Kwanza ningependa kuchukua nafasi hii kuwashukuru wasomaji na wanablog wenzangu wote mlionipa pole kwa msiba uliotupata. Kusema kweli kama walivyosema baadhi ya wanablog kuwa ule ulikuwa ni msiba wa taifa kwani roho za watu zaidi ya 20 zimepotea wakiwemo watoto ambao bado walihitaji kuishi na kutimiza ndoto zao.
wakati mwingine unaweza kukufuru mungu kw kuhoji kile kilichotokea, lakini kama maandiko matakatifi katika vitabu vya dini hususana hizi dini zetu mbili ambazo ndizo dini kuu hapa nchi yaani ukristo na uislamu, vilivyoeleza kuwa yote mema na mabaya yanatoka kwake yeye na hatupaswi kuhoji mamlaka yake.
Lakini kama si hivyo naamini tungekuwa tunamlaani sana Mungu pale tunapoondokewa na wapendwa wetu.
Ukweli ni kwamba msiba ule uliotupata nilionyeshwa kabisa na mwenyezi Mungu katika njia ya ajabu sana. Ni kiasi cha wiki nilikuwa nasumbuliwa na malaria kiasi cha kulazwa Hospitalini na kutundikiwa Drip za Kwinini. Nakumbuka siku mbili kabla yakupata msiba ule niliota ndoto ya kustaajabisha sana, niliota kuwa nimeenda kijijini kwa bibi Koero kumtembelea na nilipofika kule kijijini nilipokewa na bibi Koero lakini hakuwa na furaha sana kama nilivyokuwa nimemzoea, nilipomdadisi sababu ya kutofurahishwa na ujio wangu, alinijibu kwa kifupi tu kuwa anajisikia vibaya.
Siku iliyofuata aliniomba nimsindikize shambani kwake ili akanioneshe mazao aliyolima, tulipofika shambani nilishangaa kukuta matuta mengi ya viazi vitamu yakiwa yamestawi barabara, niliruka kwa furaha, kwani mimi huwa napenda sana viazi vitamu, bibi alionekana kunishangaa, nilipomdadisi kuwa kwanini haonekani kufurahia mazao yake, aliniambia kuwa, sina haja ya kufurahia kustawi kwa vile viazi kwani havina ishara nzuri katika familia yetu. nilimdadisi anifafanulie maana ya kusema vile, aliniambia tukae chini anieleze.
Aliniambia kuwa hapo zamani enzi za mababu zao, ilikuwa kama mtu akilima viazi kisha vikastawi sana na kuonesha ishara ya mavuno ya kutosha, waliamini kuwa hiyo sio ishara nzuri katika familia husika, kwani ni lazima pangetokea maafa makubwa au kupata msiba wa mtu mzito katika familia, kwa hiyo hata yeye hawezi kufurahia kustawi kwa yale mazao kwani sio ishara nzuri katika ukoo wetu.
Nilijikuta nikilia kwa sauti, baada ya kusimuliwa habari ile na bibi Koero, nilishtuliwa na mama, alipokuja kuniamsha baada ya kusikia kilio changu. Ilikuwa ni saa kumi za alfajiri, nilimsimulia mama na bada ya kumweleza juu ya ile ndoto aliniambia kuwa sina haja ya kuamini kwani ni mambo ya kishetani, hata hivyo tulisali na mama kisha nikarudi kulala, lakini sikupata usingizi kutokana na kuogopa, ikabidi niamke na kuanza kusoma mtandao na baadae ndio nikaandika ile habari ya siku ya kufa kwangu, nilijikuta tu nikiandika na kuiweka hapa kibarazani kwangu.
Jioni nilipata email kutoka kwa kaka Shabani, Mzee wa Utambuzi. Email yake ilinifumbua macho na kuuona ukweli mpana zaidi, kwamba ile makala yangu haikuashiria jambo jema. kwani baada ya kusoma ile makala yangu niliyoipa kichwa cha habari kiisemacho SIKU YA KUFA KWANGU, kaka Shabani aliniandikia akiniambia kuwa ile makala imemtisha sana na aliniambia kuwa haiashirii jambo jema. Alitaka kujua zaidi hali yangu na pia kujua niliwaza nini mpaka kuandika makala ile.
Sikuweza kumjibu kutokana na kutingwa, lakini siku iliyofuata wakati najiandaa kumjibu na labda kumtaka ushauri juu ya ile ndoto niliyoota ndipo tukapokea taarifa za maafa yaliyotokea kijijini kwa mama ya kuporomoka kwa mlima kulikosababishwana mvua kubwa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 20 wakiwemo shangazi na mjomba wake na mama pamoja na watoto wao.
Ulikuwa ni msiba mzito sana kwetu kwani alikuwa ndiye shangazi yake mama pekee aliyebaki, baada ya shangazi zake watatu kufariki miaka kumi iliyopita.
Safari yetu nayo ya kuelekea msibani iligubikwa na mauzauza mengi, kwani wakati tunakwenda, mimi ndiye niliyekuwa nikiendesha gari na tulipofika Korogwe kwenye kona za msambiazi niligonga Kondoo ambapo alikufa pale pale, nilibabaika kidogo ikabidi dada yangu anipokee na kuendesha yeye.
Leo wakati tunarudi tulisimama Korogwe ili kupata chakula cha mchana, na baada ya kupata chakula tukarejea kwenye gari ili kuendelea na safari, ni hapo ndipo tukagundua kuwa kitasa cha mlango kimevunjwa na mkoba wa mama uliokuwa na fedha, simu zake mbili za mkononi na Kamera umeibwa, tulijaribu kuwauliza watu waliokuwa jirani na gari letu, lakini hatukupata ushirikiano, tuliamua kuondoka lakini tulipofika ya maeneo ya Kwedikwazu, mdogo wangu Jarome ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha gari akagonga mnyama jamii ya kicheche au sijui ni fungo, hata sijui alikuwa ni mnyama gani maana alikuwa akiendesha kwa spidi kubwa kidogo. Ilibidi tumshauri apunguze mwendo hadi tukafika Dar.
Kilichotuuma ni kuibiwa kwa kamera ya mama ambayo ilikuwa na picha nyingi za kumbukumbu ya mazishi ya wale wahanga wa maporomoko ya mlima. Ni jambo ambalo lilitufadhaisha sana.
Tumerejea salama, na wote tuwazima wa afya