujumbe wa maneno ya Kiswahili kama vile yale yanayopatikana kwenye khanga. Hilo nililisema baada ya mwanafunzi mwenzetu mmoja kuvaa fulana ambayo aliiandika maneno ya Kiswahili kwa kutumia Marker Pen ambapo aliandika “MTACHONGA SANA” nadhani labda alikuwa akipeleka ujumbe kwa mahasimu wake ambao alitofautiana nao.

Hilo naona sasa limetimia. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao wamekuwa wakichapisha fulana kwa maneno yenye ujumbe tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya jamii kwa kipindi hicho. Zamani tulizoea kuwa wanawake ndio wanaozodoana kwa kutumia maneno ya kwenye Khanga.

Kwa mfano maneno kama, “Utakufa nacho kijiba cha roho” Chuki nichukie roho yangu niachie” “kama unaweza panda juu ukazibe” Nakadhalika, nakadhalika, yalikuwa ni maneno yanayopatikana kwenye khanga peke yake na hiyo ndio iliyokuwa silaha pekee inayotumika na wanawake katika mapambano miongoni mwao hasa katika maeneo ya uswahilini.

Kwa kawaida kama wanawake wametofautiana katika mambo fulani fulani, badala ya kugombana kwa kupigizana kelele ilikuwa mtu ananunua khanga yake yenye ujumbe anaoutaka umfikie mbaya wake na kivaa makusudi ili kufikisha ujumbe aliokusudia kwa mwenzake.
Niliwahi kusimuliwa wakati fulani kuwa hata wale wanawake wanaochukuliana mabwana, nao walikuwa wakipambana kwa kuvaliana khanga zenye ujumbe wa kuzodoana na wakati mwingine mtu anaweza kumchokonoa mwenzake kwa kuvaa khanga zenye ujumbe tofauti tofauti hata saba kwa siku na kujipitisha kwa mbaya wake ili kumpa ujumbe aliokusudia na mara nyingi ilikuwa ni kawaida kwa mahasimu hao kuanza kurushiana maneno na hata kupigana hadharani kutokana na mmoja kukerwa na maneno ya kwenye khanga alizovaa mwenzie.

Tofauti na zamani, siku hizi mambo yamebadilika, na sasa sio khanga pekee, bali hata fulana siku hizi zimekuwa zikibeba ujumbe tofauti tofauti ukiwemo wa maneno ya kuzodoana. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao huchapisha ujumbe wa maneno ambayo tulizoea kuyaona kwenye khanga na kuyaweka kwenye fulana na hata Blouse na watu wamekuwa wakizigombea.

Sio kwamba sifurahii ubunifu huo wa mavazi, bali ninachojaribu kutahadharisha hapa ni aina ya ujumbe unaowekwa kwenye hizo fulana, kuwa usije ukatufikisha mahali watu wakatumia nafasi hiyo kuweka ujumbe wa matusi au hata maneno ya uchochezi, kwani kuna uwezekano ukatufikisha mahali tusipopatarajia.

Naamini wengi mtakuwa ni mashahidi wa hizi fulana au blouse za mitumba zinazoingia kutoka katika nchi za Magharibi na Ulaya ambazo zina ujumbe wa maandishi au hata picha tofauti tofauti. Tumekuwa tukishuhudia ujumbe wa Matusi au hata uchochezi wa kiubaguzi kupitia fulana hizo, lakini kwa kuwa zimeandikwa kwa kiingereza au lugha zao inakuwa ni vigumu walio wengi kung’amua maana halisi ya ujumbe huo labda mpaka mtu aambiwe, wengi tunachojali ni uzuri wa fulana lakini sio ujumbe ulioko katika fulana hizo.

Monday, December 7, 2009

BARUA YA WAZI KWA DADA YASINTA NGONYANI.....

Dada Yasinta Ngonyani

Kwako dada yangu mpendwa Yasinta Ngonyani mzaliwa wa Ruhuwiko Songea mkoani Ruvuma. Habari za siku nyingi na shikamoo zikufikie hapo ughaibuni ulipo, vipi kile kidole chako ulichijichoma na sindano ukishona nguo ya mwanano Camilla kinaendeleaje. Dada nilipokea taarifa za kujichoma kwako na sindano kwa masikitiko sana na sikuamini kuwa hata Ughaibuni mnatumia sindano za mkono kushona badala ya cherehani. Hata hivyo nakupa pole zako japo uliumia kwa uzembe mtupu.

Nashukuru barua yako uliyonitumia nimeipata jana ingawa mwandiko wako ulinipa shida sana kuusoma, na nimeshangaa sana kuwa hata watu walioko ughaibuni wanakuwaga na miandiko mibaya namna hii, usidhani nakukosea adabu dada yangu, naomba uniwie radhi kwani siwezi kuvumilia maudhaifu ya wengine na ndivyo nilivyoumbwa.

Dada dhumuni la barua hii nikutaka kujibu barua yako ya hivi karibuni ambayo ulinishauri eti niolewe kwa kuwa naanza kuzeeka sasa, dada katika barua yako hiyo umeeleza mengi sana juu ya faida za kuolewa. Umedai kuwa kuolewa ni kuondoa nuksi ili usife bila kuvaa pete ya ndoa, na pia ni fahari maana utakuwa huwajibiki kutunza familia hata kama unafanya kazi, kwani hiyo ni kazi ya mwanaume.

Umesema kuwa kwa mujibu wa mila na desturi tulizorithi kutoka kwa mababu na mabibi zetu ni kwamba wanaume ndio wanaowajibika kuwahudumia wake zao na watoto, yaani mwanamke hatakiwi kutoa hata senti tano kuchangia pato la familia kwa kuwa sio jukumu lake, kwani hilo ni jukumu la mume kwa maana yeye ndiye anayehakikisha familia yake inapata kila kitu, ikiwapo chakula, malazi, mavazi, na vipodozi kwa mkewe ili apendeze zaidi. Umesema kuwa kwa kawaida mwanamke ni pambo la nyumba kwa hiyo akibebana na majukumu ni saa ngapi atakuwa ni pambo la nyumba.

Pia umetoa sababu za kisayansi eti kwa jinsi mwanamke anavyozidi kuzeeka basi na mayai yake ya uzazi nayo yanazeeka kwa hiyo nikifikisha umri fulani nitakuwa sina uwezo wa kupata watoto wangu mwenyewe na kama nikibahatika kuwapata watakuwa mataahira au watumiaji wa mihadarati au Vibaka na wapiga debe.

Ukadai kuwa fahari ya ndoa ni watoto kwa hiyo kama nisipozaa ndoa yangu itaota mbawa, hata kama mume wangu atanipenda, mawifi na ndugu wa mume watachonga sana hadi niachike kwani katika ndoa za Kiafrika ndugu wana nguvu sana na wana uwezo wa kuamua hatima ya ndoa yenu watakavyo.

Ulitoa ushahidi mwingine kuwa wanaume wa siku hizi wanapenda kuona wanawake wanaowazidi umri kwa zaidi ya miaka 15 mpaka Ishirini kwa kuwa hao bado damu inachemka, kwa hiyo kwa jinsi ninavyozidi kuzeeka na ndivyo ninavyozidi kupoteza sifa ya kuolewa na kuwa disqualify kama ulivyosema mwenyewe kwa lugha ya kiingereza.

Niliisoma barua yako kwa makini sana na nilitafahari kwa kina, na ili kujiridhisha ikabidi na mimi nifanye utafiti wangu, unajua si vyema sana kuamini kila unaloambiwa hata kama ni kutoka kwa baba au mama yako mzazi. Dada sifa kubwa niliyo nayo ni kutokuwa dodoki kama alivyosema hayati mzee wa Mwitongo Mwalimu Nyerere.
Dada kuwa dodoki maana yake ni kubeba kila unaloambiwa bila kupima na kudadisi ili kujiridhisha, kama unavyojua dodoki ukilichovywa kwenye maji taka litatoka na kila aina ya uchafu, na ndio maana nikasema kuwa sitaki kuwa dodoki.

Katika utafiti wangu dada nimegundua kuwa madai yako hayana ukweli, kwani wanawake wengi walioolewa wanajuta sana na watamani kuachika kutokana na manyanyaso ya wanaume.

Dada kwa mujibu takwimu za chama cha mambo ya wanawake, kuna wanawake wengi wamepeleka malalamiko yao huko wakitaka kuachika kutokana na manyanyaso kutoka kwa waume zao. Wanawake hao wanadai kuwa kigezo wanachotoa wanaume hao kuwanyanyasa ni mahari waliyolipa kwa wazazi wao.

Wanawake hao wanadai kuwa manyanyaso wanayopata yanategemea kiwango cha mahari waliyotozwa hao wanaume wao, kwa hiyo inakuwa ni vigumu kwa wale waliolipiwa mahari kubwa kudai talaka kwa kuwa wazazi washakula chao mapema kwa hiyo hawana uwezo wa kurudisha mahari ya watu na hivyo wanajaribu kutafuta wafadhili toka nje ili wawanasue katika ndoa hizo za mateso.

Wanawake hao wanatafuta uwezekano wa kubadili mila na desturi zetu ili wanawake ndio wawe wanaoa na kulipa mahari kama wahindi kwani kule India wenzetu wanawake ndio wenye sauti kuliko wanaume na ndio maana India na Pakistani zimewahi kutawaliwa na wanawake kama vile mama Indira Gandhi na Benaziri Bhuto ambao wote waliuwawa kwa husuda tu, na wale wanaume wanaotaka mfumo dume kama huu uliotamalaki huku kwetu

Dada kama wewe ni msomaji wa vitabu vitakatifu vya dini zetu hizi za mapokeo utakubaliana na mimi kuwa hata mwenyezi Mungu amewapendelea sana wanaume kiasi cha kuwapa kibri. Hebu soma maandiko matakatifu ya Biblia katika kitabu cha Waefeso 5, 22:24.

Dada maandiko hayo ndiyo yanawapa wanaume kibri kwa kudai kuwa wao ndio vichwa vyetu wakati vichwa vyetu tunavyo na tunatembea navyo.

Kwa hiyo dada ushauri wako kwangu nauona kama unataka kunipalia makaa ya moto ili tufanane wakati mie nimeshawashitukia wanaume zamani sana.
Najua utashangazwa na uamuzi wangu kwa kuwa ulitegemea nikubaliane na ushauri wako lakini napenda kukukatisha tamaa kuwa mie nimeshawashitukia wanaume siku nyingi.

Dada mimi ni mjanja………..LOL

Friday, December 4, 2009

MATEJA NA UTAMU WA TENDO LA KUJAMIIANA!


Mimi kwa kawaida ni mdadisi sana, na naomba nikiri kuwa udadisi wangu uliwahi kuniletea matatizo wakati fulani. nakumbuka nilikuwa naendesha gari katikati ya jiji, na wakati nimesimama kwenye taa za kuongozea magari,akaja mama mmoja ombaomba ambaye namkadiria kufikisha umri wa miaka 60 hivi.
Alionekana kuwa na afya njema tu. Alipofika pale nilipo aliniomba pesa, nilitoa kiasi cha fedha na kumpa, lakini nilimuuliza kwa upole kwamba kwa nini anaomba barabarani wakati afya yake ni nzuri tu. mama wee....alinishambulia kwa matusi na kama sio taa za barabarani kuniruhusu labda angenipasulia kioo cha gari langu, kwani nilimuona kupitia kioo cha pembeni akiokota kitu nadhani kwa ajili ya kunirushia, lakini alichelewa kwani nilishafika mbali. Tukio hilo lilinikumbusha tukio lililompata dada yangu Yasinta Ngonyani na mwendawazimu wa Ruhuwiko Songea.

Ngoja nirejee kwenye kile nilichotaka kusimulia leo. Nimesema kuwa mimi ni mdadisi sana, na udadisi wangu naona saa utaniletea matatizo, lakini sitaki kuacha na sijui ni kwanini. Juzi nikiwa kwenye Intenert Cafe moja iliyopo maeneo ya Mikocheni nilikutana na kaka mmoja ambaye ni mtumiaji wa madawa ya kulevya, maarufu kama Teja. Kijana huyo ambaye nilisoma naye shule moja akiwa amenitangulia darasa moja mbele, alikuwa akisifika sana kutokana na kuwa na akili sana darasani wenyewe tulikuwa tunaita akili za Nature, na mpaka tukawa tunamuita Nature kutokana na kuwa na akili ambazo sio za kawaida.

Alifanikiwa kufaulu na kuendela na masomo ya sekondari, nasikia alifaulu kidato cha nne na kuingia kidato cha tano na kupangiwa kwenda shule moja maarufu mkoani Tanga na huko ndipo alipojitumbukiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na kuwa Teja kiasi cha kusababisha kufukuzwa shule na kurejea jijini na kuendela na tabia hiyo.

Nilipokutana naye pale cafe nilipiga naye stori mbili tatu na ndipo nikamuuliza swali, kwamba kwa nini amejiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya wakati alikuwa na maendeleo mazuri shuleni. Nilimuona akibadilika ghafla kama vile amekasirika, niliona mambo si shwari, ikabidi nimuwahi kumuomba radhi kwa swali langu la kijinga, lakini aliniambia kuwa hajakasirika, na kwa upole akaniuliza swali......

"Samahani Da' mdogo Koero, hivi unajua utamu wa tendo la kujamiiana?" Nilishangazwa la swali lile, lakini kwa kuwa niliyataka mwenyewe nikajikuta nikimjibu kuwa nafahamu. Kisha akaniuliza tena..... "Je Unajua utamu wa tendo la kujamiiana unadumu kwa muda gani katika ubongo wa binadamu?" Duh! hili lilikuwa ni swali gumu kwangu na nilijua sasa na mimi nimepatikana maana nilijifanya kuwa mdadisi, lakini sasa mambo yananigaeukia.

Nilijikakamua na kumjibu kwa kifupi. "Sijui maana sijawahi kufanya utafiti huo"
Yule kijana kwa upole akaniambia, "kwa kuwa umeuliza swali basi nitakujibu tena kwa ufasaha ili wakati mwingine usije ukauliza tena kwa mtu mwingine"

Aliniambia kuwa kwa mujibu wa tafiti mbalimbali imebainika kuwa utamu wa tendo la kujamiiana unadumu katika ubongo wa binadamu kwa sekunde tano tu, mtu anapofikia kileleni, lakini mtu anapotumia madawa ya kulevya, yaani pale anapojidunga dozi, ule utamu anaoupata ambao unafanana na utamu wa tendo la kujamiiana unadumu kwa dakika kumi na tano.
Kisha akaendelea kusema kuwa, kama utamu wa kujamiiana ambao hata hivyo unadumu kwa sekunde tano tu, lakini watu wanaupenda kupita kiasi huku wengine wakihatarisha maisha yao dhidi ya gonjwa la ukimwi na wengine wakitiana ngeu au hata kuuana kwa sababu ya utamu huo, kwa nini yeye asiamue kuwa Teja ambapo anaweza ku-enjoy kwa takribani dakika kumi na tano bila bughdha kwa kitu ambacho hakimpi usumbufu.

Wakati wote akinipa darasa hilo nilibaki nimemtumbulia macho kwa mshangao na nisiamini kile alichokuwa akinisimulia. Kusema kweli sikuwa na swali la nyongeza, nilimshukuru kwa majibu yake nikamuaga ili niondoke, lakini alinitaka nimuachie hela akapate kete yake ili apate stimu kwani nilimvurugia stimu yake kwa kumuuliza lile swali.

Sikutaka kugombana naye, nilitoa kiasi cha pesa na kumpa, kisha nikaondoka. Yaani kiranga kiliniisha, maana sikutegemea yale majibu ambayo yalikuwa na ushahidi wenye utafiti ambao hata sikujua kama utafiti ule una ukweli kiasi gani.

Hata hivyo kwa umbeya wangu nimeona niiweke hii habari hapa kibarazani ili nilete changamoto toka kwa wadau na wasomaji wa blog hii.