Thursday, April 15, 2010

KILA MWELEKWA NA TEMBO…..

Waelekwa na Tembo

Upo msemo mmoja kwa watu wa Pwani usemao Kila mwelekwa na Tembo haachi kugea kani. Huu ni moja ya misemo mingi katika jamii zetu. Je msemo huu una maana gani?
Msemo huu unamaanisha kwamba yule abebwaye na Tembo haachi madaha au maringo.
Katika familia zetu hizi za Kiafrika, sina uhakika sana na za wenzetu huko Ughaibuni, na ndio maana ningependa kuzungumzia zaidi familia za Kiafrika kwa kuwa ndizo ninazozifahamu zaidi.
Katika malezi ya familia zetu hizi za Kiafrika, huwa inatokea mtoto mmoja akawa ni kipenzi cha wazazi yaani baba na mama ukilinganisha na watoto wengine.
Hii haijalishi mtoto huyu anacho kipato au hana, anaweza akawa ni mkorofi na asiyejali wazazi au hata kujijali yeye mwenyewe.
Lakini kama bahati ya kupendwa imemdondokea hakuna wa kupinga. Nasikitika kwamba bahati hii sikuipata mimi katika familia ya mzee Japheti Kisarika Mkundi na mama Namsifu Kiangi Mkundi.
Hata hivyo sina maana kuwa sikitiko hilo ni lawama, la hasha, bali ni namna wazazi wetu wanavyowapenda zaidi baadhi ya watoto wao.
Watoto wa aina hii mara nyingi nao hawaishiwi vituko, ninaamini ni kutokana na kutambua kwao wao ni Kipenzi cha wazazi.
Inaweza ikatokea labda watoto mnaishi huko mjini na mkaamua kuwapelekea wazazi fedha za matumizi,na nguo. Lakini unaweza kushangaa kukuta pesa kapewa kiasi na nguo vile vile.
Wakati mwingine unaweza kukuta wazee wanavaa nguo zenye viraka, chafu na hazistahili kuitwa nguo kwa kiasi fulani, lakini mtoto wao huyo mpendwa kapewa nguo ambazo mlitaka wazazi wajisitiri.
Wazazi hawa hawajijali wao kwanza, bali humwangalia kipenzi chao, na kufanya mambo ambayo yatampendeza. Tena mambo yenyewe ni upendeleo, na yenye kila dalili za kumjali zaidi mtoto huyo kuliko wenyewe.
Na ikitokea mtoto huyo anasababisha vurugu au ugomvi katika familia au kwa watu wengine, kisha walalamikaji wakayafikisha kwa wazazi wake. Utashangazwa licha ya ushahidi wa wazi kuonyesha mtoto wao ni mkorofi, lakini wazazi watamtetea.
Hivyo ndivyo ilivyo katika baadhi ya familia zetu hizi, na watu tumeyakuta hayo na tumeyazoea na pengine na sisi tunayatumia katika familia zetu au tutayatumia huko siku za usoni.
Jambo hili lipo ni katika familia, lakini pia hata katika masuala ya uongozi shiranga hilo lipo. Iwe ni kwenye uongozi katika sehemu za kazi au hata katika uongozi wa kisiasa.
Ni rahisi kujionea upendeleo wa wazi kabisa na wakati mwingine unazusha malumbano miongoni mwa viongozi wenyewe.
Leo ningependa kuzungumzia uongozi wa nchi, na hapa nataka kuzungumzia mamlaka ya juu kabisa ya nchi yetu hii.
Niliwahi kusimuliwa kuwa hata enzi za Hayati baba wa taifa Mwalimu J.K Nyerere, kulikuwa na baadhi ya viongozi ambao walikuwa wakigea kani.
Ilikuwa hata wafanye makosa ya wazi lakini mzee wa Mwitongo huko Mara alikuwa akiwahamisha kutoka sehemu hizo na kuwapeleka sehemu nyingine na huko pia waliendelea kuvurunda.
Lakini aliwavumilia tu, mpaka alipong’atuka madarakani na kujipumzikia hadi kifo chake kilipomkuta. Mungu amlaze mahali pema.
Zilipita awamu mbili baada ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Awamu ya pili ya Rais Mstaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Naye alikuwa na watu wake waliokula Tende na Halua, akaja Rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamini Mkapa, na yeye alikuwa ana wapendwa wake ambao walikunywa Asali na Maziwa.
Sasa tuko kwenye awamu ya nne ya mheshimiwa Jakaya Kikwete, hapa ndipo ninapopata kizunguzungu kabisa na mambo kuwa vululuvululu.
Maana hao waliopata bahati ya kuelekwa na Tembo siyo kwamba wana gea kani tu bali pia wanadhulumu kila kitu na kuwaacha wanyonge wakiteseka, wasijue la kufanya.
Awali kulikuwa na taarifa zilizotolewa na wapinzani pale Temeke Mwembe Yanga kuwa kuna mabilioni ya fedha yametafunwa, lakini wenye mamlaka wakayapuuza madai hayo, na kuonekana kama vile ni uzushi.
Na wengine wakatuhabarisha wanakwenda mahakamani kumshtaki Dr Slaa, lakini mtu mmoja tu alihoji busara za hao wanaotaka kwenda mahakamani naye ni waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba.
Mzee huyu alisema waziwazi kuwa endapo watakwenda mahakamani, wataumbuka na yatazuka mambo ambayo wenyewe wanadhani hayajulikani kwa baadhi ya watu. Ngebe zao ziliishi na hawakwenda mahakamani, ingawaje hawakukoma kuchokonoa.
Sasa baada ya kuchokonoana kwa muda mrefu ndipo kukazuka songombingo la kutajana miongoni mwao, sababu wapinzani walisema kama mhusika hakufanya basi kwa mamlaka yake aliachia suala hilo lifanyike, hivyo awajibike.
Na la maana zaidi, bila shaka sote ni mashahidi wa kile kilichotokea baadaye. Nina hakika baada ya watunga sheria wa chama tawala kule Mjengoni, na pengine ni kutokana na kuchoshwa na vitendo hivyo au ni kutokana na kutoswa na kunyimwa mgawo, wakachachamaa.
Mpaka mwenye mamlaka ya kuiongoza nchi akaridhia wateule wale warejeshe ile akiba waliojichotea ghalani la sivyo wasije wakamlaumu………Ebo! mtu ajichotee tule tuakiba twetu ghalani bila ya ruksa yetu halafu anaambiwa tena kwa kubembelezwa kuwa arejeshe mwenyewe kwa hiyari yake la sivyo asije akalaumu…….
Kimya kimya tukasikia magwiji kukwiba wamerejesha mkwanja na ili kutufumba macho wakakamatwa wachuja nafaka kadhaa na kufikishwa kwa Pilato.
Pamoja na kukamatwa kwao kuna kiini macho huko mpaka leo kuna tamthiliya inaendelea huko ikisubiri oktoba uchaguzi upite mambo yaishe kimya kimya…..ni nani asiyetujua kwa kusahau, na mwanzo wake wameenza na kuzusha mijadala mingine ili kufunika funiko la chuma kwa wachotaji wale.
Hivi sasa, kumeibuka mengine tena, kuwa waelekwa na tembo wamechota ile akiba walioirejesha, kule kwenye ghala letu kuu, wakisingizia Kilimo kwanza.
Hivi inakuwaje mambo haya lakini, mbona kwa wenzetu wako macho, na hawakubali ujinga huu?
Hivi karibuni tumeshuhudia kule Kazykhstan, Rais aliyekuwepo madarakani ambaye hata hivyo walimchagua wenyewe kwa kura nyingi tu lakini wamemtoa madarakani na kinga ya kumlinda kisheria imeondolewa.
Si hivyo tu kule Thailand tumeshuhudia wananchi wakivunja uzio wa jengo la Bunge na kulivamia Bunge kiasi cha kusababisha Waziri mkuu na wabunge kuondolewa kwa Helikopta.
Kwa Thailand kila mmoja anaelewe kile kilichomkuta Thaksin Shinewatra. Alipoondolewa kwa madai ya rushwa na ubadhirifu alipigiwa kelele, lakini leo wananchi walewale waliompigia kelele walipochagua serikali nyingine kumbe nayo ni yaleyale.
Sasa wanamgeukia Shinewatra, na ndiyo maana wakaamua kuvamia mjengoni ili kieleweke maana iliwachosha kuona wadokozi wakiendelea kumaliza ghala yao.
Namini hata sisi tunaweza kukataa ujinga huu, kama wao wameelekwa na Tembo na sisi tumeelekwa na Mungu tuone ni nani mjanja.
Hebu tujiulizeni wote hivi mambo haya mpaka lini, tunahitaji kuamka na kusema basi imetosha.
Nchi haina huduma muhimu za kijamii, hospitali huko vijijini hakuna, na kama zipo hazina dawa, wananchi wanalazimika kutembea umbali wa kilomita kadhaa kufuata huduma hizi huku watu wakiwapoteza wake zao na watoto kutokana na vifo wakati wa kujifungua kutokana na huduma duni.
Huduma ya maji ni duni wakati tuna mito na maziwa nchi nzima, achilia mbali huduma za barabara, kuna mikoa mingine haifikiki kutokana na miundombinu duni.
Fedha hizi licha ya kusaidia kilimo kwanza lakini pia zingeweza kuboresha huduma za kijamii hapa nchini.
Angalia watu katika Kilimo Kwanza wanachota Viatirifu,vocha za pembejeo na kadhalika. Hawa wanajulikana, lakini hawachukuliwi hatua zozote.
Halafu hivi sasa ndio kwanza wameshaanza kuzindua mpango wao wa kuwakamua wananchi hawa masikini kwa njia ya mtandao, tena uzinduzi wenyewe umefanywa kwa mbwembwe na shajara iliyogharimu fedha za walipa kodi.
Yaani kwa sasa tumekuwa tukichotewa ghala yetu halafu tunageukiwa hata ghala za majumbani mwetu zichotwe. Hivi sisi ni watu wa aina gani tusiotambua maana ya maendeleo?
Au maendeleo ni hizo kamari za kuchangia chama ili kiendelee kutuchotea ghala yetu ibakie tupu? Wakati wachotaji na waidhinishaji uchotaji wapo tena walikaa meza za mbele kabisa kuchangishana, na hawajashukuliwa hatua zozote.
Wapare wanayo methali moja inasema "Mshughu kurughe" yaani ni kama M’baazi kujipika, kwamba unaweza kuvuna mbaazi na kisha shina lake likatumika kama kuni na kuzipika mbaazi hizo.
Na ndicho tunachokishuhudia sasa, wananchi kukaangwa na fedha zao, tuchange fedha ziwawezeshe kuingia madarakani kisha tukione cha mtema kuni.
Ndugu zangu, tusipotatua kero ya leo, itakuwa kero ya kesho, na tusipotatua kero ya kesho itakuwa kero ya leo.
Together we can…………..

5 comments:

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Da Koero, sina hakika na kwingineko lakini nadhani hii inatokea Afrina na hususani Tanzania kwa sana!

Unadhani ni tatizo la mifumo ama uelewa wa watawala wetu? Watawala wako kwa ajli ya nani??

Na nini mchango wa wanachi katika kuhakikisha kuwa watawala wanafanya kile ambacho wananchi walitarajia?

NI MASWALI YA KIJINGA kwa kuwa mwanafalsafa mmoja alisema "kiongozi ni kioo cha jamii. kama kiongozi ni mbaya basi wale waliomchagua ni wabaya zaidi kuliko yeye kwa kuwa walimuona yeye ni afadhali afadhali kuliko wao" :-(

Is this how we are made up? :-(

Sintashangaa kuona bado hao hao waeleka tembo tunawarejesha kuendelea kulea yale ambayo tunaona si sawa kwa kuwa ati tulipewa vitenge, chai, wali, t-shirt, kanga, jerojero n.k

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

"What luck for rulers that men do not think" - Adolf Hitler.

“You can fool some of the people all the time, and those are the ones you want to concentrate on.” - George W. Bush (II)

"I am not a liberator. Liberators do not exist. The people liberate themselves." - Che Guevara

Sina la kuongezea.

Yasinta Ngonyani said...

nanukuu "Hebu tujiulizeni wote hivi mambo haya mpaka lini, tunahitaji kuamka na kusema basi imetosha.

Nchi haina huduma muhimu za kijamii, hospitali huko vijijini hakuna, na kama zipo hazina dawa, wananchi wanalazimika kutembea umbali wa kilomita kadhaa kufuata huduma hizi huku watu wakiwapoteza wake zao na watoto kutokana na vifo wakati wa kujifungua kutokana na huduma duni.

Huduma ya maji ni duni wakati tuna mito na maziwa nchi nzima, achilia mbali huduma za barabara, kuna mikoa mingine haifikiki kutokana na miundombinu duni." mwisho wa kunukuu. Ni kweli kabisa pamoja tutaweza. Kwani ni kweli kuna watu wengi sana katika dunia hii wanahitaji mahitaji haya kuliko wanaopata sasa.

Unknown said...

Mimi hii nimeipenda.....

"Wapare wanayo methali moja inasema "Mshughu kurughe" yaani ni kama M’baazi kujipika, kwamba unaweza kuvuna mbaazi na kisha shina lake likatumika kama kuni na kuzipika mbaazi hizo.

Na ndicho tunachokishuhudia sasa, wananchi kukaangwa na fedha zao, tuchange fedha ziwawezeshe kuingia madarakani kisha tukione cha mtema kuni."

Markus Mpangala. said...

"If attackers and atacked are equally matched in strength, only able general will fight". by Sun Tzu.