Friday, October 29, 2010

WANANCHI WENZANGU,SAFARI HII TUSIDANGANYIKE!


Unapokuta nchi ambayo wananchi wake wamekata tamaa kutokana na kutelekezwa na serikali iliyoko madarakani huku ikiacha uchumi umekumbatiwa na matajiri wachache wasio na utu, basi huna haja ya kuchanganyikiwa badala yake inabidi ujiulize unachojifunza kutoka katika nchi hiyo.

Huenda umejifunza hatari ya wananchi hao kuendelea kukishabikia chama hicho na kuendelea kukipa ridhaa ya kuwaongoza kwa kuahidiwa maisha bora na matarajio yasiyotekelezeka na yaliyoshindwa ndani ya miaka mitano iliyopita.

Lakini huenda pia umejifunza jinsi ilivyo rahisi kuwadanganya na kuwahadaa masikini kwa kuwapa vitu kama fulana, kofia na khanga ili waendelee kukupa mamlaka ya kuwaongoza hata kama huna tija kwao.

Wewe mwananchi amka, kura yako ndio zahanati yako, ndio barabara yako, ndio shule yako, ndio miundo mbinu yako na ndio itakayokuwezesha kujijengea makazi bora.

Sasa hivi tusidanganyike……..tuchukue maamuzi magumu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu tubariki tupate kiongozi anayejua muarobaini utakaomaliza matatizo yetu ya kiuchumi.

Ahsanteni kwa kusoma maandishi haya

Monday, October 25, 2010

Friday, October 22, 2010

KAKA MATONDO, USIONE KIMYA NIKO HUKU!

Jana nimekumbuka sana kublog, ni takribani mwezi na siku kadhaa sijaonekana humu, na hiyo ni kutoakana na kuwa bize katika kuzifukuzia ngawira.

Leo nimekutana na makala ya kaka yangu Matondo akinitafuta nikaoni si vyema nikikaa kimya, unaweza kumsoma kaka Matondo akimlilia dada dada yake Koero kwa kubofya hapa

Nimekuwa bize mno mwayego, na kama mjuavyo kuwa maisha ya siku hizi kila mtu anajichomea kamuhogo kake na familia yake. Kwa hiyo na mie bado niko huku Arusha najichomea kamuhogo kangu.

Nawasalimu wote na nawatakia siku njema.

Thursday, September 23, 2010

JE NI SAHIHI KIJANA KUTAFUTIWA MWENZA NA WAZAZI ANAPOFIKIA UMRI WA KUOA AU KUOLEWA?

Mwenzenu jana nilikuwa na mjadala hapa nyumbani, na mada kuu ilikuwa ni juu ya namna nzuri ya kupata mwenza.

Dada yangu mkubwa ndiye aliyeanzisha huo mjadala kwa kumuuliza mama kama ni vyema mtu kutafutiwa mke au mume wa kuoa au kuolewa, au kila mtu anawajibika kujitafutia mwenyewe mwenza wake na kuanza maisha?

Mama alikuwa na haya ya kusema. Alisema kuwa kimsingi hapo zamani wazazi walikuwa wakiwatafutia watoto wao wenza wa kuoa au kuoelwa na lengo kuu lilikuwa ni kutaka mtoto wao aangukie katika mikono salama na mojawapo ya vigezo vikuu vilivyokuwa vikiangaliwa ilikuwa ni historia ya ukoo husika, kwa mfano, je ukoo huo unaanguka kifafa? Je ni ukoo wa wachapa kazi kwa maana ya kujituma kwa kufanya kzi kwa bidii ( Ikumbukwe kuwa zamani kazi kuu ilikuwa ni kilimo). Je Sio ukoo wenye mkono mrefu, yaani sio wezi ( Sijui kwa nyakati hizi kuna haja pia ya kuwajumuisha na mafisadi yaani kama ukoo una hulka ya ufisadi)

Jambo lingine lilikuwa ni kuangalia kama ukoo unashambauliwa na magonjwa sugu, kama vile anemia (Upungufu wa damu wa mara kwa mara) Kansa, kisukari na maradhi mengine yaliyokuwa yakitafsiriwa kuwa yanaweza kuushambulia ukoo.

Sina hakika kama vigezo hivyo bado vinazingatiwa kwani kule vijijini bado utaratibu a kutafutiana wenza upo lakini sio kwa kiwangom kama cha zamani kwa sababu ya mabadiliko yaliyoikumba jamii, kwani kila mtu sasa na lwake.

Kulizuka hoja mbalimbali ambazo kama nikiziweka hapa nitawachosha, na lengo langu ni kutaka kuwashirikisha wasomaji wa kibaraza hiki kisichoisha visa na mikasa kutafakari kwa p

Monday, September 20, 2010

WAKATI IDADI YA WASALANDIAJI NA WAMEZEA MATE TONGE IKIONGEZEKA, MASHARTI NAYO YAONGAZEKA PIA.

Kazi ipo.....


Ni jambo ambalo sikulitarajia kuwa kumbe pamoja na kunangwa kuwa sioleki na sitakuwa na ndoa imara lakini soko langu liko juu kiasi hiki!

Kusema kweli nimekuwa na wakati mgumu hasa maana kuna wengine ambao wao wamepitia mlango wa nyuma na kuleta CV zao ili kutaka bahati iwadondokee, lakini hata hivyo hilo sio tatizo, bali wasiwasi wangu ni kuwa mzee Mkundi kaongeza masharti kadhaa ambayo nahisi kuna ambao watadondokea pua.

Masharti yenyewe ni haya yafuatayo:

*Mtarajiwa hatakiwi kuwa na umri wa ubarubaru yaani umri wake uwe umefikia kati ya miaka 40 hadi 45, kwani vijana wa umri wa ubarubaru wanakuwa wasumbufu kwa sababu bado ujana unawazuzua.
*Mtarajiwa anatakiwa awe ni mkristo wa dhehebu la sabato (Hili sharti nadhani litakuwa gumu maana mweh! kwa nyakati hizi dini zina vijimambo vyake)
*Mtarajiwa hatakiwi awe mlevi wa kilevi chochote na asiwe anavuta sigara.
*Mtarajiwa anatakiw awe ni mtu wa nguvu kazi asiwe anachagua kazi.
*mtarajiwa anatakiwa awe mtanashati, mpole kiasi, awe na tabia njema na mwenye upendo wa dhati .

Sifa nyingine za ziada zitapewa kipaumbele…..LOL

Haya mwenye sifa hizo aweke CV zake hadharani, hata wale wenye kupitia nyuma ya pazia karibuni kwenye kinyang’anyiro.

Friday, September 17, 2010

KOERO UTAOLEWA NA NANI? BADO NI KITENDAWILI, LAKINI LABDA MARKUS AU MTANGA…………….LOL

Najua wengi watashangaa maana wanajua mie sioleki, lakini naamini mmeona wenyewe jinsi wanaume hao wawili wanavyojifaragua, kwa mie binti kimwana.

Nakumbuka kuna mdau mmoja aliwahi kudai tena humu humu kwenye kibaraza cha Vukani kuwa mie sifai kuolewa na sitakuwa na ndoa imara kwa sababu eti nina kiherehere na kiroho papo cha kudai haki za wanawake.

Lakini Waswahili walishawahi kusema kuwa kama ni kibaya waachie wenzio……… sasa je kiko wapi?

Najua wahafidhina watatia fitina (hata hivyo nimeshawazoea) lakini wakae wakijua kuwa bahati imenidondokea….LOL

Ila kuna jambo moja, niliwahi kumuuliza bibi Koero kuhusiana na swala la wapiga emcheku kugongana kwa binti mmoja, Je inakuwaje? Jibu lilikuwa ni rahisi sana……. Ni kwamba watakaribishwa mmoja baada ya mwingine kupata mlo na baba mkwe na yule atakayekuwa anakata matonge makubwa ya ugali aka nguna na kula ugali mwingi unaofikia kilo moja kasorobo ndiye atakayepewa jiko,kwani hiyo ni ishara kuwa huyo atakuwa ni mkulima hodari na binti yao hatakufa na njaa.

Hivyo nawaomba wamezea mate na wasalandiaji waanze kuchukua mazoezi ya kumega matonge makubwa…. La sivyo hakuna ndoa….LOL

Na kwa maandalizi, wiki ijayo mwanamwali nawekwa ndani kusubiri hatima ya ndoa yangu……..je ni nani atapata bahati ya kujivinjari na kimwana……. Usikose kusoma hapa.

Wednesday, September 8, 2010

JELA MIAKA MITATU, KISA DADA WA KIJANA KANIKATAA!

Niliamua kurudi shamba na kuwa mkulima


Kwa kifupi sana ni hivi. Mwaka 1975 nikiwa mwalimu kijana bado, nilifanya jambo ambalo kwa wakati ule wala halikunisumbua ingawa lilikuwa baya sana.
Bila shaka, wale wanaokumbuka mfumo wa elimu wa wakati ule wanajua kuhusu wanafunzi waliokuwa wanaitwa maripita ambao walikuwa ni wale wanaoanguka mtihani wa darasa la saba shule fulani na kwenda kudurusu darasa hilo kwenye shule nyingine.
Serikali ilikuwa inakataa kabisa wanafunzi kukariri tena darasa la saba au la nyuma yake baada ya kuanguka mtihani. Nikiwa shuleni kule Mbeya mwanafunzi mmoja ambaye baba yake alikuwa na urafiki na mkuu wa shule niliyokuwa nafundisha alikuja kudurusu darasa.Siku alipokuwa anakuja kuripoti, nilikuwepo mimi ofisini kama mwalimu mkuu msaidizi.
Kijana huyo aliletwa na dada yake ambaye alikuwa anafanya kazi hospitali ya mkoa. Nilimpokea kijana yule nikijua kwamba anarudia shule.Baadaya kumpokea na kujua dada yake anapofanyia kazi, niliona nami ningepata. Kama mkuu wa shule alipata fedha kupitia Yule kijana kudurusu darasa, nilijua na mimi ningepata rushwa ya mwili.
Nilimwandikisha kijana huku nikisema kwamba, kudurusu darasa ni mbayasana. Yule dada wa kijana alisema ni kweli, lakini ni suala la kusaidiana.Nilitania kwakusema, “nasi tukija kuomba msaada hospitalini itabidi tusaidiwe.” Yule dada alisema hakuna tabu. Basi kijana alianza masomo darasa la saba nami nilianza kumfuatilia dada yake kule hospitali ya mkoa. Nilifuatilia kwa miezi miwili bila mafanikio zaidi ya ahadi tu.
Nilijua kwamba, Yule muuguzi, dada wa yule kijana alikuwa anataka tu kuvuta muda ili mdogo wake amalize masomo ili anitolee nje. Ilibidi nimwambie kwamba, kama asiponikubalia ombi langu, mdogo wake ni lazima angeanguka mtihani kwani ningekwenda kuchongea mkoani kuhusu kudurusu kwake.Yule dada aliniambia, kama hilo ndilo lengo langu, ni vizuri nikalifanya.
Kuanzia hapo sikufuatilia tena na nilipania kumchongea Yule mdogo wake, jambo ambalo sikujua kwamba, lingemdhuru na bosi wangu, yaani mwalimu mkuu. Ni kweli nilikwenda mkoani na kutoa taarifa kisiri kwa wanaohusika.Ukweli ni kwamba kijana Yule ambaye alikuwa na uwezo sana darasani alishindwa baada ya jina lake kukatwa na mkuu wa shule kushushwa cheo.
Nilifurahi sana baada ya matokeo hayo. Nilikwenda kule Hospitalini kumjulisha Yule dada mtu kwamba mimi ndiye niliyemwangusha mdogo wake.
Yule dada alilia nikiwa hapohapo, huku moyo wangu ukiwa umeridhika. Jioni ya siku ile ile, Yule kijana alikuja nyumbani kwangu hapo shuleni na kuniuliza ni kwa nini nimemfanyia roho mbaya . Nilimwambia amuulize dada yake na kumsisitiza kwamba sio mimi bali ni sheria zanchi.Yule kijana aliondoka huku akisema, Mungu ndiye anayejua kulipa au kutoa hukumu kwa haki.
Nilicheka na kumwambia aende akafie mbali. “Dada yako ni ndege mjanja amenasa kwenye tundu bovu” Nilimpigia kelele. Aligeuka na kunitazama kwa muda, halafu aliondoka. Nadhani angekuwa na nguvu angeweza kunipiga ngumi nyingi sana, lakini hakuwana ubavu.Miaka ilipita na nikawa nimesahau kabisa jambo lile. Ilikuwa ni miaka 25 baadae, mwaka 2000 ni kwamba mwaka 1995 niliacha kazi ya ualimu na kurudi kwetu Iringa. Nilianzisha biashara na kuwa mfanyabiashara.
Mwaka huo 2000 nilipata matatizo ambayo yalinifikisha mahakamani.Kesi iliendelea kwa mwezi mmoja, kabla ya kutolewa hukumu. Haikuwa kesi kubwa, wala ambayo ingenitisha kwa kweli, Haya hukumu yake kwa mujibu wa wanasheria ambao niliwauliza, hakimu alikuwa anaruhusiwa kutoa faini au kifungo cha nje. Sijui walinidanganya kunipa moyo au vipi.
Lakini siku ya hukumu hakimu alinihukumu kwenda jela miaka Mitatu adhabu ya juu kabisa ya kosa langu. Nilibabaika sana na wala sikuamini kama nimehukumiwa kwenda jela. Wakati nikipelekwa kufungiwa selo Yule hakimu aliyenihukumu alinijia na kuniambia.“Siyo mimi, bali sheria za nchi. Nadhani safari hii dada yangu sio ndege mjanja tena.” Ilinichukua muda, lakini polepole akili ilizibuka wakati nikiwa jela mwezi wa pili, ambapo nilikumbuka lile tukio la mwaka 1975. Sijui nilihisi nini, lakini niliumia sana.
Sipendi kukumbuka nilivyoishi kwa huzuni kule jela, nikijutia ufedhuli ule nilioufanya kwa kijana yule wakati ule.Baada ya kumaliza kifungo changu, bado nikiwa na harufu ya jela nilikwenda nyumbani kwa hakimu yule na kubisha hodi. Alifungua mlango na kunikaribisha ndani kwake bila kinyongo. Nilimsalimia na kumwambia moja kwa moja. “Naomba radhi kwa yale niliyokufanyia wakati ule….”Yule hakimu alinikata kalma na kusema, “hukufanya lolote baya, ilikuwa ni sheria kweli. Kama ambavyo nami nimetimiza sheria za nchi.
Wala huna haja ya kuomba radhi, labda tu kwa sababu, wewe ulikuwa unalipa kisasi baada ya dada yangu kukukataa, wakati mimi sikutimiza wajibu wangu kwa kinyongo.”Niliinuka na kutoka nje, nikielekea kwangu. Maisha yalikuwa ndiyo kwanza yanaanza na uzee umeingia . Kisa kujisahau.
Hii simulizi nimependa sana. Ukitaka kujua nilipoipata basi waweza kubofya hapa

Wednesday, September 1, 2010

YATOKANAYO NA WASIFU WA DK. BEN CARSON

Dk. Ben CarsonDk
Nimependezwa sana na maoni ya wasomaji wa kibaraza hiki kuhusiana na mada niliyoiweka wiki iliyopita ya wasifu wa Dk. Carson.

Naomba nikiri kuwa maoni ya kaka yangu Mubelwa Bandio yalinifanya nijiulize maswali kadhaa ambayo ningependa kuwashirikisha wasomaji ili tutafakari kwa pamoja:

Maswali yenyewe ni haya yafuatayo:

*mama yake aliolewa akiwa na umri wa miaka 13 na mchungaji mzee kwa kukimbia shida za pale nyumbani kwao, ambapo pia aliachika na kuachiwa kuwalea watoto wawili pake yake.

*mama huyu aliishia darasa la tatu, ambapo sio kiwango kizuri cha elimu cha kujivunia, lakini kwa shida sana alilazimika kufanya kazi zaidi ya tatu ili ahakikshe anawatengenezea wanae hao future.

*Carson alikuwa mbumbumbu darasani, lakini kutokana namsimamo wa mama yake wa kuwalazimisha kusoma libarary, alipata mwamko na kusoma kwa bidii hadi kufikia kuwa daktari bingwa wa upasuaji.

Haya ni mafanikio makubwa kwa mama huyu (Mwanamke huyu) ambaye hakupata elimu kubwa. Je kuna wazazi wangapi ambao wana elimu ya kutosha tu lakini malezi kwa watoto wao yamewashinda?

Hata hivyo kuna jambo moja nimeliona kwa upande waserikali ya Wamarekani, nalo ni lile la kutambua mchango unaofanywa na wataalamu mbalimbali nchini humo.

Pamoja na Carson kupata tuzo nyingi, lakini Rais wa Marekani wa wakati huo G W Bush alitambua mchango wake na kumwalika Ikulu na kumpa tuzo ya Uhuru ambayo ni tuzo kubwa kutolewa nchini humo na Rais.

Je ni wataalamu wangapi au niseme ni Watanzania wangapi ambao wanatoa au wametoa mchango mkubwa hapa nchini hata wengine wakapoteza maisha yao au wakawa wameathirika kwa kiasi kikubwa lakini mpaka leo hii hawajawahi kupewa tuzo yoyote na Rais au hata kutambuliwa na Serikali?

Je hakuna haja ya kuliomba bunge lijalo litunge sheria itakayounda jopo la watu ambao kwa kuzingatia vigezo maalum wateue mtu mwenye sifa fulani kulingana na kile alichokifanya katika jamii na kukabidhi jina lake kwa rais ili apewe tuzo kubwa na ya heshima?

Tuzo hiyo isiwe ni tuzo tu ya kawaida bali pia iwe ni tuzo itakayoambatana na fedha za kutosha na kuwe na sherehe maaluma wakati wa kukabidhi tuzo hiyo.

Hilo naamini litawezekana kwani huko mikoani kuna watu wamefanya mambo makubwa lakini kutokana na urasimu yanaishia kwenye makabati ya wakuu wa wilaya au wenyeviti wa vijiji.

Nataka kuwasha moto......

Saturday, August 28, 2010

TAFAKARI A LEO: BEN CARSON, DAKTARI ALIYETHIDITISHA KUWA HAKUNA MTOTO MPUMBAVU

Dk. Ben Carson akivishwa nishani ya Uhuru na Aliyekuwa Rais wa Marekani G. W. Bush


Mojawapo ya vitabu vyake vilivyojizolea umaarufu



Mapacha Ladan na Laleh Bijan wa Iran ambao Operesheni yao iliyoongozwa na Ben Carson ya kuwatenganisha haikufanikiwa, walifariki wote wawili


Daktari Benjamin S. Carson (amezaliwa tar. 18 Septemba, 1951) ni daktari na mtaalamu wa Nyurolojia, na pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Nyurolojia kwa watoto katika hospitali ya Johns Hopkins huko nchini Marekani. Alitunukiwa na raisi medali ya uhuru mwaka 2008

HISTORIA YA ELIMU.

Benjamin Solomon Carson alizaliwa katika eneo la Detroit katika jimbo la Michigan. Mama yake, Sonya Carson, aliacha shule akiwa katika daraja la tatu na kuolewa na Robert Solomon Carson, aliyekuwa mchungaji mzee zaidi katika eneo la Tennesee, wakati mama yake Ben akiwa na umri wa miaka kumi na tatu tu.

Wakati Carson akiwa na umri wa miaka nane tu, wazazi wake waliachana. Mama Carson aliachwa kuwalea Benjamin na kaka yake Curtis, yeye mwenyewe. Alifanya kazi katika sehemu mbili au hata tatu kwa mara moja ili aweze kuwatosheleza watoto wake wawili. . Mwanzoni Carson alikuwa na maisha magumu shuleni. , hali iliyopelekea kuwa wa mwisho mara kadhaa katika darasa lake. Alikuwa akiitwa majina mbalimbali kutokana na hali hiyo, hivyo ikapelekea kukua kwa hasira kali ndani yake.


Akiwa amedhanmiria kubadilisha maisha ya mtoto wake, mama yake Carson akazuia muda wake wa kuangalia televisheni na kumzuia kutoka nje kila siku hadi pale atakapokuwa amemaliza kazi zake za shule kila siku. Mama yake Carson alimtaka Kusoma vitabu viwili kutoka maktaba na kuandika taarifa juu ya vitabu hivyo kila wiki, bila kujali elimu yake ndogo, hata hivo hakuweza kusoma vitu ambavyo vilikuwa vimeandikwa.


Lakini mapema, Carson alimshangaza mwalimu wake na wanafunzi wenzake kufuatana na maendeleo yake. Anakumbuka “Ni wakati ule ndipo nilipogundua kuwa sikuwa mpumbavu” anagundua baadae. Carson anaendelea kuwashangaza wanafunzi wenzake na ndani ya mwaka mmoja alikuwa na ujuzi na kuwa katika nafasi ya juu katika darasa lake.


Baada ya kugundua kuwa alitaka kuwa daktari wa magonjwa ya akili, Carson alimaliza shule na matokeo mazuri yenye heshima na hivyo alijunga na chuo kikuu cha Yale ambapo alipata shahada yake ya kwanza katika maswala ya saikolojia ya akili. Pschology. Baada ya kutoka Yale, aliendelea na shule ya udaktari ya michigan, ambapo hapo ndipo nia yake ya kuwa daktari wa magonjwa ya akili ilipobadilika na na kuwa daktari wa mishipa.

Uwezo wake mkubwa wa kuona na uwezo wake wa kufikiri haraka ulimfanya awe daktari wa upasuaji mzuri zaidi Baada ya kumaliza shule yake ya udaktari, alikuwa daktari wa mishipa msaidizi katika hospitali ya Johns Hopkins katika jimbo la Baltimore. Akiwa na umri wa miaka 33, alikuwa profesa wa hospitali na pia mkurugenzi wa idara ya upasuaji mishipa ya watoto.


KAZI ZAKE ZA MAPEMA.


Mwezi wa tisa mwaka 1987, Carson alifanya upasuaji wa kutenganisha mapacha wenye umri wa miezi saba, waliokuwa wameungana katika sehemu ya kichwa. Carson alikuwa ndiye kiongozi wa upasuaji huo mgumu, Mwaka 1997, Carson pamoja na timu yake, walienda Afrika ya Kusini, kuwatenganisha Lukas na Joseph Banda kutoka Zambia. Watoto wote wawili waliweza kuishi baada ya upasuaji na hakuna hata mmoja wao aliyepata uharibifu wa ubongo. Watoto hao wa Banda walikuwa ni watoto wa kwanza walioungana kwa upande wa juu wa vichwa vyao kuweza kuishi baada ya upasuaji. Upasuaji huo ulifanyika kwa saa 28.


Mwaka 2003, Carson alikuwa moja kati ya madaktari waliofanya upasuaji wa watu wazima waliokuwa wameungana katika sehemu ya vichwa, Ladan na Laleh Bijan. Lakini wote hawakuweza kuishi baada ya upasuaji. Alipoulizwa kwa nini alikubali kufanya upasuaji wa kubahatisha kiasi hicho alisema, ndugu hao walikuwa wamekubali bora wafe kuliko kuendelea kuishi wakiwa wameungana.


MAISHA BINAFSI.


Carson amepokea tuzo mbalimbali katika miaka mbalimbali, kama vile, Shahada za heshima za Udaktari 40, pia ni mwanachama katika chama cha American Academy of Achievement, Horatio Alger Association of Distinguished Americans, Alpha Omega Alpha Honor Medical Society Ushirikiano wa yele, (Bodi ya wakurugenzi wa Chuo kikuu cha Yale) na mashirika mengine mengi. Pia ni mwanzilishi na mkurugenzi wa The Carson Scholar Fund, ambayo huwasaidia wanafunzi kutoka katika historia tofauti tofauti walio na vipaji maalumu katika masomo.


Mwaka 2007, Carson alijumuishwa katika Chuo kikuu cha Indiana Wesley, katika Society of World Changes na kupokea nishani ya heshima ya udaktari alipokuwa akiongea katika Chuo hicho. Aliporudi, alirudi na rafiki yake alyeitwa Tony Dungy ambaye naye alikujuishwa katika jamii. Tarehe 19 mwezi wa 9 mwaka 2008, Carson alopokea nishani ya raisi ya uhuru kutoka kwa Raisi George W. Bush


UTAALAMU NA MAGONJWA.


Carson ameandika vitabu vitatu vilivoongoza katika mauzo na vilivyochapishwa na Zondervan shirika la kimataifa la uchapaji la kikristo, Vinavoitwa : Gifted Hands (Mikono Yenye Vipawa: Hadithi Ya Ben Carson) , The Big Picture, na Think Big Kitabu cha kwanza cha Historia ya maisha ya mtu, na vitabu vingine viwili ni kuhusu filosofia ya maisha yake hususani katika mafanikio yake yanayoenda sambamba na imani yake kwa Mungu.Carson ni Mkristu katika dhehebu la sabato.

Mwaka 2002, Carson aliamuriwa kusitisha kuonekana katika maeneo yenye umati wa watu, baada ya kupata matatizo ya kiafya ya kwake mwenyewe. Mwezi wa sita alikutwa na dalili za kuwa na Saratani ya Kibofu cha mkojo, lakini kwa bahati nzuri, saratani hiyo ikiliweza kukutwa katika muda muafaka.

Lakini pamoja na hayo, Carson alibadilisha mfumo wake wa maisha, Bado anafanya upasuaji kwa zaidi ya watoto mia tatu (300) kwa mwaka lakini amekuwa akijaribu kupunguza muda wake.Carson amekuwa akifanya kazi kuanzia saa 7:00 asubuhi na kumaliza saa 8:00 usiku, lakini tangu agundulike kuwa na saratani amekuwa akifanya kazi na kuondoka saa 6:15, jioni. Hii inampa muda zaidi wa kukaa na mke na watoto wake watatu (3).

Makala ya video kuhusu maisha ya Carson inayoitwa Gifted Hands: Kitabu kinachohusu, hadithi ya Ben Carson kilitolewa na Zondervan mwaka 1992, hali iliyopelekea mwaka 2009, filamu ya Televishen iliyotolewa ikiwa na Jina hilo hilo, katika TNT tarehe 07/02/2009, na kushinda tuzo ya Academi ya Gooding jr ikiongozwa na Kimberly Elise akimwelezea mama yake.

Friday, August 27, 2010

JE UMEWAHI KUZITUMIA HIZI?







Nimezikuta kwenye mkoba wa Mzee Mkundi

Thursday, August 26, 2010

MLININUKUU VIBAYA!

Sikuwa na maana hiyo, nahitaji sana kura zenu!

Sunday, August 22, 2010

Friday, August 20, 2010

Labda USIMTISHE MTOTO wako!

Kaka Simon wa tatu kushoto......LOL

Kuna kitu WATU wengi hawajui kuhusu MIE Simon KITURURU,...... ila ukweli ni kwamba mkono wangu wa kulia haufanyi kazi vizuri kama inavyotakiwa ,...


... kwa KIFUPI hata UKIWA sio mbali sana siwezi nikakurushia jiwe kama nataka kukubwenga JIWE kirahisi na MKONO WA KULIA.Na tatizo lilianza kisa nilikuwa naficha siri eti kwa kumuogopa BABA.:-(


STORI fupi laini na YA KWELI :Tulikuwa tunaishi SONGEA na moja ya vitu MDINGI alikuwa hapendi ikiwa pamoja na KUWA MCHAFU , kufeli mtihani enzi hizo nikisoma SHULE ya MSINGI MFARANYAKI (kitu ambacho nilikuwa sifeli) ,....


..... nilikatazwa kupanda juu ya MITI aka kuparamia miti kimichezo.Siku moja mie na marafiki zangu tukaenda kuiba maembe aka KUTUNGUA MAEMBE yasiyo yetu shambani kwa WANAFUNZI WA SONGEA GIRLS.


Enzi hizo shamba la songea GIRLS lilikuwa kubwa na sisi tulikuwa tunaingilia upande wa UWANJA WA MEDICAL karibu na nyumba za mwisho mwisho za walimu enzi hizo za miaka ya NAINTINI EITEZ( (Kumbuka ni miaka mingi sijafika Ruvuma sijui maeneo hayo yakoje siku hizi)Basi BWANA katika kuwinda maembe bolibo na embe sindano tukaupata mti ambao mbivu zilikuwa zimenona juu kabisa.


Na mie ambaye hukatazwa kupanda miti nilikuwa kiongozi kuparamia juu kabisa kutikisa mti.Kilichotokea ni kwamba,....... katika kutikisa tawi ili kudondosha maembe tawi likakatika na kilichofuata nilijikuta chini nikijiuliza niko HAI au NIMEKUFA,..........na chaajabu hata marafiki zangu wakinisemesha nilikuwa siamini kama niko hai kwa KUWASIKIA kwa kuwa nilikuwa nahisi kuwa labda hata MFU akisemeshwa huwa anasikia.:-)


Katika kufupisha stori hii ya kweli;... ....nilivyoanguka nilitegua mkono wa kulia na baadaye nikaja stukia labda na kitu kingine mkononi kiliharibika.:-(


KIKUBWA:Kwa kuwa kwanza nilikatazwa kupanda miti na PILI miye na marafiki zangu tulikuwa tunaiba maembe ya wana SONGEA GIRLS nilifikiri sio busara kusimulia hicho kitu nyumbani. NILIFICHA maumivu na ugonjwa kisa NAMUOGOPA BABA....


.....na kwa bahati nzuri ilikuwa ni kipindi cha baridi SONGEA na maswala ya SWETA na JACKETI pamoja na MAIGIZO kuwa NIKO BOMBA yaliniwezesha kuficha nimeumia mpaka mkono ukapona kinamna. TATIZO ni kwamba mkono ulivyopona mpaka leo hauwezi kumlenga MBAYUWAYU bila msaada wa mkono wa kushoto.Kwa kifupi :


Nilijitia udhaifu wa mwili KWA KUFICHA UGONJWA kisa NAOGOPA KUCHAPWA. na BABA:-(Unajua tena AKILI ZA KITOTO).
Stori hii nimeipenda sana na nimeweka hapa ili wasomaji wa kibaraza hiki wapate kujifunza kupitia simulizi hii ya kweli ya kaka yangu Simon Mkodo Kitururu. kwa kumsoma zaidi waweza kubofya hapa

Monday, August 16, 2010

HURUMA HII YA DAKIKA ZA MWISHO SI BURE!

Akasema, 'Sihitaji kura zenu'

Kama kuna chama ambacho unaweza kukiita chama cha watu wenye kujua kuchezea watu shere basi chama hicho ni CCM. Tena siyo haba shere zao. Na hapo ndipo ninapojiuliza kuwa, nini hatima ya nchi hii baada ya uchaguzi mkuu ujao?

Nakumbuka wakati ule wa kilele cha ugomvi wa serikali na Chama cha Wafanyakazi, TUCTA juu ya maslahi ya watumishi wa umma, Mheshimiwa Raisi kwa maneno yake mwenyewe akiongea na wazee wa jijini Dar es salaam alitamka dhahiri bila kumung’unya maneno kuwa hata (Wafanyakazi) wagome miaka 8 hataongeza chochote kwani serikali haina hizo fedha, na kufanya hivyo ni kusababisha huduma muhimu za kijamii kutotekelezeka.

Mheshmiwa alienda mbali zaidi na kusema kuwa anajua viongozi wa TUCTA wana agenda ya kisiasa kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu lakini hahitaji kura za wafanyakazi. Kwa maneno yake mwenyewe alitamka ‘sihitaji kura zenu’. Kisha akadai kwamba wakiendelea na msimamo wao atawaambia Polisi wawatandike virungu na kusambaratisha mgomo wao.

Lakini leo hii baada ya kuona kuwa wafanyakazi hawakuridhishwa na matamshi yale na washindani wao wakuu CHADEMA wanayatumia kama mtaji wa kisiasa wamezinduka na kuwaongezea wafanyakazi wa umma mishahara kimya kimya.

Halafu kwa sababu walishajua wamechemsha wakawahi kuwatisha viongozi wa TUCTA ili wasitoe msimamo wao kwa niaba ya wafanyakazi, yote hiyo ni katika kuficha aibu.

Je hizi fedha wamezipata wapi?, Je huduma muhimu za kijamii si zitadorora kama walivyosema? Je hii sio rushwa ya wazi wazi kabisa? Haya maswali yanapaswa kufanyiwa tafakuri na wafanyakazi kabla ya kupiga kura, maana wakumbuke msemo usemao ‘bure ya ghali’

Na katika hali ya kushangaza muongoza kitengo cha propaganda wa CCM Bwana Hizza Tambwe, eti anadai kuwa Wananchi hawakumuelewa Mheshimiwa Raisi, hivi aliongea Kikwere, Kimakua, Kibena, Kipare au Kiswahili? Naomba mnidadavulie hapo wenzangu. Haki ya nani hivi jamani!!!
Yaani!!! Hapana jamani hili siyo kabisa!! Aaaah, naomba tuwekane wazi maana inawezekana labda katika mkutano ule na wazee wa jijini Dar es salaam aliongea Kikwere, Kikurya au Kizaramo. Lakini inawezekana Watanzania wote waliosikia ile hotuba siku ile wasimuelewe mheshmiwa kweli? Hivi ni kweli watu milioni karibu 39 wamnukuu mheshimiwa mkuu wa nchi kauli ile, halafu mkuu wa kitengo cha Propaganda anasema wananchi hao milioni 39 hawakumwelewa Rais?

Ndiyo maana nimekumbuka jinsi Jenerali Ulimwengu, katika gazeti la Raia Mwema la jumatano Agosti 11, 2010 akichambua katika safu yake ya RAI YA JENERALI alisema; ‘Msekwa ameajiri Wahuni’. Akitoa mifano ya uundaji wa chama cha mapinduzi CCM mwaka 1977 kuwa mwenendo wa chama hicho sasa ni chama-tawala, hivyo hata wahuni wamepewa ajira ya kuzungumza uhuni kwa kihuni.
Amezungumza kitu muhimu kwamba unaweza usiwe mwanamapinduzi lakini ukajiunga na chama cha mapinduzi. Sasa kwa hali hii ndiyo usemi wake unatimia kwenu wafanyakazi, tayari kitengo kisicho na wanamapinduzi kinasema hamkumwelewa mheshimiwa mkuu wa nchi.

Kwa kweli kila nikumbuka kauli ya mheshimiwa Rais na kauli ya mkuu wa kitengo cha propaganda inanishangaza sana kuona hali hii kipindi hiki. Kwanza Propaganda inayofanyika ni uhuni na inaratibiwa kihuni kwa masuala ya msingi kabisa. Na kama ilivyo Propaganda yenyewe basi kila kitu ni uhuni mtupu. Lakini waungwana hapa najiuliza maswali na kujielekeza kidogo kwenye kiini.

Ama kweli CCM ni mabingwa wa siasa za kimkakati, na mkakati wa kurejea ikulu unajengwa kwa gharama yoyote, na msije kushangaa, damu ikamwagika. Hivi ni nani asiyejua kuwa madaraka ni matamu? Nani asiyejua kuwa ajenda ya kwanza ya chama cha mapinduzi ni kushinda uchaguzi? Hivi kusudio la kitengo cha Propaganda ni lipi jamani?

Naomba kuwatahadharisha wafanyakazi kuwa hii huruma ya serikali dakika za mwisho sio bure wanataka kura zenu, ni vyema mkaanza kusoma alama za nyakati, kwani huruma hii itawahenyesha kwa miaka mitano. Msije mkatarajia kuongezewa mishahara kwa miaka mitano ijayo, itakuwa ni kujidanganya, na itakula kwenu!
Nawakumbusha hili ili mfahamu kuwa gwiji wa michezo ya kuigiza William Shakespeare aliwahi kuandika katika kitabu chake cha Timmons of Athens kwamba ‘Hakuna kinachochochea dhambi kama huruma’. Hiki ndicho ninachowatahadharisha wafanyakazi wa nchi hii.
Kama CCM wanataka kura za wafanyakazi, basi wawe wakweli wa nafsi, japo wahenga walisema kuwa mtu mzima hakosei, lakini kwa hili itabidi wakubali kuwa walikosea na mheshimiwa kama alivyozungumza na wazee pale Diamond Jubilee na kudai kuwa wafanyakazi wana hiyana, akusanye umati ule kwa mara ya pili na kukiri wazi kuwa aliteleza, na aseme ukweli kuwa fedha hizi alizoongeza kinyemela amezipata wapi?

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi hii ni rushwa hata kama watasema suala hili lilikuwa kwenye mchakato. Ina maana waziri Kapuya anatumia muda huu kuhakikisha mkuu wake anarudi kileleni hata kwa kuvunja sheria ya uchaguzi?


Kama ndiyo hali halisi ni kwanini basi iwe sasa na siyo baadaye? Tunakataa rushwa a.k.a mlungula, unaokuja kwa mtindo kama huu. Na hapa wataonesha kwamba ni huruma kwenu kuwaongezea hako kamshahara. Nasema hivi wafanyakazi msitegemee huruma hiyo ni haki yenu hivyo ili haki itimizwe ni lazima maamuzi myachukue kwa tahadhari kabisa hiyo nyongeza, la sivyo, basi na nyie, msikubali kudanyanyika, kwani kama alivyosema mwenyewe, ‘akili ya Mgaya mchanganye na ya kwenu’ basi na mie nawaambia, “huruma hii ya dakika za mwisho si ya bure, ina gharama zake, muwe macho”.


Kama hamuamini, tusubiri ile kauli ya mheshimiwa Rais(endapo atashinda tena) kuwafukuza kazi baadhi ya wafanyakazi. Kwa sasa watakuwa wanyenyekevu sana kwani wanajua bila hiyo hawawezi kuzipata kura zenu. Na mkae mkijua kwamba nchi hii ni yenu na hakuna sababu zozote za msingi kushindwa kusimamia hoja zetu.


Leo nasema hili kwa moyo mweupe kabisa, naamini kila mwenye akili atazingatia ninachosema, kwani nimesema awali kwamba akili zenu changanyeni na za kuambiwa kisha …… jazeni wenyewe. Jamani si kila mshika ngalawa anajua kupalaza mtumbwi, nina maanisha kwamba si kila kauli za huruma sasa zinalenga huruma kwenu wafanyakazi, bali kura zetu na mengine watajaza mbele ya safari.