Wednesday, April 7, 2010

MKE ASIYE NA MUME, AKAMCHUMBIE NANI?


Niolewe na nani mie!
Isingekuwa vigeni, mwanamke kuchumbia
Ningepita mitaani, mume kujitafutia,
Nisimuudhi Manani, ndio nimejizuia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Ndege maingainga, si jambo la kujitakia,
Mume mwema natamani, vipi tajitafutia?
Na mwanamume haini, sitaki kunichumbia,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Nimetulia nyumbani, sina mume kunioa,
Wanifuatao ndani, si wachumba wa kuoa,
Hutaka kunirubuni, maasini kunitia,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Ndege maingainga, si kosa langu sikia,
Niliolewa zamani na mume mwenye udhia,
Kanitia kilabuni, pombe kumchuuzia
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Mimi nikamuamini, huku machozi nalia,
Mume hii kazi gani, alokataza jalia?
Kheri tukate kuni, mimi nitakuuzia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Akapanda hasirani, na maneno akafyoa:
Mke wee mke gani, dini lini ulijua!
Alipozidisha kani, ndoaye nikajivua.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Wako mabwana wa shani, ningependa kunioa,
Hawamtii shetani, Munguamewaongoa,
Nao wamomashakani, kwa mabibi walooa,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?


Tu wema hatujuani, wake na waume pia,
Twaingia mashakani, kwa wenzi waso murua,
Namlilia Manani, mume mwema kunioa,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?



Nawe muombe, ndoa yenu kutulia,
Tusikuone mwakani, viragoumepania,
Mke na mume nyumbani, mumche Mola Jalia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?





Shairi hili limetungwa na Sheikh Amri Abedi, nami limenivutia nikaona niliweke hapa ili tujifunze kwa pamoja

11 comments:

Faustine said...

..Ingawa uelewa wangu wa mashairi ni mdogo, shairi hili ni zuri....
Ila nataka kusema kwamba kupata mme/mke mzuri katika maisha ni bahati.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Faustine: Umenena vema!

Koero: Maua yako tele shambani,
Sherti weye mweenyewe uwende shambani upate kujichumia unalotaka...lol
Ukichagua vibaya utaula wa chuya...lol

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli ni shairi zuri sana na limetulia. Lakini jamani hivi Uzuri wa mke ni nini? Ni uzuri wa sura au ni Tabia?

Jacob Malihoja said...

Kaka Chaha, umesema vyema, maua ni mengi ni kazi ya mtu kuchagua ila huko kuchagua ndio unakuwa mtihani mkubwa maana wengi huenda mikono nyuma wakishafika mtihani mtupu! wengi huvaa ngozi ya kondoo wakishafika hugeuka kuwa chi, kule kwa watani zangu wasukuma kuna jamaa linaitwa Shing'weng'we, hili jamaa liliwahi kwenda kuoa mahali, likiwa kijana tanashati, lakini kufika huku yule binti ndio akagundua kuwa ni lishing'weng'we. Kwakweli ni kumuomba Mungu, maana zamani zile za kujuana famiia siku hizi hazipo tena!

Koero Mkundi said...

Namnukuu kaka Malihoja,

"kule kwa watani zangu wasukuma kuna jamaa linaitwa Shing'weng'we, hili jamaa liliwahi kwenda kuoa mahali, likiwa kijana tanashati, lakini kufika huku yule binti ndio akagundua kuwa ni lishing'weng'we. Kwakweli"

Mwisho wa kunukuu.

jamani hili neno "Shing'weng'we" lina maana gani kaka Malihoja...naogopa nami nisije mpata huyo Shing'weng'we wangu nikawa nimeuingia mkenge.....msaada tafadhali...LOL

Faustine said...

...@Yansinta..Uzuri wa mke ni tabia...sura ni bonus...

MARKUS MPANGALA said...

MSAADA HAPA TAFADHALI MNANIUA BUREE MBAVU ZANGU "Shing'weng'we"

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Ninamalizia kitabu cha mashairi huru ambacho nimeamua kukiita "Mashing'weng'we". Niliwahi kugusia shairi mojawapo kutoka katika kitabu hicho hapa:

http://matondo.blogspot.com/2009/01/falsafa-ya-mlevi-1_30.html

Bwana Malihoja umenikumbusha mbali kwani hadithi za Mashing'weng'we bado nazikumbuka sana. Menyewe ni mazimwi yenye tabia ya kumeza watu na yanaweza kumeza hata kijiji kizima. Lakini pia yana uwezo wa kujigeuzageuza sura - mara vijana watanashati waungwana, mara mashujaa hodari, mara...Usiku unapoingia hata hivyo ni lazima yarudie hali ya "ushing'weng'we" na hapo ndipo kizungumkuti kinapoanzia. Kwa hivyo ni kweli kwamba kijana muungwana wakati akitongoza anaweza kuwa ameuficha tu "ushing'weng'we" wake na usiku ukiingia basi anarudia hali yake halisi.

Kama walivyodokeza wadau hapo juu, mimi pia naamini kwamba linapokuja suala la kuchagua mwenzi wa maisha, hakuna fomyula bali ni kubahatisha tu kwani binadamu ni kiumbe tata mno na si rahisi kumwelewa.

Vinginevyo kama wewe ni mlokole funga na umwombe Mungu akuchagulie. Nimesikia mara nyingi watu wakisema kwamba mwenzi mwema hutoka kwa Mungu....

Unknown said...

Kielelezo no 1 cha uzuri
Ndo maana ukiwa na umbo zuri watu hawasemi ww nzuri
Wanasema anashape nzuri

Unknown said...

Sura ndo uzuri wa mwanamke
Shape na vingine vinafuatia

Unknown said...

Lau ingekua tabia
Tusingeoa maana tabia ya mtu huwezi ijua
Mwanamke anapopita barabarani as kuwa anatembea tabia unsjuaje??
Hadi kugeuza shingo kumwangalia je umeona tabia nzuri kwake au umbo lake na sura yake nzuri